TANZANIA NA UJERUMANI ZAKUBALIANA KUENDELEZA TAFITI ZA MASALIA YA MIJUSI KATIKA ENEO LA TENDAGURU MKOANI LINDI

March 12, 2018
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudence S. Milanzi (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin Ujerumani (Berlin Museum of Natural History), Prof. Johannes Vogel kuhusu masalia ya mjusi wa Tanzania yaliyofadhiwa katika makumbusho hiyo.

.....................................................

Ujerumani na Tanzania zimekubaliana kuendeleza tafiti za masalia ya mijusi katika eneo la Tendaguru mkoani Lindi.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi kutembelea Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin (Berlin Museum of Natural History) nchini Ujerumani yanapohifadhiwa pia masalia ya mijusi waliopatikana eneo la Mlima Tendaguru mkoani Lindi.

Maj. Gen. Milanzi aliongoza msafara wa Tanzania ulioshiriki maonesho ya Kimataifa ya utalii ya ITB Berlin 2018 yaliyohitimishwa jana nchini Ujerumani. Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 7 mwezi huu yalihusisha taasisi 5 za Serikali na Makampuni binafsi 60 kutoka Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho hiyo, Prof. Johannes Vogel alimueleza Maj. Gen. Milanzi kuwa shughuli kubwa inayofanywa na makumbusho hiyo ni utafiti kwa ajili ya maendeleo ya sayansi, elimu na ufahamu wa mambo mbalimbali kuhusu Dunia, viumbe pamoja na mazingira ili maarifa na ufahamu huo usaidie binadamu kutawala maisha yake na mazingira yanayomzunguka.

Akizungumzia fursa zilizopo za kushirikiana kutafiti maeneo yalikopatikana masalia ya mijusi hao na viumbe wengine Prof. Johannes alisema, Makumbusho yake ipo tayari kushirikiana na Wanasayansi wa Tanzania ili kujenga uwezo wa kufanya utafiti na kupata matokeo yatakayochangia katika hazina ya maarifa na sayansi ya viumbe na mazingira.

“Ili kuwa na utafiti endelevu, ni vema kwa nchi ikawekeza kwa wataalamu wake ili kuendeleza utafiti na maendeleo ya sayansi.  Hivyo tupo tayari kushirikiana ili kujenga uwezo kwa wasomi wa Tanzania kuweza hatimaye kufanya utafiti na kuleta maendeleo kwa nchi yao” alisema.

Akizungumzia kuhusu masalia ya mijusi waliopatikana Tendaguru na ambayo yanahifadhiwa katika makumbusho hiyo, alisema badala ya kuwarudisha nchini Tanzania, ni vema wakachukuliwa kuwa elimu, utafiti na maendeleo ya sayansi yanayopatikana kutokana na kuwafanyia utafiti ni kwa maendeleo na ustawi wa dunia nzima.

“Ichukuliwe kuwa huu ni urithi wa dunia nzima na hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa urithi huu hauachi ukapotea.  Hivyo, ni vema tukaimarisha utafiti katika eneo walikopatikana ili kupata masalia mengi zaidi na kuitangaza Tanzania katika Nyanja za utafiti.

“Makumbusho yangu ipo tayari kufanya ziara ya kuimarisha mazungumzo na mamlaka za Tanzania mapema iwezekanavyo ili utafiti katika eneo la Tendaguru uendelee kwa manufaa ya Tanzania na Dunia nzima”. alisema Prof. Johannes. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Milanzi aliahidi kuwapa ushirikiano ili kuwezesha tafiti hizo kufanyika kwa ajili ya ustawi wa sayansi na uchumi wa nchi zote mbili.  Alimkaribisha Prof. Johannes na timu yake kuja Tanzania mapema iwezekanavyo ili kujadili na kukamilisha makubaliano ya kuendeleza tafiti hizo.

Awali, Maj. Gen. Milanzi alipata fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdalla Possi. Miongoni mwa mambo waliyozungumza ni pamoja na masalia hayo ya mjusi wa Tanzania anayehifadhiwa katika moja ya makumbusho nchini humo.

Balozi Possi alisema kuwa kwa maoni yake haoni kuwa wazo la kuhamisha masalia hayo kurudishwa Tanzania kuwa litakuwa na tija kwa maendeleo ya utalii na utafiti wa sayansi kwa nchi yetu. 

Alitoa baadhi ya sababu kuwa sio kweli kuwa masalia hayo ndiyo kivutio kikubwa pekee kinachofanya wanasayansi na watalii wengi kutembelea makumbusho hiyo na hivyo kuipa mapato makumbusho hiyo. 

“Makumbusho inapata ruzuku kutoka serikalini na kiingilio ni sehemu ndogo sana ya mapato ya makumbusho hiyo.  Fedha nyingi za kufanyia shughuli za Makumbusho ya Berlin zinatokana na fedha zinazolipwa kwa ajili ya kufanya utafiti na si viingilio katika makumbusho” alisema Dk. Possi.

Alisema makumbusho hiyo ina mikusanyo mingi ya viumbe mbalimbali zaidi ya milioni 30 ikiwemo ya mijusi kutoka nchi nyingine duniani.  Mkusanyiko huo kwa pamoja unatoa mvuto kwa watafiti na watalii kutembelea na kufanya shughuli zao chini ya makumbusho hiyo. 

Dk. Possi alisema kuendelea kuwepo masalia hayo katika makumbusho hiyo kuna manufaa zaidi ya kuitangaza Tanzania kiutalii na utafiti wa kisayansi kuliko masalia hayo yatakapoondolewa katika makumbusho hiyo na kurejeshwa nchini Tanzania. 

Alisema kuwepo masalia hayo katika makumbusho hiyo ni kama Balozi wa utalii na utafiti wa kisayansi anayeitangaza Tanzania sehemu mbalimbali duniani. 

Akizungumzia mchakato unaoendelea hivi sasa hapa nchini wa kuandaa Utambulisho mpya wa Tanzania (National Branding), Balozi Possi alishauri kuwa ni vema mabadiliko yatakayopelekea kuondokana na utambulisho unaotumika hivi sasa ukaangaliwa kwa umakini kwa kuwa kuna hatari ya kupoteza msisitizo uliopo katika vivutio maarufu vya utalii nchini na kutoa fursa kwa washindani kutangaza utalii wao kupitia vivutio hivyo.

Alisema endapo hakuna athari kwa kutumia utambulisho wa sasa ambao ni maarufu (Tanzania the Land of Kilimanjaro, Serengeti and Zanzibar), ni vema zikaangaliwa pia athari zitakazopatikana kwa kuachana na “brand” inayotumika hivi sasa.

Alisema kuwa baadhi ya vitu vinavyotumika kwenye utambulisho wa sasa tayari ni “brand”.  Alitoa mfano kuwa Mlima Kilimanjaro ni Brand maarufu na inayojiuza, hali kadhalika kwa Serengeti na Zanzibar.

VIDEO: MBUNGE CHUMI AWATOA HOFU WANANCHI JUU YA UPATIKANAJI WA UMEME

March 12, 2018
  Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi akiongea na viongozi wa chama cha mapinduzi jimbo hilo walipokutaka mjini mafinga kuzungumzia changamoto za jimbo hilo na nini kifanyike kutatua changamoto hizo
  Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi akiwa na viongozi mbalimbali wa chama cha mapinduzi 

Na Fredy Mgunda,Iringa.

 MBUNGE wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi amesema kuwa vijiji vyote vya jimbo hilo vitapatiwa umeme wa LEA ambao unafadhiliwa na serikali kwa lengo la kuchochea maendeleo ya wananchi waliopo vijijini

Chumi amewatoa hofu hiyo wananchi wa jimbo hilo juu ya upatikanaji wa umeme wa LEA wakati alipofanya mkutano na viongozi wa chama cha mapinduzi wa kata zote wa jimbo hilo.

Lakini mbunge huyo alitoa dira ya muelekeo wa jimbo hilo kimaendeleo kwa kuwakumbusha wapi walikotoka na wapi wanaendelea

AFUNGUA MKUTANO WA 14 WA MAAFISA MAWASILIANO WA SERIKALI JIJINI ARUSHA.

March 12, 2018
Waziri wa Habari,Sanaa,Utamduni na Michezo Dkt Harson Mwakyembe akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Chama cha maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) unaofanyika kwa siku tano jijini Arusha.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa 14 wa Chama cha maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kinachotajwa kama Kikao kazi wakifuatilia kwa karibu Hotuba mbalimbali zilizotolewa wakati wa Ufunguzi wa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari ,Sanaa,Utamaduni na Michezo ,Susan Mlawi akizungumza wakati wa mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji wa Serikali ,Dkt Hassan Abbas akizungumza katika mkutano hu unaofanyika katika Ukumbi wa mikuano ya Kimataifa (AICC) jijini Arusha.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa 14 wa Chama cha maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kinachotajwa kama Kikao kazi wakifuatilia kwa karibu Hotuba mbalimbali zilizotolewa wakati wa Ufunguzi wa mkutano huo.
Mwenyekiti wa Chama cha maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) ,Pascal Shelutete akitoa taarifa ya TAGCO kwa washiriki wa Mkutano huo .
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ,Hudson Kamoga akifuatilia hotuba zilizotolewa wakati wa mkutano huo.
Katika Mkutano huo pia kumetolewa Vyeti kwa Wadau walioshiriki katika kufanikisha mkutano huo .
Mmoja wa Wadau  waliosaidia katika kufanikisha mkutano huo akipokea cheti kutoka kwa Waziri wa Habari,Sanaa,Utamaduni na Michezo ,Dkt Harson Mwakyembe. 
Washiriki wa Mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi,Dkt Harson Mwakyembe ,Waziri wa Habari,Sanaa ,Utamaduni na Michezo .

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini .

WAZIRI wa Habari,Utamaduni ,Sanaa na Michezo ,Dkt Harson Mwakyembe amewaagiza Maafisa Habari wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria,Kanuni na Taratibu za serikali huku akiwataka kuzingatia malengo ya kitaifa waliyojiwekea katika kikao kilichopita.

Mbali na agizo hilo Dkt Mwakyembe pia amesema serikali haita wavumilia maafisa habari ambao hawatambui wajibu wao  huku akiwafananisha na maafisa habari hewa  ambao wanageuza tovuti za Serikali kuwa magofu badala ya kuwa na habari mbalimbali zenye tija na maendeleo kwa taifa la Tanzania.

Dkt Mwakyembe ameyasema hay oleo wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Habari,Mawasiliano na Uhusiano Serikali ,kinachofanyika katika Ukumbi wa mikutano ya Kimataifa (AICC) jijini Arusha kinachowakutanisha zaidi ya Maafisa Habari zaidi ya 300 kwa lengo la kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Katika kikao hicho kinachoenda sambamba na Mkutano Mkuu wa 14 wa Chama cha maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO)kinafanyika wakati kukiwa bado kuna changamoto katika kada ya maafisa Habari wa taasisi za Umma ikiwemo uharaka wa ufikishaji wa taarifa za serikali kwa umma .

Katika mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Habari Maelezo na Msemaji wa Serikali ,Dkt Hassan Abbas amewakumbusha washiriki wa mkutano huo kuenenda kimkakati huku akitoa nukuu za mcheza filamu Mashuhuri nchini Marekani ,Anord Schwazniger .
Naye Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa ,Tanzania ,Alvaro Rodriguez amesema serikali ina umuhimu mkubwa wa kufundisha na kuhabarisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia zinazo iunganisha Dunia .

“Umoja wa Mataifa unaiona Tanzania ya leo na kesho yenye mafanikio mengi sana,Demkorasia ,kufikia uchumi wa kati ,Elimu Bure,kupiga vita rushwa ni kati ya vitu vinavyoipa Tanzania sifa ya nchi iliyo tayari kuleta maendeleo ya nchi kwa ajili ya wananchi.”alisema Rodriguez.

Katika mkutano huo TAGCO ambacho ni chama kisicho cha kiserikali (NGO) kikiwa na madhumuni ya kukuza Mawasiliano na kuongeza Usambazaji wa  Taarifa ndani ya serikali na kati ya serikali na Wananchi  kimekabidh vyeti kwa Wadhamini wa mkutano huo ikiwemo Kampuni ya Clouds Media Group.
Mwisho .
ECOBANK TANZANIA KUFADHILI WANAFUNZI SHULE ZA SERIKALI

ECOBANK TANZANIA KUFADHILI WANAFUNZI SHULE ZA SERIKALI

March 12, 2018

Ecobank nchini Tanzania kuanzia mwaka huu inaanzisha mpango wa kutoa zawadi ya ufadhili kwa wasichana wanaofanya vyema katika masomo yao kwenye shule za serikali.
Aidha pamoja na ufadhili huo ili kuwaweka katika hali ya kuwa na uzoefu na kazi zao wanazosomea, watakuwa wanahakikisha wakati wa likizo wanawafanyia mpango wa kujishughulisha na kazi hizo ili kuwa na uzoefu.
Hayo yamesema na Mkurugenzi Mkuu benki hiyo nchini Mwanahiba Mzee wakati wa hafla ya mchapalo iliyofanyika hoteli ya Serena kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani mwishoni mwa wiki.
Alisema taasisi yake inaona umuhimu wa kumwezesha mtoto wa kike kusonga mbele kama moto wa taasisi hiyo ya kifedha unavyosema ‘press for progress’ ikimaananisha kujikita katika kutafuta maendeleo.
Alisema mwanamke anafanyakazi nyingi hivyo ni vyema kumwandaa tangu mapema ili kujua majukumu yake kama mzalishaji mkuu kwenye familia.
Alisema kwa sasa hawajaamua wanaanzia ngazi gani za ufadhili, lakini wanataka kufanya kitu tofauti chenye kulenga kupromoti maendeleo ya mtoto wa kike kama maazimio ya Beijing yanavyotaka kufikia asilimia hamsini kwa hamsini katika ngazi za kiutendaji.
Alisema sherehe hiyo ambayo inaambatana na siku ya mwanamke duniani inasherehekewa katika nchi 33 zenye benki hiyo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kibenki wa kuhakikisha kwamba wanawake wanasonga mbele kwa kuwa idadi yao ni asilimia 49.55 ya watu waliopo duniani na wanahaki ya kusaidia kukua kwa uchumi wa dunia, wa kaya na wakwao wenyewe kwa kuwezeshwa.
Anasema pamoja na ukweli kuwa wanawake wameachwa nyuma kwa miaka mingi, taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha kwamba inakuwa na asilimia 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030 huku hapa nchini inakaribia asilimia 49.
Alisema wakati sherehe hiyo ni kusherehekea mafanikio na kujifunza kutoka kwa wanawake waliofanya vyema, wanawake wanatakiwa kujiuliza wamesaidiaje wanawake wenzao kufikia ngazi ya juu kabisa ya uwezo walionao.
Alisema katika taasisi yake wametengeneza mpango wenye vipengele vitano vya kuhakikisha kwamba suala la jinsia linazingatiwa. Alitaja vipengele hivyo kama kushawishi fikira za jinsia katika maeneo ya kazi kuona kwamba kuna mizania. Kukabili fikira mgando dhidi ya wanawake, kuwezesha mwanamke kuonekana wazi, kushawishi kuinua wanawake kwa kutwaa huduma bora wanazozitoa na kusherehekea mafanikio ya mwanamke.
Alisema amefurahishwa na jinsi wanawake majasiri kama Getrude Mongella walivyoweza kupigania haki za wanawake wakikabiliana na makandokando yake na kufanikisha maazimio ya Beijing ambayo yanatumika kumkomboa mwanamke.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alisema pamoja na kupokea maelekezo ya mama Mongella kuhusu ustawishaji wa mwanamke, aliwataka wanawake kuwa wajasiri na kupambana na hali zao bila kujali wanatoka katika mazingira gani.
Alisema yeye alisoma katika shule ambazo sasa zinaitwa za Kayumba (shule za Upe) akianzia Mizumbwini Kibada hadi Kurasini kabla ya kupata nafsi ya kusoma Masjid Quba iliyopo Sinza na Alharamain alipomalizia kidato cha sita.
Unaona nimesoma shule za kawaida tu, siri kubwa ni kujituma na kujitambua. Nilijituma kwani niliona familia ya mama yangu ni watu maskini japo familia ya baba yangu walikuwa wanajiweza, nilisema lazima nimsaidie mama yangu.
Mwanahiba alisisitiza katika mazungumzo yake kwamba kujituma kunasaidia sana kwani hata yeye alipo ajiriwa kwa mara ya kwanza kama karani na kulipwa sh laki moja hakujali kwani alijua ni nafasi yake ya kujifunza japo alikuwa na MBA.
Aidha alisema kwamba alijifunza kwa bidii na kujenga kuaminika wakati akiwa Stanbic hali iliyompatia heshima ya jina lake kupelekwa katika mamlaka za Benki ambako alipita michujo mbalimbali na kufanikiwa kupata nafasi ya Ukurugenzi Mkuu Ecobank.
Naye Mama Mongella, mwanasiasa mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake aliyeshiriki Mkutano wa Beijing, akitoa nasaha zake, alimtaka Mkurugenzi wa Ecobank kuwapatia wanawake mitaji ili waweze kumiliki viwanda vyao waweze kuajiri na kufukuza.
Aidha aliwataka wafanyakazi wa benki hiyo kutomwangusha mkurugenzi wao na kuhakikisha wanajituma zaidi hasa benki inapowania kuwa na asilimia 50 kwa 50 katika utendaji wake.
Alisema wakati taifa hili linaelekea katika viwanda benki hiyo inayoendeshwa na mwanamama inastahili kupigania maslahi ya wanawake ili wawe na viwanda na kuchangia katika uchumi badala ya wao kuwa wasindikizaji.
"Si kuwakorogea uji wanaofanya viwandani bali wao ndio wawe wenye restaurants (migahawa) … wenye viwanda.." alisema mama Mongella.
Aidha aliwataka wanawake wanapopata nafasi ya kuajiriwa wawe makini katika utumishi wao na kuacha kuwataka mabosi ndio wawapigie magoti.
Pamoja na kutaka wanawake waendelezwe aliitaka jamii isisahau watoto wakiume kwani nao wanastahili kupata haki za elimu ili waweze kuwa watu bora na wanaoelewa.
Kama sasa kuna matatizo je kama wasipoenda shule wakabaki kuwa wapumbavu matatizo si yatazidi zaidi, alihoji mama Mongella.
Alkiwataka wanawake katika kila nafasi yao kufanya vyema na kuaminika huku wakiwasaidia wanawake wenzao kusonga mbele ili waweze kuwa na chakula cha kutosha kuwawezesha kufanya maamuzi yaliyoshiba pia.
Akizungumzia tasnia ya habari alisema kwamba toka walipotoka katika mkutano wa Beijing waandishi wa habari wamekuwa ndio wenye mabadiliko makubwa wakiwabeba wanawake katika muonekano mzuri na kumshauri Mkurugenzi huyo kuwatumia waandishi kuonesha watu mambo makubwa yanayofanywa na wanawake.
Alisema yeye na mafanikio aliyonayo sasa ni matokeo ya uamuzi wa kutaka kukabiliana na matatizo ya kiuchumi ambapo aliona jinsi mwanamke wa kijijini anavyohangaika na kusema ataendelea kupigana kumbadilisha mwanamke awe katika maisha bora.
Alisema amebahatika kuwa na watoto watatu wote wanaume, lakini amesema mabinti watakaoingia katika mji wake atahakikisha kwamba anawahoji wamefanya nini au wanampango gani wa kusaidia wanawake wenzao.
Katika hafla hiyo ya mchapalo wanawake walibadilishana mawazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na wakati wa kujifunza na kushangilia mafanikio ya mwanamke.
Mshehereshaji Babbie Kabae (kulia) akitambulisha wageni waalikwa kwenye hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mjasiriamali mwenye uthubutu ambaye pia ni mteja wa Ecobank Tanzania, Halima Mamuya akijitambulisha na ku-“share” uzoefu wake katika ujasiriamali wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kutoka kushoto ni Ofisa Uchumi na Mipango wa jiji la Mwanza, Bertiller Masawe, Mjasiriamali Chance Bishikwabo, Mgeni rasmi Mwanasiasa Mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake, Mama Getrude Mongella pamoja na Mkurugenzi Mkuu Ecobank Tanzania, Mwanahiba Mzee wakisikiliza kwa umakini shuhuda za Mama Mamuya.
Mkurugenzi Mkuu Ecobank Tanzania, Mwanahiba Mzee akizungumza kabla ya mgeni rasmi ambapo alielezea kwa undani safari ya maisha kama mwanamke wakati hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mgeni rasmi Mwanasiasa Mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake, Mama Getrude Mongella akitoa nasaha zake kwa wageni waalikwa na wafanyakazi wa Ecobank Tanzania (hawapo pichani) wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mchungaji Basilisa Ndonde akielezea kuhusu nafasi ya mwanamke katika familia na majukumu yake kama mke wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mgeni rasmi mwanasiasa mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake, Mama Getrude Mongella akipiga selfie na baadhi ya wageni waalikwa wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mgeni rasmi mwanasiasa mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake, Mama Getrude Mongella katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni waalikwa wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Miamala Ecobank Tanzania, Wende Mengele.
Mkuu wa kitengo cha Masoko na Mawasiliano Ecobank Tanzania, Furaha Samalu (kulia) katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni waalikwa wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Baadhi ya wageni waalikwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Ecobank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.