Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa
cha Zanzibar Dkt Issa Haji Zidi akizungumza na vijana katika mjadala
kuhusu uzazi wa mpango katika uislamu ulioandaliwa na Kitengo cha
Shirikishi cha Afya ya mama na mtoto kwenye ukubi wa Chuo cha Mafunzo
Kilimani Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Sayansi
ya Afya ya Mbweni Asha Ali Khamis akionyesha moja ya dawa za kisasa za
uzazi wa mpango katika mjadala huo.
Mmoja wa washiriki wa mjadala
kuhusu uzazi wa mpango katika uislamu Dosa Omar Machano akitoa mchango
wake kuhusu umuhimu wa uzazi wa mpango.
Mshiriki wa mjada huo kutoka Mkoa
Kaskazini Unguja Asha Makame Mohd akichangia mada zilizowasilishwa.
Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia
mada zilizowasilishwa katika mjadala kuhusu uzazi wa mpango katika
uislamu uliofanyika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani.
………………………………………………………..
Na RAMADHANI ALI –MAELEZO ZANZIBAR
Mhadhiri na Mtafiti wa masuala ya
Kiislamu kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Dkt. Issa Haji
Zidi amesema Dini ya Kiislamu haipingani na uzazi wa mpango na
ulikuwepo tokea wakati wa Mutume Muahmmad hivyo amewashauri waislamu
kuzitumia kwa ajili ya kulinda afya zao.
Akizungumza katika mjadala kuhusu
uzazi wa mpango katika Uislamu ulioandaliwa na Kitengo Shirikishi cha
Afya ya uzazi na mtoto katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani, Dkt.
Zidi alisema lengo la uzazi wa mpango ni kulinda afya ya mama na mtoto
aliezaliwa kabla ya mtoto mwengine.
Alisema zipo njia za asili za
uzazi wa mpango zilizokuwa zikitumiwa na masahaba wakati wa Mtume
Muhammad lakini hivi sasa njia hizo zinaonekana kuwa ngumu kwa
watumiaji na zipo njia za kisasa ambazo ni salama na za uhakika zaidi.
Alisema tafiti zinaonyesha kuwa
familia nyingi, hasa za vijijini zenye kipato kidogo, ambazo
zinapinga mpango huo zimekuwa zikikabiliwa na matatizo ya kiuchumi na
afya na kupelekea wanaume kuwatelekeza wake zao.
“ Uzazi wa mpango ni makubaliano
ya mke na mume kutumia visaidizi katika uzazi ili kuchelewesha uzazi
kutokana na matatizo ya kiuchumi na kiafya na wala sio njia ya kuua ama
kupunguza watoto,” alisisitiza Dkt. Zidi.
Ameongeza kuwa lengo jengine la
uzazi wa mpango ni kulinda hadhi ya mwanamke na kuhofia kukosa utulivu
ndani ya nyumba kutokana na watoto wengi wasioweza kuhudumiwa.
Mwalimu wa chuo cha Sayansi ya
Afya Asha Ali Khamis alisisitiza umuhimu wa wazazi wawili kukubaliana
kunyonyesha mtoto miaka miwili na kupata mapumziko ya mwaka mmoja
kabla ya kuzaliwa mtoto mwengine.
Aliwaeleza washiriki wa mjadala
huo ambao wengi ni wanafunzi wa Vyuo vikuu vya Zanzibar, taasisi za
Serikali na NGO kwamba zipo njia za muda mfupi, muda mrefu na njia ya
kudumu na zote ni salama pamoja na baadhi ya watumiaji kupata
mabadiliko madogo madogo ya kimwili.
“Mabadiliko ya kiafya yanayotokea
kwa baadhi ya watu wanaotumia dawa hizi isiwe tatizo kwani mara nyingi
hutokea katika siku za mwanzo wakati mwili bado haujazoea, ” alisema
mwalimu Asha.
Akitoa takwimu za mama wanaopoteza
maisha wakati wa kujifungua Zanzibar , muwezeshaji kutoka UMATI
Mwanajuma Othman alisema kila wanawake laki moja 288 hufariki.
Alsema idadi hiyo ya vifo ni
kubwa ikilinganishwa na nchi nyengine hasa ikizingatiwa kuwa vifo hivyo
vinaweza kuepukika ikiwa hatua muafaka zitachukuliwa mapema.
Baadhi ya washiriki wa mjadala
huo walionyesha wazi wazi kuwa baadhi ya familia zimekuwa na mashaka
ya kutumia dawa za uzazi wa mpango kutokana na imani zao za dini na
kuhofia matatizo ya afya zao .