ORYX GAS WATOA MITUNGI 1000 KWA MAMA NA BABA LISHE UZINDUZI WA KAMPENI YA PIKA KIJANJA

September 08, 2024

 KAMPUNI ya Oryx Gas imetoa mitungi 1000 kwa Mama na baba lishe wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Azimio la Kizimkazi iliyolenga kuunga mkono jitihada za Rais, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan  katika kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya Kupikia.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Septemba 8, 2024 Jijini Dar es Salaam Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuokoa maisha yao kwa  kutumia Nishati Safi ya Kupikia ambayo itawaepusha na madhara yanayotokana na Nishati isiyo safi ikiwemo athari katika mfumo wa upumuaji.

Dkt. Biteko amesema, Rais Samia licha ya kuwa kinara wa Afrika kwenye kampeni ya kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia, pia amedhamiria kuwaondoa kina Mama na Baba Lishe wa Tanzania katika matumizi ya Nishati isiyo safi na pia kuboresha hali zao kwa kutumia Nishati safi ya Kupiki ambapo ametoa mitungi 2,000 kwa kundi hilo kama njia ya uhamasishaji wa nishati hiyo.

"Nipende kumpongeza sana Mhe Rais kwa kuibeba ajenda hii ya Nishati safi ya Kupikia na kwa maono aliyonayo, nitoe agizo kwa Watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha Wizara inashirikisha wadau kwenye kampeni hii ili iweze kufanyika kwa ufanisi na hivyo kumuunga mkono Mhe. Rais." Amesema Dkt. Biteko.

Amesema kampuni ya Oryx Gas imekuwa ikitoa ushirikiano kwa Serikali na wamekuwa wakishiriki katika matukio mblimbali ya kugawa mitungi ya gesi na majiko yake kwa wananchi sambamba na utoaji mafunzo ya matumizi salama ya nishati safi ya kupikia.

Akitoa takwimu za hali ilivyo kwa sasa, Dkt. Biteko amesema watu Bilioni 5.8 duniani ndio wanatumia Nishati Safi huku Bilioni 2.4 wakitumia Nishati isiyo safi ambapo Afrika Pekee ina watu milioni 933 wanaotumia Nishati isiyo safi na hivyo kuwataka wadau kuuganisha nguvu kuunga mkono matumizi ya Nishati iliyo safi.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na  Baba na Mama Lishe nchini na ndio mana kwenye hafla hiyo ya Azimio la Kizimkazi wamealikwa ili kuwahamasisha kuondokana na matumizi ya Nishati chafu na hivyo kuboresha mazingira yao ya ufanyaji kazi kwa kuwapatia Mitungi ya gesi kama Nishati mojawapo iliyo safi.

Amesema kimsingi muktadha wa Mhe Rais kama Kinara wa Nishati safi ya Kupikia Afrika ni utekelezaji pia wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoelekeza Watanzania kupatiwa  Nishati Safi ya Kupikia kwa wakati na kwa gharama nafuu na ndio maana mitungi takriban 450,000 iliamuliwa iuzwe bei ya ruzuku ili kuwafikia wananchi.

Akizungumza wakati akitoa salamu za Oryx kwa Serikali pamoja na wageni waalikwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Benoit Araman amesema Oryx Gas Tanzania inafanya kazi bila kikomo kila siku ili kutekeleza maono ya Rais Samia ya kwamba asilimia 80 ya Watanzania ipate nishati ssafi ifikapo 2034. 

“Mpango huu utafanikiwa tu ikiwa tumejitolea kutumia nishati safi ya kupikia kila siku.Leo hii katika muendelezo ule ule wa kuunga mkono jitihada za Rais Samia tunakabidhi mitungi ya gesi yq Oryx 1000 kwa Mama na Baba Lishe ambao wameungana nasi katika hafla hii ya Pika Kijanja.”

Pia amemshukuru Waziri wa Nishati, Dk Biteko na Naibu Waziri Kapinga kwa kuwashirikisha ambapo mbali ya kutoa mitungi ya gesi wametoa mafunzo yq matumizi salama ya nishati safi ya kupikia.

Akizungumzia faida na kutumia nishati safi ya kupikia ,Benoit amesema kiafya nishati safi inasaidia kuokoa maisha kwani kumekuwa na vifo vinavyotokana na magonjwa ya upuamuji yayanayosababishwa na matumizi yq nishati chafu.

“ Nchini Tanzania, wananchi 33,000 wanakufa kila mwaka kutokana na kuvuta pumzi ya moshi na chembe chembe zinazotokana na mkaa na kuni. Kupika na Oryx LPG kutasaidia kumaliza changamoto hiyo ya kiafya lakini kwa mazingira  kupika kwa nishati safi huzuia ukataji miti na hivyo kulinda mazingira”

Ameongeza kuwa kupika kwa nishati safi husaidia kuzuia  wanawake kufanya kazi ngumu ya kutumia muda mwingi kukusanya kuni kutoka msituni.Pia kupika kwa nishati safi husaidia kuwaweka wanawake katika hali ya usalama kwani porini kumekuwa na hatari nyingi.
















PROFESA MKENDA -SERIKALI IMEWEKA MSUKUMO KATIKA MASOMO YA SAYANSI

September 08, 2024








Serikali imeweka msukumo katika masomo ya Sayansi ikiwa ni pamoja na kujenga shule 26 za wasichana zinazotoa masomo ya Sayansi.

Hayo yamesemwa hii leo tarehe 8.Sep. 2024  na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda kwenye  Marathon ya ERB (Bodi ya usajili wa Wahandisi Nchini)

Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali imeanzisha Skolashipu kwa wanafunzi wa kidato cha sita watakao faulu vizuri zaidi masomo ya Sayansina kwenda chuo kikuu kusoma masomo ya Uhandisi, Tehama, Hisabati na Elimu tiba ambao kupitia ufadhili huo wanalipiwa gharama kwa asilimia mia moja huku lengo la Serikali ni kuchochea wanafunzi wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi.

Profesa Mkenda ameongeza kuwa hakuna Nchi Dunianj inayoendelea bila Sayansi ya Teknolojia hivyo Serikali itaendelea  kuongeza nguvu kwenye masomo ya Sayansi ili kupata wanafunzi waliobora kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.


Lengo la mbio za ERB ni kuwainua na kuwawezesha wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi na kuwezesha, Walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi kwa Mkataba.


Huu ni msimu wa kwanza wa ERB Marathon na mbio hizi zitakuwa zinafanyika kila mwaka ifikapo mwezi wa tisa huku wakimbiaji mia saba na kuendelea wakialikwa kushiriki mbio hizi.


Waziri Mkenda ameweka historia ya aina yake kwa kuweza kumaliza kilomita kumi jambo ambalo limewafurahisha wanariadha wengi zaidi.


Mbio hizo zilianzia katika uwanja wa UDASA kupitia Samu Nujoma, Makomgo juu na mwisho ni katika viwanja vya UDASA vilivyopo katika Chuo kikuu cha Dar es salaam.

REA YAENDELEA KUTEKELEZA DHAMIRA YA RAIS SAMIA KWA VITENDO

September 08, 2024


WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) umeanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kila Mwananchi anatumia Nishati Safi ya Kupikia.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema hayo Jijini Dar es Salaam Septemba 08, 2024 wakati wa uzinduzi wa Kipindi maalum cha Pika Kijanja na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan maarufu kama Azimio la Kizimkazi.

“Mhe. Rais wakati anazindua Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 Mwezi Mei mwaka huu alitoa maagizo maalum kwa REA; kwakuwa tumefanya vizuri katika kusambaza umeme vijijini huku nako kwa kushirikiana na wadau wengine tuhakikishe asilimia 80 ya Watanzania wanatumia Nishati Safi za Kupikia ifikapo mwaka 2034,” alisema Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy alibainisha kuwa Wakala umeanza kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais kwa namna mbalimbali ikiwemo kuhamasisha wananchi kutumia Nishati Safi za Kupikia kwa kuondokana na fikra kuwa bidhaa za Nishati Safi ni ghali ama si salama na kwamba chakula kinachopikwa kwa Nishati Safi hakina ladha.

“Tunaendelea kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kwamba suala la ladha ya chakula linategemea umahiri wa mpishi ama viungo vinavyotumika na sio nishati inayotumika kupikia,” alisema Mhandisi Saidy

Mhandisi Saidy alisema Wakala unaendelea kuwezesha upatikanaji wa Nishati Safi za Kupikia kwa kushirikiana na watoa huduma ambapo REA inawapa fursa watoa huduma kujitangaza ili kuwezesha wananchi wengi kufahamu uwepo wa teknolojia rafiki za nishati safi za kupikia.

Alibainisha kuwa Serikali kupitia REA inatoa ruzuku ili kuwezesha wananchi wamudu kununua bidhaa za Nishati Safi za Kupikia na kujionea ubora wa bidhaa hizo kwa lengo la kuendelea kuhamasisha wananchi wengi wahame kutoka kwenye kutumia nishati zisizokuwa salama.

“Serikali imetoa ruzuku ili kila mwananchi aweze kumudu gharama; Mathalan kwenye mitungi ya gesi (LPG) na vichomeo vyake Serikali kupitia REA imeidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kitumike kusambaza Mitungi ya Gesi ya kilo 6 itakayonufaisha watanzania wapatao 452,445 kwa bei ya ruzuku,” alifafanua.

Mhandisi Saidy alibainisha kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya mia moja zianze kutumia Nishati Safi za Kupikia na kwamba katika utekelezaji wake, REA imeandaa miradi ya kufikisha bidhaa na teknolojia za Nishati Safi za Kupikia kwenye taasisi hizo.

“Tunatekeleza agizo la Mhe. Rais na tumeanza na Magereza wao wana maeneo 211 tutakayoyafikishia Nishati Safi za Kupikia pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwenye Kambi 22 na Shule kongwe zipatazo 52; kwa kifupi kila taasisi yenye watu zaidi ya mia itafikiwa,” alisema Mhandisi Saidy.

Sambamba na hilo, Mhandisi Saidy alisema REA inafanya kazi kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo linazalisha mkaa rafiki na kwamba REA inakwenda kuiwezesha STAMICO kununua mashine tatu za kuzalisha mkaa rafiki ili iweze kufikisha huduma kwenye maeneo mengi zaidi.

Aidha, Mhandisi Saidy alisema REA hadi sasa imefanya vizuri kwenye suala zima la kusambaza umeme vijijini ambapo hadi sasa utekelezaji umefika asilimia 99 na kwamba nguvu iliyotumika kusambaza umeme itatumika pia katika kuhakikisha wananchi wote wanapata Nishati Safi za Kupikia.





MONGELA AZUNGUMZA NA VIONGOZI WA CHAMA NA WAZEE KATA YA BULUNGWA, HALMASHAURI YA USHETU

September 08, 2024

 Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, John Mongella, akizungumza na Viongozi wa chama na Jumuiya ngazi ya Kata na Matawi,mabalozi,Wazee maarufu na viongozi wa Kimila katika kata ya Bulungwa,Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga,leo Septemba 8,2024.


Mongella anaendelea na ziara yake ya siku saba mkoani Shinyanga yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2024, kuimarisha uhai wa chama sambamba na kujitambulisha.










TMA YAWAKUMBUSHA WAHANDISI KUZINGATIA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI.

September 08, 2024

 WAHANDISI nchini wamekumbushwa umuhimu wa huduma za hali ya hewa sambamba na kuchangia gharama za upatikanaji wa huduma hiyo katika utekelezaji wa miradi yao.


Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa amesema hayo hivi karibuni katika mada iliyowasilishwa kwenye Mkutano wa 21 wa Wahandisi uliyojumuisha wahandisi wa ndani na nje ya nchi katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Dkt. Kabelwa ameeeleza kuwa, katika hotuba ya Waziri wa Fedha ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2024/25, kifungu cha 158 ilijumuisha mapendekezo ya mabadiliko ya kufanya marekebisho ya sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, sura 157 kuhusu Ada za Hali ya hewa kwa usalama wa uendeshaji wa miradi ya ujenzi.

“Lengo la hatua hiyo ni kuongeza mapato yatakayowezesha utoaji wa huduma mahsusi za hali ya hewa ili kuongeza tija na ufanisi wa utendaji kazi na kuimarisha usalama wa watu na mali katika maeneo ya miradi ya ujenzi, ambapo mchakato wa upatikanaji wa huduma hizo unahitaji uwekezaji wa miundombinu ya kisasa na gharama kubwa za uendeshaji”. Amefafanua Dkt. Kabelwa.