UMOJA WA ULAYA WAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SHILINGI BILIONI 130 KUSAIDIA UPATIKANAJI UMEME VIJIJINI

November 02, 2017
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Amina Shaban (kushoto) akiupokea ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya, ukiongozwa na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo Bw. Neven Mimica (katikati) na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Bw. Roeland van de Geer, walipokuwa wanawasili Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa msaada wa Euro milioni 50 kwa Tanzania.
 Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango wakimsikiliza kwa makini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akitoa maelezo ya ujio wa ugeni huo kuwa ni neema kwa nchi ya Tanzania kwani Umoja wa Ulaya wametoa msaada wa Euro Milioni 50 utasaidia vijijini 3600 nchini kupata  umeme.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) na akimweleza jambo Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Mr. Neven Mimica wakati wa hafla fupi ya Umoja wa Ulaya (EU) kutiliana saini makubaliano ya msaada wa Euro milioni 50 kwa ajili ya kusaidia usambazi wa umeme vijijini kupitia Mradi Kabambe wa Kusambaza umeme Vijijini (REA).
  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiwa pamoja na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Bw. Neven Mimica wakisaini Mkataba wa  msaada wa fedha za kusaidia usambazaji wa umeme Vijijini (EURO milioni 50) katika ukumbi wa  Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Mr. Neven Mimica, wakibadilishana hati za makubaliano ya msaada wa ruzuku ya kiasi cha EURO Milioni 50 katika ukumbi wa wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiwa na Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na Maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini mkataba wa msaada wa utekelezaji wa nishati ya umeme vijijini katika ukumbi wa Wizara ya fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiagana na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Bw. Neven Mimica, baada ya kusaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 50 ambazo Umoja huo umeipatia Tanzania kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini REA.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
TANZANIA imezidi kupata neema kutoka Jumuiya ya Kimataifa ambapo Novemba 2, 2017, Umoja wa Ulaya (EU) umeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 50, takriban Shilingi bilioni 130 kwa ajili ya kufadhili Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mkataba wa Makubaliano hayo umetiwa saini Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Neven Mimica.
Msaada huo umelenga kuwasaidia raia wa Tanzania kufikiwa na huduma nafuu ya nishati ya umeme kwa kupanua uwezo wa gridi ya Taifa pamoja na mtandao wa usambazaji umeme.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada huo mkubwa utakaoiwezesha nchi kuwa na umeme wa uhakika utakaochangia ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu wake.
“Umoja wa ulaya ni wadau wetu muhimu wa maendeleo kutokana na misaada muhimu na mikubwa wanayotupatia, na kusadia agenda yetu ya maendeleo” alisema Bw. James
Alisema kuwa kiasi cha msaada wa Euro milioni 50 kilichotolewa na Umoja huo bila masharti yoyote si kidogo, na kwamba kitasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme utakaochangia kuimarika kwa sekta ya viwanda itakayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Bw. Doto James alisema kuwa tangu Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini REA uanze miaka 9 iliyopita, idadi ya vijiji vilivyounganishiwa umeme imeongezeka kutoka vijiji 400 mwaka 2008 hadi kufikia vijiji 4395 hivi sasa.
Alisema kuwa ni matarajio ya Serikali kwamba ifikapo mwaka 2020, vijiji vyote 12,000 hapa nchini vitakuwa vimeunganishwa na nishati hiyo hivyo kuchochea shughuli za uzalishaji viwandani na kiuchumi kwa wananchi, vitaimarika.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Neven Mimica, amesema kuwa msaada huo wa Euro milioni 50 wanaoutoa ni sehemu ya msaada wa Euro milioni 207 ambazo wanachama wengine wa Umoja huo, ikiwemo Sweden, Uingereza, Norway na Benki ya Dunia, watatoa kufanikisha mradi huo wa usambazaji umeme vijijini kupitia REA.

WAZIRI MAKAMBA AWASILISHA TAARIFA KWA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA

November 02, 2017
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba  (wa pili kushoto)hii leo amewasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Kamati ya Pamoja  ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya Muungano kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.  Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu Bi. Butamo Kasuka Phillip na Katibu Mkuu Mhandisi Joseph Malongo. Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Muungano Bw. Baraka Baraka.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria Bi. Najma Murtaza Giga (kulia) akiongoza kikao cha Kamati yake wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya pamoja ya masuala ya Muungano. Kushoto ni Bw. Dunford Mpelumbe Katibu wa Kamati.


Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia majadiliano mara baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya pamoja ya masuala ya Muungano.

Sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wakifuatilia majadiliano katika kikao hicho
 

TANZANIA YATHIBITISHA KUCHEZA CHALENJI ZOTE 2017, PIA KUANDAA MWAKANI

November 02, 2017
Baada ya kupita miaka miwili bila kuchezwa kwa mashindano ya kuwania Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki, michuano hiyo imerejea tena msimu huu na Tanzania imethibitisha kushiriki.
Nchi wanachama Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu  Tanzania (TFF), Kidao Wilfred amethibitisha kikosi cha kwanza cha ‘Taifa Stars’ kushiriki na matarajio ya kufanya vema michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Novemba 25, 2017 hadi Desemba 9, mwaka huu.
Kidao amesema kwamba uteuzi wa timu za kwanza kwa kila nchi mwanachama wa Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki ni makubaliano ya viongozi wa CECAFA waliokutana kwa pamoja huko Sudan, Septemba, mwaka huu.
Kutokana na makubaliano hayo ya kuita timu za kwanza, michuano hiyo itaathiri kidogot ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuwa wachezaji wengi wanaounda kikosi hicho, wanatoka timu za VPL.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura amesema: “Tutakaa kama kamati na kuangalia siku ya Jumatano na Alhamisi baada ya michuano hiyo na kupanga ratiba ya mechi ambazo zitapanguliwa wakati wa michuano ya Chalenji.”
Mbali ya michuano hiyo, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika Bujumbura nchini Burundi kuanzia Desemba 12, 2017 hadi Desemba 22, mwaka huu.

HII HAPA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA

November 02, 2017
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), hii hapa tena wikiendi hii.
Mechi moja inachezwa kesho Ijumaa Novemba 3, 2017 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ambako mwenyeji Majimaji FC itacheza na Stand United ya Shinyanga.
Mchezo huo wa Songea utaanza saa 10.00 jioni (1600h).
Jumamosi kutakuwa na michezo mitano ambako minne itaanza saa 10.00 jioni (1600h) wakati mwingine utakuwa saa 1.00 usiku (1900h).
Michezo hiyo ya Jumamosi itakuwa ni kati ya Singida United itakayocheza na Young Africans kwenye Uwanja wa Namfua mkoani Singida wakati Tanzania Prisons itakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba  mjini Bukoba, Kagera.
Njombe Mji kwa upande wake watakuwa wenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe huku Mtibwa Sugar ikisafiri kutoka Morogoro kwenda Mtwara kucheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona. Hizo ni mechi zitakazochezwa saa 10.00 jioni.
Mchezo pekee utakaofanyika saa 1.00 usiku utakuwa ni kati ya Azam FC na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam.
Jumapili kutakuwa na michezo miwili ya Ligi Kuu ambako Lipuli ya Iringa itakuwa mwenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Samora wakati Simba itakuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Mechi hizo zitaanza saa 10.00 jioni.

RC GEITA ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA LIPA KWA MATOKEO HALMASHAURI YA MJI GEITA

November 02, 2017

Mhandisi Robert Lughumbi Mkuu wa Mkoa wa Geita pamoja na viongozi wa Mkoa na Wilaya Geita na kamati ya usalama ya Mkoa  wakikagua miundombinu ya shule ya Msingi Nguzombili wakati wa ziara ya Mkuu huyo wa Mkoa Halmashauri ya Mji Geita.
Mhandisi Robert Gabriel Mkuu wa Mkoa wa Geita akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita(Wakwanza kushoto) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nguzombili wakati wa ziara yake katika Shule hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita akiingia ndani ya moja ya darasa lililojenjwa chini ya mpango wa lipa kwa matokeo shule ya Msingi Nguzo Mbili.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Geita Mhandisi  Modest Apolinary  akifafanua jambo kuhusu utekelezaji miradi ya lipa kwa matokeo kwa Mkuu wa Mkoa wakati wa ziara yake shule ya msingi Nguzombili iliyopo Halmashauri ya Mji Geita.