RAIS BANDA AMEWAFUKUZA KAZI MAWAZIRI WAKE WOTE KUTOKANA NA UFISADI

October 11, 2013
Rais wa Malawi, Joyce Banda amelifuta kazi baraza lake la mawaziri kutokana na kuongezeka kwa visa vya ufisadi serikalini.

Maafisa wa serikali wamekuwa wakipatikana na pesa zikiwa zimefichwa chini ya vitanda vyao na kwenye magari yao, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Raphael Tenthani.


Mwezi jana afisa mmoja mkuu katika wizara ya fedha Paul Mphwiyo, aliyeonekana kuwa afisaa mmoja mkuu serikali ambaye anaonekana kupinga sana ufisadi, alipigwa risasi na kujeruhiwa.

Wahisani wa kimataifa wamekuwa wakimtaka rais Banda kuchukua hatua kukabiliana na ufisadi.

Malawi ni taifa masikini na hutegemea sana msaada kutoka kwa Muungano wa Ulaya na nchi zengine za kimagharibi.
 

Banda amesema kuwa mawaziri wapya watateuliwa hivi karibuni bila ya kutoa maelezo zaidi na aliitisha mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri kabla kutangaza kulivunja.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari Banda alisema kuwa ameunda jopo maalum likijumuisha polisi na maafisa wa serikali kufanya ukaguzi wa matumizi ya pesa za serikali katika idara zote za serikali.

Mwandishi wa BBC nchini humo anasema kupigwa risasi kwa bwana Mphwiyo ndio ilikuwa mwanzo wa taarfa kuwa baadhi ya maafisa wa serikali wanashirikiana na wafanyabisahara kuifilisi serikali katika utoaji wa kandarasi na mikataba bandia.

Washukiwa wanne walikamatwa kuhusiana na kupigwa risasi kwa afisa huyo huku takriban maafisa kumi wa serikali wamekamatwa wakisubiri kusikilizwa kwa kesi zao kuhusiana na ufisadi.

AU KUJADILI UHUSIANO WAKE NA ICC

October 11, 2013
Marais wa Afrika wanakutana wikendi hii mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kujadili uhusiano wa bara la Afrika na mahakama ya kimataifa ya jinai ICC.

Mkutano huu maalum umeitishwa baada ya ICC kukataa ombi la wanachama 54 wa Muungano wa Afrika kurejesha kesi za Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto nyumbani

Viongozi hao wanatarajiwa kujadili hoja ya kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo.

Baada ya miezi kadhaa ya kutofautiana kati ya ICC na AU, viongozi wa Afrika wanakutana katika makao makuu ya AU katika kile kinachosemekana ni kutafakari upya uhusiano wa bara hilo na mahakama ya ICC.

Kwa mujibu wa AU, mahakama hiyo ya ICC imekosa kushughulikia ombi lililowasilishwa na AU mwezi Mei kuhusu kesi za Kenya. AU inasema kuwa ICC ina njama za kibaguzi dhidi ya viongozi wa kiafrika.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanakabiliwa na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu katika mahakama hiyo.

Kesi yao inahusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2007/2008 ambapo zaidi ya watu 1100 waliuawa.

Hata hivyo viongozi hao wamekanusha madai hayo.

Bunge la Kenya ambalo lina idadi kubwa ya wabunge wa mrengo wa Jubilee unaotawala nchi, tayari lieanzisha hoja ya kuondoa Kenya kutoka katika mahakama ya ICC.

Lakini serikali ya Kenya imesema haijashinikiza

nchi za Afrika kujadili hoja ya kujiondoa ICC licha ya kuungwa mkono na majirani zake kama Uganda na Rwanda.

Naibu mwenyekiti wa AU Erastus Mwencha, ameambia BBC kuwa swala hilo sasa ni zaidi ya kutaka tu kujiondoa ICC.

Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa huenda AU isikubali kwa ujumla kujiondoa ICC. Baadhi ya nchi kama Ghana na Botswana tayari zimepinga hatua ya kujiondoa ICC.

SIMBA YAIVAA PRISONS, YANGA MGENI BUKOBA VPL

October 11, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inakamilisha raundi ya nane kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kwa mechi tatu zitakazochezwa Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.

Simba ina fursa ya kuendelea kukamata usukani wa ligi hiyo iwapo itaishinda Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne Chale inashika nafasi ya kumi na moja katika msimamo wa ligi hiyo.

Ili iendelee kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 24 mwaka huu, Tanzania Prisons ambayo katika mechi yake iliyopita ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting inalazimika kuifunga Simba.

Licha ya sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting, Simba inayoongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Azam na Mbeya City matokeo mazuri katika mchezo huo ni muhimu kwao kama ilivyo kwa wapinzani wao Tanzania Prisons.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 ambapo tiketi zitauzwa uwanjani kwenye magari maalumu kuanzia saa 4 kamili asubuhi.

Mabingwa watetezi Yanga wao watakuwa mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wanaofundishwa na Mganda Jackson Mayanja akisaidiwa na Mrage Kabage.

Kagera ambayo inapishana na Yanga kwa tofauti ya pointi moja ilipoteza mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya kulala kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex. Wakati Yanga ikiwa katika nafasi ya nne kwa pointi 12, Kagera Sugar ni ya sita kwa pointi kumi na moja.

Iwapo Kocha Ernst Brandts atawaongoza vijana wake wa Yanga kuibuka na ushindi katika mechi hiyo na Simba kufanya vibaya kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons huenda akakamata uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.

Mwamuzi Zakaria Jacob wa Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya Ashanti United na Coastal Union itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.

Raundi ya tisa ya ligi hiyo inaanza keshokutwa Jumapili (Oktoba 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers (Mabatini, Mlandizi), Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na JKT Ruvu (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu, Turiani).

Mechi zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam TV kupitia TBC1 wikiendi hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.

NYALLA, NYAULINGO, NYENZI WASHINDA RUFANI

October 11, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewarejesha warufani wote watatu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Samwel Nyalla, Ayubu Nyaulingo na Ayoub Nyenzi walikata rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwaondoa katika uchaguzi huo ambapo wote wanagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali.

Akisoma uamuzi wao leo (Oktoba 11 mwaka huu) mbele ya Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF, Jaji Luanda amesema baada ya kusikiliza hoja za Mrufani Nyalla walipitia Kanuni za Uchaguzi za TFF na kugundua yafuatayo;

Ibara ya 10(3) imeweka masharti makuu mawili ya ujazaji wa fomu za kugombea uongozi. Fomu hiyo ni lazima iwe na saini ya mgombea na ni lazima ithibitishwe na viongozi wa shirikisho.

Kamati imepitia Kanuni za Uchaguzi haijaona sehemu fomu hiyo ya uongozi imeambatanishwa ili kuifanya kuwa Kanuni ya Uchaguzi. Ni maoni ya Kamati kuwa ni vizuri fomu za kugombea zikawa ni sehemu ya Kanuni za Uchaguzi.

Kwa vile Kanuni za Uchaguzi za TFF za 2013 pia hazijaainisha nini adhabu kwa mgombea aliyekosea kujaza Fomu namba 1 ya kugombea uongozi, Kamati inaona itakuwa si haki kumnyima mgombea nafasi ya kushiriki katika uchaguzi kwa vile tu fomu yake haijajazwa vipengele vyote.

Nyalla aliondolewa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa maelezo kuwa si mtu makini anayeweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu baada ya kushindwa kujaza Fomu namba 1 kipengele cha 15 kinachohusu malengo ya mgombea uongozi.

Kwa upande wa Nyaulingo ambaye aliondolewa kwa kukosa uzoefu uliothibitika kulingana na Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, Kamati ya Rufani imeamua ifuatavyo;

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.

Mrufani alifafanua historia yake katika masuala ya michezo kuanzia alipokuwa anasema Chuo Kikuu kuanzia 2005-2009 na pia ushiriki wake kama mchezaji wa Rukwa United iliyowahi kushiriki Ligi ya Mkoa wa Rukwa na ligi nyingine za kitaifa.

Kwa kusoma maana ya ‘Familia ya TFF’ iliyoko kwenye utangulizi wa Katiba ya TFF, pamoja na Ibara ya 29(3) na 29(6) ya Katiba hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Mrufani ana sifa za kugombea uongozi wa Shirikisho na amekidhi kigezo cha sifa za ugombea.

Ameshiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu kama mchezaji na mtawala, hivyo kutimiza kigezo kilichohitajika cha ushiriki katika uongozi na utawala wa mchezo wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.

Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani anapewa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi.

Kuhusu Ayubu Nyenzi aliyeondolewa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, na pia kushindwa kuthibitisha uraia wake mbele ya Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani katika uamuzi wake imesema;

Imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.

Baada ya uchambuzi wa kina, Kamati imeona kuwa kulingana na maelezo yaliyotolewa na Mrufani na viambatanisho vilivyowasilishwa, Kamati haina shaka kuhusu uraia wake. Uthibitisho wa uraia unapaswa kufanywa kwa umakini na taasisi yenye mamlaka ya kiserikali kufanya hivyo.

Kamati pia imejiridhisha kupitia Fomu namba 1 iliyojazwa na kusainiwa na Mrufani kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010, Nyenzi ameshika nyadhifa za utawala wa mpira wa miguu na hasa katika klabu ya Yanga, uzoefu unaomfanya kuwa na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi katika TFF kulingana na Ibara ya 29(3) ikisomwa pamoja na Ibara ya 29(6).

Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani atashiriki katika uchaguzi wa TFF kwa nafasi anayogombea.

Wakati huo huo, Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF inakutana keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu), kufanyia mapitio (revision) ya uamuzi wa Kamati ya Maadili kwa waombaji uongozi wanane kama ilivyoombwa na Sekretarieti ili kutoa mwongozo wa utekelezaji wa uamuzi huo.

VITAMBULISHO KURIPOTI KOMBE LA DUNIA

October 11, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Maombi ya vitambulisho kwa waandishi wa habari (Accreditation) wanaotaka kuripoti Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) yataanza kupokelewa kwa mtandao Desemba 7 mwaka huu kupitia akaunti ya FIFA Media Channel.

Mwisho wa kupokea maombi hayo itakuwa Januari 31 mwakani, hivyo kwa waandishi wanaotaka kupata vitambulisho hivyo ni lazima wawe na akaunti ya FIFA Media Channel pamoja na utambulisho wa mtumiaji wa akaunti hiyo (user ID).

Kwa mujibu wa FIFA, kila nchi itapewa idadi maalumu ya nafasi kwa waandishi (waandishi wa kawaida pamoja na wapiga picha) baada ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia kumalizika ambapo vigezo mbalimbali vitazingatiwa ikiwemo nchi kufuzu kwa fainali hizo.

Hivyo, nchi ambayo itakuwa imefuzu itakuwa na nafasi zaidi kulinganisha na zile ambazo hazitakuwa na timu katika fainali hizo za Brazil.

Mgawanyo wa nafasi zitakazotolewa kwa Tanzania utapangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kulingana na maombi yatakayokuwa yamewasilishwa FIFA kupitia FIFA Media Channel.

TFF inatoa mwito kwa waandishi wa habari za mpira wa miguu ambao hawana akaunti FIFA Media Channel kuhakikisha wanakuwa nayo mapema ili waweze kutuma maombi yao.

FDL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI HII

October 11, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote matatu inaendelea wikiendi hii ambapo kundi B litakuwa na mechi moja tu kati ya Lipuli na Mlale JKT itakayochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.

Transit Camp itakwaruzana na Tessema katika Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Polisi Dar itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam katika mechi za kundi A zitakazochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu).

Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kuzikutanisha Friends Rangers na Villa Squad.

Timu zote nane za kundi C zinashuka viwanjani kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kusaka pointi tatu. Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Dodoma na JKT Kanembwa ya Kigoma.

Pamba na Mwadui zitacheza katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Polisi Tabora itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati uga wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma utatumika kwa mechi kati ya Polisi Mara na Stand United ya Shinyanga.

KAMOTE KUZICHAPA NA NJIKU OCTOBA 16 MKWAKWANI

October 11, 2013
NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
BONDIA Allen Kamote wa Tanga anatarajiwa kupanda ulingoni kuzichapa na  Deo  Njiku wa Morogoro katika pambano la kuwania ubingwa wa Dunia WBF litakalokuwa la raundi kumi na mbili lenye uzito wa kg 61 ambalo litafanyika katika uwanja wa Mkwakwani Octoba 16 mwaka huu.

Pambano hilo linatarajiwa kuanza majira ya saa kumi jioni siku ambayo 
itakuwa ni siku ya Idd Mosi(Idd Al-Haji) litakalo tanguliwa na mapambano nane ya utangulizi .

Mratibu wa Pambano hilo,Abasi Mwazoa alisema maandalizi yake
yanaendeleo vizuri na kuyataja mapambano ya utangulzi kuwa ni bondia Rajabu Mahoja wa Tanga ambaye atapanda ulingoni kuzichapa na  J.J Ngotiko wa Tanga watakaocheza pambano la raundi kumi lenye uzito wa kg57.

Mwazoa aliongeza kuwa bondia Khamis Mwakinyo wa Tanga atazichapa na 
Haruna Magali wa Morogoro katika pambano la raundi sita lenye uzito wa kg 64 wakati Saimon Zabron na Mohamed Kibari wote wa Tanga watachuana kwenye pambano la raundi sita lenye uzito wa kg 61.

Aliyataja mapambano mengine kuwa ni bondia Said Mundi wa Tanga 
atazichapa na David Maina wa Kenya katika pambano la raundi sita lenye uzito wa kg 61 ambalo linatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu.

Pambano mengine yatakuwa ni bondia Zuberi Kitandula wa Tanga 
atazichapa na Hajji Juma wa Tanga katika mpambano utakaokuwa wa raundi nane lenye uzito wa kg 55 huku Jumanne Mohamed wa Tanga atapanda ulingoni kuzichapa na Obote Ameme wa Dsm wataocheza pambano la raundi nne lenye uzito wa kg 57.

Mratibu huyo alilitaja pambano la mwisho la utangulizi litakuwa ni 
kati ya bondia Alli Boznia wa Kenya ambaye atazichapa na Jacob Maganga wa Tanzania litakalokuwa la raundi nne lenye uzito wa kg 69.

USHINDI WA BAO 3-0 WAMPA KIBURI MWALALA.

October 11, 2013

Na Oscar Assenga, Muheza.
KOCHA Mkuu wa timu ya Halmashauri FC ya Muheza, Benard Mwalala (wa kwanza kulia katika picha juu) amesema ushindi walioupata dhidi yao na Lushoto Shooting ya wilayani humo katika mchezo wa Ligi ya Mkoa wa Tanga ni ishara nzuri kwao kuendelea kufanya vizuri mechi zao zifuatazo.

Mwalala alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kumalizika mchezo huo ambapo timu hiyo iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 mchezo uliochezwa uwanja wa soka Jitegemee wilayani hapa.

Katika mchezo bao la kwanza la Halmashauri lilipatikana katika dakika ya 15 kupitia Ramadhani Msumi ambaye alipachika mabao mawili na dakika ya 44.

Mpaka timu zote zinakwenda mapumziko, Halmashauri FC walikuwa wakiongoza katika mchezo huo ambapo ulikuwa na upinzani kwa timu zote kushambuliana kwa zamu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo timu zote ziliingia uwanjani hapo zikiwa na hari ya mchezo baada ya kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji wao.

Wakionekana kujipanga na kuwakamia wapinzani wao,Halmashauri FC iliweza kuendeleza wimbi la ushindi langoni mwa Lushoto Shooting na kufanikiwa kuandika bao lao la tatu kwenye dakika ya Gao Jaffari dakika ya 75.

Mwalala alisema malengo yao msimu huu ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mashindano hayo ili iweze kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa wa mikoa na hatimaye ligi daraja la kwanza pamoja na ligi kuu siku zijazo.

MASHINDANO YA MKONGE CUP KUANZA KESHO.

October 11, 2013

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
MICHUANO ya Kombe la Mkonge Cup inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho (leo) kwenye mashamba ya mkonge yaliyopo sehemu mbalimbali hapa nchini.

Akizungumza na Tanga Raha, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo,Lai Mpuma alisema mashindano hayo msimu huu yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na maandalizi yaliyofanywa na timu shiriki.

Mpuma alisema timu shiriki katika michuano hiyo zimepangwa katika makundi manne ambapo katika kundi A kutakuwa na timu za China State ambao watafugua pazia la mashindano hiyo kwa kucheza na New Msowero katika uwanja wa soka Rudewa.

Alisema katika kundi B timu ya Toronto na Magoma hizo ndio zitafungua pazia la michuano hiyo katika uwanja wa Toronto wakati Mkumbara na Mazinde wao watacheza pia katika uwanja wa soka Mkumbara.

Aidha aliongeza kuwa katika kundi C timu zitakazofungua pazia la mashindano hayo ni Kauzeni na Amboni Sp Mill katika uwanja wa soka Kauzeni wakati Lugongo na Muheza Estate nao wakicheza kwenye dimba la Lugongo.

Mwenyekiti huyo alisema michezo mengine itakayochezwa siku hiyo ni Sakura ambao watacheza na Tancord kwenye dimba la soka Sakura huku Mwera na Kumburu wakihitimisha mechi hizo katika uwanja wa soka Mwera.

WABAKAJI WAADHIBIWA KWA KUKATA NYASI KENYA

October 11, 2013
NA MWANDISHI WETU,KENYA
Wakenya wameghadhabishwa sana na hatua ya wanaume watatu waliombaka msichana mmoja na kutupa mwili wake kwenye choo kuamrishwa na polisi kukata nyasi kama adhabu kwao.

Msichana huyo alishambuliwa na kubakwa akiwa njiani kutoka kwa mazishi ya babu yake katika kijiji kimoja Magharibi mwa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa za gazeti la Daily Nation nchini Kenya, uti wa mgongo wa msichana huyo ulivunjika wakati wa ubakaji na sasa amelazimika kutumia kiti cha magurudumu.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu pamoja na wabunge wamelaani polisi kwa kukosa kuchunguza madai ya msichana huyo.

Msichana huyo alinukuliwa akisema kuwa anataka waliomfanyia kitendo hicho kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Idara ya polisi inawachunguza polisi waliopokea malalamishi ya msichana huyo , alisema Halima Mohammed , kamanda wa polisi katika jimbo la Busia ambako kitendo hicho kilitokea.

Hii bila shaka inaonyesha wazi ulegevu wa polisi katika kukabiliana na vitendo kama hivi na ambao wakenya wanahisi kuwa unakumba idara ya polisi , hasa baada ya mashambulizi ya kigaidi nchini humo wiki mbili zilizopita.

Msichana huyo aliwafahamu vyema waliombaka na polisi walirekodi kesi dhidi ya watatu hao.

Wanakijiji waliwapeleka watatu hao kwa polisi baada ya kusikia taarifa za kitendo hicho.

Lakini waliamrishwa kukata nyasi katika bustani la makao ya polisi na kisha baadaye kuachiliwa, alisema mamake mwathiriwa.

Masaibu ya msichana huyo yalijadiliwa na kamati ya bunge kuhusu usalama na kusema kuwa kitendo hicho ni cha kushutua sana na lazima wakifanyie uchunguzi.

Kwa mujibu wa Bi Mohammed, mama ya msichana huyo aliamrishwa kumsafisha mwanawe ili ushahidi wowote dhidi ya washukiwa uweze kupotea.

Msichana huyo sasa amelemazwa na kulazimishwa kutumia kiti cha mgurudumu.

WAKAGUZI SYRIA WASHINDA TUZO YA AMANI YA NOBEL.

October 11, 2013
Tuzo ya amani ya Nobel, mwaka huu imekwenda kwa shirika la kudhibiti silaha za kemikali duniani OPCW.

Shirika hilo kwa sasa linasimamia shughuli ya kuharibu silaha za kemikali za Syria ambazi zilitumiwa kwa mauaji ya raia wa nchi hiyo mjini Damascus mwezi Agosti.

Kufuatia uamuzi huu, kamati ya Nobel nchini Norway imetambua kazi ya shirika hilo ambalo linaendesha shughuli ya kuharibu silaha za kemikali, kama sehemu ya azimio la kimataofa la kuharibu silaha za kemikali ambalo limesemekana kufanikiwa sana duniani.

Shirika hilo la kuzuia matumizi ya silaha za kemikali , pia husimamia azimio la silaha za kemikali duniani ambalo limefanikiwa kuharibu asimilia 80 ya zana za kemikali duniani.

Syria inatarajiwa kuwa nchi ya 131 kutia saini azimio hilo.

Nchi hiyo inasemekana kuwa na idadi kubwa ya silaha za kemikali duniani.

Tuzo ya leo kwa OPCW itaonekana kama hatua ya kutia moyo kwa shirika hilo kuendelea na kusaidia katika kutatua mgogoro wa kisiasa unaoendelea Syria

Waakilishi wa shirika hilo wataalikwa kupokea medali na tuzo ya dola milioni 1.2 za kimarekani wakati wa sherehe zitakazofanyika mwezi Disemba.