KITOKOLOLO RAPA WA FM ACADEMIA AHAMIA BENDI YA MASHUJAA

KITOKOLOLO RAPA WA FM ACADEMIA AHAMIA BENDI YA MASHUJAA

June 16, 2014

…………………………………………………………………….
BENDI ya Mashujaa imemchukua rapa, Kalidjo Kitokololo ‘Kuku’ kutoka bendi ya  FM Academia na kusaini naye  Mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza kwenye ukumbi wa Milenium Business  Park leo , Kijitonyama, Dar es Salaam Mkurugenzi wa Mawasiliano wa bendi hiyo, Maximillian Luhanga amesema  kupatikana kwa  Chitokololo ni furaha kubwa kwao.
“Kalidjo anakuwa rapa wa tatu katika bendi ya Mashujaa , baada ya Saulo John maaurufu  Ferguson na Sauti ya Radi, ambao wote ni wakali, kwa marapa hao wote tunaamini bendi yetu itakuwa inatisha sana,”amesema Luhanga.  
Maxmilian Luhanga  amesema Kitokololo anaanza kazi mara moja baada ya kusaini mkataba mpya.
Kwa upande wake, Kitokololo mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amesema  amekuja Tanzania kutafuta maisha na Mashujaa imempa ofa nzuri ndiyo maana amejiunga na bendi hiyo.
Amesema ameondoka vizuri FM Academia akiwa amewaaga vizuri wenzake ambao wameridhia kuondoka kwake.
  Kitokololo amesema kwamba amejiunga na Mashujaa akimfuata  King Dodo  ambaye kimuziki ni baba yake , King Dodoo  ndiye aliyemleta nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Mashujaa itamtambulisha rasmi mwanamuziki huyo katika onyesho maalum litakalofanyika ukumbi wa Letasi Lounge Ijumaa wiki hii.
Mashujaa pia wanatarajiwa kuwa na ratiba ndefu mara baada ya mfungo mtukufu wa ramadhani ambapo Maximillian Luhanga amewaambia mashabiki wa bendi hiyo nchini kote kukaa mkao wa kula, Kwakuwa bendi hiyo itakuwa na ziara karibu mikoa yote ya Tanzania ili kutoa burudani kwa mashabiki wao.
Waziri Mkuchika: Tanzania ni nchi ya pili Afrika Mashariki kwa Utawala Bora na Vita dhidi ya Rushwa

Waziri Mkuchika: Tanzania ni nchi ya pili Afrika Mashariki kwa Utawala Bora na Vita dhidi ya Rushwa

June 16, 2014


Brass Band ya Jeshi la Polisi ikiongoza maandamano ya Maadhimishi ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salam. 2 
Watumishi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wakipita mbele ya meza Kuu wakati wa Maandamano Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salam. 3 
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Hab Mkwizu akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi  Mmoja jijini Dar es Salam. 4 
Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora Kapteni Mstaafu George Mkuchika akizungumza kuzindua Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi  Mmoja jijini Dar es Salam. 5 
Baadhi ya watumishi wa Umma wakifuatilia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salam. 6 
Afisa Habari wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Robi Bwiru akimueleza jambo mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Wizara hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi  Mmoja jijini Dar es Salam. 7 
Baadhi ya wananchi wakipata maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki , wakati walipotembelea banda la Wizara hiyo.
Picha na Hussein Makame-MAELEZO
Hussein Makame-MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika amesema kuwa Tanzania inashika nafasi ya pili kati ya nchi tano za Shirikisho la Afrika Mashariki katika suala la Utawala Bora na vita dhidi ya Rushwa.
Waziri Mkuchika amayasema hayo wakati akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza, Serikali ya Tanzania ilitangaza vita dhidi ya Rushwa na imekuwa ikiimarisha mapambano dhidi ya adui huyo hadi katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
“Katika nchi za Afrika Mashariki suala la Utawala Bora na Vita dhidi ya Rushwa, Tanzania tunashika nafasi ya pili, Rwanda ni ya kwanza, ya tatu ni Uganda na ya nne ni Kenya” alisema Waziri Mkuchika.
Waziri Mkuchika alikuwa akizungumzia madai yanayotolewa na baadhi ya watu hapa nchini kuwa Serikali ya Tanzania haina dhamira ya kupambana na Rushwa.
Alikanusha madai hayo na kusema kuwa Serikali ya Tanzania ina dhamira ya kupambana na Rushwa ndio maana imepitisha Sheria dhidi ya Rushwa,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) ina matawi kila mkoa na kila wilaya.
Alisema  kiashiria kingine cha kuthibitisha kuwa Serikali ya Tanzania inapamabana na Rushwa ni kufikishwa mahakamani kwa watu wanaotuhumiwa na Rushwa.
Hata hivyo, alibainisha kuwa mtumishi wa Takukuru hawezi kuwafikisha watu mahakamani bila ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.
Hivyo aliwataka Watanzania wote kutambua kuwa wana wajibu wa kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili kufanikisha vita hiyo dhidi ya Rushwa.
Waziri Mkuchika aliwakumbusha Watanzania kuwa mtumishi yeyote wa umma kumhudumia mwananchi ni haki yake, hivyo mtumishi anayeomba Rushwa ili atoe huduma anashiriki katika tendo la Rushwa.
Kutokana na hali hiyo, aliwaomba watumishi wajiepushe na Rushwa kwani Rushwa inawanyima watu haki, kukiwa na malalamiko anayepata haki ni yule anayetoa Rushwa.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwaka huu inasema “Mkataba wa Misingi na Kanuni za Utumishi wa Umma Barani Afrika ni Chachu ya Kuimarisha Utawala Bora na Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi”.
TFF YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA GEORGE MPONDELA

TFF YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MSIBA WA GEORGE MPONDELA

June 16, 2014



http://shaffihdauda.com/wp-content/uploads/2014/05/tff.jpg


Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga, George Mpondela kilichotokea jana (Juni 15 mwaka huu) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa klabu ya Yanga, Marehemu Mpondela anatarajiwa kuzikwa Alhamisi (Juni 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, na msiba upo Kigamboni Mnarani.
Mpondela alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1994 baada ya kumshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu George Ndaombwa.
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu nchini kwani, Mpondela enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi katika klabu yake ya Yanga.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Mpondela, na klabu ya Yanga na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Taratibu zaidi za mazishi zitatolewa na Yanga baada ya kufanya mawasiliano na familia ya marehemu Mpondela. Bwana ametoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina.
SIMBA YAMKAZIA MALINZI, YASEMA UCHAGUZI UKO PALE PALE, YAMFUTA WAMBURA MOJA KWA MOJA

SIMBA YAMKAZIA MALINZI, YASEMA UCHAGUZI UKO PALE PALE, YAMFUTA WAMBURA MOJA KWA MOJA

June 16, 2014


 http://shaffihdauda.com/wp-content/uploads/2014/06/ndumbaro-may28-2014.jpg
TAARIFA RASMI YA MWENYEKITI WA KAMATI YA UCHAGUZI WA SIMBA SC, WAKILI DKT. DAMAS DANIEL NDUMBARO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUPINGA MAAMUZI YA RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI KUSIMAMISHA UCHAGUZI WA SIMBA SC

Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, ilifanya mkutano wake kawaida tarehe 15 Juni 2014 kujadili mambo mbalimbali ambayo yanayohusu uchaguzi mkuu wa Simba Sports Club ambao umepangwa kufanyika tarehe tarehe 29 Juni 2014. Kamati ya Uchaguzi ya Simba sports Club inapenda kuujulisha umma, hususan wapenzi wa Simba Sports Club mambo yafuatayo:
1. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, kwa mujibu wa Ibara ya 10(6) ya Kanuni za uchaguzi za TFF toleo la mwaka 2013, ndiyo chombo pekee chenye mamlaka ya kutangaza, kubadilisha, kusimamisha au kufuta tarehe ya Uchaguzi ya Simba Sports Club. Kwakuwa Kamati haijafanya hivyo, wala hakuna mdau yoyote aliyeleta hoja ya kusimamisha uchaguzi, tunawajulisha kuwa uchaguzi wa Simba Sports Club upo pale pale kama ambayo Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilivyopanga. Maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vema na Uchaguzi utafanyika tarehe 29 Juni 2014 kama ilivyopangwa hapo awali.
2. Kamati imesikia kupitia vyombo vya habari kuwa TFF imesimamisha uchaguzi wa Simba Sports Club mpaka hapo Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club itakapoteua Kamati ya Maadili. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club inapenda kusema yafuatayo:
i. Mamlaka ya kusimamisha uchaguzi ni kazi ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kwa mujibu wa ibara 10 (6) ya Kanuni za Uchaguzi, 2013
ii. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilipoanza mchakato wa uchaguzi ilitoa tamko kuwa: “kwasababu Simba Sports Club haina kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Rufaa ya uchaguzi, wala Kamati za Maadili kwa mujibu wa ibara za 16 (e) na (f) ya Katiba ya Simba Mwaka 2014, vyombo husika vya TFF vitatumika”. Kulikuwa hakuna pingamizi toka kwa mtu yoyote juu ya kauli hiyo, ikiwemo TFF.
iii. Tarehe 26 Mei 2013, Rais wa TFF aliialika Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club katika chakula cha mchana. Katika mkutano huo, kauli ya aya (ii) hapo juu ilirejewa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilikabidhi rasmi mchakato mzima wa uchaguzi na kutoa ufafanuzi kuwa kamati husika za TFF zitahusika, jambo ambalo halikupingwa na TFF.
iv. TFF iliruhusu Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF kusikiliza Rufaa za uchaguzi za Simba, hivyo basi haiwezi kuzuia Kamati zake nyingine kusikiliza Masuala ya kimaadili. “Estopel” inawazuia TFF kufanya hivyo sasa.
v. Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club, isipokuwa watatu tu, ni wagombea katika uchaguzi huu. Na hao watoto tayari wapo kwenye Kambi za Kampeni za uchaguzi hii ambazo zipo bayana kabisa. Kuiagiza Kamati ya Utendaji ya Simba iunde Kamati ya Maadili kusikiliza kesi za maadili dhidi yao wenyewe ni kukiuka msingi wa haki ya asili (natural justice). Ni dhahiri kuwa haki haiwezi kutendeka kwa wajumbe wa kamati ya utendaji ya Simba Sports Sports Club, ambao ni watuhumiwa katika masuala ya maadili, wachague majaji wa kuwahukumu. Hapo haki haitatendeka.
Ifahamike kuwa, baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club kuteua Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club, Kamati hiyo haina mamlaka tena ya kujadili, kuingilia au kuteua chombo kingine kufanya shughuli zinazohusu uchaguzi ukizingatia kuwa wajumbe wake ni wagombea.
vi. Katika Uchaguzi Mkuu wa TFF wa Mwaka 2013, ambao ulimuingiza Jamal Malinzi Madarakani, FIFA walikuja, wakongea na pande zote na hatimaye, walisema kuwa; “tunapendekeza kuwa uchaguzi mkuu usimame ili kuunda kamati mbalimbali”. Mapendekezo hayo yalipokelewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Bw. Deo Lyato, na hatimaye ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF ndio iliyotangaza kusimamisha Uchaguzi na sio Sepp Blatter.
vii. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ni Kamati huru ambayo haipaswi kuingiliwa na Chombo chochote kile. Ili kulinda uhuru huo, tunalazimika kukanusha matamshi ya TFF kuhusu kusitisha Uchaguzi Mkuu wa Simba Sports Club. 
3. Malalamiko ya Kimaadili Kupelekwa FIFA.
Kwa mujibu wa Ibara ya 11 (9) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, 2013, inatoa mamlaka kwa Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kupeleka masuala ya maadili katika kamati ya maadili ya TFF. Tarehe 9 Juni 2014, Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilipeleka Masuala ya Maadili katika Kamati ya Maadili ya TFF. Kwakuwa TFF imekataa kusikiliza masuala ya maadili ambayo yanakiuka Kanuni za maadili, Katiba za Simba, TFF na FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, itapeleka Masuala ya Maadili FIFA ili haki itendeke.
4. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilijadili kuhusu vitendo vya wagombea kupiga kampeni kabla ya muda wa kampeni ulioruhusiwa. Kwa mujibu wa Mchakato wa Uchaguzi ya Simba Sports Club, muda wa kampeni unaanza tarehe 24 -28 Juni 2014. Hapo awali kamati ilibaini kuwa wagombea wawili wa nafasi ya urais; Michael Richard Wambura na Evans Aveva walifanya vitendo vya kampeni siku ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea. Tarehe 25 Mei 2014, Kamati iliwapa ONYO KALI la maandishi wagombea hao na kuwataarifu kuwa hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kuondolewa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi. 
Baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kumuondoa Bw. Michael Richard Wambura katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Mkuu wa SImba Sports Club, Bw. Wambura aliitisha Mkutano na waandishi wa habari, aliitukana Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, na kutoa matamshi ambayo ni Kampeni.
Baadaya ya Kamati ya Rufaa ya uchaguzi ya TFF kumrejesha Bw. Wambura katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Simba, Bw. Wambura aliitisha tena mkutano wa waandishi wa habari, aliisifu kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, kwa mara kwanza aliisifu Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club na kutoa matamshi ambayo ni wazi kuwa ni kampeni. Baadhi ya Matamshi aliyoyatoa kupitia vyombo vya habari ni kama ifuatavyo:
i. “Simba Sports Club inahitaji zaidi wadhamini na sio wafadhili”
ii. “Wafadhili kazi yao in kutoa fedha mfuko wa kushoto na kuepeleka mfuko wa kulia”
iii. “Simba ilikuwa na viwanja vitatu lakini kimoja kimeuzwa na wajanja na vimebaki viwili tu”
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilitafakari matamshi hayo, na kubaini kuwa hiyo ni kampeni ya waziwazi wakati muda wa kampeni bado haujaanza.
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ililipa jambo ili uzito wa kipekee kwasababu Mkosaji amekuwa na tabia ya kurudia kosa hilo hata baada ya kupewe onyo la maandishi.
HIVYO BASI: Kwa mujibu wa mamlaka ya kikanuni, hususan Ibara za: 6 (1) (a) – (g); 6 (1) (L) na 14(3) za Kanuni za uchaguzi za TFF – 2013, Bw. Michael Richard Wambura anaondolewa Katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa Simba Sports Club, 2013, kwa kosa la kurudia kufanya kampeni kabla ya muda wa kampeni ambao umepangwa,".
HAKIKISHENI TUNAKUWA NA CHAKULA CHA KUTOSHA DKT. BILAL AWAAMBIA G77+CHINA

HAKIKISHENI TUNAKUWA NA CHAKULA CHA KUTOSHA DKT. BILAL AWAAMBIA G77+CHINA

June 16, 2014

SA 3Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (wa pili kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wenzake waliohudhuria na kuzungumza katika mkutano huo wa sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya nchi za G77 na China uliofanyika jana Juni 15, 2014, jijini Santa Cruz, Bolivia. Picha na OMR0001Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza katika mkutano wa maadhimisho ya miaka 50 ya nchi za G77 na China, uliofanyika jijini Santa Cruz, Bolivia jana Juni 15, 2014. Picha na OMR 002Sehemu ya washiriki na wawakilishi wa viongozi wa mataifa mbalimbali katika mkutano huo.Picha na OMR 003Sehemu ya washiriki na wawakilishi wa viongozi wa mataifa mbalimbali katika mkutano huo.Picha na OMR 004Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (katikati) akiwa na baadhi ya Viongozi kutoka mataifa mbalimbali wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika juzi usiku Juni 14, jijini Santa Cruz, Bolivia. Picha na OMR
…………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Maalum, Santa Cruz, Bolivia
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amezitaka nchi wanachama wa G77+China, kuhakikisha zinaboresha kilimo ili ziwe na hifadhi ya kutosha ya chakula kwa wananchi wake. 
 
Akihutubia mkutano wa mwaka kwa nchi za G77+China ambao pia ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya umoja wa nchi hizi, unaofanyika jijini St Cruz De Sierra, Dkt Bilal alisema nchi za umoja huu zina maeneo mazuri kwa kilimo na hivyo ni muhimu kuyatumia maeneo haya katika kuzalisha chakula kwa lengo la kuhifadhi na kuwa na usalama wa chakula nyakati zote.
 
Dkt. Bilal alisema, nchi hizi kwa pamoja zinahitaji kuwa na kauli moja kuhusu masharti yanayowekwa na nchi kubwa hasa katika kilimo na kuelezea kuwa ili mafaniio makubwa yapatikane, lazima uwepo uwekezaji wa ndani katika kilimo sambamba na serikali za nchi hizi kuchangia shughuli za uzalishaji ili kuwa na kilimo chenye tija kwa wakulima na kinachoweza kuchangia usalama wa chakula.
 
Kuhusu suala la mazingira, Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwaeleza wajumbe wa G77+China kuwa, maazimio yaliyofikiwa Rio+20 na mapendekezo kuhusu ‘Kesho tunayoitaka’ yanazihitaji nchi hizi kupaza sauti zake kwa pamoja kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwani suala hili kwa sasa haliwezi kutatuliwa na nchi moja bali linahitaji nguvu ya kila mtu duniani.
 
Makamu wa Rais alifafanua kuwa bila kuwa na mazingira bora maendeleo endelevu yatabakia ndoto na pia kufanikisha Malengo ya Milenia kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa itakuwa vigumu kama suala la mazingira litaachwa kwa kila nchi kufanya inavyotaka.
 
“Kundi hili lina kazi kubwa iliyo mbele yetu na hasa kuhusu malengo mapya ya maendeleo baada ya kukamilika kwa muda wa Malengo ya Milenia mwakani. Tunahitajika kubuni njia za kuzipatia nchi zetu maendeleo katika Nyanja za uchumi, kijamii na mazingira ili tufanikiwe vema,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
 
Katika hotuba hiyo Mheshimiwa Makamu wa Rais pia alizungumzia kuhusu umuhimu wa nchi hizi kuweka msisitizo wa kuwapa wananchi maji safi na salama, umuhimu wa kuwa na nishati inayotosheleza matumizi ya uzalishaji, uwepo wa huduma bora za afya na elimu ili kupiga hatua kwa haraka baina ya wananchi wa nchi hizi. “Nafahamu kufanikisha haya yote ni kazi kubwa lakini hatuna muda wa kusubiri. Ni lazima tufanye kazi ili kubadili hali iliyopo,”alifafanua.
 
Mkutano huo ambao umekamilika jana kwa mwenyeji wake Rais Evo Morales kuwashukuru wanachama wa G77+China walioweza kushiriki mkutano huo, pia ulionesha nia kwa wanachama wa nchi hizi kutafuta majibu ya changamoto ya ukosefu wa ajira unaokabili wananchi wengi wa nchi hizi. Viongozi wengi walisisitiza kuwa, suala la ajira hasa kwa vijana linatakiwa kutazamwa upya na hasa ukizingatia rasilimali zilizopo katika nchi za G77+China ili zitumike katia kutengeneza ajira mpya zitakazoweeza kusaidia kuboresha maisha ya watu wa nchi hizi kwa miaka mingi ijayo.