NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI ALIPOTEMBELA BANDA LA TPA

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI ALIPOTEMBELA BANDA LA TPA

January 16, 2024



Banda la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA limeendelea kuwa kivutio kwa Watembeleaji wa maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Zanzibar yanayoelekea ukingoni.

Mbali na unadhifu wa Banda linalopambwa na picha kubwa za Bandari mbalimbali, kivutio kingine ni mifano ya Meli na Vitendea kazi Bandarini ambavyo vinavutia kundi la Wanafunzi ambao hupenda kuja kwa wingi kujionea operesheni za kibandari zinavyofanyika.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPA Bw. Masanja Kadogosa, ni miongoni mwa Wageni Maarufu waliotembelea Banda hilo Wiki hii.


TANZANIA, ANGOLA ZASAINI HATI ZA MAKUBALIANO KUONGEZA USHIRIKIANO

January 16, 2024

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi leo Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakionesha Hati za Makubaliano ya Ushirikiano baada ya kuzisaini leo

Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya afya, Zanzibar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiwasilisha hotuba ya ufunguzi katika mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Angola, uliomalizika leo Zanzibar

Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António akichangia jambo katika mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Angola, uliomalizika leo Zanzib



Meza Kuu katika Pichay a pamoja, katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António. Wengine pichani ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (wa pili kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Zambia, anayewakilisha pia Tanzania nchini Angola, Mhe. Lt Gen Mathew Edward Mkingule (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje - Angola, Balozi Carlos Sardinha Dias (mwenye Kamba ya njano shingoni) na Balozi wa Angola nchini Tanzania, Mhe. Mhe. Sandro de Oliveira.




Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Angola zimesaini Hati tatu za Makubaliano ya Ushirikiano (MoUs) katika sekta ya mafuta na gesi, kuondoleana visa kwa wenye hati/pasi za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na ushirikiano katika sekta ya afya.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.), Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi Téte António wakati wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Angola uliomalizika leo Zanzibar.

Waziri Makamba amesaini hati mbili za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi na kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi. Aidha, Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amesaini hati ya ushirikiano katika sekta ya afya

Mara baada ya kusaini kwa Hati hizo, Waziri Makamba alisema Tanzania na Angola zina uhusiano wa kihistoria ulioanzishwa na viongozi wakuu wa Kitaifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Agostinho Neto walianzisha uhusiano huo kwa matarajio yao kuwa uhusiano huo utoe manufaa kwa nchi zote mbili.

“Leo kupitia mkutano wetu tumesaini Hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola. Hati hizo ni pamoja na hati ya makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi, Hati ya makubaliano ya kuondoleana visa/pasi kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za kikazi pamoja na hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta ya afya,” alisema Waziri Makamba.

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya uhusiano wa kisiasa, ulinzi, elimu, afya, mafuta na gesi, uchumi wa buluu, usafiri wa anga, kubadilishana visa, kusafiri bila visa kati ya nchi zetu mbili na hatimaye tumeingia makubaliano ya ushirikiano.

Kuadhalika, viongozi hao pia wamekubaliana kuyafanyia kazi masuala mbalimbali husasan uwepo wa ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya Kongamano la bishara na uwekezaji na kuziwezesha sekta binafsi kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano zaidi.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Balozi António amesema Angola imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) na kuelezea utayari wake wa kushirikiana katika nyanja walizokubaliana kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Tanzania na Angola ni marafiki wa siku nyingi, kupitia makubaliano tuliyosaini leo tumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa yetu, tuahidi kuyatekeleza yale yote tuliyokubaliana katika mkutano wetu ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu,” alisema Balozi António.

Aidha, kuhusu kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Luanda pamoja na kufanya kongamano la biashara na uwekezaji ili kuwawezesha wananchi wetu kubadilisha uzoefu na kuendelea kukuza sekta binafsi kwa mataifa yote mawili,” alisema Balozi António.




WANANCHI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA RED EYES

WANANCHI CHUKUENI TAHADHARI DHIDI YA RED EYES

January 16, 2024



Wizara ya afya imewaasa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa macho mekundu (Red eyes) Maambukizi ya Kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis” iliyoibuka nchini hivi karibuni.


Hayo yamesemwa leo Januari 15, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof Pascal Ruggajo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali Prof Tumaini Nagu wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa awali ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa kuathiri watu wengi nchini.


Prof. Ruggajo amesema dalili ya ugonjwa huo ni pamoja na macho kuwasha, kuchomachoma, kuuma, macho kutoa machozi na kutoa tongo tongo za njano.


"Taarifa za uchunguzi zinaonesha Maambukizi ya Kirusi hiki kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalamu “Viral Keratoconjunctivitis” ni maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa. Hakuna tiba maalumu kwa ugonjwa huu na hata bila tiba dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili". Amesema Prof Ruggajo.


Prof. Ruggajo amesema mwenendo wa ugonjwa huo unaonyesha kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wanaofika katika Vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wanasumbuliwa na ugonjwa huo. 


“Katika kipindi cha Desembe 22, 2023 hadi Januari 11, 2024 kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaosumbuliwa na ugonjwa huu kufika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya matibabu, kwa mfano katika mkoa wa Dar Es Salaam kuna wagonjwa wapya 869 huku hali ya kawaida katika kipindi cha mwezi Desemba 2023 kulikuwa na wagonjwa 17 pekee” amefafanua Prof. Ruggajo.


Aidha amesisitiza suala la usafi ni jambo muhimu katika kuzuia maambukizi kusambaa kwa wengine Kutokana na tabia ya ugonjwa huu kusambaa kwa kasi, maambukizi haya huleta mlipuko ambao husambaa kupitia kirusi kwa asilimia zaidi ya 80%.


Prof Ruggajo amewashauri wananchi kutokutumia dawa zisizo rasmi na ambazo hazijaandikwa na daktari kwa wakati huo na kutotumia dawa za macho anazotumia mgonjwa mwingine ili kuepuka madhara kwa kuwa dawa za macho ni tofauti na kwa matumizi tofauti.

SEKTA YA AFYA KUENDELEA KUWEKA KIPAUMBELE AJENDA YA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

SEKTA YA AFYA KUENDELEA KUWEKA KIPAUMBELE AJENDA YA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

January 16, 2024

 


Na. WAF - Dodoma


Sekta ya Afya kuendelea kuweka kipaumbele ajenda ya kupunguza vifo vya mama na mtoto katika vikao vinavyofanyika ngazi zote za Mkoa ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ikiwa ni malengo ya Taifa na Dunia. 


Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo Januari 15, 2024 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi chenye lengo la kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, mama na watoto.


“Kupunguza vifo vya mama na mtoto ni malengo ya Dunia lakini pia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni dhamira yake hivyo sisi watendaji wake ni lazima tupambane nayo kwa kumuunga mkono Rais na Dunia kwa ujumla.” Amesema Mh. Senyamule.


Amesema, ni vyema Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Kijiji awe anashiriki vikao vya kikanuni katika ngazi zote za Halmashauri ili aweze kutoa taarifa ya hali ilivyo juu ya vifo vinavyotokea pamoja na changamoto zake.


“Kama kuna mama mjamzito ambae hafiki katika vituo vya kutolea huduma za Afya tupate taarifa ili watendaji wa Wilaya na Kijiji wazidi kutoa rai na kuelimisha kupitia mikutano yao ya hadhara kwa wananchi.” Amesema Mhe. Senyamule.


Aidha, Mhe. Senyamule ametoa wito kwa Waganga Wakuu wa Wilaya kupeleka taarifa za Wilaya juu ya vifo vya mama na mtoto kila wiki katika ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kuondoa vifo visivyo na ulazima kwa kushirikiana na wataalamu.


Katika hatua nyingine, Mhe. Senyamule amesema Serikali imedhamiria kupunguza tatizo la Kansa ya Uzazi kwa wanawake hivyo amewahimiza akinamama kujitokeza kupima ili waweze kupata matibabu haraka kwa kuwa huduma hiyo inatolewa bila malipo.


Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Afya ya Uzazi Mama na Mtoto, Dkt. Ahmad Makuwani amesema Wizara ya Afya imeongeza kiwango cha watumiaji wa Vituo vya Afya wakati wa kujifungua na kufikia asilimia 81 ambapo 2016 tulikuwa na asilimia 63.


“Hii ina maana kwamba katika kila wajawazito 10, wajawazito 8 wanajifungulia katika Vituo vya kutolea huduma za Afya hivyo tumepunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 katika kila vizazi hai Laki Moja hadi vifo 104 katika kila vizazi hali Laki Moja ambavyo vimepungua kwa asilimia 80". Amesema Dkt. Makuwani.

VIFO VYA WATOTO WACHANGA VIMEPUNGUA KANDA YA KATI-RC SENYAMULE

January 16, 2024

 




Na Mwandishi wetu,Dodoma
Kanda ya kati imeendelea na jitihada za kupunguza vifo vya watoto wachanga NCHINI ambapo takwimu zinaonesha vifo vimepungua kutoka 1929 kwa mwaka 2021 hadi 1630 Mwaka 2023, licha ya vifo vya Uzazi  kuongezeka kutoka 151 mwaka 2021 Hadi vifo 165 mwaka 2023.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amebainisha hayo wakati akifungua Mkutano wa Afya ya Uzazi na mtoto wa Kanda ya kati wenye lengo la kupunguza vifo vya kina mama vitokanavyo na Uzazi na vifo vya watoto wachanga unaofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma.

"Takwimu zinaonesha kwa Kanda ya kati vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 1929 mwaka 2021 Hadi 1630 Mwaka 2023, vifo vya Uzazi vimeongezeka kutoka 151 mwaka 2021 Hadi vifo 165 mwaka 2023 hivyo mtumie fursa ya Mkutano huu kujadili kwa kina sababu ya vifo hivyo ili kuweka mikakati madhubuti ya kusaidiwa kupunguza vifo hivyo.

Mhe.Senyamule amewataka waratibu wa Afya ya Uzazi na mtoto wa Wilaya, Mikoa na Kanda kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia vifo vya kina mama vinavyotokana na Uzazi.

"Nachukua fursa hii kuwaomba mtumie Mkutano huu kupanga mikakati kabambe na mahsusi ya kuboresha huduma ikiwemo kusimamia uwajibikaji wa watumishi kwa kuzingatia kauli mbiu ya Mkutano huu 'UONGOZI NA UWAJIBIKAJI NI CHACHU KATIKA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI  NA VIFO VYA WATOTO ", amesema Senyamule

Aidha, Mhe. Senyamule ameweka wazi sababu zinazochangia vifo vya Uzazi ikiwa ni pamoja na kutokwa damu nyingi mara baada ya kujifingua, kifafa cha Mimba, kupasuka kwa Mji wa Uzazi na uambukizo mkali ambapo vifo hivyo vinaweza kuzuilika hivyo ni wajibu wa kikao hicho kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo ili kupunguza na kuzuia vifo vitokanavyo na Uzazi.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma ya Uzazi na mtoto Wizara ya Afya Dkt.Ahmed Makuhani amesema 81% ya vituo vya Afya vina majengo ya kujifungulia, wamefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na Uzazi kwa 80% pia kuhakikisha wanawekeza katika Uzazi wa mpango pamoja na kuhakikisha watoto wa like wenye umri wa Miaka 14 wanapatiwa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa 90%.

Mkutano huo wa Kanda ya kati umewajumuisha waganga wakuu wa mikoa na Wilaya, Wauguzi wakuu wa Mikoa na Wilaya, waratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto, wanafanyakazi wa Sekta ya Afya pamoja na wadau mbalimbali wa Huduma za Afya ya Uzazi na mtoto wa Kanda ya kati ambayo inajumuisha mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara pamoja na Wilaya zake zote.