JIJI LA TANGA LAMWAGA MIKOPO YENYE THAMANI YA ZAIDI YA BILIONI 2

October 29, 2022

 




Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman Shiloo akizungumza wakati wa kukabidhi hundi kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kwa ajili ya vikundi vya kiuchumi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kutoka katika asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya ndani kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt Sipora Liana

Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt Sipora Liana akizungumza wakati wa halfa hiyo 
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt Sipora Liana akizungumza wakati wa halfa hiyo kulia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shilloo
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Jiji la Tanga Bw. Simon Mdende akizungumza wakati wa halfa hiyo
Meza kuu wakifuatilia matukio mbalimbali
Meza kuu wakifuatilia matukio mbalimbali
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman Shiloo wa tatu kutoka kushoto akieleza jambo kabla ya kukabiudhi hundi hizo
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman Shiloo akikabidhi hundi kwa moja ya vikundi vya wakina mama wajasiriamali Jijini Tanga 
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Mhe. Abdulrahman Shiloo katika akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa kutoka taasisi za kifedha Jijini Tanga mara baada ya kukabidhi mikopo hiyo kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga dkt Sipora Liana na kulia ni Mkuu wa Idara ya  Maendeleo ya Jamii Jiji la Tanga Bw. Simon Mdende
Sehemu ya wanufaika wa mikopo hiyo wakiwa kwenye halfa hiyo
Sehemu ya wanufaika wa mikopo hiyo wakiwa kwenye halfa hiyo
Sehemu ya wanufaika wa mikopo hiyo wakiwa kwenye halfa hiyo

Na Oscar Assenga,TANGA.


HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imefanikiwa kuongeza kiwango cha utoaji wa fedha za mikopo kwa vikundi vya kiuchumi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu kutoka katika asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya ndani, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shillingi Billion 2,088,530,000.00 zimetolewa kama mikopo isiyo na riba kwa makundi hayo ili kuwawezesha kiuchumi, kulinganisha na Million 943 kwa mwaka 2020/2021. 

Kiwango hicho cha fedha, kinajumuisha fedha zilizopangwa kutoka Bajeti ya mapato kwa mwaka huo, kiasi cha Billion 1,115,607,800.00 pamoja na fedha za marejesho ambazo nazo zimeingia katika mzunguko wa ukopeshaji. 

Akikabidhi mfano wa hundi zenye thamani ya shillingi million 377 kwa vikundi 43 (Wanawake vikundi 31 wakipokea jumla ya shillingi million 266, Vijana vikundi 6 Tsh. 83 M na wenye ulemavu vikundi 6 Tsh. 28 M), ambapo vinahitimisha awamu ya nne ya utoaji kwa mwaka 2021/2022. 

Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga  Abdulrahman Shiloow amewataka wanavikundi hao kuzingatia mipango yao na kufanya biashara zenye tija ili warudishe mkopo na kupata faida ya kazi na kubadili hali zao za maisha. 

Amesema fedha hizo sio za bure, ni mkopo, hivyo wanapaswa kufanya utafiti wa biashara sio kuiga kwa mwingine. 

Mheshimiwa Shiloow ambaye alikabidhi hundi hizo kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, aliwataka wakazi wa Jiji la Tanga kuwa na imani na Mbunge wao kwa jinsi anavyofanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo,  na kwamba kila shughuli ya maendeleo, mkono wake upo, na kwamba alipenda awepo katika tukio hilo. 

Awali, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Dkt. Sipora Liana alisema vikundi vinavyopata mkopo safari hii vimetumia njia ya mtandao katika kujaza taarifa zao na kwamba elimu na mafunzo yametolewa kwao na maafisa kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamii. 

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Jiji la Tanga Bw. Simon Mdende amesema hali ya marejesho inakwenda vizuri na kwamba vipo vikundi vilivyomaliza mkopo na sasa wanapata kwa awamu ya pili.

TSAP YAIBUKA NA TAFITI ZITAKAZOBORESHA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI.

October 29, 2022

 



Afisa Mauzo kutoka kampuni ya Pembejeo za Mifugo ya "Afrifarm" Bw. Emanuel Senge (kushoto) akimuonesha Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bw. David Lyamongi (kulia) chakula cha Mifugo kinachouzwa na kampuni hiyo mara baada ya Bw. Lyamongi kufika kwenye banda hilo jana (28.10.2022) ikiwa ni muda mfupi kabla hajafunga Kongamano la chama cha wanataaluma wa sayansi ya uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) lililokuwa likifanyika mkoani humo. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Jeremiah Temu.


Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma wa sayansi ya uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) Dkt.Jonas Kizima akiainisha maazimio ya kongamano la chama hicho kwa mwaka huu wakati wa kilele cha kongamano hilo lililokuwa likifanyika jijini Arusha, jana (28.10.2022).



-Dkt. Kizima aziweka wazi..

Kongamano la  Chama cha wanataaluma wa sayansi ya uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) lililokuwa likifanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 26 mwaka huu limefikia tamati jana (28.10.2022) ambapo baada ya majadiliano ya kina yaliyokuwa yakihusu tafiti mbalimbali zilizolenga kuboresha sekta za Mifugo na Uvuvi, wataalam hao wamefikia maazimio kuhusu tafiti hizo.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kongamano hilo, Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. Jonas Kizima amesema kuwa wanataaluma hao kwa pamoja wamebaini kuwa ni lazima zifanyike tafiti za kutafuta vyakula mbadala na vyenye ubora  vya Mifugo na samaki ili viwasaidie wadau wanaojishughulisha na shughuli za ufugaji kuzalisha zaidi.

“Lakini tumeona athari za mabadiliko ya tabia nchi yanavyoathiri sana uzalishaji wa Mifugo kwa hiyo tumekubaliana ni lazima zifanyike tafiti ambazo zitaibua aina ya malisho na mifugo inayoweza kukabiliana na mabadiliko hayo” Ameongeza Dkt. Kizima.

Dkt. Kizima amebainisha jambo jingine walilobaini kupitia kongamano la wataalam hao kwa mwaka huu  ni umuhimu wa bima ya Mifugo ambapo wamejadili kwa kina umuhimu wa bima hiyo na kuainisha manufaa mbalimbali ambayo mfugaji anaweza kupata kupitia bima hiyo.

“Kingine ambacho kimefanyika kupitia kongamano la mwaka huu ni wasilisho la namna ambavyo taratibu za kitafiti zinapaswa kupata kibali cha maadili yanayohusu utafiti huo hivyo kuanzia sasa kabla hujachapisha tafiti zako kwenye majarida ya mitandaoni ni lazima uwe na kibali hicho kitakachoonesha ni kwa kiasi gani umezingatia maadili ya taaluma hiyo” Amesema Dkt. Kizima.

Awali akizungumza katika hotuba yake ya kufunga kongamano hilo aliyoisoma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo Bw. David Lyamongi amesema kuwa mkoa huo kwa sasa unatekeleza maazimio ya wanataaluma hao kwa vitendo kupitia elimu ya namna ya kuboresha shughuli za ufugaji inayotolewa na Vyuo vya Nelson Mandela, Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) kituo cha Tengeru na Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC).

“Mkoa wetu ni moja ya mikoa inayofanya shughuli za ufugaji kwa kiasi kikubwa na tayari tumeshaanza kufuga kisasa kwa kupunguza idadi ya mifugo na kuiboresha michache inayobaki ili kumuongezea tija mfugaji mwenyewe na Taifa kwa ujumla” Amesema Bw. Lyamongi.

Akizungumzia kuhusu  kuongeza idadi ya washiriki kwenye Kongamano lijalo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Zabron Nziku ametoa wito kwa wataalam wa sekta za Mifugo na Uvuvi waliopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kushiriki kwenye kongamano hilo ili waweze kuongeza ujuzi utakaowawezesha kwenda kuwahudumia vizuri wananchi kwenye maeneo yao.

“Lakini pia nitoe rai kwa wadau wa sekta binafsi wanaojishughulisha na sekta za Mifugo na Uvuvi, kushiriki kwa wingi na kuja kutoa elimu juu ya bidhaa mbalimbali wanazozalisha ili wawatumie wataalam  wanaoshiriki kongamano hili kama mabalozi wa bidhaa zao pindi watakapoenda kule chini kwa watumiaji wa bidhaa hizo” Amehitimisha Dkt. Nziku.

Mbali na majadiliano ya kina kuhusu tafiti za Mifugo na Uvuvi, Kongamano hilo la Chama cha wanataaluma wa sayansi ya uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi (TSAP) kwa mwaka huu liliambatana na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanataaluma wa chama hicho kwenda kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha utalii wa ndani nan je kupitia filamu yake ya “Royal Tour”.