WAZALISHAJI WA CHUMVI MTWARA WATAKIWA KUZALISHA CHUMVI KWA KUZINGATIA VIWANGO

November 01, 2023

 


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas akizungumza wakati akifungua Mafunzo  kwa wadau wa chumvi kutoka katika Mkoa wa Mtwara leo Novemba 1,2023.

****************

WAZALISHAJI wa Chumvi mkoani Mtwara wametakiwa kuendelea kuzalisha na kufungasha chumvi iliyo bora kwa kuzingatia viwango, ubora na usalama ili kulinda afya ya mlaji pamoja na kupata masoko mengi ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa leo Novemba 1,2023 na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas wakati akifungua mafunzo kwa wadau wa chumvi kutoka katika Mkoa wa Mtwara.

Amesema mafunzo hayo yametokana na maombi ya wadau hao kupitia vikao mbalimbali vya kamati jumuishi ya kutatua changamoto za sekta ya chumvi nchini. Vikao hivyo vilijumuisha taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na TBS.

"Mafunzo haya yamekuja kwa wakati muafaka ambapo Serikali imeazimia kwa dhati kuendeleza viwanda ili kutoa ajira katika kada mbalimbali pamoja na kuziwezesha bidhaa zetu kushindana katika masoko ya ndani, kikanda na ya kimataifa ". Amesema

Aidha ameipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa maandalizi mazuri ya mafunzo na ameomba utaratibu wa kufanya mafunzo kama hayo kwa wadau wa chumvi uwe endelevu.

Pamoja na hayo amesema kuwa azma ya serikali ni kukuza sekta ya viwanda ili tuweze kujitosheleza katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Kwa upande wake Meneja wa kanda ya kusini (TBS), Mhandisi Saidi Mkwawa amesema lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha wadau wa chumvi wanakuwa na uelewa na kuzalisha chumvi iliyokidhi ubora.

‘Katika mafunzo haya tumewashirikisha pia wadau muhimu ambao ni TIRDO na SIDO ili kuhakikisha elimu hii inakuwa na tija zaidi na mwisho wa siku muweze kuzalisha bidhaa bora’ alisema Mkwawa.

Mafunzo haya yatafanyika pia mkoani Lindi siku ya kesho Novemba 2,2023
Meneja wa TBS kanda ya kusini Mhandisi Said Mkwawa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wadau wa chumvi kutoka katika Mkoa wa Mtwara leo Novemba 1,2023.

PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI (AFDP) YASAIDIA WAKULIMA KUKABILIANA NA ATHARI ZITOKANAZO NA MABADILIKO YA TABIA NCHI.

November 01, 2023

Mtaalamu wa Masuala ya Ufuatilia na Tathmini Bw. Bernard Ulaya kutoka katika Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) akizungumza wakati Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa maendeleo ya Kilimo (IFAD) Ulipotembea Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Nchini Mkoani Arusha (TOSCI).

Mtaalamu wa masuala ya Lishe na Jinsia kutoka Mfuko wa Kimataifa wa maendeleo ya Kilimo (IFAD) Bi. Florence Munyiri akizungumza mbele ya wataalamu hawapo katika picha, mara Ujumbe huo kutoka IFAD ulipotembelea Taasisi ya Tafiti za Mbegu za Kilimo (TARI) Seriani Arusha.


Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD),na wataalamu wakiwa katika kikao na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bw. Missaile Albano Musa, kabla ya Ujumbe huo kuanza ziara ya kutembelea baadhi ya Taasisi za Kilimo zinazotekeleza Programu ya kuelendela Kilimo na Uvuvi (AFDP) Mkoani humo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Bw. Missaile Albano Musa,na Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD),na wataalamu kabla ya Ujumbe huo kuanza ziara ya kutembelea baadhi ya Taasisi za Kilimo zinazotekeleza Programu ya kuelendela Kilimo na Uvuvi (AFDP) Mkoani humo.

NA; MWANDISHI WETU – ARUSHA

Imeelezwa kuwa, Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) imesaidia wakulima katika kufahamu na kutumia njia bora za kilimo cha kisasa zitakazowapelekea kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya Tabianchi.

Akizungumza wakati Ujumbe kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo (IFAD)ulipotembelea kituoni hapo Novemba 1 mwaka huu , Mtafiti kutoka Taasisi ya Tafiti za Mbegu Nchini (TARI) tawi la Seriani Arusha Bw. Shida Nestory amesema, Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi zake za Tafiti za Kilimo, (TARI) Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar, umesaidia wakulima katika kufahamu na kutumia njia bora za kilimo cha kisasa.

TARI Seriani Mkoani Arusha inatekeleza kupitia zao la maharage na Mahindi ambapo kwa mazao yote mawili mradi umewasiaidia kuwafikia wakulima ambapo mabwana shamba wanapewa mafunzo ya namna ambavyo wakulima wawaweza kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi kupitia teknolojia mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya aina za mbegu mbazo zinaweza kustahimili kwenye maeneo ya ukame.

“Tari inawaelimisha wakulima juu ya matumizi ya teknolojia ya kuvuna maji na kuwa na uhakika wa kulima katika misimu tofauti na matumizi ya mbegu bora ambazo zinaweza kukinzana na magonjwa.” Alisisitiza

Kwa Upande wake Mtaalamu wa masuala ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka katika Programu hiyo inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Bw. Bernard Ulaya alisema, Lengo la Timu hii ya IFAD kufanya ziara katika taasisi hizo ni kuangalia maendeleo ya program, mafanikio, changamoto zilizopo ili kama kuna maeneo yanayoweza kuboreshwa yaboreshwe.

“katika kituo cha Seriani program imeweza kuwasaidia kuwa na kitalu Nyumba mbacho kitaweza kuwasiaidia katika tafiti zao za kuweza kuzalisha mbegu mama na mbegu kwa matumizi ya wakulima.” Alifafanua

Wageni hao kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) pamoja na wataalam watatembelea maeneo hayo ya Kilimo katika Mikoa ya Arusha, Manyara Tabora, Morogoro na Dodoma kwa Upande waTanzania Bara Pamoja na Sekta ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu katika baadhi ya mikoa ya Unguja na Pemba.
PROFESA JAMAL ATOA SHULE KUHUSU MABADILIKO YA TABIA NCHI

PROFESA JAMAL ATOA SHULE KUHUSU MABADILIKO YA TABIA NCHI

November 01, 2023

 

John Bukuku


Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Prof. Jamal Katundu amesema ongezeko kubwa la watu na kukua kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi hapa nchini linatarajiwa ama linatishia kupunguza kiwango cha upatikanaji wa maji kwa mtu na kufikia mita za ujazo 883 ifikapo mwaka 2035.
Amesema hayo wakati wa warsha ya wadau kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ustahimilivu katika maeneo ya nchi.
Prof. Jamal amesema hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi kwa maeneo kame ya nchi kama hakutakuwa na mikakati mathubuti ya kukabiliana na tabianchi

Amesema kwa mkoa wa Dodoma ambao ni makao makuu ya nchi, kustawi kwa kuongezeka kwa idadi ya watu na kukua kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na za kijamii kumeisukuma Wizara ya Maji kuendelea na utekelezaji wa mipango mbalimbali ili kuwezesha upatikanaji wa vyanzo vya maji safi.

Prof. Jamal amepongeza watekelezaji wa Mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ustahimilivu katika nyanda kavu za kitropiki kupiitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Wizara ya Maji
Utekelezaji wa mradi utawawezesha kuunganisha wataalam wa Wizara ya Maji kupitia kituo Mahiri cha Rasilimali za Maji na watafiti wabobezi kutoka SUA, na nchi za Uingereza, India na Niger.

PILSNER LAGER SASA NI MDHAMINI MKUU WA SIMBA SC

November 01, 2023


"Kampuni inayoongoza ya kuzalisha bia, Serengeti Breweries Limited (SBL), imesaini makubaliano ya miaka mitatu kudhamini Klabu ya Michezo ya Simba ambapo klabu hiyo itapokea ufadhili wa shilingi bilioni 1.5 kutoka kwa kampuni kupitia bia yake - Pilsner Lager.


Awali ilikuwa mdhamini mkuu wa Taifa Stars hadi katikati ya mwaka huu na sasa ni mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Taifa ya Tanzania kupitia bia yake nyingine, Serengeti Premium Lite. Ahadi ya SBL ya kusaidia soka nchini Tanzania inaendelea kukua kwa kasi.

"Wakati fursa ya kudhamini Simba SC ilijitokeza, tulihisi wajibu na fahari kubwa katika kutoa msaada wetu kwa moja ya vilabu bora vya Tanzania, ambavyo vinajulikana kwa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki nchini. Leo, tunafuraha kutangaza makubaliano ya udhamini ya miaka 3 na Simba SC kupitia bia yetu bora, Pilsner Lager.

Tuna dhamira ya kutoa rasilimali muhimu kwa Simba Sports Club ili kufikia mafanikio makubwa zaidi. Ushirikiano huu unazidi kuwa zaidi ya kukuza tu bidhaa zetu; ni kuhusu kuendeleza urithi unaovuka vizazi," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, alipoanzisha udhamini huo leo.

Mkurugenzi Mtendaji pia alieleza shukrani zake kwa TFF kwa dhamira yao isiyo na kifani ya kusaidia vilabu vya mpira wa miguu nchini Tanzania na michezo kwa ujumla, na kuhakikisha dhamira hiyo hiyo kutoka kwa udhamini wa Serengeti Breweries Limited kwa Simba SC kupitia chapa yake ya bia ya Pilsner Lager.

"Udhamini huu umekuja wakati muafaka wa kupunguza baadhi ya vikwazo vya kifedha tulivyonavyo katika klabu yetu ambavyo vimezuia utekelezaji wa baadhi ya mikakati ya kimkakati. Udhamini huu pia bila shaka utaiwezesha klabu yetu kufanya vizuri katika ligi ya kitaifa na pia katika Ligi ya Mabingwa ya Afrika," alisema Imani Kajura.

SBL ni mdhamini mzoefu wa mpira wa miguu nchini Tanzania, akiwa ameanzisha mkataba wa miaka minne na Taifa Stars kuanzia 2017 hadi 2011, na kisha miaka sita ya kuwasaidia timu ya taifa ya soka kuanzia 2017 hadi Juni 2023. Katika muda wa miaka kumi, Taifa Stars imefanikiwa kufuzu mara kadhaa kwa Kombe la Mataifa ya Afrika na kuboresha nafasi yake katika viwango vya FIFA.






PROF. KABUDI AWAFUNDA VIONGOZI VIJANA UMUHIMU WA KISWAHILI PAMOJA NA HISTORIA YA HARAKATI ZA UKOMBOZI KUSINI MWA AFRIKA

November 01, 2023

 


Prof Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb) ameshiriki Kutoa Mafunzo ya uongozi kwa Viongozi Vijana kutoka UWT na UVCCM, ambapo Leo tarehe 01 Novemba katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere amewafunza viongozi Vijana Umuhimu wa Lugha ya Kiswahili na namna Lugha yetu ilivyotumika kipindi cha Harakati za Kupigania Uhuru wa Nchi za Kusini mwa Afrika.

Pia Prof. Kabudi amewafunza namna Mwalimu Nyerere alivyopambana kuhakikisha Tanzania tunakuwa wa moja kama nchi licha Kutofautina Makabila na kutufanya nchi za Africa kwa Pamoja kuzungumza lugha moja ya Kiswahili.

Mafunzo haya ya viongozi vijana 50 kutoka UWT na UVCCM yenye lengo la kuwaanda viongozi vijana ambao watakwenda kulitumikia taifa Pamoja chama na kuwafanya Vijana hao Kuwa Mabalozi wazuri kwa kuwafundisha vijana wenzao elimu waliyoipata kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha, Mkoa wa Pwani.




RAIS WA UJERUMANI KUKUTANA NA FAMILIA ZA MASHUJAA WA VITA YA MAJIAMAJI

RAIS WA UJERUMANI KUKUTANA NA FAMILIA ZA MASHUJAA WA VITA YA MAJIAMAJI

November 01, 2023

 



Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Dkt. Frank Walter Steinmeier Novemba 1, 2023 amewasili Uwanja wa Ndege wa Songea Mkoani Ruvuma kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani hapo.

Rais Mhe. Dkt. Steinmeier amepokelewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Songea Mjini Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Viongozi wa Serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.

Akiwa mkoani hapo Mhe. Steinmeier atatembelea Makumbusho ya Mashujaa waliopigana vita ya Majiamaji pamoja na kukutana na familia za waliopigana vita hiyo.

       

UZALENDO KIGEZO KUSIMAMIA DAWATI LA KUPINGA UKATILI VYUONI: SERIKALI

November 01, 2023


Na WMJJWM Iringa

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amewataka Wakuu wa vyuo Vya Elimu ya Juu na Kati kuteua Waratibu Dawati la Jinsia waadilifu, katika kutatua changamoto za ukatili wa kijinsia vyuoni.

Mpanju amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya namna bora ya uanzishaji wa madawati ya jinsia kwa Wakuu wa Vyuo na Waratibu Madawati ya Jinsia katika taasisi ya elimu ya juu na elimu ya kati Mkoani Iringa Oktoba 31, 2023.

“Nasisitiza uwezeshwaji wa Madawati hayo ya Jinsia kwa kutumia Rasilimali za Serikali au kupitia wadau kuhakikisha madawati haya yanafikika kiurahisi kwa kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano ya utoaji wa taarifa za ukatili wa kijinsia," amesema Mpanju.

Mpanju ameelekeza wajumbe wa Madawati ya Jinsia kuendesha Elimu ya kutokomeza matendo ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi na wanajamii ndani ya Vyuo husika kwani kutokomeza matendo ya ukatili na unyanyasaji kwa wakati kwenye taasisi za Elimu ya juu na ya kati ndio lengo mahsusi la kuundwa kwa madawati hayo.

"Nitoe rai kwa vyuo vya elimu ya juu na kati kuhakikisha wanaanzisha ‘Madawati ya Jinsia’ katika vyuo vyao kwa kutumia Mwongozo wa Uanzishaji, Uendeshaji na Ufuatiliaji wa Dawati la Jinsia wa mwaka 2021 ambao ulishatolewa na unapatikana pia katika tovuti ya Wizara.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Cyril Komba akifafanua mwongozo wa Dawati la Jinsia kwenye Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya Kati amesema majukumu yake ya msingi ni kuona ukatili unakomeshwa.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais - utumishi Staricko Meshack akitoa mafunzo kuhusu Daftari la Usajili wa matukio ya ukatili wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu na kati amesisitiza kutumika kwa madaftari hayo.



TADB YAADHIMISHA MWEZI WA SARATANI YA MATITI KWA ELIMU NA VIPIMO KWA WANAFANYAKAZI WAKE

November 01, 2023

 Na Mwandishi Wetu


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendesha semina ya mafunzo ya uelewa wa saratani ya matiti , saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, saratani ya tezi dume na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa wafanyakazi wake.

Semina hiyo iliyoambatana na upimaji kwa wafanyakazi hao, iliendeshwa kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kukabiliana na Saratani nchini.

Akiongea wakati wa semina hiyo, Mkuu wa rasilimali watu na utawala wa TADB Bi. Noela Ntunkamazina alisema kuwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, (ORCI) TADB wameungana na mataifa mengine kuwaongezea uelewa wa saratani mbalimbali wafanyakazi wake mwezi Oktoba ambao unatambulika kama mwezi wa kuongeza uelewa wa Saratani ya matiti.

“Kwa kutambua kuwa saratani ni ugonjwa unaoathiri jinsia zote na kwa kuelewa kuwa kupitia upimaji wa afya mara kwa mara saratani hugundulika mapema na hivyo kwa kupata tiba sahihi muathirika huweza kupona, kama TADB tumeona vyema kuwapa wafanyakazi wetu fursa ya kupata elimu na kupima ilikufahamu hali zao za kiafya,” alisema.

Daktari Bingwa magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Sadiq Siu alibainisha kuwa saratani ya matiti ni saratani ya pili inayoongoza kwa vifo vya wanawake nchini ikitanguliwa na saratani ya shingo ya uzazi. Pia alibainisha kuwa saratani ya matiti inaathiri siyo tu wanawake bali hata wanaume.

“Naipongeza TADB kwa kuona umuhimu wa kuwaletea wafanyakazi wake fursa hii muhimu ya kupata uelewa wa saratani mbalimbali na pia kupata nafasi ya kupima saratani ya matiti, saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya tezi dume. Ni jambo muhimu kwa taasisi nyingine kuiga na kuwaelimisha wafanyakazi wake. Kwa pamoja tunajukumu la kuchangia kupunguza vifo vitokanavyo na saratani. Ugonjwa huu unakua kwa kasi. Ikumbukwe kuwa kwa kugundulika mapema na kuzingatia matibabu sahihi, saratani inaweza kutibika.

Bi. Felister Rutta mmoja wa wafanyakazi wa TADB aliishukuru menejimenti ya benki hiyo kwa kuwaletea semina hiyo ambayo alisema itawasadia wanyakazi kuufahamu ugonjwa huo na hivyo kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza ndugu jamaa na marafiki.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Sadiq Siu (wa kwanza kushoto aliyesimama)akitoa mada juu ya saratani ya matiti, saratani ya mlango wa shingo ya kizazi na saratani ya tezi dume kwa wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ikiwa ni sehemu ya benki hiyo kuadhimisha mwezi wa saratani ya matiti kwa kutoa elimu kwa wafanyakazi wake pamoja na kuwafanyia vipimo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) wakifuatilia kwa makini mada juu ya saratani ya matiti, saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, saratani ya tezi dume iliyokuwa ikitolewa na Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Sadiq Siu ikiwa ni sehemu sehemu ya benki hiyo kuadhimisha mwezi wa saratani ya matiti kwa kutoa elimu kwa wafanyakazi wake pamoja na kuwafanyia vipimo.






TANZANIA – UJERUMANI KUJIKITA ZAIDI KATIKA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI

November 01, 2023

 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani zimeeleza dhamira yao ya kujikita zaidi katika kuendeleza na kukuza ushirikiano wa kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya pande zote mbili.

 

Hayo yamebainishwa na Viongozi Wakuu wa mataifa hayo mawili rafiki, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza katika mkutano huo Rais Samia ameeleza kuwa licha ya Tanzania na Ujerumani kuwa ushirikiano mzuri na wa muda mrefu katika shughuli mbalimbali za maendeleo hususani katika sekta ya Afya, elimu, usambazaji wa maji safi na salama, hifadhi ya mazingira, ulinzi na usalama, haki za binadamu na utawala bora na hifadhi ya maliasili  bado kuna fursa kubwa ya kukuza zaidi ushirikiano wa kibiashara na uchumi kwa manufaa ya watu wa pande zote mbili. 

 

 “Katika mazungumzo yetu tumeelekeza timu za pande zote mbili kukaa na kufanya majadiliano ya mara kwa mara ili kubaini maeneo mapya ya ushirikiano ambayo yatatusaidia kupiga hatua kwa haraka zaidi katika kukuza biashara na uwekezaji kwa manufaa ya watu wetu” Alisema Rais Samia. 

 

Katika hatua nyingine Rais Samia ameeleza kuwa katika mazungumzo na mgeni wake Rais Frank-Walter Steinmeier wamekubaliana kufungua majadiliano katika masuala kadhaa ya kihistoria ikiwemo kuhusu suala la mabaki ya kale ya Tanzania yaliyohifadhiwa nchini Ujerumani. 

 

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier ameeleza kuwa Ujerumani itaendelea kufungua milango ya ushirikiano zaidi kwa Tanzania katika kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya sasa na vizazi vijavyo. 

 

“Ujerumani tutatendelea kujikita katika kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo kuongeza nguvu ya kusaidia maendeleo ya nishati jadilifu nchini Tanzania na uchumi wa kidijiti ambao utatengeneza ajira nyingi zaidi kwa vijana. Tunafanya haya yote tukiamini kuwa  hatusherekei urafiki wetu pekee bali maendeleo ya kiuchumi” Alieleza Rais Frank-Walter Steinmeier

 

Mbali masuala ya biashara na uchumi Rais Frank-Walter Steinmeier ameipongeza  Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na  Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa hatua kubwa iliyopiga katika kuboresha mazingira ya Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala Bora. 

 

Rais Frank-Walter Steinmeier ametumia fursa hiyo kuzishukuru familia za wahanga wa Vita vya Majimaji za jijini Songea kwa kumwalika kuzitembelea huku akieleza kuwa ni faraja kubwa kwake ikiwa ni mwendelezo wa ishara ya utayari wa kusonga mbele pamoja licha ya yaliyojiri katika historia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier wakizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuhitimisha mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam

 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akizingumza na waandishi wa habari kuelezea yaliyojili kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier Ikulu jijini Dar es Salaam

 Rais wa Jamhuri ya Washirikisho la Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier akizingumza na waandishi wa habari kuelezea yaliyojili kwenye mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Ikulu, jijini Dar es Salaam

 Waziri wa Utalii na Mambo ya kale Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said akifuatilia mkutano kati ya Rais Samia na Rais wa Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier na waandishi wa habari uliokuwa ukuiendelea Ikulu jijini Dar es Salaam