Na Benny Mwaipaja, WFM
Naibu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Tao Zhang
ameahidi kufungua madirisha ya mikopo kwa nchi ya Tanzania kutokana na
jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali za kukuza uchumi.
Bw.
Zhang aliyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), katika ofisi za
Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.
“Shirika
la Fedha la Kimataifa limeziona jitihada za kukuza uchumi wa nchi
ambapo mpaka sasa Tanzania inaongoza katika nchi za Afrika Mashariki na
ipo juu ya wastani wa ukuaji wa uchumi Barani Afrika” Alisema Bw. Zhang.
Ameishauri
Serikali kuendelea kushirikiana na Sekta binafsi katika ukuaji wa
Uchumi ili uchumi huo uwe endelevu. Aidha ameitaka Serikali kuwa na
mfumo shirikishi wa kifedha utakao wanufaisha wananchi wengi.
Naye
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), amesema
kuwa juhudi za Tanzania kwa sasa ni kuchochea ukuaji wa Kilimo na
kuongeza uzalishaji wenye tija
“Umasikini
haujatatuliwa kwa kiwango ambacho Serikali ingependa kukiona, kwa kuwa
mpaka sasa watu walio katika umasikini na ukosefu wa huduma za lazima
ni takribani asilimia 34.4 “, aliongeza Dkt. Mpango
Kama
nchi imeamua kwenda kwenye uchumi wa kati na jambo ambalo linatiliwa
mkazo ni upatikanaji wa umeme wa kutosha na wenye bei nafuu.
Amesema
kuwa Serikali imefanya juhudi za kupeleka umeme mpaka vijijini lakini
bado kazi hiyo haijakamilika. Pia suala la miundombinu ya ya
usafirishaji ni changamoto, ukiwemo usafiri wa reli kutoka Mashariki
hadi Magharibi mwa nchi ambao ni wazamani na umeharibika.
“Serikali
imeamua kujenga Reli yenye kiwango cha Kimataifa (Standard gauge)
ambayo ni ya gharama, na kwa makadirio ya awali zinahitajika Dola
Bilioni 7.6, lakini umechukuliwa uamuzi huo ili kuharakisha
Maendeleo”aliongeza Dkt. Mpango
“Tayari
tumeanza ujenzi wa reli hiyo kwa fedha za ndani kwa takribani Kilometa
200 kutoka Dar es salaam mpaka Morogoro na tutaendelea na ujenzi kadri
fedha zinavyo patikana” alifafanua Waziri Mpango.
Amesema
kuwa, kumekuwa na tatizo la ahadi za Wahisani kutotekelezwa kwa wakati
jambo linalofanya baadhi ya shughuli za maendeleo kutotekelezwa kwa
wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) anaeziwakilisha nchi 23
za Afrika, Bw. Maxwell Mkwezalamba, alisema ni vema Serikali
ikaendelea kuangalia vipaumbele katika ujenzi wa miundombinu ili iweze
kuchochea uchumi.
“Suala
la ajira hasa kwa vijana linatakiwa kufanyiwa kazi na pia kuweka
mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa Sekta Binafsi kwa
kuwa Sekta Binafsi imekuwa na mchango mkubwa katika Maendeleo kwa nchi
nyingi Duniani” Alishauri Bw. Mkwezalamba.
Ameishauri
Tanzania kuendelea kuwekeza kikamilifu katika Sekta ya Elimu kwa kuwa
ni moja ya eneo ambalo kama likifanyiwa kazi kikamilifu litaleta Matokeo
chanya na ya haraka katika ukuaji wa Uchumi.
Akitoa
ufafanuzi wa hoja hizo, Waziri Mpango, amesema Serikali imeendelea
kuhakikisha kunakuwa na viwanda vingi ili vijana wengi waweze kupata
ajira. Aidha tayari Tanzania imeanza kutekeleza Elimu bure kuanzia
darasa la kwanza hadi kidato cha nne ili kutoa fursa kwa watu wengi
zaidi kupata elimu.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) anaeziwakilisha nchi 23
za Afrika, Bw. Maxwell Mkwezalamba (wa pili kulia) akieleza kuwa
Tanzania inakua kwa kasi kiuchumi jambo ambalo linawavutia viongozi
wengi kufuatilia kwa karibu maendeleo yake, alipokutana na Waziri wa
Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto), katika
Ukumbi wa Wizara Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akiongoza
Mkutano kati yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF) anaeziwakilisha nchi 23 za Afrika, Bw. Maxwell
Mkwezalamba (mbele kulia) ambapo alisema mahitaji makubwa wa nchi ni
maendeleo ya kilimo na upatikanaji wa nishati ya umeme ili viweze
kuchochea uchumi wa viwanda. Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa
Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (kushoto) na
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
anaeziwakilisha nchi 23 za Afrika, Bw. Maxwell Mkwezalamba ( kulia)
wakipeana mkono baada ya kumalizika kwa Mkutano kati yao uliohusu suala
la Uchumi katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es
salaam.
Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (watatu
kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)
anaeziwakilisha nchi 23 za Afrika, Bw. Maxwell Mkwezalamba (wa tatu
kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Maafisa waandamizi
wa Wizara hiyo baada ya kumalizika kwa mkutano kuhusu hali ya uchumi
katika Ukumbi wa Wizara Jijini Dar es Salaam.