Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimuhoji Afisa ardhi Manispaa
ya Morogoro Bw. Abenance Kanomoga (wa kwanza kushoto), kwanini amekaa na
hati za wananchi kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kuwajulisha wahusika
kuja kuzichukua.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akigawa hati kwa wakazi wa Bigwa mkoani Morogoro..
Baadhi ya wananchi wa mkoani Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ajiongea na wananchi wa mkoani Morogoro.
…………………………………………………………………………
Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi katika ziara yake ya mkoani
Morogoro (17-10-2016) ameendelea kutekeleza program ya kurasimisha
makazi holela kwa wananchi 116, ambapo amegawa hati 60 za awali na
kumuagiza Afisa ardhi kuhakikisha anatoa hati zilizobakia ndani ya mwezi
mmoja.
Serikali kupitia Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika mpango wake wa kuboresha maendeleo
ya wananchi na makazi yao, imeanzisha program ya kurasimisha makazi
holela kwa wananchi. Mpango huu ni wakupima, kupanga na kuwapatia hati
wananchi waliojenga katika makazi yasio na mpangilio rasmi.
Akiwa mkoani morogoro Mhe. Waziri
alitembelea baadhi ya makazi ya wananchi hao katika kata ya Bigwa na
kujionea jinsi wananchi wanavyounga mkono juhudi za serikali katika
kurasimisha makazi holela.
Wananchi hao wa Bigwa kwa umoja wao walipima ardhi zao na kufuata utaratibu wa mipango miji kwa mujibu wa taratibu za serikali.
Aidha, Lukuvi alifanya ziara ya
kushtukiza katika Masijara ya Ardhi ya Manispaa ya Morogoro, na kukuta
idadi kubwa ya hati za wananchi zimekaa zaidi ya mwaka mzima bila ya
kuwafikia wahusika. Alihoji juu ya suala hilo, na kutoa agizo kwa
Mkurugenzi wa Manispaa hati hizo kuwafikia walengwa ndani ya mwezi
mmoja.
Baada ya ziara hiyo Mheshimiwa
Waziri aliongea na wananchi wa Morogoro katika ofisi za Manispaa ya
Morogoro na kusikiliza kero zao mbalimbali za ardhi na kuzitatua
papohapo. Katika mazungumzo yake aliwataka wananchi waunge mkono juhudi
za serikali kurasimisha makazi yao ili waweze kuishi katika makazi
salama yanayotambulika na pia waweze kufaidika na ardhi yao kama kupata
mikopo Benki au katika mambo mengine ya maendeleo yao.