WATENDAJI WA SERIKALI WAMETAKIWA KUWA NA HURUMA KWA WAZEE

July 27, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.

WATENDAJI wa Serikali wametakiwa kuwa na huruma kwa wazee hasa katika utoaji huduma mbalimbali ikiwemo za matibabu,malazi na mahitaji yao muhimu kwani wengi wao hushindwa kupewa kipaumbele wanapohitaji huduma hizo kutokana aina ya maisha waliyonayo kwenye jamii zinazowazunguka.

Hayo yalibainishwa na washiriki kwenye warsha ya siku mbili iliyokuwa ikihusu huduma za wazee kwenye maeneo ya watendaji zinapewa kipaumbele iliyoratibiwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Old Nguvumali Women Centre (Ongwece) yenye makazi yake nguvumali jijini Tanga ambapo ilihusisha watendaji wa kata kutoka halmashauri ya jiji la Tanga na wakuu wa idara.

Akizungumza katika warsha hiyo,Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mabokweni,Hamza Omari alisema  serikali haina budi kuhakikisha inawasaidia wazee wa aina zote hapa nchini kwa kutenga bajeti maalumu ambayo itawahudumia kwenye mahitaji yao muhimu kutokana na wazee wengine kutopata msaada kwenye jamii zao.

Masoud alisema wazee wengi hawana utambulisho wa matibabu na kusema endapo watafanikiwa kuwekewa utaratibu wa kuwa na vitambulisho itasaidia kuondokana na adha ambazo wamekuwa wakikutana nazo mara kwa mara wanapokuwa wakihitaji huduma hiyo muhimu

Aidha aliongeza kuwa wakati umefika kwa jamii kubadilika na kuwathamini wazee ikiwemo kuacha kusema wazee wamepitwa wakati kwani hata nao watakuja kuwa miongoni mwao siku zijazo na huenda wakakutana na hali kama hizo endapo watashindwa kuwajali na kuwaheshimu wakati huu.

Naye Hanafi Maoud ambaye ni Ofisa Mtendaji kata ya Chumbageni alisema tatizo kubwa lililopo kwenye jamii nyingi hapa nchini ni kupotoka kimaadili na kushindwa kuwaheshimu na kuwapa kipaumbele wazee kama ilivyokuwa  hapo zamani.

Aidha aliiomba asasi zisizo za kiserikali iendelee kuhamasisha jamii ili kuweza kuona umuhimu wa wazee kutokana na wengi wao kuwa na mchango mkubwa sana lakini pia akiitaka serikali kuhakikisha inawahudumia wazee wasiojiweza kwa asilimia mia moja.

Kwa upande wake,Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Jiji la Tanga,Kassim Sengasu alishauri jamii kuangalia mfumo gani ambayo unaweza kutumika kuwaangalie wazee baada ya kustaafu kwa kushirikiana na taasisi za kidini kwani wakiziweka pembeni wazee hao watakuwa kwenye hali ngumu sana.

Hata hivyo,Mwezeshaji wa Warsha hiyo,Lucas Munako alisema dhana ya uzee ipo rasmi kwenye mfumo wa serikali na imejikita katika umri kwa mujibu wa miongozo iliyopo kuanzia miaka sitini na kutaka wazee wangewekewa utaratibu mzuri wa kuwawezesha ili kuweza kujikimu katika maisha yao.

"UWT yatakiwa kuvunja Makundi"

July 27, 2013
Na Mwandishi Wetu,Tanga.
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja  wa Wanawake Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT)Sophia Simba amewataka wanachama ndani ya  umoja huo kuvunja makundi yaliopo miongoni mwao na waelekeze nguvu zao katika kutimiza majukumu yao lengo likiwa ni kuimarisha umoja huo.

Simba ambaye pia ni Waziri wa Jinsi na Watoto alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo kwa viongozi na watendaji wa UWT kanda ya kaskazini iliyokuwa na malengo ya mpango mkakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku yaliyofanyika katika ukumbi wa CCM Hall mkoani Tanga.

Licha ya kuzungumzia suala hilo lakini pia watakuwa na mikakati ya UWT katika kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015 ambapo amewataka makatibu wa umoja huo ngazi ya chini kuhakikisha wanakuwa karibu na wanachama wao na kuacha tabia ya kuwapigia simu na kuwauliza maswali ya kuwa leo kuna mkutano au la.

Aidha aliwataka makatibu hao kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani viongozi wanapaswa kujinyenyekeza na kwenda vijiji lengo likiwa ni kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye maeneo yao pamoja na kuupa nguvu umoja huo.

Waziri Simba amewataka makatibu na wenyeviti kuwa wapo kwenye wakati mgumu sana hivyo wasigawanyike na kueleza akigundua viongozi wenye tabia kama hiyo hawatawavumilia badala yake wataondolewa kwani viongozi wa namna hiyo watashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Aidha amewataka UWT kuwa wakakamavu ili kuweza kuuimarisha umoja huo ikiwemo kuwa karibu na wakina mama ili uweza kuweza kuwasikiliza shida zao pamoja na kuwatetea pale wanapoona wakionewa katika jamii zao zinazowazunguka.

Shirikisho la waislamu lafuturisha Tanga

July 27, 2013
Na Burhan Yakub,Tanga.
Shirikisho la Taasisi za Kiislamu Mkoa wa Tanga(SHITA),limetimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwake   likiwa limefanikiwa kuondoa tofuati za kimitizamo zilizokuwa zikiwagawa waisamu miaka ya nyuma.

Kuondolewa kwa tofauti hizo kumewezesha waislamu wa Mkoa wa Tanga kujenga mshikamano uliodumisha amani  na hivyo kuwashangaza wengi waliokuwa wamezoea kushuhudia mitafaruku ya mara kwa mara.

Mwenyekiti wa Shirikisho hilo,Omari Guledi alitoa taarifa hiyo jana jioni alipokuwa akizungumza na waislamu waliohudhuria futari iliyoandaliwa na Shita Jijini hapa.

“Shita ilipokuwa ikianzishwa miaka mitano iliyopita wengi walidhani haitafanikiwa chochote lakini hivi sasa imejenga mshikamano miongoni mwa taasisi zilizokuwa zikipingana na kusababisha waislamu kuwa kitu kimoja”alisikika akisema Guledi.

Katibu wa shirikisho hilo,Ahmed Mustaffa alisema baada ya kufanikiwa kuziunganisha taasisi hizo,hatua inayofuata sasa kwa Shita ni kuanza kuzijengea uwezo wa kiuchumi ili ziweze kujiendesha zenyewe badala ya kutegemea misaada .

Katika hafla hiyo viongozi wa taasisi mbalimbali za kiislamu waliipongeza Shita kwa kuwaunganisha waislamu kuwa kitu kimoja licha ya kuwa hijitokeza tofauti ndogondogo lakini hukaa pamoja na kuzitatua.

TANZANIA YATOLEWA MICHUANO YA CHAN

July 27, 2013
Na Boniface Wambura,Uganda.
Tanzania (Taifa Stars) imeshindwa kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) kwa mara ya pili mfululizo baada ya leo (Julai 27 mwaka huu) kufungwa mabao 3-1 na Uganda Cranes, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-1.

Stars ambayo ilicheza fainali za kwanza zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2009 ilimaliza kipindi cha kwanza katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Kampala ikiwa sare ya bao 1-1.

Wenyeji ndiyo walioanza kufunga bao dakika ya saba katika mechi hiyo iliyochezeshwa na Kanoso Abdoul Ohabee kutoka Madagascar. Frank Kalanda alifunga bao hilo akimalizia mpira uliopigwa ndani ya eneo la hatari la Tanzania.

Bao hilo halikuonekana kuichangaza Taifa Stars, kwani ilitulia na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 18 mfungaji akiwa Amri Kiemba kutokana na pasi nzuri ya Mrisho Ngasa kwenye kona ya eneo la mita 18.

Dakika ya 32 nusura Taifa Stars ipate bao, lakini mkwaju maridadi wa Mrisho Ngasa ambao tayari ulikuwa umempira kipa HAmza Muwonge uligonga mwamba kabla ya kuokolewa na mabeki wa Uganda Cranes.

Mabao mengine ya Uganda Cranes yalifungwa dakika ya 48 kupitia kwa Brian Majwega na lingine dakika ya 63 mfungaji akiwa tenda Kalanda kutokana na makosa ya Salum Abubakar kupokonywa mpira wakati akiwa katika nafasi nzuri ya kutoa pasi kwa mwenzake.

Kocha Kim Poulsen alifanya mabadiliko dakika ya 43 kwa kumuingiza Simon Msuva badala ya Frank Domayo aliyeumia, na dakika ya 78 akawaingiza kwa mpigo Haruni Chanongo na Vincent Barnabas badala ya David Luhende na John Bocco. Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo.

Kikosi cha Stars kilipangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David Luhende/Vincent Barnabas, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Frank Domayo/Simon Msuva, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo, Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itarejea nyumbani kesho (Julai 28 mwaka huu) saa 4 usiku kwa ndege ya PrecisionAir.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
+256 793910742
Kampala