WAZIRI JAFO AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA HOTELI ZANZIBAR

January 07, 2024

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo amesema Wananchi wa Zanzibar wanastahili kujivunia maendeleo yaliyopatikana kwa muda mfupi.


Amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hoteli ya Kiwengwa Tembo Beach iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Waziri Dkt. Jafo ameeleza kuwa uwekezaji wa miradi ikiwemo afya, elimu, miundombinu na uwanja wa ndege unaofanyika chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya Awamu ya Nane ni fursa kubwa kwa wananchi kwani inawaletea kipato pamoja na kukuza uchumi.

Amesema viongozi hao wakuu wa Serikali hizo mbili pia wameonesha dhamira ya kuifanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na mapinduzi ya viwanda ambavyo vimekuwa ni sehemu ya uwekezaji na hivyo kukuza uchumi.

Dkt. Jafo amefafanua kuwa viongozi wamefungua milango ya uwekezaji mkubwa wa ndani na nje ya nchi kwa kujenga na kuimarisha miundombinu muhimu, itakayoweza kutoa fursa za kimaendeleo kwa Wananchi.

Pamoja na hayo, Waziri Dkt. Jafo ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuzingatia uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili dunia.

Amesema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta zinazoingiza mapato hasa utalii, kwa hiyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuhifadhi mazingira zikiwemo kupanda miti.

Vilevile, Dkt. Jafo ametoa wito kwa wananchi kutunza na kusafisha fukwe zilizopo katika maeneo mbalimbali ili ziwe katika mazingira safi na ya kuvutia ikiwa ni sehemu ya kukuza uchumi wa buluu kama ambavyo unachagizwa na Serikali.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hoteli ya Kiwengwa Tembo Beach iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hoteli ya Kiwengwa Tembo Beach iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akizungumza na mwekezaji Hussein Muzamil wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hoteli ya Kiwengwa Tembo Beach iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Bw. Shariff Ali Shariff.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hoteli ya Kiwengwa Tembo Beach iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Rashid Hadid Rashid na mbele ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Bw. Shariff Ali Shariff.

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Hoteli ya Kiwengwa Tembo Beach iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR AWEKA JIWE LA MSINGI SKULI YA SEKONDARI YA KONDE- PEMBA

January 07, 2024

 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya selimu ili kuendana na fikara na falsafa za waasisi wa mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya kuwapatia elimu bure kwenye mazingira mazuri wananchi wake bila ya ubaguzi wa aina yoyote.


Hayo yamesemwa na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akiweka Jiwe la Msingi katika Ujenzi wa Skuli ya Sekondari Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema kuwa shabaha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kutatua changamoto ya nafasi katika skuli zetu za Maandalizi, Msingi na Sekondari ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia watoto kutembea masafa marefu ya kutafuta huduma ya elimu kwa kuondosha utaratibu wa wanafunzi kuingia katika mikondo miwili ya asubuhi na jioni.


Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali inaendelea kujenga na kuimarisha Vyuo vya Mafunzo ya Amali kila Wilaya ili kutoa fursa kwa vijana ambao watakosa sifa ya kuendelea na masomo waweze kujiunga katika vyuo hivyo ambapo kwa sasa serikali imo katika mchakato wa ujenzi wa vyuo vya Amali vitano (5) ambavyo vitawasaidia wananchi kuweza kujiajiri pindi watakapo maliza masomo yao.

Aidha Serikali inazidi kuwawekea mazingira bora wanafunzi wanaoendelea na masomo ya elimu ya juu kwa kuongeza bajeti kutoka shilingi za Kitanzania Bilioni 19.53 kwa mwaka 2020/2023 hadi kufikia Bilioni 29.5 kwa mwaka 2020/2024 sambamba na kuongezewa posho ya kujikimu kutoka shilingi laki moja na thelathini hadi kufikia laki moja na hamsini kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya Zanzibar na laki moja na themanini kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya Tanzania Bara ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi zaidi kujiunga na Vyuo Vikuu.

Sambamba na hayo Makamu wa pili wa Rais amewataka wananchi kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na serikali ya kuleta maendeleo, pamoja na kuwataka wanafunzi kuitumia fursa waliyonayo mashuleni kujipatia elimu pamoja na kuepuka vitendo vya viovu ikiwemo uvutaji wa bangi, wizi na ubaradhuli kwani yote hayo hayana mustakbali mwema wa maisha yao.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Ali Abdulghulam Hussein amesema Rais wa Zanzibari na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Hussen Ali Mwinyi ameboresha maslahi ya walimu kwa kuwaongezea mishahara sambamba na kuwaajiri walimu zaidi ya (2000) lengo ikiwa ni kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika katika ufundishaji na usimamizi wa wanafunzi ili kupata matokeo mazuri yatakayotoa wataalamu wazuri watakaoitumikia nchi yao na Taifa kwa Ujumla.


Ghulam amesema wananchi wanapaswa kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo ni mkombozi wa Wazanzibari wanyonge waliotawaliwa na kunyanyaswa na wakoloni waliowanyima nafasi ya kupata haki yao ya elimu

Amewataka walimu, wanafunzi na wananchi kuwakemea vikali wale wote wanaoyadharau na kuyabeza Mapinduzi na badala yake wawe mstari wa mbele katika kuelimishana juu ya umuhimu wa Mapinduzi kwa kizazi kijacho.


Akisoma Taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi wa mradi wa Skuli ya Konde Sekondari, Naibu Katibu Mkuu Mkuu Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Mwanakhamis Adam amesema kukamilika kwa ujenzi wa skuli hiyo kutatoa nafasi kwa wanafunzi kuingia skuli kwa mwongo mmoja tu wa asubuhi na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani ambapo kila darasa litachukua wastani wa wanafunzi 45 tu.


Dkt. Mwanahamis amefahamisha kuwa ujenzi huo wa Skuli ya gorofa tatu(3) utakaokidhi mahitaji yote ya kusomea na kusomeshea hadi kumalizika kwake utagharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 6.2 ambapo wanafunzi 1845 watapata nafasi ya kusoma skulini hapo.



JUMUIYA YA WAZAZI TUMIENI RASILIMALI ZILIZOPO KUJENGA NA KUENEZA MAFANIKIO YA CCM-DKT.BITEKO

January 07, 2024

 -Akabidhi Pikipiki na kofia ngumu Jumuiya ya Wazazi (CCM) Zanzibar


-Awataka kutumia pikipiki hizo kuieneza CCM

-Azuru Kaburi la Hayati Abeid Amani Karume

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameitaka
Jumuiya ya Wazazi ya CCM kutumia rasilimali walizonazo katika
kukijenga na kukieneza Chama cha Mapinduzi (CCM) katika maeneo
mbalimbali ya nchi na kuzungumza na wananchi kuhusu kazi kubwa za
maendeleo zinazofanywa chini ya Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt.Doto Biteko ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
(Kundi la Wazazi), amesema hayo wakati akizungumza na Viongozi wa
Jumuiya ya Wazazi ya CCM-Zanzibar wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dogo Mabrouk. Kikao kilifanyika katika Afisi
Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini
Magharibi.

“Kama wewe ni Mwenyekiti wa Mkoa, Katibu wa Mkoa au kiongozi yoyote
yule, kwa kutumia rasilimali ulizonazo tembelea maeneo ya mkoa wako,
Wilaya na Vijiji hata mara moja, zungumza na makundi mbalimbali
ikiwemo Wajumbe wa Kamati za utekelezaji za Jumuiya yetu na waeleze
kuhusu masuala ya kujenga na kueneza Chama. Hii inawezekana,
tujipange, tufanye ziara hata kama ni kidogo, polepole tutafanya
makubwa kadri tutakavyoendelea, tuwe mstari wa mbele kueleza mafanikio
ambayo CCM na Serikali yake wameyafanya.” Amesisitiza Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amesema kuwa, Jumuiya ya Wazazi ya CCM ni Jumuiya kubwa
ndani ya Chama hivyo inapaswa kufanya kazi za kukijenga Chama kwa
ukubwa huo kwa kuwa inabeba makundi yote ndani ya CCM na haina mipaka
au ukomo wa mtu kuwa sehemu ya Jumuiya.

“ Nikitolea mfano Jumuiya yetu ya Wanawake, inahusu Wanawake katika
Chama, Jumuiya ya Vijana umri fulani ukifika unakuwa hauna vigezo,
lakini Jumuiya hii haina mipaka hivyo inapaswa kuwa na nguvu kubwa,
tutumie ukubwa wa Jumuiya hii kuwasaidia Mwenyekiti wetu na Makamu
Mwenyekiti upande wa Zanzibar katika kujenga Chama na kuzungumza kwa
ukubwa yale yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika.” Ameeleza Dkt.
Biteko

Ameongeza kuwa, Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu
Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi wanataka
kuona viongozi wa Chama katika ngazi mbalimbali wanawasaidia kazi
ikiwemo ya kueleza mafanikio makubwa ya kimaendeleo yanayoendelea
kufanyika na kazi kubwa inayofanywa na viongozi hao katika
kuwaunganisha Watanzania, kuwa na maridhiano na kujenga uchumi wa
nchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa,
Dogo Mabrouk amemshukuru Dkt.Biteko kwa kuithamini Jumuiya hiyo na kwa
kuiwezesha kwa vitendea kazi ambavyo vitaboresha utendaji wa Jumuiya
kwenye mikoa sita ya Zanzibar na kuahidi kuwa wataendelea kumpa
ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, Dkt. Biteko alizuru katika Kaburi
la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume lililopo
Kisiwandui Zanzibar.

Aidha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ambaye ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amekabidhi PikiPiki Sita kwa ajili ya Jumuiya ya Wazazi (CCM),
Zanzibar pamoja kofia ngumu kwa ajili ya Jumuiya hiyo kwenye Mikoa
Sita ya Zanzibar.

Amesema kuwa, pikipiki hizo ni mali ya Jumuiya ya Wazazi (CCM) ambapo
ameelekeza kuwa, pikipiki hizo zikafanye kazi ya siasa kama
ilivyokusudiwa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiomba dua katika Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume lililopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Kundi la Wazazi), akizungumza na Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM-Zanzibar wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Dogo Mabrouk. Kikao kilifanyika katika Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa
Mjini Magharibi.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambayeni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (Kundi la Wazazi), akikabidhi pikipiki Sita na kofia ngumu kwa Viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM-Zanzibar. Makabidhiano yalifanyika katika Afisi Kuu ya CCM iliyopo Kisiwandui, wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

VIONGOZI WA DINI WAOMBWA KUWEKA MKAZO KATIKA KUSIMAMIA MAADILI.

January 07, 2024

 Na Mwandishi wetu


Viongozi wa dini wameombwa kuendelea kusimamia imara na kukemea matendo maovu yanayopelekea mmomonyoko wa maadili hususan kwa vijana hasa katika mazingira ya yanayoendeshwa zaidi na ulimwengu wa kidijitali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan katika Ibada Maalum ya Kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mufindi, Mkoani Iringa, tarehe 07/012024.

Waziri amehimiza malezi bora kwa watoto na ikiwezekana jamii kurejea utamaduni wa kitanzania wa mtoto kulelewa na kuonywa na jamii nzima inayomzunguka.

“Serikali inatambua kuwa Viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuwahimiza wananchi maadili mema na maisha ya uadilifu,” Alifafanua

Waziri amenukuu maandiko Matakatifu kutoka Waraka wa Mtume Paul kwa Wagalatia Sura ya 6: 1-3 yanayosihi kuonya na pale inapobainika mmoja katika jamii amekwenda kinyume kwa kutenda kosa lolote.

Amewaaomba viongozi hao kueendelea kutekeleza jukumu hilo ipasavyo ili kulilinda Taifa dhidi ya janga la mmomonyoko wa maadili.

“Tunaamini kwa kupitia Imani yetu na kukua kwa kanisa, ni kukua kwa Imani ya dini, hivyo kutachochea maadili na kusaidia kupambana na vitendo vibaya vya rushwa na kuimarisha utawala bora” Alibainisha

Aliendelea kusema kuwa, Mambo mazuri yatakayofanywa na washirika wa Dayosisi hiyo yataleta ari na chachu kwa watu wengine ambao sio wanashirika Dayosisi.

Waziri amesema kwamba licha ya Nchi ya Tanzania kutoegemea upande wowote katika masuala ya dini (Secular State) sehemu kubwa ya wananchi wanaamini katika Mungu kupitia dini na madhehebu mbalimbali.

Aidha, Alifafanua kuwa Serikali inaendelea kutambua uwepo wa dini nchini na umuhimu wake katika kulinda tunu za amani na utulivu pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Waziri ametumia nafasi hiyo kupongeza na kushukuru Kanisa la Kilutheri Tanzania hasa kwa wale waliopata Dayosisi mpya na Mhashamu Askofu Mpya, kuwana matarajio makubwa sana kwa Dayosisi hiyo Mpya.

Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Mufindi Muhasham Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula, amesema kanisa linahitaji kushirikiana na Serikali kutoa elimu ya kujitegemea ili kusaidia vijana kupata ujuzi.

Alisema, Elimu ya Ufundi ni muhimu sana kwa vijana hasa wanaomaliza elimu ya msingi bila kwenda sekondari na wanaomaliza elimu ya sekondari bila kwenda juu zaidi.

“Kanisa linajipanga kuendeleza elimu ya ufundi katika chuo chetu cha Mafinga Lutheran vocation centre ikiwezekana kuanza mchepuo ufundi kama tawi la chuo kikuu kisaidizi cha Iringa,” Alisema Baba Askofu

Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhashamu Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ameomba Viongozi wanaomsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumsaidia kwa dhati na kuepuka kuunda makundi ya kumkwamisha.

Tunamuombea Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu Hassani na tunamuunga mkono yeye pamoja na wengine wote wenye mamlaka na nafasi katika nchi yetu.

“Tunaomba kila mmoja asimame kikamilifu katika nafasi yake awatumikie watanzania wasasa na vizazi vijavyo,” alifafanua Mhashamu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akisalimiana na Askofu wa Jimbo la Mufindi Mhashamu Askofu Dkt. Anthony Kipangula mara baada ya ibada ya kuwekwa wakfu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akipokea kwa niaba zawadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhashamu Baba Askofu Dkt. Fredrick Shoo, mara baada ya ibada ya Kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mufindi.

Waumini Mbalimbali katika picha wakifuatilia ibada ya kuwekwa wakfu Askofu wa Jimbo la Mufindi Mhashamu Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula na Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi ya Mufindi, Mchungaji Kete Ulula iliyofanyika katika ushirika wa Mafinga.

DKT. BITEKO AFUNGUA JENGO LA AFISI MAMLAKA YA MAJI ZANZIBAR

January 07, 2024


Awapongeza Rais Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi kwa maono na miongozo yao

kutekeleza Miradi ya kimkakati

-Aipongeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini kupitia ZAWA kwa
kukamilisha Jengo lenye ubora na hadhi ya juu

-Ataka ZAWA kutoa huduma bora


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko,
amefungua Jengo la Afisi ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) lililoko
eneo la Madema, Zanzibar na kupongeza mafanikio na ushindi wa
kufanikisha miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar.

Dkt Biteko amesema, kuelekea Kilele cha Mapinduzi ya Zanzibar, watu
waliopewa dhamana ya kusimamia miradi hiyo ambayo Serikali imepeleka
fedha nyingi, wafanye kazi kwa uaminifu kwani watatatoa hesabu si tu
kwa waliowaweka madarakani, au Wananchi bali kwa Mwenyezi Mungu,
hivyo wafanye kazi kwa uaminifu mkubwa.

"Nitoe wito kwenu ZAWA hakikisheni mnawahudumia vema Wazanzibari, ili
waone fahari ya kuhudumiwa na ninyi, na nitoe wito kwetu Sisi tuliopo
madarakani kuhakikisha tunatoa huduma kwa weledi wa hali ya juu kwa
maslahi ya Wananchi wetu" Alisisitiza Dkt. Biteko

Aidha, alipongeza pia Wizara ya Maji kwa kuwajali wafanyakazi wake kwa
kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa wafanyakazi wake ikiwa ni
kuwajengea jengo lililoondoa changamoto ya nafasi kwa wafanyakazi
hususani kwenye jengo la awali.

Dkt Biteko amesema, ujenzi wa Jengo Hilo la ghorofa 4 lililogharimu
kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 92.18 kama mkopo toka Benki ya
Exim Kutoka India kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
unahusisha Ofisi za wafanyakazi, Maabara, Ukumbi wa Mikutano, Maegesho
na Ukumbi wa Mazoezi na kuipongeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini
kwa kujenga jengo lenye hadhi na ubora wa hali ya juu.

"Niwashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassani na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt.
Hussein Ali Mwinyi kwa maono na miongozo yao iliyopelekea kukamilika
kwa miradi mikubwa na ya kimkakati yaani wanaupiga mwingi" Alisisitiza
Dkt. Biteko.

Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri Maji,
Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Shaibu Kaduara, amesema ujenzi wa
jengo hilo ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo
Maji na tayari miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa ili kutatua
kero ya Maji visiwani Zanzibar na kuongeza kuwa wataendelea na kasi
hiyo bila kulala ili kuwaletea maendeleo wanachi wa Zanzibar.

Alimpongeza Mhe. Dkt. Biteko kwa ushirikiano ambao Zanzibar inapata
hususani kwa miradi ya Umeme hususani uimarishaji wa miundo mbinu ya
umeme, kwa kutekeleza mradi wa kuleta umeme kutoka Tanzania Bara,
kilovolt 220 kutoka Rasi Kilomoni na ule wa Pemba kwa Msongo wa
Kilovoti 132 na kuishukuru Serikali kwa Kufanikisha miradi hii.

"Zanzibar ndio nchi pekee Afrika Mashariki, na pengine Duniani kwa
kuwajali wananchi wake kwa kuwapatia Maji ambayo wanayachagia na sio
kulipia Maji" Alisisitiza Mhe. Kaduara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)
Mhandisi. Dkt. Salha Mohamed, amesema ujenzi wa jengo hilo ulianza
mwezi Machi, 2021 ikiwa ni sehemu ya uhuishaji na ustawishaji Maji
Zanzibar chini ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maji chini ya
miradi mitatu ambapo wa kwanza ni wa Mfenesini na Dole unaogharimu
Dola za Kimarekani Milioni 26,167, 200, Awamu ya pili unaogharimu
kiasi cha Dola za kimarekani Milioni 27,740,731, ambao umejenga
matanki makubwa sita, matatu chini, na matatu juu, na ya tatu ni ile
inayohusiaha Masongini, Kwarara na ZAWA kwa ujenzi wa matanki matano,
na unagharimu kiasi cha zaidi ya milioni 35.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (kulia mbele) akifunua kitambaa kuashiria ufunguzi wa Jengo la Mamlaka ya Maji Zanzibar uliofanyika wilayani Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 8 Januari 2024. Kushoto mbele ni Waziri Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Shaibu Kaduara.

KASEKENYA AWAAGIZA TANROADS KUFUNGUA MAWASILIANO YA DARAJA LA MTO RUKWA

January 07, 2024

 Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameutaka Wakala wa Barabara Nchini ( TANROADS), kuhakikisha wanafungua mawasiliano ya Barabara la kutoka Katavi kwenda Songwe kupitia Bonde la Mto Rukwa.


Kasekenya ameyasema hayo leo wakati akikagua daraja hilo ambalo limeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha na hivyo kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya mikoa hiyo.

“Niwaagize TANROADS kuhakikisha kazi inaendelea bila kusimama na mawasiliano yanarudi kama ilivyokuwa hapo awali, maana daraja hili ni muhimu kwa wananchi wa kata ya Mto wisa na kata ya Zimba,lakini pia na mkoa wa Rukwa na Songwe kwa ujumla” amesema Kasekenya.

Aidha, Kasekenya ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya barabara ili iweze kuendelea kutumika na kuacha kufanya kazi kwenye vyanzo vya maji, kwani barabara ni za wananchi wenyewe na sio za Serikali.

Katika Upande mwingine, amewataka TANROADS na Bodi ya Mfuko wa Barabara,( ROAD FUND) kuhakikisha wanazitembelea barabara mara kwa mara katika kipindi hiki cha mvua za El nino.

“ TANROADS na ROADS FUND kuna haja kubwa kupita kwenye haya maeneo ya barabara na madaraja kupata tathmini ya mahitaji na changamoto ili wanapokuja kuomba fedha za dharura waweze kupewa ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa haraka”, amesema Mhandisi Kasekenya.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Mgeni Mwanga amesema tayari timu ya wataalamu kutoka sehemu mbalimbali wameshafika na wanahakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kurudisha mawasiliano ya daraja hilo.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Bw. Nyakia Ally amesema kuwa mvua kubwa iliyonyesha imesababisha madhara kwenye mashamba, nyumba, barabara pamoja na madaraja na wanawashukuru TANROADS kwa kuweza kuanza kazi ya kurejesha daraja lililokatika.

“ Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita, kupitia Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kuweza kutujengea daraja la muda tukiwa tunasubiria kurejeshewa kwa daraja la awali ambalo mawasiliano yake yamekatika” amesema Nyakia

Kurejeshwa kwa daraja la mto Rukwa ambalo linakunganisha Mkoa wa Rukwa, Katavi na Songwe kutaimarisha uchumi, biashara na uwekezaji wa wananchi katika mikoa hiyo.




Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa  kurejesha mawasiliano ya  Daraja la kutoka Katavi kwenda Songwe kupitia Bonde la Mto Rukwa, ambalo limekatika kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani humo.