Na Oscar Assenga, Tanga
MKURUGENZI
wa haki za binadamu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa
Tanga, Jonathan Bahweje amewataka wafanyabiashara kuacha kupandisha bei vyakula
kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kuhamasisha chama hivi karibuni katika viwanja vya Mwembe Mawazo, Bahweje amewataka wafanyabiashara hao kumkumbuka Mungu kwani mwezi huo ni waheri na baraka.
Amesema kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakivitumia vipindi vya mwezi wa ramadhani kwa kupandisha bei vyakula na kujisahau kuwa ni mwezi wa Baraka na hivyo kuwataka kumkumbuka Mungu na kuwapa wepesi wafungaji.
Amesema
imekuwa kawaida kwa wafanyabiashara kuufanya mwezi wa Ramadhani kuwa ni kipindi
cha kujitajirisha na kuwataka kuacha kufanya hivyo kwani kutasababisha kuwapa
ugumu wafungaji.
Bahweje amewataka wafanyabiashara hao kuufanya mwezi huo kuwa ni wakutafuta Baraka na kupata malipo kutoka kwa Mungu lengo likiwa ni kutoa nafasi kwa waumini kufunga mwezi huo na kutouona mgumu.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya, Khalid Rashid, aliwataka wakazi wa Chumbageni kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kuwaondoshea kero ambazo zinawakabili likiwemo wimbi la wizi wa madirishani usiku.
Amesema kero
hiyo ambayo imeshindwa kupatiwa ufumbuzi na chama chenye Udiwani na hivyo
kuadhimia kikifanikiwa kuchukua nafasi ya kuongoza kero hiyo itakuwa ya kwanza
kuikomesha.
Amesema chama hicho kimeshindwa kuleta umoja na mshikamano na kuunda ulinzi shirikishi na badala yake matumaini ya kusogeza maendeleo yameshindikana na hivyo kuwataka wakazi hao kukiunga mkono chama hicho katika chaguzi zijazo.
Rashid amewataka wakazi hao kuacha kufanya makosa kwa kutokichagua Chadema kwani chama hicho kiko na sera za kumkomboa Mtanzania kutoka katika dimbwi la umasikini na kumuingiza katika maisha ya utajiri kwani nchi iko na rasilimali nyingi.
Mwisho.