AZAM YAPIGWA 3-0 NA KAIZER CHIEFS

August 05, 2013
Na Mahmoud Zubeiry, Johannesburg, Afrika Kusini

AZAM FC imeanza vibaya ziara yake ya mechi za kujipima nguvu mjini hapa, baada ya kufungwa mabao 3-0 na wenyeji, Kaizer Chiefs katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa mazoezi wa wa timu hiyo, eneo la Nachurena.

Azam iliyoondoka nchini jana mchana kwa ndege ya Shirika la Afrika Kusini, kuja Johannesburg, Afrika Kusini kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya, katika mchezo wa leo iliathiriwa na uchofu wa safari na hali ya hewa ya baridi, hivyo kucheza chini ya kiwango.
Azam FC

Timu hiyo yenye maskani yake, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, iliyoondoka na kikosi chake kizima, kasoro wachezaji wawili tu majeruhi, kiungo Mkenya, Humphrey Mieno na mshambuliaji Mganda, Brian Umony, imefikia katika hoteli ya Randburg Towers.

Azam jana ilifanya mazoezi yake ya kwanza kwenye Uwanja wa Wits University asubuhi na jioni na Kocha
Mkuu wa timu hiyo, Muingereza Stewart Hall amefurahishwa na mazingira ya kambi na Uwanja wa mazoezi.
Baada ya mchezo wa leo, Azam itashuka tena dimbani Agosti 7, kumenyana na Mamelodi Sundowns kabla ya kuivaa Orlando Pirates Agosti 9 na Agosti 12 itamaliza ziara yake kwa kumenyana na Moroka Swallows.

Azam inatarajiwa kurejea nchini Agosti 13 tayari kwa mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kuashiria kufungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC, Agosti 17, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Safari hii Azam, washindi wa pili mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu wamepania kutwaa Ngao mbele ya Yanga, baada ya mwaka jana kufungwa na Simba SC na kocha Muingereza Stewart Hall anajiandaa kikamilifu kwa ajili hiyo.

TENGA AMSHUKURU MSAJILI KWA KUSAJILI KATIBA YA TFF

August 05, 2013

Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amemshukuru Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kwa kusajili Katiba ya TFF toleo la 2013 kutokana na marekebisho yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika Julai 13 mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo (Agosti 5 mwaka huu), Rais Tenga ameishukuru Serikali, Msajili, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara na Naibu wake Amos Makala kwa ushirikiano ambao wametoa kwa TFF katika kufanikisha suala hilo.

Amesema baada ya kupokea usajili huo, kinachofuata ni Katibu Mkuu wa TFF kumwandikia rasmi Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ili aanzishe mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa TFF.

Kuhusu kauli ya Naibu Waziri Makala kuwa marekebisho hayo yasingeweza kusajiliwa kwa sababu hayakufuata Katiba ya TFF, Rais Tenga amesema alikuwa ana haki ya kusema hivyo kwa sababu hakuwepo kwenye Mkutano huo, na kuongeza:

“Makala hakuwepo kwenye mkutano ndiyo maana alisema hivyo. Ana haki ya kuuliza, nina hakika sasa atakuwa ameeleweshwa na ameelewa kwa sababu ni msikivu. Kuhusu marekebisho hayo kupigiwa kura, hilo  lisingewefanyika kwa sababu hakukuwa na mjumbe aliyepinga marekebisho,” amesema.

Rais Tenga amesema marekebisho hayo yalipitishwa kwa kauli moja (unanimous) hivyo hakukuwa na sababu ya kuanza kunyoosha mikono kupiga kura, kwa maana hiyo mkutano ulipitisha marekebisho kwa asilimia 100 wakati Katiba ilikuwa ikihitaji theluthi mbili tu.

“Hakukuwa na dispute (mabishano) kuhusu marekebisho, isipokuwa wajumbe walitumia muda mwingi kuboresha kanuni na kutoa ushauri wa aina ya watu ambao wangeingia kwenye kamati mbalimbali zikiwemo zile mpya za Maadili,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa vile wote walioingia kwenye Mkutano Mkuu huo Maalumu ni watu wa mpira wa miguu wasingeweza kupinga marekebisho kwa vile yametokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

“Labda itokee aliyeingia kwenye mkutano alikosea njia. Mtu yeyote wa mpira wa miguu ni lazima afahamu kuwa maagizo ya FIFA ni lazima yatekelezwe, na Katiba ya TFF inasema hivyo,” amesema Rais Tenga.

Pia Rais Tenga amewataka wapenzi wa mpira wa miguu kushawishi watu wenye sifa na uwezo wa kuongoza kujitokeza kwa wingi wakati Kamati ya Uchaguzi itakapotangaza mchakato na tarehe ya uchaguzi huo.

AZAM YAANZA ZIARA KWA KUIKABILI KAISER CHIEFS

August 05, 2013

NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM.
  
Makamu bingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Azam wanaanza rasmi ziara ya mechi za kirafiki nchini Afrika Kusini leo kwa kuikabili timu ya Kaiser Chiefs ambayo inacheza Ligi Kuu ya nchi hiyo (PSL).

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Azam, Jaffer Idd aliyefutana na timu hiyo, mechi hiyo inachezwa jijini Johannesburg ambapo baada ya mechi hiyo watacheza nyengine za majaribio kabla ya kuanza msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara.

Ngao ya hisani inatarajiwa kuchezwa Agosti 17 mwaka huu katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo timu hizo zitachuana ikiwa ni kiashiria cha ufunguzi wa ligi hiyo.

Idd anapatikana kwa namba +27788847399.

MWANRI AAGIZA KUKAMATWA KWA MKANDARASI

August 05, 2013
Na Mwandishi Wetu,Handeni

NAIBU Waziri wa nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)Aggrey Mwanri ameiagiza Halmashauri ya wilaya ya Handeni  kumtafuta na kumfikisha kwake mara moja mkandarasi aliyepewa zabuni ya ujenzi wa barabara Sindeni hadi Komsangazi yenye umbali wa kilomita 21 kwa kiwango cha changarawe  kufuatia kutoroka katika kituo chake cha kazi kwa zaidi ya miezi mitatu sasa .

Mwanri alitoa agizo hilo baada ya kufanya ukaguzi wa barabara hiyo iliyotengewa zaidi ya shilingi milioni 160 kwa ajili ya  ukarabati kiwango cha changarawe kisha kutelekezwa baada ya Mkandarasi wa Kampuni ya Lenguyana costraction company kuondoka katika kituo chake cha kazi.

“Nini maana yake yaani mtu apewe hela kazi haijakwisha halafu haonekani bila maelezo yoyote tu jamani hili halikubaliki na nataka atafutwe na aletwe kwangu mara moja hatua gani zitafuata najua mimi mwenyewe”,alisema Mwanri .

Naibu Waziri huyo alisema hali hiyo inasikitisha na imekuwa ikichukuliwa mazoea kwa miradi mingi kutokamilika na wakandarasi kufanya maamuzi wanayotaka wao kinyume cha mikataba huku halmashauri husika zikifumbia macho suala hilo.

“Nimepita kwenye miradi mbalimbali kwenye halmashauri mbalimbali katika ziara yangu hii ya kikazi gharama ya fedha zinazotumika hailingani kabisa na kiwnago cha ubora kwenye miradi husika na hali wanaopata shida ni wananchi na katika hili sasa tutaonana wabaya “,alisisitiza.

Kuhusiana na mradi wa Bwawa la maji unaotekelezwa kaika halmashauri hiyo Mwanri aliagiza miundo mbinu ya maji kwa binadamu itiliwe mkazo kufuatia wananchi kupata shida ya maji hatua ambayo husabababisha wakazi wake kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ya mara kwa mara.
 
Hata hivyo kwa upande wake Mhandisi wa maji wilayani Handeni Richard Macha akitoa maelezo kuhusu mradi huo unaotarajiwa kuhudumia zaidi ya wakazi 31,800 waliopo katika Kata ya Kata wilayani Handeni alisema bwawa hilo  litakalokuwa na meta za ujazo wa maji 563,000 hadi kukamilika kwake litagharimu zaidi ya shilingi milioni 747.8 fedha zilizotolewa na Benki ya dunia na baadhi ni nguvu za wananchi .

SERIKALI YATOA WIKI MBILI KWA UONGOZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA LUSHOTO.

August 05, 2013
Na Mwandishi Wetu,Lushoto

SERIKALI imetoa wiki mbili kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Lushoto kuorodhesha majina ya baadhi ya wakuu wa idara pamoja na watendaji wengine ambao wanadaiwa kuhusika na ufujaji wa fedha zilizotakiwa kutekeleza miradi ya maendeleo wilayani humo.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa nchi Ofiisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Agrey Mwanri wakati alipokuwa akizungumza na Viongozi wa chama na serikali pamoja na wananchi wa wilaya humo kufuatia kutokamilika kwa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo katika sekta ya elimu ,afya na miundo mbinu.

Mwanri alisema wakati umefika sasa kwa serikali kuchukua hatua kali na za kisheria dhidi ya watendaji ambao wanashindwa kutimiza majukumu yao ya kazi sambamba na kutumia fedha za umma kwa matumizi yao binafsi.

 Alitolea mfano kuwa wapo baadhi ya walimu ambao  wamefuja fedha za ujenzi wa madarasa kisha mkuu wa idara hiyo kumhamisha mwalimu kutoka kituo kimoja kwenda kingine hatua ambayo alimwagiza Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Maweni anayetuhumiwa kuhujumu fedha za ujenzi wa madarasa akamatwe mara moja kisha afikishwe katika vyombo vya sheria.

“Hela zinaliwa halafu mnachofanya ni kubadilishana tu vituo vya kazi badala ya sheria kuchukua mkondo wake…. si haki hata kidogo DED nataka majina ya wahusika haraka iwezekanavyo hatupo kwa ajili ya matumbo yetu tupo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi”,alisema Naibu Waziri huyo.

Hata hivyo aliwataka wananchi katika vijiji mbali mbali kutoa taarifa mapema kwa Mkuu wa wilaya  hiyo Majjid Mwanga endapo viongozi wa serikali za vijiji vyao watashindwa kufanya mikutano na kuwasomea taarifa za fedha za mapato na matumizi ya maeneo yao kwa wakati muafaka.

“Hawa hawa viongozi wenu wa serikali za vijiji ndio wanaowahujumu kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wasio waadilifu sasa kama hamsomewi taarifa za fedha za matumizi na mapato Mkuu wenu wa wilaya huyu hapa mleteeni taarifa hizo ili sheria ichukue mkopo kwa ajili ya kulea uzembe hata kidogo tunataka miradi ya maendeleo iliyokusudiwa kuwanufaisha wananchi ifanikiwe”,alisisitiza Mwanri.
 

WATU WASIOJULIKANA WAVAMIA SHAMBA DARASA KOROGWE.

August 05, 2013
Na Mwandishi Wetu,Korogwe

WATU wasiojulikana wamevamia na shamba darasa la mahindi lenye ukubwa wa zaidi ya Hekari 10 na kuvuna mahindi lishe zaidi ya magunia 100 ambayo serikali ilikuwa ikitumia shamba hilo kwa kuwaelimisha wananchi kuhusu mbinu bora za kilimo cha kisasa.

Wakizungumza katika shamba la utafiti lililopo eneo la Msambiazi wilayani Korogwe,baadhi ya watalaam wa kilimo na wakulima wanaohusika na utafiti huo wamesema hatua hiyo imekuwa ikizorotesha jitihada za utaoaji wa elimu ya kilimo cha kisasa kwa wakulima na wameomba hatua za makusudi kwa mamlaka husika kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo.

“Kusema kweli inashangaza sana kwani sisi wananchi tulishaanza kuona manufaa ya matumizi ya mbegu hii ya mahindi lishe kuanzia uaandaji wa shamba,kupanda,kupalilia na ilibaki kuvuna na imetuhamasisha sana kwamba mbegu hizi zinabeba mahindi makubwa na mazuri na kwa wakati muafaka sasa hawa wanaovuna kabla ya wakati sijui wana maana gani”,alisema Seleman Mbaruku Mkulima wa wilayani Korogwe.

 Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Halmashauri ya mji wilayani Korogwe Mwanaidi  Mfinanga akielezea ubora wa mahindi lishe alisema mahindi hayo yanavirutubisho vingi ambavyo huwasaidia zaidi watoto wadogo,watu walioathirika na virusi vya ukimwi ili kupata viini lishe .

“Laiti wangejua umuhimu wa mahindi haya wasingefanya uharibifu huu…mahindi haya yanakila virutubisho ambavyo mtoto mdogo anaweza kunywa uji wake bila kutia maziwa nah ii itasaidia sana kuondokana na tatizo la utapiamlo hasa kwa wananchi wale ambao hali zao ni duni hata katika upatikanaji wa mlo kwa siku “,alifafanua Mfinanga.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Halamashauri ya wilaya ya Korogwe Richard Komba akielezea hali ya chakula wilayani humo alisema uzao wa mwaka huu umeimarika na kwamba wataungana na wenzao waliovuna kwa wingi katika kusaidia kutoa elimu ya kilimo bora ili kuepuka baa la njaa mara kwa mara na kuomba chakula cha msaada .

“Kusema kweli kutokana na hali ya hewa kuwa nzuri kwa mwaka huu hali ya chakula pia itaimarika na tunaamini hakuna kijiji kitakachoomba chakula cha msaada ila hawa wenzetu ambao wanavamia na kuiba hadi mashamba darasa hilo sasa ni tatizo na watatuletea shida tusipokuwa makini”,alisema Komba.