WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ATEMBELEA KIWANDA CHA KUUNGANISHA MATREKTA YA URSUS KILICHOPO KIBAHA. PIA ATEMBELEA ENO LA UWEKEZAJI LA KAMAL BAGAMOYO

May 23, 2017
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka benki mbalimbali nchini ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo kutoa mikopo kwa vikundi vya kilimo ili viweze kupata fedha za kununulia matrekta.

Amesema Serikali imedhamiria kuimarisha Sekta ya kilimo ili kwenda sambamba na adhma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Mei 23, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha kuunganisha Matrekta URSUS-TAMCO, Kibaha mkoani Pwani.

Amesema kiwanda hicho kinalenga kuboresha sekta ya kilimo nchini na kuongeza uzalishaji wa malighafi za viwandani kwa kuwa wakulima watakuwa na zana za kisasa.

Aidha, amevitaka vyuo vya kilimo nchini kununua matrekta hayo kwa lengo la kufundishia wanafunzi wake ili wanapohotimu wawe na uwezo wa kutumia zana hizo vizuri na kwenda kuwasaidia wakulima katika maeneo yao.

Pia Waziri Mkuu ametoa wito kwa Halmashauri nchini kuendelea kupanga matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya kilimo, uwekezaji, makazi, biashara na huduma za jamii, hivyo kuepuka migogoro ya ardhi kwa siku zijazo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Bw. Mlingi Mkucha amesema wataunganisha matrekta 2,400,  harrow 2,400 na majembe 2,400 katika mradi huo wa kiwanda cha kuunganisha matrekta URSUS-TAMCO ikiwa ni mkataba wa awali.

Amesema kiwanda hicho kina wafanyakazi 27 kwa hatua za mwanzo. Aidha, idadi hiyo itaongezeka kutokana na mahitaji ambapo baadhi ya wafanyakazi watapewa mafunzo nchini Poland na watakaporudi watakuwa wakufunzi wa watakaoajiriwa.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa kiwanda hicho kimeazima wafanyakazi wengine wakiwemo watano kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, 10 kutoka vyuo mbalimbali vya ufundi nchini, wawili kutoka CAMARTEC ambao wanashirikiana na wataalamu 10 kutoka URSUS kuunganisha matrekta.

Bw. Mkucha amesema wafanyakazi 10 kutoka Tanzania wanatarajiwa kwenda nchini Poland kufanya mafunzo mahsusi na watakaporejea watakuwa wakufunzi kwa watumishi wengine watakaoajiriwa katika kiwanda hicho.

Amesema mbali na ujenzi wa kiwanda hicho cha kuunganishia matrekta ya URSUS, mradi unahusisha uanzishwaji wa vituo vinane kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja na kuuzia matrekta, zana na vifaa vingine.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Everest Ndikilo amesema miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya viwanda mkoani humo ni pamoja na kukatika kwa umeme, hivyo ameliomba Shirika la Umeme Tanzania (TANECO) kuongeza vituo vya kupozea umeme.

Awali Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Charles Mwijage amesema kwa sasa nchini kuna viwanda vikubwa 393 kati yake 84 viko mkoani Pwani, ambapo amewaomba viongozi wa mkoa huo kutenga maeneo kwa ajili ya wanawake na vijana kuanzisha viwanda vidogo.

Mara baada ya kutembea kiwanda cha kuunganisha matrekta URSUS-TAMCO Waziri Mkuu alitembelea eneo la uwekezaji la Kamal (Kamal Indusrial Estate) lililoko katika Kata ya Kerege wilayani Bagamoyo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MEI 23,2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama moja kati ya mtrekta aina URSUS yanayounganishwa kwenye karakana ya TAMCO mjini Kibaha Mei 23, 2017.Kulia kwake ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akikagua matrekta aina ya URSUS yanayounganishwa katika karakana ya TAMCO mjini Kibaha Mei 23, 2017. Wengine pichani kutoka kulia kutoka kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NDC Mlingi Elisha Mkucha, Waziri wa Viwanda, Biahara na Uwekezaji, Charles Mwijage, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evaresti, Ndikilo na kulia kwake ni Mbunge wa Kibaha mjini Silvestry Koka.

BALOZI WA UINGEREZA NCHINI TANZANIA AMTEMBELEA RC MAKONDA.

May 23, 2017


  Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda akimkaribisha mgeni wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. Sarah Cooke,alipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar  na kufanya nae mazungumzo yenye lengo la kuongeza na kuimarisha Ushirikiano uliopo baina ya jiji la Dar es salaam na London, nchini Uingereza.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda akizungumza na mgeni wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. Sarah Cooke,alipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. SARAH COOKE, amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe PAUL MAKONDA na kufanya nae mazungumzo yenye lengo la kuongeza na kuimarisha Ushirikiano uliopo baina ya jiji la Dar es salaam na London, nchini Uingereza.

Katika mazungumzo yao, Mhe MAKONDA na Bi. COOKE wamekubaliana kuongeza kasi ya Ushirikiano baina ya majiji makubwa mawili Dar es salaam Tanzania na London nchini Uingereza, makubaliano ambayo yatasaidia kupatikana kwa vifaa vya kisasa vya kuzuia na kupambana na majanga kama vile moto na mafuriko, ambapo Mhe MAKONDA ameomba kupatiwa magari ya kisasa ya shughuli za kuzima moto na uokoaji.

Mhe MAKONDA pia ameomba kusaidiwa vifaa maalum vya UTAMBUZ*I wa mifumo ya teknolojia ya kamera za kisasa zitakazofungwa *barabarani kwa ajili ya kusaidia USALAMA wa magari, raia na mali zao mifumo ambayo inafanya kazi katika jiji la London nchini Uingereza, hatua itakayokwenda sambamba na ujengewaji UWEZO kwa maofisa wa polisi wa Mkoa wa Dar es salaam katika matumizi ya mifumo hii.

Katika kukabiliana na changamoto ya MIGOGORO ya ARDHI mkoani Dar es salaam, Mhe MAKONDA ameomba kusaidiwa kuwajengea uwezo maafisa ARDHI na Mipango miji wa Mkoa wa Dar es salaam katika matumizi ya kisasa ya upimaji na upangaji ardhi, mafunzo ambayo yatakwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kupima ardhi, jambo litakalosaidia kuondoa KERO ya upatikanaji wa HATI pamoja na vibali vya UJENZI Mkoa wa Dar es salaam.

Katika mazungumzo hayo, Mhe MAKONDA na Bi. COOKE wamejadili suala la uanzishwaji wa JIJI la FIKRA (brain storming center ) kwa ajili ya kuwakutanisha vijana wabunifu kama ilivyo kwa Tech City Uingereza.

Katika kuhitimisha mazungumzo yao, Mhe MAKONDA na Bi. COOKE kwa pamoja wamekubaliana kuzikutanisha timu za wataalamu kutoka London na Dar es salaam za kukabiliana na Majanga haraka iwezekanovyo.

Bi. COOKE, kwa upande  wake amefurahishwa na jinsi Mkuu wa Mkoa anavyopambana na vita ya dawa za kulevya ambayo imeathiri nguvu kazi kubwa sana katika jiji la Dar es salaam na kumuhakikishia kuwa Serikali ya Uingereza inaunga mkono jitihada zote zinazofanywa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam.

Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.

23/05/2017.
Kliniki ya Afya ya Akili kutolewa kupitia Hospitali zote za Rufaa nchini- Dk.Kigwangalla

Kliniki ya Afya ya Akili kutolewa kupitia Hospitali zote za Rufaa nchini- Dk.Kigwangalla

May 23, 2017
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dkt. Khamisi Kigwangalla amekutana na viongozi wa Chama Cha Walemavu wa Afya ya Akili (TUSPO), waliomtembelea Bungeni jana Mei 22.2017, Bungeni Dodoma. Viongozi hao walikaribishwa na Wabunge wawakilishi wa Watu wenye changamoto mbali mbali za ulemavu nchini, Mhe. Amina Mollel (Mb.) na Mhe. Stella Ikupa (Mb.). Katika kikao hicho Dkt. Kigwangalla ameweza kujadiliana nao mambo mbalimbali viongozi hao wa TUSPO ikiwemo uanzishwaji wa Kliniki ya Afya ya Akili kupitia Hospitali zote za Rufaa za Mkoa hapa nchini. “Nimekutana na Viongozi wa TUSPO ambao wanashughulika na masuala ya Afya ya Akili. Tulijadili mambo mengi na niliwaelezea mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwenye eneo hili, ikiwemo Uanzishwaji wa Kliniki za Afya ya Akili kwenye Hospitali zote za Rufaa za Mkoa nchini nzima. Lakini pia Uanzishwaji wa Rehabilitation Centers kwenye kila kanda na usambazaji wa Madaktari bingwa wa Afya ya Akili na wataalamu wote wanaohitajika kutoa huduma hizi kwenye Hospitali na vituo hivi” Ameeleza Dkt. Kigwangalla. Aidha, ameongeza kuwa, amewaahidi uongozi huo wa TUSPO, kuwa atafuatilia juu ya hatua ambayo mchakato wa kukamilisha muundo wa kisheria (legal framework) ulipofikia na sababu za kukwama kwake toka sheria ya afya ya akili ilipotungwa mwaka 2008. “Serikali ya awamu ya tano ni sikivu kwa wananchi wake bila kubagua. Nina aahidi kulifuatilia sualala uanzishwaji wa Baraza la Afya ya Akili, kwani tayari sheria ilishatungwa muda mrefu. Na kwamba ni kwa nini Baraza la Afya ya akili halijaanzishwa toka sheria itungwe mpaka leo na kwa nini mpaka leo hakujawa na kanuni za Afya ya akili kuelekeza juu ya mambo mbalimbali” alieleza Dkt. Kigwangalla ambapo amewaahidi kuwapa taarifa ya utekelezaji wa masuala hayo kwenye Bunge la Mwezi November 2017.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dkt. Khamisi Kigwangalla akizungumza na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Walemavu wa Afya ya Akili (TUSPO), waliomtembelea Bungeni jana Mei 22.2017, Bungeni mjini Dodoma.
Kuhusu Magonjwa ya Akili: Magonjwa ya akili ni magonjwa ambayo yanaathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, na hivyo kuwa na tabia au mwenendo uliotofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila, desturi, na nyanja nyingine za kijamii. Tabia hizo zinatokana na ugonjwa wa akili kuathiri ufanisi na shughuli za mtu husika (mgonjwa) au huathiri jamii nzima inayomzunguka endapo mgonjwa huyo hatopatiwa matibabu stahiki na kwa wakati muafaka. Kwa Tanzania imeeelezwa kuwa baadhi ya wagonjwa wengi wa akili hawafiki katika vituo vya kutolea huduma za afya na badala yake kuishia kwenye tiba za jadi au kutelekezwa na kunyanyapaliwa huku takwimu za zinaonyesha kuwa Tanzania ina idadi ya watu takriban milioni 45 na kutokana na taarifa ya afya ya akili kwa mwaka 2014/15 inaonyesha kuwa idadi ya watu 817,532 wanaugua magonjwa mbalimbali ya akili nchini, hii ni karibu asilimia 2 ya watanzania wote. Pia idadi hii ni ongezeko la wagonjwa 367,532 ukilinganisha na takwimu za mwaka 2013/14 walikuwa ni 450,000. Kati ya wagonjwa wote wa akili kwa mwaka 2014/15 wanawake ni ni 332,000 na wanaume ni 485,532. Mkoa wa Dar-Es-Salaam unaongoza kwa kuwa n awagonjwa wengi nchini ukifuatiwa na mkoa wa Dodoma na mkoa wa mwisho ni Lindi. Idadi hiyo ya wagonjwa ni wale walioweza kuhudhuria katika vituo vya kutolea huduma ya afya hapa nchini.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dkt. Khamisi Kigwangalla (mwenye koti nyeusi kulia) akifanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Chama Cha Walemavu wa Afya ya Akili (TUSPO), waliomtembelea Bungeni jana Mei 22.2017, Bungeni mjini Dodoma.

MKURUGENZI MANISPAA YA UBUNGO NDG JOHN L. KAYOMBO AFANYA KIKAO CHA MARIDHIANO NA KANISA LA KKKT KABLA YA KUVUNJWA UKUTA ULIOJENGWA KWENYE ENEO LA SHULE YA MSINGI UBUNGO PLAZA

May 23, 2017
  Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akizungumza wakati wa kikao na Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Ubungo ulioongozwa na Mchungaji kiongozi wa usharika huo, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Pwani, Kiongozi wa Kamati ya Ujenzi wa kanisa hilo na baadhi ya wazee wa kanisa. Leo tarehe 23, Mei 2017
Muonekano wa ukuta wa kanisa la KKKT Usharika wa Ubungolinalotakiwa kuvunjwa
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisikiliza kwa makini maelezo ya viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Ubungo wakati wa kikao cha pamoja cha maridhiano ya utatuzi wa mgogoro wa Eneo la ardhi. Leo tarehe 23, Mei 2017
Darasa lililokabidhiwa na Uongozi wa kanisa la kiinjili la Kilutheli Tanzania Usharika wa Ubungo kwa Uongozi wa Manispaa ya ubungo mbele ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg john Lipesi Kayombo
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akikagua majengo ambayo yamejengwa na kanisa la KKKT yakiwa yameingia katika eneo la shule ya Msingi Ubungo Plaza sambamba na viongozi wa kanisa hilo baada ya kikao cha pamoja na Uongozi wa Kanisa hilo Usharika wa Ubungo. Leo tarehe 23, Mei 2017
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisalimiana na Mchungaji kiongozi wa kanisa La Kiinjili la Kilutheli Tanzania Mchungaji Goodlisten Nkya alipozuru katika ofisi za kanisa hilo kwa ajili ya kikao na Uongozi wa  (KKKT) Usharika wa Ubungo. Leo tarehe 23, Mei 2017
Muonekano wa Majengo ya Shule ya Msingi Ubungo Plaza yatakayofanyiwa marekebisho mara baada ya ujenzi wa Madarasa nane kukamilika
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisisitiza jambo wakati wa kikao cha pamoja na Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Ubungo ulioongozwa na Mchungaji kiongozi wa usharika huo, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Pwani, Kiongozi wa Kamati ya Ujenzi wa kanisa hilo na baadhi ya wazee wa kanisa. Leo tarehe 23, Mei 2017
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akizungumza akizungumza na Afisa Mtendaji wa Kata ya Ubungo,Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa National Housing, Waalimu wa Shule ya msingi ubungo Plaza sambamba na viongozi wengine mara baada ya kikao na Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Ubungo. Leo tarehe 23, Mei 2017
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuzuru kwa katika ofisi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Ubungo leo tarehe 23, Mei 2017
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akikagua majengo ambayo yamejengwa na kanisa la KKKT yakiwa yameingia katika eneo la shule ya Msingi Ubungo Plaza sambamba na viongozi wa kanisa hilo baada ya kikao cha pamoja na Uongozi wa Kanisa hilo Usharika wa Ubungo. Leo tarehe 23, Mei 2017.

Na Mathias Canal, Dar essalaam

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo Leo tarehe 23, Mei 2017 amefanya mazungumzo na Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Ubungo ulioongozwa na Mchungaji kiongozi wa usharika huo, Katibu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Pwani, Kiongozi wa Kamati ya Ujenzi wa kanisa hilo na baadhi ya wazee wa kanisa.

Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za usharika wa KKKT Ubungo kilikuwa na Agenda ya kujadili nanma bora ya uvunjaji wa Ukuta wa eneo la kanisa hilo ambao umeingia katika eneo la Shule ya Msingi Ubungo Plaza Jambo linalopelekea Kushindwa kuanza ujenzi wa madarasa nane mapya kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo ambao kwa sasa wanasoma katika madarasa ambayo majengo yake si rafiki kwa ajili ya usomaji.

Alisisitiza kuwa ujenzi huo utakuwa maalumu kwa ajili ya kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe Kisare Makori alilolitoa Mei 19, 2017 wakati wa mkutano wake na walimu wa shule hiyo sambamba na wananchi wa Mtaa huo ukiwajumuisha Afisa mtendaji wa Kata na wajumbe wa mitaa.

WAKULIMA WA NDIMU BWEJUU, ZANZIBAR, WALILIA SOKO

May 23, 2017

Na mwandishi wetu, Zanzibar
Umoja wa Wakulima wa Ndimu wa Kikundi cha Juhudi Zetu kilichopo Bwejuu, mjini Unguja wametoa kilio chao cha kukosa soko la ndimu wanazozalisha kwa uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Wakizungumza na ugeni huo, wakulima hao wamesema kwa muda mrefu sasa wamekosa soko la uhakika la mazao yao kwa kukosa mnunuzi wa uhakika licha ya kulima kisasa na kupata mazao mengi.
Mmoja wa wakulima hao Bw. Shafi Hamadi Mussa amesema kuwa kwa muda mrefu sasa wamekosa soko la uhakika la mazao ya hali inayorudisha nyuma ari ya kuendelea kulima zao hilo.
“Tunakatishwa tamaa kwa kukosa soko la uhakika licha uwekezaji mkubwa tunaoufanya katika kulima kisasa,” Bw. Mussa alisema.
Bw. Mgana Khatibu Mgana, mkulima mwengine wa Umoja huo amesema changamoto ya ukosefu wa masoko inaweza kutatuliwa kwa kupatiwa mkopo nafuu wa kununulia mitambo ya uchakataji wa mazao ambayo itatumika kuongeza thamani kwa mazao yao.
“Tunauomba uongozi wa Benki ya Kilimo kutukopesha pesa za kununulia mitambo ya kuchakata mazao yetu ili kuepuka adha ya ukosefu wa masoko wa mazao haya,’ Bw. Mgana alisema.
Akijibu kilio cha wakulima hao, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga alisema Serikali imesikia kilio cha wakulima hao kwa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kusaidia kukabiliana na mapungufu ya wakulima nchini kote ili kuhuisha upatikanaji wa mikopo katika sekta ya kilimo na kuchagiza mapinduzi katika  kilimo nchini.
Aliongeza kuwa Benki yake imejipanga kuendeleza uongezaji wa thamani wa mazao yote ya wakulima nchini kwa kuanzia na baadhi ya mazao ili kupata picha halisi ya uhitaji wa rasilimali fedha kwa wakulima.
“Katika hatua za awali, Benki imeainisha Minyororo Kumi na Nne (14) ya Ongezeko la Thamani ya Bidhaa za Kilimo zitakayopewa kipaumbele katika kutoa mikopo ni pamoja na Kilimo cha Nafaka (Mahindi na Mchele), Kilimo cha Mazao ya Viwandani (Miwa na Korosho) na Ufugaji wa Ng’ombe (Ng’ombe wa Nyama na Maziwa),” Bw. Assenga alisema.
Aliongeza kuwa Benki inatoa mikopo kwa Kilimo cha Mbogamboga (Matunda, Mboga Mboga na Viungo), Kilimo cha Mbegu za Mafuta ya Kupikia (Alizeti na Ufuta) na kwa upande wa Kilimo cha Mazao ya Misitu ni Ufugaji wa Nyuki na mazao yake.
Mengine ni Kilimo cha Ufugaji wa Kuku (Kuku wa Kienyeji na wa Kisasa) na Kilimo cha Samaki (Ufugaji wa Samaki).
Bw. Assenga aliwaahidi wakulima hao kuwa TADB itafanyia kazi maombi yao ili kuona namna ya haraka itakayotatua changamoto zao.
Zaidi ya vipaumbele vilivyoainishwa, TADB pia imejipanga kusaidia minyororo mingine ya ongezeko la thamani ya mazao ya Kilimo kwa utaratibu  maalumu kadiri ya upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na kusimamia uendeshaji wa fedha mbalimbali zinazoelekezwa na Serikali ama wafadhili kwenye Sekta ya Kilimo.

Muchunguzi: Kuogopa kucheza Biko ni dalili ya kukaribisha umasikini

May 23, 2017
 
Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Biko, Grace Kaijage, kulia akimkabidhi nyaraka halali za Benki ya NMB zinazoonyesha kuingizwa kwa fedha za mshindi wao Sospeter Muchunguzi pichani kushoto jumla ya Sh Milioni 10 alizoshinda katika Bahati Nasibu yao ya Ijue Nguvu ya Buku, droo iliyochezeshwa Jumapili. Makabidhiano hayo yamefanyika jana jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSHINDI wa droo ya saba ya Sh Milioni 10 kutoka kwenye Bahati Nasibu ya Biko 'Ijue Nguvu ya Buku', Sospeter Muchunguzi, amekabidhiwa fedha zake huku akisema kuwa kuogopa kucheza Biko ni dalili ya kukaribisha umasikini.

Muchunguzi aliyasema hayo jana katika benki ya NMB jijini Dar es Salaam wakati anakabidhiwa fedha zake na Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Biko, Grace Kaijage.

Akizungumza kwa msisitizo mkubwa, Muchunguzi mwenye ndoto za ujasiriamali alisema kwamba watu wote waliofanikiwa katika maisha yao walithubutu katika mambo waliyokusudia kuyafanya, hivyo ni budi kila mmoja kupita njia hiyo.
Sospeter Muchunguzi katikati akisaini nyaraka za benki ya NMB kwa ajili ya fedha zake kuingizwa kwenye akaunti yake katika benki hiyo jana baada ya kuibuka kidedea katika droo ya Biko ya Sh Milioni 10. Kulia ni Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Biko Grace Kaijage na kushoto ni Afisa wa NMB.


Alisema uhakika wa kushinda ni mkubwa ikiwa mtu ameamua kweli kuingia katika sekta ya michezo ya kubahatisha, hususan mchezo wa Biko ambao hata uchezaji wake upo wazi na hakuna dalili zozote za kudanganya washindi.

“Nilipoona utaratibu wa Biko ni mzuri nikathubutu kucheza huku nikiamini kwamba endapo naweza kuibuka na ushindi naweza kusogea katika hatua moja kwenda nyingine hivyo Watanzania wenzangu hakuna haja ya kuogopa ili tusonge mbele.

“Nimefurahi kupata fedha hizi kutoka Biko maana hata uchezaji wao kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kwa kufanya miamala kwenye simu za Tigo, Vodacom na Airtel kwa kuandika kuingiza namba ya kampuni ambayo ni 505050 na kumbukumbu namba ya 2456 ni rahisi hali inayoweza kumfanya kila mtu amudu kucheza mahala popote na wakati wowote,” Alisema Muchunguzi.

Naye Grace Meneja wa Huduma kwa Wateja wa Biko, aliwataka Watanzania kila pembe za nchi kucheza kwa wingi ili wajiwekee mazingira ya kushinda zawadi za papo kwa hapo kuanzia Sh 5000, 10,000, 20,000, 50,000, 100,000, 500,000 na Sh Milioni moja zinazotoka kila wakati, huku pia donge nono la Sh Milioni 10 likitolewa katika droo ya Jumatano na Jumapili.

“Lengo letu ni kutoa zawadi nono kwa kila mshindi wetu, hivyo umnachotakiwa kufanya ni kucheza Biko kwa wingi kwa kununua tiketi kuanzia Sh 1000 na kuendelea ili mshinde, maana kucheza mara nyingi zaidi ndio njia ya kufanikisha ushindi,” Alisema Grace na kuongeza kuwa tiketi moja inatoa nafasi mbili, ikiwamo ya ushindi wa papo kwa hapo pamoja na nafasi ya kuingia kwenye droo ya kuwania Sh Milioni 10.

Kwa mujibu wa Grace, washindi wao wanaoshinda zawadi za papo kwa hapo wanatumiwa fedha zao kwa kupitia simu walizocheza na wale wa droo kubwa wakikabidhiwa katika benki ili kuleta usalama wa fedha wanazotoa kwa washindi wao.