KARAFUU FURSA MPYA KWA WAKULIMA WA MIKOA YA MOROGORO NA TANGA

KARAFUU FURSA MPYA KWA WAKULIMA WA MIKOA YA MOROGORO NA TANGA

December 27, 2023










Na Mwandishi Wetu

MIKOA ya Morogoro na Tanga imepewa kipaumbele cha kulima zao la karafuu katika mpango wa pamoja wa serikali na wadau wa kilimo kutoka sekta binafasi na taasisi zisizo za kiserikali.

Ongezeko la Mkoa wa Tanga katika ulimaji wa karafuu kitaifa limetangazwa katika Mkutano wa Wadau wa Kilimo na Mazingira waliokutana jijini Dar es Salaam.

Wadau hao wamesema zao la karafuu limeonesha kustawi katika mikoa hiyo miwili, hivyo waamini ikipewa kipaumbele itaongeza uzalishaji.
- Advertisement -


“Morogoro ndiyo iliyotangulia na mwaka jana tu ilizalisha tani 2,000 sawa na nusu ya uzalishaji wa Zanzibar wa jumla ya tani 4,000, hivyo ongezeko la Tanga ni wazi Tanzania itakuwa mzalishaji mkubwa wa karafuu,” walisema wadau.

Ulimaji wa karafuu Tanzania Bara umetokana utafiti na ushauri wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), taasisi inayowashirikisha wadau katika sekta binafsi katika kulima mazao na kuendeleza minyororo ya thamani ya mazao hayo.

Akitangaza uamuzi wa kuiongeza Tanga kwenye mpango huo wa zao la karafuu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga, amewambia wajumbe wa jukwaa la Wadau wa Kilimo na Mazingira kwamba utafiti umeonyesha kuwa mkoa huo unaweza kulima kwa mafanikio zao la karafuu.

Kirenga ameeleza kuwa zao la karafuu ni zao la thamani kubwa na ni sehemu ya mazao muhimu ya viungo na pia ni muhimu katika mazao ya mboga, matunda, mizizi na maua (hortculture) ambayo yana masoko yanayaotabirika duniani.

Alisema endapo Watanzania watachangamkia fursa zilizomo katika ulimaji wa zao la karafuu, basi uchumi wa mkulima mmoja mmoja na wa Taifa utaimarika na kukifanya kilimo kiwe na tija.

“Mazao ya viungo hususani karafuu yamekuwa na soko imara na la uhakika. Sasa bei elekezi ya kilo moja ya karafuu ni kati ya shilingi 14,000 hadi 18,000. Bei hizi zinaonyesha ni jinsi gani zao hili likipewa kipaumbele litakavyokuwa na maana kwa mkulima mdogo na pia likawa ni zao letu lenye tija kubwa katika soko la kimataifa”, Kirenga alilieleza jukwaa hilo.

Aliongeza kuwa karafuu ni zao la msingi Zanzibar na wao ndiyo wazalishaji wakuu wa zao hilo, wana masoko makubwa na ya uhakika.

“Hivi karibuni Tanzania Bara imeanza kuzalisha zao hili katika baadhi ya mikoa miwili. Uzalishaji umekuwa na mwelekeo mzuri kwani mikoa hii sasa inazalisha kwa wingi zaidi karafuu ikilinganishwa na Zanzibar ambao ndio waanzilishi. Mikoa hiyo kwa sasa ni Morogoro na Tanga”, alisema Kirenga.

Sasa hivi serikali inawashirikisha wadau wengine kuinua pato la Mtanzania kufikia dola za Marekani 3,000 kabla ya mwaka 2025.

Tanzania sasa inahesabiwa kuwa nchi yenye uchumi wa kati wa chini baada ya pato la Mtanzania kuvuka dola za Marekani 1,096, kigezo kinachotumiwa na Benki ya Dunia katika kupima umaskini wa watu katika taifa lao.

Ili kulifanya zao la karafuu likubalike kwa wakulima Mkoa wa Morogoro na SAGCOT wameshirikiana serikali ya mkoa kuwapeleka Zanzibar wakulima 20 wa Morogoro kujifunza ulimaji wa zao hilo.

Tayari ulimaji wa zao hilo umeimarika katika Wilaya za Morogoro Vijijini, Kilombero; katika Halimshauri ya Wilaya ya Mlimba na sasa imeongezeka Wilaya ya Mvomero.

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli, ameeleza uingizaji wa kilimo cha karufuu katika mkakati wa kuinua pato la mkulima una maana kubwa kwa wilaya yao.

Alisema ulimaji wa zao hilo unawaletea wakulima fursa tele na kwani wadau wamejizatiti kuunga mkono ulimaji wa zao katika wilaya yao.

“Wilaya yetu imekuwa ikiathiriwa na kilimo kisichokuwa na tija. Uwepo wa mazao kama haya ya kimkakati utapelekea kuinua maisha ya mwananchi mmoja mmoja. Tumethibitishiwa kuwa ardhi yetu itasitawisha zao la karafuu kama tutazingatia maelekezo ya wataalamu,’’ alisema Nguli.

Meneja wa SAGCOT, Mkoa wa Morogoro, John Banga alieleza kuwa Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa iliyopewa kipaumbele cha kuzalisha kilimo cha mazao ya viungo, na hasa karafuu, huku akianisha sababu zake ni kwamba mkoa una hali ya hewa inayofaa na afya ya udongo ni himilivu kwa zao la karafuu.

“Ndani ya miezi miwili wakulima wamegawiwa zaidi ya miche 150,000 ili waweze kuendeleza kilimo cha karafuu. Jambo kubwa na zuri wapo wadau ambao wamekuja kuunga mkono juhudi hizi za kulima karafuu katika milima ya Morogoro. Kilimo cha karafuu kwa njia hii kitasaidia katika kutunza afya ya mazingira ya misitu. Tutajiepusha na uchomaji wa maeneo na ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa,’’ alisema Banga.

DAWA ZA KULEVYA AINA YA HEROIN NA METHAMPHETAMIN KILOGRAMU 3,182 ZAKAMATWA JIJINI DAR ES SALAAM NA IRINGA.

December 27, 2023

 Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Tanzania (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine katika operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam na Iringa kati ya tarehe 5 hadi 23 mwezi Disemba, 2023. Watu saba wamekamatwa kuhusika na dawa hizo ambapo wawili kati yao wana asili ya Asia.


Kiasi hiki cha dawa za kulevya kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya methamphetamine na kilogramu 1001.71 aina ya heroin zilizokamatwa katika wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni jijini Dar es Salaam pamoja na wilaya ya Iringa mkoani Iringa.

Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya. Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani.

Aidha, dawa hizi zilizozikamata zilikuwa zimefungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za kahawa na majani ya chai. Mbinu hii inatumika kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wake na kukwepa kubainika.

Ukiacha dawa ya heroin inayotengenezwa kwa mchanganyiko wa kemikali kutoka kwenye mimea ya afyuni (opium popy) inayolimwa katika nchi za Asia na baadhi ya kutoka Amerika, dawa aina ya methamphetamine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na cocaine.

Dawa hii huwa kwenye mfumo wa vidonge, unga au chembechembe mithili ya chumvi ang’avu yenye rangi mbalimbali ambayo huzalishwa kwenye maabara bubu kwa kuchanganya aina mbalimbali za kemikali bashirifu.

Dawa hii ni hatari kwa afya ya mtumiaji, madhara yake ni makubwa na hayatibiti kirahisi kwani mtumiaji hupata madhara ya kudumu kwenye ubongo na hivyo hupunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu, kusababisha uraibu na kuathiri mfumo mzima wa fahamu.

Kiasi cha dawa za kulevya zilizokamatwa, endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingeweza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku. Hivyo, ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa a Kulevya, inatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwani mafanikio haya yametokana na ushirikiano unaotokana na wananchi wanaotoa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na weledi na uzalendo mkubwa wa maafisa wa Mamlaka katika udhibiti wa biashara ya dawa za kulevya.

Pia, Mamlaka inatoa onyo kwa wote wanaoendelea kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha badala yake wajikite kwenye biashara nyingine halali kwani Mamlaka imejizatiti kukomesha biashara ya dawa za kulevya kwa kufanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha,Mamlaka inaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Mamlaka katika kutekeleza kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Tukishirikiana, kwa umoja wetu tutaweza kuokoa vizazi vyetu na taifa letu dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.