MALAIKA BENDI YAFUNIKA TANGA BILA BELLA.

November 24, 2013


Na Oscar Assenga, Tanga.

BENDI Mpya ya Mziki wa Dansi nchini Malaika Music Band jana iliweza kuwakonga nyoyo vilivyo mashabiki wake bila ya kuwepo kwa mwimbaji wao nguli Christian Bella katika onyesho ambalo lilifanyika kwenye ukumbi wa Tanga Hotel Jijini Tanga.


Onyesho hilo ambalo lilianza saa nne usiku lilikuwa la aina yake mara baada ya waimbaji wa bendi hiyo akiwemo Toto the Bingwa na wengine ambao kila mmoja aliweza kucheza kwa staili ya aina yake kitendo ambacho kilifanya mashabiki waliojitokeza kushuhudia onyesho hilo kulibuka kwa shangwe na nderemo.


Wakizungumzia onyesho hilo baadhi ya wakazi waliohudhuria walisema bendi hiyo ni moto wa kuotea mbalimbali licha ya kuwa mpya ambapo pia waliitabiria mafanikio makubwa kwa siku za usoni kutokana na kukamilika kila idara.


Edgar Mdime ambaye ni mkazi wa Chuda jijini Tanga alisema ladha nzuri waliokuwa wameikosa kwa muda mrefu waliweza kuipata siku hiyo kutokana na umahiri wa bendi hiyo kuanzia wapigaji vinanda,waimbaji na wachezaji hali iliyomlazimu kuhsindwa kukaa kwenye kiti na badala yake muda wote kucheza.


Mdime alisema kuanishwa kwa bendi hiyo kutaleta changamoto kubwa sana hapa nchini hasa kwa baadhi ya bendi ambazo zinafanya kazi kwa mazoezi na kuitaka kuendelea na kuwapa raha watanzania.


Kwa upande wake,Meneja wa Masoko wa Bendi hiyo,Mwisho.

TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHA CHADEMA

November 24, 2013

SOMA HAPA TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHA CHADEMA

Mh.Zitto Kabwe akiongea na vyombo vya habari leo


1. Utangulizi

Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu.

Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.


Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.

2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu

Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.

i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

  • Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
  • Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
  • Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
  • Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.

ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.

iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.

iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.

v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:

  • Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
  • Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.

vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:

  • Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
  • Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
  • Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.


3 . Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:

  1. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
  2. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.


4. Hitimisho
Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.

Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.

Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.

Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa demokrasia. Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama chetu.


Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.

24 Novemba, 2013

ADC YAPATA PIGO TANGA.

November 24, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
CHAMA  cha  siasa  cha ADC   kilichokuwa kikijiimarisha Mkoani hapa, kimepata pigo baada ya kuondokewa na viongozi wake  watatu  wa  ngazi ya Mkoa na Wilaya waliyohamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA).
 
Viongozi hao  wa ADC  waliyokihama chama hicho na kujiunga na Chadema  na nyazifa zao ni Kamishina wa Mkoa wa Tanga, Jadi Bamba, Mwenyekiti wa wanawake Wilaya ya Handeni, Mwanamvua  Mganga na Katibu wa Chama  wa  Wilaya ya  hiyo, Hamida Msumeno.
 
Wakizungumza mara baada ya kupokea  kadi mpya za uanachama wa Chadema, viongozi hao walieleza sababu za kukihama chama chao cha ADC  kuwa zinatokana na kuridhishwa na siasa za Chadema  ambazo hazipo Chama kingine.

Walisema kuwa  hawakuhama kwa kurubuniwa bali  ni baada  ya  kubaini kuwa ADC  hakuna kazi za siasa ambazo walizitegemea kuwepo kwa ajili ya kukomboa wananchi wa Tanzania na kwamba Chama makini ni Chadema.
 
Akiwatangaza  katika sherehe za kuwapokea wanachama hao wapya, Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje alisema kuwa  viongozi hao ni mashujaa na kwamba anatarajia watakuwa chachu ya vuguvugu la kisiasa ndani ya Mkoa wa Tanga.
 
Bahweje  alisema kuwa si viongozi hao pekee lakini anampango wa kupokea wengine kutoka vyamba mbalimbali vya siasa ikiwemo CCM  ambacho alidai kuwa kimekuwa mufirisi kwa kuwa na viongozi wasiyo na maono juu ya wananchi na taifa kwa ujumla.
 
Aidha aliwaomba wananchi na wanaCCM kwa ujumla kukiunga mkono Chadema kwa madai kuwa ndicho chenye malengo na mikakati ya  kulikomboa taifa hili kutokana na kuendesha siasa za kistaarabu na zenye kuleta matumaini.
 

JAMII YASHAURIWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUCHEMSHA MAJI.

November 24, 2013
Na Oscar Assenga,Muheza
 
JAMII ya watanzania imehimizwa kujenga utamaduni wa kuchemsha maji ya kunywa na kuyatumia,matumizi ya dawa za kutibu maji ‘water guard’ na matumizi ya vyoo bora utaratibu ulioelezwa kuwa utawasaidia kujiepusha kupatwa na magonjwa ya mlipuko.
 
Meneja wa shirika la PSI mkoani Tanga,Geofrey Mwankenja alitoa rai hiyo juzi kwenye maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani,utumiaji wa vyoo bora na uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira ambapo kimkoa ilikuwa kata ya Mhamba huko Muheza.
 
Akiwahutubia wakazi kata hiyo ya Mhamba,Mwankenja alisema ili watu wengi hususani wale wanaoishi maeneo ya vijijini kuweze kunusurika  kupata magonjwa ya mlipuko ni vyema wananchi wakachukua tahadhari kwa kuchemsha maji kabla ya kutaka kuyatumia.
 
Mwankenja alisema kuwa taratibu zote za kiafya zikizingatiwa ni dhahiri kuwa wananchi wengi wataepuka adui maradhi kama yale ya mlipuko ambapo aliwasisitiza wakazi wa Mhamba kunawa mikono kwa sabuni pindi wanapotoka maliwato kujisaidia hatua aliyoieleza kuwa itasaidia kuokoa maisha ya watanzania waliowengi hususani watoto.
 
Akizungumzia shughuli zilizofanywa na shirika la PSI kwenye maadhimisho hayo ya siku ya kunawa mikono,Mwankenja alisema wameweza kutoa elimu juu ya wananchi kutumia vyoo shughuli ambayo imefanyika kwa baadhi ya vijiji vya wilaya ya  Muheza.
 
Alisema kuwa pia elimu hiyo wameweza kuitoa kwa njia ya sinema,sanaa ya ngoma,matumizi ya mabango na hata matangazo kupitia vipaza sauti vilivyofungwa kwenye magari yao ambapo kata nane za wilaya ya Muheza ziliweza kuelimishwa.
 
Mbali na kueleza hayo Mwankenja pia alisema,PSI ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kuisaidia serikali kupambana na majanga mbalimbali imesaidia kukabiliana na  ugonjwa wa Ukimwi,malaria,magonjwa ya mlipuko na kuelimisha jamii kuhusu uzazi wa mpango.
 
Katika hayo Mwankenja alitanabaisha kwamba wamefanikiwa kuwapatia dawa za kutibu maji ‘water guard’ bure waathirika wa VVU huku wananchi wengine wakielimishwa na kushauriwa kununua dawa hizo kwa bei nafuu ya Tsh 200/= ili kuboresha afya zao.
 
Awali akiMwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Tanga aliyekuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Marcel Clemence alisema zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanaohudhuria vituo vya huduma za afya nchini wanaugua magonjwa yatokanayo na usafi wa mazingira na maji.
 
Clemence ambaye ni kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Tanga alisema takwimu hizo ni kwa mujibu wa wizara ya afya na ustawi wa jamii (WAUJ) ambapo magonjwa ya kuhara yanachangia zaidi ya asilimia 54 ya wagonjwa wote wanaohudhuria vituo vya huduma.
 
Aliendelea kusema kuwa taarifa za shirika la kuhudumia watoto la umoja wa mataifa UNICEF zinaonyesha kwamba ugonjwa wa kuhara kuwa miongoni mwa magonjwa matano yanayoongoza kwa kuua watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
 
Clemence alisema,wakati kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema ‘Usafi ni ustaarabu unaanza na sisi,tumia choo bora,nawa mikono kwa sabuni,okoa maisha ya watoto na jamii kwa ujumla’ taarifa zinasema mtoto mmoja hufariki dunia kila baada ya sekunde 20 kwa kukumbwa na magonjwa yatokanayo na mazingira machafu na ukosefu wa vyoo.

KILIMANJARO STARS KUAGWA KESHO.

November 24, 2013
Release No. 009
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 24, 2013

KILIMANJARO STARS KUAGWA KWA HAFLA
Kikosi cha Kilimanjaro Stars kinaagwa kesho (Novemba 25 mwaka huu) tayari kwa safari ya Nairobi, Kenya kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza kutimua vumbi Novemba 27 mwaka huu.

Hafla ya kuiaga timu hiyo itafanyika saa 5 asubuhi kambini kwao katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. Msafara wa Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager utaongozwa na Ahmed Idd Mgoyi.

Wachezaji waliomo katika msafara huo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).

Hata hivyo, washambuliaji Samata na Ulimwengu watajiunga na timu hiyo jijini Nairobi, Desemba Mosi mwaka huu wakitokea Lubumbashi ambapo Novemba 30 mwaka huu TP Mazembe itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Benchi la Ufundi la timu hiyo linawajumuisha Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa Makipa), Leopold Tasso (Meneja wa Timu), Dk Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa Timu), Frank Mhonda (mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza Vifaa).

Kilimanjaro Stars ambayo ipo kundi B katika michuano hiyo itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.

Boniface Wambura
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)