TANZANIA YAPONGEZWA KUBORESHA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI, ALJAZEERA YAAHIDI KUTOA MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI TZ

October 22, 2023

 


Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma akiwa na Mkurugenzi wa Aljazeera Sami Elhag
#Tanzania yasifiwa kuboresha Mazingira ya Kazi kwa wanahabari na viongozi wa IFJ


Na: Mwandishi wetu. Arusha

maipacarusha20@gmail.com

Shirika la Utangazaji la kimataifa la Aljazeera limekubali , kushirikiana na Chama Cha wafanyakazi katika wa Vyombo vya habari nchini (JOWUTA) kutoa mafunzo kwa wanahabari ya usalama kazini na uandishi wa habari za uchunguzi.

Makubaliano hayo yalifikiwa katika mkutano wa ndani wa wanahabari Afrika , ulioandaliwa na shirikisho la kimataifa la waandishi wa habari Afrika (IFJ) ikiwa ni mfululizo wa vikao vya pembeni vinavyoendana na Kikao cha 77 Cha Tume ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu(ACHPR) ambavyo vinaendelea jijini Arusha.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Aljazeera wa masuala ya jamii na Haki za Binaadamu,Sami Elhag amesema aljazeera ipo tayari kusaidia wanahabari wa Tanzania ili kufanya kazi kwa ufanisi.

Elhag amesema miongoni mwa maeneo ambayo wataweza kusaidia ni mafunzo kwa wanahabari katika masuala ya usalama, jinsi la kuandika habari za uchunguzi lakini pia ya kuboresha Utendaji wa kazi na kubadilishana uzoefu..


Alisema wanahabari Duniani wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama na tayari kituo cha aljazeera wanahabari wake wamepatwa na changamoto mbalimbali.

Ahadi hiyo ya Aljazeera ilitolewa kutokana na maombi ya Mwenyekiti wa JOWUTA,Mussa Juma kuomba wanahabari nchini kupata fursa ya mafunzo na ziara za kubadilishana uzoefu.

Juma alisema, wanahabari wanakabiliwa na changamoto za kiusalama wakiwa kazini hasa wanapokwenda kuandika habari sehemu zenye migogoro, maslahi duni na lakini wengi hawana ujuzi wa kutosha wa uandishi wa habari za uchunguzi na Vita na kukabiliana na majanga.


Awali Katibu wa IFJ Louis Thomasi alisema wanahabari maeneo mengi Duniani wanakabiliwa na changamoto za kiusalama kazini lakini pia na uwepo wa sheria ambazo ni kandamizi.


Amesema kuna haja ya wanahabari kupatiwa mafunzo ya kiusalama lakini kupatiwa huduma muhimu ikiwepo maslahi na kuwepo sheria ambazo zitakuza Uhuru wa Vyombo vya habari na Uhuru wa kujieleza.

Thomasi alitaka Serikali barani Afrika kuwa na sheria rafiki ambazo zinasaidia wanahabari kufanya kazi vizuri na hivyo kuchangia ukuaji wa demokrasia na Maendeleo.

Awali Mwakilishi wa Shirika la kimataifa la A19, Alfred Bulakali alisema hakuna Demokrasia kwenye taifa lolote bila kuwepo Uhuru wa Vyombo vya habari na Uhuru wa kujieleza.

Bulakali alisema Uhuru wa Vyombo vya habari ni oxygen ya demokrasia hivyo ni muhimu serikali barani Afrika kutoa Uhuru kwa vyombo vya habari.


Tanzania yapongezwa kuboresha Uhuru wa Vyombo vya habari

Hata hivyo Tanzania ilipongezwa katika mkutano huo kutokana na kuendelea kuboresha Mazingira ya kufanya kazi kwa wanahabari ikiwepo kuendelea na maboresho ya sheria mbalimbali na kutoa Uhuru wa kujieleza na kukusanyika.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo , Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo Rodney Thadeus alisema serikali ya Tanzania imeboresha mazingira ya wanahabari kufanyakazi na Uhuru wa kujieleza.


Thadeus alisema Rais wa Tanzania,Dk Samia Suluhu Hassan mara baada ya kuingia madarakani alitaka kupitiwa sheria za habari na kuboresha zoezi ambalo linaendelea vizuri.


Alisema kwa wanahabari Tanzania wamehakikishiwa Uhuru wa kufanyakazi lakini pia kwa kutokana na maboresho ya sheria makosa ya kitaaluma.yameondolewa kuwa ya kijinai,kutakuwa na baraza huru la habari na kuanzishwa Mfuko wa kusaidia wanahabari kielimu.

"Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa habari katika maboresho ya sheria na serikali inawahakikishia mazingira mazuri wanahabari"alisema

Akizungumza maombi ya mafunzo kwa wanahabari yaliyotolewa na JOWUTA , Thadeus alitaka mafunzo hayo kuhusisha pia maafisa habari wa Serikali.

"Suala la mafunzo na kubadilishana uzoefu linapaswa pia kuwafikia maafisa habari ambao ndio wanafanya kazi na waandishi lakini pia wengi wao ni waandishi na watangazaji ambao wanahitaji pia mafunzo",amesema.

Wakili Mary Mwita na Wakili Mgusuhi Maswi kutoka Mawakili wa Umoja wa Pan Afrika( PALU ) wakitoa mada zao walisema ni muhimu wanahabari kufanyakazi katika mazingira Salama wakiwepo Wanahabari wanawake ambao wamekuwa waathirika wa ukatili katika vyombo vya habari.


Wakili Mwita alisema, waandishi wanahabari wamekuwa wahanga wa ukatili hivyo ni muhimu kuendelea kujengewa uwezo lakini pia kuwepo na sheria ambazo zinawalinda.

Katibu wa Umoja wa waandishi wa habari nchini Kenya,(KUJ) Erick Oduor alisema ni muhimu kuwepo na muongozo katika kusimamia masuala ya Ulinzi na Usalama kwa wanahabari.


"Kenya tayari tunamuongozo na tupo tayari kushirikiana na JOWUTA na wadau wengine kuwepo na muongozo kama huo katika nchi zao ili kuboresha Utendaji kazi kwa wanahabari"alisema.

Akifunga mkutano huo Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa ,Mussa Juma aliwapongeza wanahabari kutoka nchi mbalimbali kushiriki mkutano huo na kuwahakikishia watafurahi amani na Utulivu wa Tanzania.


"Mkutano wetu umekuwa mzuri sana tumejadiliana mambo muhimu kuboresha sekta ya habari Afrika lakini kubwa zaidi nashukuru Aljazeera kukubali kuja kusaidia wanahabari wa Tanzania"alisema.


Juma alipongeza serikali ya Tanzania kwa kuboresha Mazingira ya wanahabari kufanyakazi tofauti na nchi nyingine na kuahidi JOWUTA itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wa habari kuhakikisha wanahabari wanafanya kazi katika mazingira Salama.

WAZIRI NCHEMBA AZINDUA MFUMO WA GPSA

October 22, 2023

 Na Mwandishi wetu - Dodoma



Matumizi sahihi na salama ya mifumo ya kieletroniki Serikalini, yametajwa kuwa suluhisho la kudumu katika kuziba mianya ya upotevu wa rasilimali za serikali ikiwemo mapato yatokanayo na vyanzo mbalimbali nchini.

Hayo yameelezwa jana jijini Dodoma na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba, wakati akipokea na kuzindua Mfumo wa Kieletroni wa Kuratibu Ununuzi wa Mafuta Serikalini, ujulikanao kama ‘GPSA Intergrated Management Information System’ (GIMIS), kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene.

Alisema kuwa, matumizi ya mifumo imara ya kielektroniki yanasaidia kuondoa mianya ya upotevu wa rasilimali za Serikali na kudhibiti watumishi wasio waadilifu, kwakuwa malipo yote ya serikali yatalipwa kupitia njia sahihi na salama katika taasisi husika.

“Tukifanya kazi kupitia mifumo ya kielektroniki tunapunguza makosa mengi ya kibinadamu, hivyo matumizi sahihi ya mifumo hii yatatuwezesha kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu ikiwa ni pamoja na eneo la ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya serikali”, alifafanua Dkt.Mwigulu.


Akieleza kuhusu mfumo huo Dkt. Mwigulu alisema kuwa, mfumo wa GIMIS unatumiwa na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), ambapo kwa sasa majukumu yote ya Wakala yanatekelezwa kupitia mfumo huo ambao umesaida kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, Dkt. Mwigulu aliielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuhakikisha inaunganisha mfumo wa Manunuzi Kielektroni (NeST) na mfumo wa GIMIS kwa kuwa, mfumo huo unatumiwa na Wizara, Mashirika ya Umma, Wakala, Ofisi za Mikoa na Halmashauri za Wilaya nchini katika kupata huduma za GPSA.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alisema kuwa, lengo la mfumo huo ni kurahisisha utendaji kazi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), katika uuzaji wa mafuta Serikalini, ili kuweka uwazi na kutunza kumbukumbu za matumizi ya mafuta katika kila taasisi ya umma.

Alisema kuwa, hadi sasa zaidi ya taasisi nunuzi 7070 zinatumia mfumo huo ambapo, taarifa za matumizi ya mafuta kwa kila taasisi zinatunzwa katika mfumo huo na kusaidia katika uandaaji na usimamizi wa mipango ya bajeti ya ofisi, pamoja na udhibiti wa matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma.
“Lengo la mfumo huu ni kuhakikisha matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma na kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea kutokana na kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi za matumizi ya mafuta”, alisisitiza.

Aliongeza kuwa, kupitia mfumo huo, Serikali inaweza kufahamu kiasi cha mafuta yaliyotumika na yaliyobaki, magari yaliyopatiwa mafuta, muda, mahali na tarehe na hivyo kuziwezesha taasisi husika kuweza kudhibiti matumizi ya mafuta ikiwa ni pamoja na kuondoa udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu.

Aidha, katika utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuunganisha mifumo ya TEHAMA Serikalini, Simbachawene alisema kuwa, Mfumo huo umekwishaunganishwa kwenye mfumo mkuu wa Serikali wa kuwezesha mifumo kubadilishana taarifa (GovESB), na umeshaanza kubadilishana taarifa na mifumo ya baadhi ya Taasisi za Umma kama vile mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali (GePG) pamoja na mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali za Taasisi (ERMS).


Mfumo wa GIMIS umesanifiwa na kujengwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kwa kushirikiana na Ofisi ya Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GP .





TAMWA – ZNZ YAOMBA MKAKATI WA KITAIFA KUBADILISHA TABIA KWA VIJANA

TAMWA – ZNZ YAOMBA MKAKATI WA KITAIFA KUBADILISHA TABIA KWA VIJANA

October 22, 2023

 

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kinashauri kuandaliwa kwa mkakati wa kitaifa wa kubadilisha tabia za vijana ili kuwanusuru na kutumbukia katika vitendo vya udhalilishaji.

Kwa mujibu wa Afisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar kuanzia Julai mpaka Septemba, 2023 ni kwamba watu 24 wamekutwa na hatia mahakamani kwa kufanya makosa ya udhalilishaji na kupewa adhabu za vifungo (kwa Zanzibar huitwa vyuo vya mafunzo) ambapo asilimia 58.3 ni vijana wa umri wa 18-29.

Hii ni kwamba, vijana wamekua wakijihusisha sana na masuala ya udhalilishaji na hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili kuwabadilisha mawazo ili kutotumbukia katika majanga haya kwa maslahi yao, watoto na nchi kwa jumla.

Takwimu hizo pia zinaonesha watu ambao bado wapo mahabusu kesi zao zinaendelea ni 48 ambapo kundi hilo la miaka 18 hadi 29 pia linaongoza ambalo linafanya asilimia 54.

Tunaishauri Serikali kuandaa mkakati wa kuelimisha vijana kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo viwanja vya michezo, skuli lakini pia kutoa taaluma kwa wazazi na walezi jinsi ya kuwafahamisha watoto wa kiume namna ya kuheshimu watoto wa kike, wanawake na watoto kwa jumla.

Takwimu pia zinaonesha kuwa masuala hayo ya udhalilishaji yanawaathiri watoto zaidi ambapo katika matukio 157 kwa mwezi Julai hadi Septemba yaliyoripotiwa, watoto ni 122 sawa na asilimia 77 katika maeneo kadhaa hasa kubakwa, kakashifiwa na kulawitiwa.

TAMWA ZNZ pia inawashauri sana vijana kushtushwa na taarifa hizi na hivyo kujipangia mipango madhubuti ya kutokuingia katika vitendo hivi ikiwemo kuacha kufuata vishawishi, kutokuendekeza mihemuko na pia kujidhibiti dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao.

Ni vyema vijana wakaelewa kuwa katika vijana hao waliotiwa hatiani wengi wao wamehukumiwa kutumikia adhabu ya miaka 11 na zaidi hivyo kupoteza kipindi kirefu cha nguvu zao katika vyuo vya mafunzo badala ya kutumia kujipanga na maisha yao.

TAMWA ZNZ pia imefarijika sana na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoa takwimu zinazoonyesha mgawanyiko wa umri wa waliofanya uhalifu ikiwemo makosa ya udhalilishaji.

Utoaji huu wa takwimu utasaidia kujua umri wa wafanyaji wa makosa mbalimbali na hivyo kuona jinsi gani nchi inaweza kujipanga katika kubadilisha tabia za makundi yaliyo hatarishi zaidi.

RAIS DKT. SAMIA SHUHUDIA UTIAJI SAINI UWEKEZAJI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM

RAIS DKT. SAMIA SHUHUDIA UTIAJI SAINI UWEKEZAJI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM

October 22, 2023

 



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali kwenye hafla ya Utiaji saini Uwekezaji na Uendeshaji wa Sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.
 Waziri wa Uchukuzi Mhe. Makame Mbarawa akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Godius Kahyarara wakitia saini Mkataba wa Nchi Mwenyeji baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai iliyowakilishwa na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Sultan Ahmed bin Sulayem kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Makame Mbarawa akipongezana na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Sultan Ahmed bin Sulayem mara baada ya kusaini Mkataba wa Nchi Mwenyeji baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA) Plasduce Mbossa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA Mhe. Balozi Ernest Mangu wakitia saini Mkataba wa Uendeshaji wa Gati namba 4 mpaka 7 za Bandari ya Dar es Salaam kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.

 Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA Mhe. Balozi Ernest Mangu akipongezana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DP World ya Dubai Sultan Ahmed bin Sulayem mara baada ya kusaini Mkataba wa Uendeshaji wa Gati namba 4 mpaka 7 za Bandari ya Dar es Salaam kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA) Plasduce Mbossa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA Mhe. Balozi Ernest Mangu wakitia saini Mkataba wa Uendeshaji wa Gati namba 4 mpaka 7 za Bandari ya Dar es Salaam kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA) Plasduce Mbossa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA Mhe. Balozi Ernest Mangu wakitia saini Mkataba wa upangishaji wa Gati namba 4 mpaka 7 za Bandari ya Dar es Salaam pamoja baina ya Kampuni ya DP World ya Dubai iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Sultan Ahmed bin Sulayem kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.      

Viongozi mbalimbali pamoja na wageni waliohudhuria hafla ya Utiaji saini Uwekezaji na Uendeshaji wa Sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.