WAZIRI MKUU AFANYA ZIARA OFISI ZA RUWASA

January 08, 2024

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kufika katika ofisi za wakala wa Maji na usafi Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Lindi (LUWASA) kufuatilia mapungufu yaliyopo ikiwemo kutotumika kwa gari la uchimbaji visima lililotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu Juni, 2023 ili kuwezesha uchimbaji wa visima vya maji.
 
“Hii wizara ina Waziri makini sana, mnafanya vitu kwa ufichouficho, sasa Waziri aje hapa, mnamuona anavyohangaika Waziri wenu, vitu vidogo vidogo hivi mpaka waziri aje na ninyi mpo, kwanini mpo hapa,” Waziri Mkuu alisisitiza na kuongeza kuwa anahitaji taarifa ya kwa nini mashine hiyo tangu imefika haijachimba kisima hata kimoja.
 
Ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Januari 8, 2024, baada ya kufanya ziara katika ofisi za RUWASA zilizopo Manispaa ya Lindi na kushuhudia mtambo wa kuchimba visima ukiwa umeegeshwa na hakuna kisima kilichochimbwa tangu ulipotolewa mwaka jana huku katika mikoa mingine iliyopewa mtambo kama huo visima vinachimbwa kama ilivyokusudiwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alihoji sababu ya kutotumika kwa pikipiki zilizonunuliwa na RUWASA Mkoa wa Lindi tangu mwaka 2021 kwa ajili ya kuzigawa kwa jumuiya za watumia maji kwa madai kuwa bado hazijapata usajili. “Huu ni uzembe haiwezekani fedha za wananchi zinapotea nyie mpo tu. Hizi pikipiki zimeanza kuharibika.”
 
Akizungumzia kuhusu pikipiki hizo Afisa Manunuzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (RUWASA) Bw. Kenedy Mbagwa alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia suala la vibali vya kutumia pikipiki hizo kutoka makao Makuu ya RUWASA bila ya mafanikio, ambapo Waziri Mkuu baada ya kupata maelezo hayo amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Lindi afuatilie suala hilo.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua pikipiki zilizotelekezwa kwenye stoo ya Wakala wa Maji na usafi na Mazingira Vijijini, (RUWASA) Mkoa wa Lindi, alipofanya ziara katika ofisi za Mamlaka hiyo zilizopo Manispaa ya Lindi Januari 8, 2024. Pikipiki hizo zilinunuliwa mwaka 2021 kwa ajili ya kuzigawa kwa Jumuiya za Watumiaji maji Mkoa wa Lindi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua moja ya mtambo uliotolewa na Serikali kwa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini, (RUWASA) kwa ajili ya kuchimba visima Mkoani humo, alipofanya ziara katika ofisi za Mamlaka hiyo Januari 8, 2024. Tangu kupokelewa kwa mitambo hiyo mwezi wa sita mwaka jana mitambo hiyo haijafanya kazi iliyotarajiwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

KAMATI YA BUNGE YAIPA KONGOLE WIZARA YA ARDHI UBORESHAJI MFUMO

January 08, 2024

 Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA


Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanya Kazi kubwa na nzuri ya Maboresho ya Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha.

Akizungumza mara baada ya hitimisho la wasilisho la kazi ya uboreshaji mfumo huo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Timotheo Mzava ameipongeza Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa na nzuri na kueleza kuwa kazi hiyo inakwenda kuacha alama kwa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha uongozi kwa kuiacha sekta ya ardhi katika mifumo bora.

" Nichukue fursa hii kumpongeza Mhe Rais kwa kazi hii nzuri, kama kamati wameridhishwa na kazi na hongereni sana na mfumo huu uende ukawe bora na kutoa huduma kwa watanzania" alisema Mhe Mzava.

Baadhi ya wabunge wamesema mfumo huo siyo tu utarahisisha na kuharakisha huduma za sekta ya ardhi bali utajibu maswali mengi yakiwemo ya kijamii.

"Niipongeze wizara ya ardhi kwa kufanyia kazi mfumo utakaojibu maswali mengi ya kijamii na ningetamani mfumo huu ungejibu maswali na changamoto za kiuchumi" alisema Mhe. Lucy Mayenga mbunge wa viti Maalum.

Mbunge Makete mkoani Njombe Festo Sanga aliipongeza Wizara kwa kuboresha mfumo na kueleza kuwa uboreshaji huo umechelewa ingawa uko katika hatua nzuri. Hata hivyo, mbunge huyo wa Makete alitaka kufahamu utayari wa wizara ya Ardhi katika kutumia mfumo hususan kwenye eneo la usalama wa mifumo.

Aidha, Mbunge wa jimbo la Tabora Mjini Emanuel Adamson mbali na kuipongeza wizara kwa kuboresha mfumo alitaka kufahamu uimara wa utekelezaji mfumo huo kwa kuwa kumekuwa na mifumo mingi lakini wakati wa utekekezaji kumekuwa na changamoto ikiwemo kuekezwa mtandao uko chini.

Mfumo huo unganishi wa usimamizi wa sekta ya ardhi unatarajiwa kuanza katika mikoa mitano ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Tanga na utarahisisha na kuharakisha upatikanaji huduma za sekta ya ardhi kwa kuwa wananchi watakuwa wakipata huduma kwa njia ya mtandao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava akizungumza wakati Kamati yake ilipotembelea kazi ya Uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha tarehe 8 Januari 2023.

Mbunge wa Viti Maalum CCM Lucy Mayenge akichangia hoja wakati Kamati ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii ilipotembelea na kupata taarifa ya kazi ya Uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha tarehe 8 Januari 2023.

Mbunge Festo Sanga akichangia hoja wakati Kamati ya Bunge Ardhi Maliasili na Utalii ilipotembelea kazi na kupata taarifa ya Uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi inayofanywa na timu ya wataalamu mkoani Arusha tarehe 8 Januari 2023.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ilipokwenda jijini Arusha kukagua kazi ya Uboreshaji Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi tarehe 8 Januari 2024.

Baadhi ya wataalamu wanaofanya kazi ya kufanya Maboresho Mfumo Unganishi wa Usimamizi wa Sekta ya Ardhi. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)


SPIKA DKT. TULIA AKUTANA NA BISHOP MUYOMBA

January 08, 2024


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa United Methodist Church Bishop Dkt. Mande Muyomba katika ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam leo tarehe 8 Januari, 2024.

.MWAMKO NI MKUBWA MAHUDHURIO KIDATO CHA KWANZA NA DARASA LA KWANZA MKOANI PWANI-RC KUNENGE

January 08, 2024
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

HALI ya mahudhurio kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza mkoani Pwani ni nzuri na inaridhisha ikiwa ni siku ya kwanza Januari 8 mwaka huu wakiripoti mashuleni.
Mkuu wa mkoa wa Pwani,Abubakar Kunenge ameridhishwa na mapokezi ya wanafunzi hao katika baadhi ya shule za sekondari na msingi halmashauri ya Mji wa Kibaha, mkoani hapo.

Akikagua hali ya mahudhurio kwenye shule ya sekondari ya wavulana ya Kibaha, shule ya sekondari Tumbi pamoja na shule ya msingi Amani iliyopo Miembesaba ,Kunenge alitoa maelekezo ya Serikali, kwamba mwanafunzi yeyote asisumbuliwe kuripoti kwasababu ya kukosa vifaa ama sare za shule.

Aidha aliwaasa watoto wa kike wasome na wapewe kipaombele.

Akiwa shule ya sekondari Kibaha, alieleza ni shule kimbilio la wazazi kwani wengi wanatamani watoto wao wasome katika shule hiyo.

" Na hii ni kutokana na ufaulu mzuri na mazingira bora ya kielimu yaliyopo ,Shule hii imetoa viongozi wakubwa akiwemo Rais mstaafu awamu ya nne dkt.Jakaya Kikwete "
Aliwataka wanafunzi wawe na nidhamu na maadili mema ,nawaasa fanyeni vizuri,someni ili kuwezesha kuja kujiajiri ama kuajiliriwa kwa manufaa yenu ya baadae.

Nae Mwalimu mkuu sekondari ya Tumbi, Fidelis Haule alieleza mwamko ni mkubwa, wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotakiwa kuripoti ni 279 ambapo hadi sasa wameripoti 241 .

Hata hivyo akielezea ufaulu ,anasema umeongezeka shuleni humo kutoka asilimia 50 hadi kufikia asilimia 80.

Alisema ,wanataka iwe shule ya mfano hivyo wamejiwekea kuwa na daraja la kwanza,A za kutosha.

Akielezea changamoto aliomba kuongezwa viti na madarasa mawili ili kukidhi mahitaji.

Akijibu baadhi ya changamoto ikiwemo upungufu wa walimu ,kuongezwa madaraja walimu Ofisa elimu mkoa wa Pwani, Sara Mlaki alieleza , Serikali inaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali ikiwemo kupandisha madaraja walimu .

Mlaki alisema Serikali inatarajia kutangaza ajira kwa watumishi 23,000 nchini ambapo kati ya watumishi hao ni sanjali na walimu .

Kwa upande wake, mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha, Mshamu Munde alieleza, darasa moja limeshaongezwa na kuhusu kuongeza viti,baada ya wiki mbili vitapelekwa.

Mwanafunzi wa shule ya sekondari ya sekondari Kibaha, Moses Damas Canisio alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujenga mazingira bora ya elimu ,kuongeza madarasa ,kuboresha miundombinu ,kuondoa ada na ujenzi wa mabweni na maabara .










ONGEZEKO LA IDADI YA MABWENI LAONGEZA UDAHILI WA WANAFUNZI WA KIKE YAKOBI

January 08, 2024


Na Jacquiline Mrisho - Maelezo

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya Yakobi iliyopo katika Kijiji cha Limage, Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe, Editor John amesema kuwa kutokana na Serikali kupeleka fedha kwa ajili ya kuongeza mabweni, udahili wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 105 hadi 433.

Ameyazungumza hayo hivi karibuni wakati akihojiwa na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari (Maelezo) ambapo amesema kuwa, jumla ya shilingi milioni 543 zilipelekwa na Serikali kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu ya elimu kwa ajili ya kidato cha tano na sita ambapo fedha hizo zimeweza kujenga mabweni matatu ya watoto wa kike, madarasa matano pamoja na matundu 14 ya vyoo.

“Tulifanikiwa kutekeleza ujenzi wa mabweni matatu ambayo yamekamilika na wanafunzi wanaishi, madarasa matatu, ofisi moja, matundu 16 badala ya 14 pamoja na samani za ndani ya mabweni ambapo ilitakiwa kununua vitanda vya deka 120 lakini kupitia matumizi mazuri ya fedha hizo, vilinunuliwa vitanda vya deka 180 na badala ya kununua viti 200 na meza 200, imewezekana kununua viti 380 na meza 380, alisema bi. Editor.

Bi. Editor ameongeza kuwa, mnamo mwezi Agosti, 2023 Serikali ilileta tena jumla ya shilingi milioni 130 kwa ajili ya ujenzi wa bweni lingine la wasichana ambalo linakaribia kukamilika. Aidha, ameishukuru Serikali kwa ujio wa fedha hizo kwani sio mara ya kwanza kuwakumbuka, hata kipindi cha kwanza cha kuanzisha kidato cha tano na cha sita, ilipeleka jumla ya shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni ambalo kwa kiasi kikubwa limewasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora na wote kufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu.

Kwa upande wake mwanafunzi, Amokile Sanga amesema kuwa, mabweni hayo yamekuwa msaada mkubwa kwani wanalala vizuri bila kubanana na ni mabweni bora kwa kuwa yamejengwa kisasa, ameeleza kuwa taaluma bora huwa inaendana na miundombinu bora hivyo kuongezeka kwa mabweni hayo kumewasaidia kuwa na taaluma bora.

"Uwepo wa mabweni haya umesaidia watoto wa kike kuwa na mazingira bora ya kupata elimu kwani wasichana wengi wanaosoma shule za kutwa hukutana na vikwazo vingi njiani ambavyo hukatisha ndoto zao za kupata elimu," alisema Amokile.

Naye mwanafunzi Nancy Abraham amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani pamoja na ujenzi wa mabweni uliosababisha udahili wa wanafunzi kuongezeka, bado alitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa matano yanayoendana na wingi wa wanafunzi hao.

Akizungumza kwa ujumla, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Njombe, Mwalimu Prochesius Mguli amesema kuwa Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu ambapo kwa mwaka 2022/23, Halmashauri ya Mji Njombe ilitekeleza baadhi ya miradi ikiwemo ujenzi wa nyumba za Walimu (2 in 1) katika Shule ya Sekondari Lunyanywi ambapo zililetwa jumla ya shilingi milioni 100 na tayari ujenzi wake umeshakamilika, pia kupitia mradi wa SEQUIP, Serikali imeleta shilingi milioni 583.1 ambayo imetumika kujenga shule ambayo itaanza rasmi mwaka 2024.