MPINA AMSIMAMISHA KAZI MTUMISHI ALIYESHIRIKI UTOROSHAJI WA KILO 2500 ZA SAMAKI KWENDA BURUNDI ZENYE THAMANI YA SHILINGI 20,850,000.

December 06, 2017



Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Mh.Luhaga Mpina  (mwenye miwani) akiangalia  maboksi ya samaki aina ya Migebuka yenye kilo 240 yaliyokamatwa katika kituo kikuu cha basi cha  mjini Kagera hapo jana.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Mh.Luhaga Mpina(mwenye miwani ) akitoa  tamko la kumsimamisha  kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana  Ayoub Ngoma kwa tuhuma za  kushiriki  katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/= hapo jana.


Moja ya boti inayotumika kwenye doria katika ziwa Viktoria na  Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina amemuagiza  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yohana  Budeba kumsimamisha  kazi mara moja Afisa wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana  Ayoub Ngoma kwa tuhuma za  kushiriki  katika utoroshaji wa samaki wenye kilo 2530 kwenda nchini Burundi zenye thamani ya shilingi 20,850,000/= hapo jana.
Akizungumza katika ofisi ya Kitengo hicho iliyopo mjini Kagera, Mpina  alisema  mnamo tarehe 03/12/2017 majira ya Saa 03:00  asubuhi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngara ilikamata gari lenye namba za uasajili T 614 CLQ aina ya Mitsubishi Canter likiwa limepakia samaki zenye uzito wa kilo 2,000 aina ya Sangara na kilo 530 wa aina ya Sato kwenye mpaka wa Murusagamba wilayani Ngara.
“Katika kipindi cha uongozi wangu, tayari nimesha waagiza Makatibu Wakuu waliopo katika Wizara yangu kutembea na  barua zilizozosainiwa za kusimamisha kazi watumishi wote wanaohujumu jitihada za Serikali ibaki kujaza jina tu. Kwa sasa hatuna hata nusu dakika ya uvumilivu kwa watu kama hawa, tutawaondoa mara moja.” Alisisitiza Mpina
Aidha, Waziri alisema Afisa huyo na Dereva wa gari hilo bwana Ayuob Sanga wanashikiliwa na polisi kwa hatua za kisheria kwa kuhusika na tukio hilo,  na kuongeza kwamba samaki hawa walikuwa wakitoroshwa kwenda nje ya nchi bila ya kufuata Sheria ya Uvuvi Na 22 ya 2003 na taratibu mbalimbali za usafirishaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi.
Afisa Mfawidhi wa Kanda wa Kitengo cha Doria na Udhibiti wa Uvuvi wa mpakani katika Mkoa wa Kagera bwana Gabrieli Mageni alimweleza Waziri Mpina baadhi ya taratibu zilizokiukwa kuwa ni pamoja na samaki hao kutopaswa kuvuliwa kwa kuwa  walikuwa wakubwa zaidi ya sentimeta 85 na wadogo chini ya sentimeta 50, msafirishaji kutokuwa na kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi, kutolipia ushuru na mrabaha wa Serikali, kutokuwa na cheti cha afya pamoja na leseni ya kuuza mazao ya uvuvi nje ya nchi.
Waziri Mpina  alisema samaki hao walitaifishwa na kugawanywa kwa wananchi wa Murusagamba, Kiteule cha Jeshi la Wananchi la Tanzania Murusagamba, Kituo cha Polisi Murusagamba pamoja na Shule ya Sekondari Murusagamba baada ya kupata kibali cha Mahakama.
Alisema  kazi hiyo ilifanyika chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngara. Luteni kanali,Michael Mtenjele. Aliongeza kuwa, uchunguzi wa awali ilibaini kuwa samaki hao walitokea kwenye kijiji cha Izigo wilayani Muleba.
Ametaja baadhi ya matukio yaliyotokea hivi karibuni kuwa ni pamoja na  kukamatwa kwa furu kilo 9100 zilizokuwa zinatoroshwa kwenda nchini Uganda ambapo zilitaifishwa na kuuzwa kwa amri ya mahakama na watuhumiwa wawili kufikishwa mahakamani kwa kosa hilo.
Kukamatwa  kwa uduvi kilo 5000 ambazo zililipiwa mrabaha na mtuhumiwa kulipa faini ya shilingi 100,000/=,kukamatwa  kwa mafurushi 6 ya Samaki aina ya Migebuka yenye kilo 240 katika kituo cha Basi cha Bukoba zilizokuwa zikitoka mkoani Kigoma kwenda Uganda ambapo mtuhumiwa alikimbia na samaki hao kutaifishwa.
Katika tukio jingine jumla ya kilo 100 za mabondo mabichi ya samaki yamekamatwa kwenye doria mpakani Mtukula na mtuhumiwa  amefikishwa polisi kwa hatua za kisheria.
Waziri Mpina amewaomba wavuvi kuzingatia Sheria na taratibu mbalimbali za uvuvi nchini ili sekta hiyo iwe na tija na kuchangia  katika  uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.
Wakichangia kwa nyakati tofauti watumishi wa kituo hicho waliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mpina kuangalia namna ya kuongeza nguvu kazi na vitendea kazi mbalimbali vitakavyosaidia kudhibiti uvuvi haramu.
Nahodha Mkuu wa kituo hicho, bwana Ernest Maguzu alisema kazi ya doria katika ziwa Viktoria imekuwa ngumu kutokana na  maendeleo  makubwa  ya teknolojia ya mawasiliano kwa kuwa wavuvi wamekuwa wakiwasiliana mara moja kutumia simu za mikononi pindi wanapoziona boti za doria zinaingia ziwani na kufanikiwa kukimbia.
Naye Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kitengo cha Udhibiti wa Ubora na Masoko bi, Theresia Temu aliiomba kuongeza udhibiti wa usafirishaji wa bidaa zitokanazo na mazao ya uvuvi nje ya nchi kwa kuwa hivi sasa Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi kutokana na wafanyabiashara kutorosha mazao hayo mipakani bila kulipa ushuru.
Bi Temu alisema kuwa inakadiriwa kuwa zaidi ya tani mia moja ya  mazao ya uvuvi yanatoroshwa kila mwezi katika mipaka ya nchi jirani hivyo jitihada za pamoja baina ya wadau mbalimbali zinahitajika ili kupambana na tatizo hili
“Mheshimiwa Waziri hili ni tatizo kubwa tunaomba Serikali kuliangalia kwa jicho la tatu namna nyingine tutaendelea kuibiwa” alisisitiza bi Temu
Waziri Mpina  alisema Halimashauri zote nchini zinatakiwa kushiriki kikamilifu katika kulinza raslimali za majini  na baharini kwa kuwa  licha ya  raslimali hizo kutoa mchango  mkubwa wa uchumi kwa taifa pia manufaa yake ni kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
“Nataka suala la uvuvi wa mabomu na nyavu za kukokota liwe historia katika nchi yetu. Tutaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote  atakaje tuhujumu” alisisitiza Mpina

Kamati ya UN kutetea haki za Wapalestina yazungumza na Waziri Dk. Mwakyembea

Kamati ya UN kutetea haki za Wapalestina yazungumza na Waziri Dk. Mwakyembea

December 06, 2017
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (kushoto) akizungumza na Balozi wa Senegal katika Umoja wa Mataifa (UN) na mjumbe wa Kamati ya UN kutetea haki za msingi za Wapalestina, Mr. Fode Seck (kulia) pamoja na Wajumbe wa Kamati maalum ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyoundwa kutetea haki za msingi za raia wa Wapalestina ilipomtembelea ofisini kwake. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akikabidhiwa kitabu cha picha na historia ya mgogoro wa Wapalestina na Waisraeli alipotembelewa na Wajumbe wa Kamati maalum ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyoundwa kutetea haki za msingi za raia wa Wapalestina. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati) akisalimiana na Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa (UN) na mjumbe wa Kamati ya UN kutetea haki za msingi za Wapalestina, Dk. Riyad Mansour (wa pili kulia) pamoja na Wajumbe wa Kamati maalum ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyoundwa kutetea haki za msingi za raia wa Wapalestina ilipomtembelea ofisini kwake. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe katika mazungumzo na Balozi wa Senegal katika Umoja wa Mataifa (UN) na mjumbe wa Kamati ya UN kutetea haki za msingi za Wapalestina, Mr. Fode Seck (kulia) pamoja na Wajumbe wa Kamati maalum ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyoundwa kutetea haki za msingi za raia wa Wapalestina ilipomtembelea ofisini kwake. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akipitia kitabu cha picha na historia ya mgogoro wa Wapalestina na Waisraeli walipo mtembelea mara baada ya kukabidhiwa. 
Wanafunzi wa chuo wakiwa kwenye mdahalo na Wajumbe wa Kamati maalum ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyoundwa kutetea haki za msingi za raia wa Wapalestina ilipomtembelea ofisini kwake.[/caption] KAMATI maalum ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyoundwa kutetea haki za msingi za raia wa Wapalestina imekutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kwa mazungumzo maalum walipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Akizungumza na Waziri Dk. Mwakyembe, Balozi wa Senegal katika Umoja wa Mataifa (UN) na mjumbe wa Kamati ya UN kutetea haki za msingi za Wapalestina, Mr. Fode Seck alisema michezo inaumuhimu mkubwa kwa jamii kwani ni kiungo kinachotumika kujenga mshikamano na kudumisha amani kwa mataifa mbalimbali na jamii kwa ujumla. Aliwahimiza wanahabari nchini kuendelea kuandika habari za Palestina kiusahihi ili kuielimisha jamii juu ya suala hilo na pia kupaza sauti na hatimaye suluhu kupatikana eneo hilo, aliwataka vijana kupenda kusoma historia za maeneo anuai ikiwemo mvutano kati ya Palestina na Israeli kwa ajili ya kujijengea uelewa wa mambo duniani. Kwa upande wake Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa (UN) na mjumbe wa Kamati ya UN kutetea haki za msingi za Wapalestina, Dk. Riyad Mansour akizungumza na waziri alitoa ombi la mechi ya kirafiki kimataifa kati ya Tanzania na Palestina kudumisha zaidi uhusiano uliopo pande mbili. Kamati hiyo ilipata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu katika mdahalo, asasi za kiraia na Jukwaa la Wahariri. Hata hivyo baada ya ziara hiyo na kumtembelea Waziri Dk. Mwakyembe kamati hiyo ilihudhuria maadhimisho ya Siku ya kutetea haki za watu wa Parestina yalioandaliwa na ubalozi wa Parestina nchini Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC).

SAVE THE CHILDREN,RAFIKI SDO WAFANYA MKUTANO WA 'KLABU ZA TUSEME' SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI SHINYANGA

December 06, 2017
Shirika la Kimataifa la Save the Children kwa kushirikiana na shirika la Rafiki SDO la mjini Shinyanga wamefanya mkutano wa ‘Klabu za Tuseme’ kutoka shule 8 za msingi na sekondari katika manispaa ya Shinyanga na halmashauri ya Shinyanga (Vijijini) kwa ajili ya kufanya tathmini juu ya klabu hizo katika kupiga vita ukatili dhidi ya watoto.
Ubalozi wa Norway waipatia UN Tanzania dola milioni 5.1 ili kufanikisha UNDAP II

Ubalozi wa Norway waipatia UN Tanzania dola milioni 5.1 ili kufanikisha UNDAP II

December 06, 2017
Ubalozi wa Norway nchini umeipatia msaada wa dola bilioni 5.1 Umoja wa Mataifa Tanzania ili kusaidia kufanikisha Mpango wa Misaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDAP II). Makubaliano hayo yamesainiwa na Balozi wa Norway nchini, Hanne-Marrie Kaarstad na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez katika ofisi za ubalozi wa Norway uliopo jijini Dar es Salaam. Akizungumza kwenye hafla hiyo, Balozi Kaarstad alisema msaada huo ni mwendelezo wa misaada ambayo inatolewa na Norway ili kufanikisha mpango wa UNDAP II ambapo kwasasa imefika dola milioni 10.5 na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali na UN katika mpango huo.
Balozi wa Norway nchini, Hanne-Marrie Kaarstad akizungumza kuhusu msaada ambao wameutoa kwa Umoja wa Mataifa Tanzania. (Picha zote na Rabi Hume)
"Lengo la msaada huu ni kuwasaidia wakimbizi waliopo Kigoma na kwa wananchi wa Kigoma kwa ujumla, makubaliano mapya tuliyosaini leo yanalenga maeneo yaliyokusudia. Kusaidia kilimo ili kuwezesha kuwepo chakula cha kutosha kwa ajili ya wakimbizi na wananchi wanaozunguka hayo maeneo ya kambi, "Sehemu nyingine ambayo msaaada huu unalenga, ni kusaidia ni kumaliza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto. Matumaini yetu msaada huu utafungua milango kwa washirika wengine wa maendeleo kuchangia ili kufanikisha mapango huu," alisema Naye Rodriguez aliushukuru Ubalozi wa Norway kwa msaada waliowapatia na kwa serikali ya Tanzania kwa ushirikiano ambao inautoa kwa Umoja wa Mataifa ili kufanikisha mpango huo.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez akizungumza kuhusu msaada ambao wameupokea kutoka Ubalozi wa Norway.
Rodgriguez alisema msaada huo utatumika kama ulivyopangwa kwa wakimbizi na wananchi waliopo mkoa wa Kigoma kwa kuhakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha kwa wakimbizi wote wanaokadiriwa kufikia 340,000, lakini pia kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia kwa watu wote. "Kwa miongo mingi, Norway imeendelea kuwa mshirika wa kuaminika kwa Tanzania na Umoja wa mataifa. Kwa kuweka mkazo katika mahitaji ya wanawake na watoto walio hatarini, rasilimali hizi zitatoa mchango muhimu katika kukidhi mahitaji ya wenye uhitaji mkubwa kama ilivyoelezwa katika Malengo ya Dunia." alisema Rodriguez.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Alvaro Rodriguez na Balozi wa Norway nchini, Hanne-Marrie Kaarstad wakisaini makubaliano ambayo yatawezesha Norway kuongeza dola milioni 5.1 katika makubaliano ya Mpango wa Misaada wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDAP II).

MHANDISI KAMWELWE ATEMBELEA MRADI WA UPANUZI WA MFUMO WA UZALISHAJI NA UGAWAJI MAJI CHALINZE UNAOTEKELEZWA NA SERIKALI KUPITIA DAWASA

December 06, 2017

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

WAZIRI WA Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isaack Kamwelwe ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi Mradi wa maji awamu ya tatu ya upanuzi wa chanzo na mtandao wa maji wa Chalinze mkoani Pwani leo Desemba 6, 2017.

Mradi huo unaotekelezwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka, (DAWASA), upanuzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa matenki na ulazaji wa mabomba, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji pamoja na ujenzi wa Ofisi mpya za Mradi.
“Mradi huu unahusisha  upanuzi wa mtambo wa kusafishia maji wa Chalinze ambao chanzo chake ni Mto Wami na lengo ni kuongeza uzalishaji kufikia mita za ujazo Elfu Tisa (9000) kwa saa kutoka mita za ujazo Mia Tano (500) kwa saa.” Amefafanua Mhandisi Kamwelwe.
Akifafanua zaidi Mhandisi Kamwelwe amesema, Mradi pia unahusisha ujenzi wa Matrenki 19, ulazaji wa mabomba ya ukubwa tofauti wenye urefu wa kilomita 1,022, ujenzi wa vizimba vya kuchotea maji 351 katika  vijiji na vitongoji vya Halmashauri za Chalinze na Bagamoyo Mkoani Pwani.
“Mradi huu ni Mkubwa na unahusisha pia baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga na Morogoro katika wilaya za Handeni na Ngerengere.” Ameongeza Waziri huyo.
Aidha Mheshimiwa Waziri, alisema Wananchi wa maeneo yatakayofaidika na Mradi huo ambao ni Mkubwa ni pamoja na wakazi wa Manga hadi Tengwe katika Mkoa wa Tanga, mji na vitongoji vya Chalinze, na baadhio ya maeneo ya Bagamoyo na Kibaha Mkoani Pwani, wakazi wa maeneo ya Kizuka A na B, Tukamisasa, Lulenge, Visakazi hadi Bwawani  pamoja na Sangasanga A na B Mkoani Morogoro.
Maeneo mengine yatakayojengwa matenki ni pamoja na Pera, Pingo, Bwilingu, Msoga, Diozile, Lugoba, Mindutulieni, Saleni, Mazizi, Msata, Kihangaiko, Kilemera, Hondogo, Miono North 3, Kimange, Rupungwi na Manga.
Kati ya matenki hayo 19 mojawapo ni tenki kuu la Mazizi lenye uwezo wa kuhifadhi lita Milioni 2, kukamilika kwa ujenzi wa tenki hiulo kutafanya kuwa tenki kubwa zaidi kuliko yote Mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kmwelwe, Mradi utrakapokamilika utagharimu dola za KImarekani Milioni 41.36 ambazo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim yta nchini humo. Hata hivyo Waziri ameonyesha kukerwa kwake na kusuasua kwa mkandarasi kumalizia kazi hiyo kwa muda uliopangwa na kwamba kama asingefuata ushauri wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Wataalamu wa Wizara yake, basi leo Desemba 6, 2017 ilikuwa siku ya kuvunja mkataba wa Mkandarasi huyo. "Hata hivyo Mkandarasi baada ya kuahidi kukamilisha mradi Februari 8, 2017, tumeona tumuache hadi muda huo, lakini akishindwa hatuna njia nyingine ni kuvunja mkataba na kutafuta Mkandarasi mwingine." Alionya Waziri Kamwele wakati akizungumza na waandishi wa Habari kwenye chanzo cha maji Mto Wami.
Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amemshukuru Waziri Kamwele na Serikali ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kwa nia yake ya dhati ya kuwaondolea kero ya maji wakazi wa Chalinze, na kwamba ana imani kubwa ya kukamilika kwa mradi huo baada ya kuulalamikia kwa muda mrefu bungeni kuwa umechelewa sana. "Mheshimiwa Waziri napenda nikushukuru sana na hasa Mheshimiwa Rais wetu Mpendwa Dkt. John Magufuli, kwa kazi nzuri ambayo Serikali inafanya katika kutatua kero za wananchi na hasa wapiga kura wa jimbo la Chalinze." Alisema Mhe. Kikwete.

 Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isaack Kamwelwe, (wane kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe.Majid Mwanga, Watatu kulia, Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete, (watatu kushoto),Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwang'ingo, (wapili kulia), Mkandarasi wa Mradi wa uboreshaji miundombinu ya maji kutoka kampuni ya WAPCOS Limited ya India, Mhandisi  P.G. Rajani na maafisa wengine, wamiwa mbele ya tenki la kusafishia maji linalojengwa chini ya mradi huo unaoendeshwa na Sewrikali kupitia DAWASA, kwenye chanzo cha Maji Mto Wami, Mkoa wa Pwani, Desemba 6, 2017


 Mhe. Mhandisi Kamwelwe, akizungumza jambo na Mhe. Ridhiwani Kikwete, walipotembelea chanzo cha Maji Mto Wami.
 Mbunge wa Bagamoyo, Mhandisi, Dkt.Shukuru Kawambwa, akimsikiliza Mhe. Waziri Kamwelwe, wakati wa ziara ya Waziri wilayani Bagamoyo kukagua ujenzi wa tenki la kuhifadhia Maji, Desemba 6, 2017. Tenkji hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 6.
 Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwang'ingo, akitumia mchoro kuelezea maendeleo ya mradi wa ujenzi wa tenki la Maji Bagamoyo Mkoani Pwani, Desemba 6, 2017
 Mhe.Waziri Kamwelwe, akisalimiana na mmoja wa mafundi wanaojenga tenki la kuhifadhia maji Bagamoyo.

 Mkandarasi wa Mradi wa uboreshaji miundombinu ya maji kutoka kampuni ya WAPCOS Limited ya India, Mhandisi  P.G. Rajani, akitumia mchoro kumueleza Waziri Kamwelwe, (wapili kuhsoto) na Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mwang'ingo, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi huo

 Taswira ya ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lita milioni 6, Bagamoyo Mkoani Pwani kama inavyoonekana Desemba 6, 2017

 Mhbe., Kamwelwe, (kulia), Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe.Majid Mwanga, (wapiili kulia) na Wakandarasi kutoka kampuni ya India ya WAPCOS.