MAELEKEZO YA DKT. SAMIA YAWAVUTIA VIJANA KUJIAJIRI KWENYE UFUGAJI

February 16, 2023
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvui Mhe. Abdallah Ulega (Mb (wa tatu kushoto) akizungumza na vijana waliojiunga mafunzo ya vitendo ya ufugaji kwa tija na biashara na kunenepesha mifugo, kwenye Kituo Atamizi kilichopo Wakala ya Elimu ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) Mkoani Tanga, kupitia programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI). (15.02.2023)



Na. Edward Kondela

Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeamua kukuza sekta ya mifugo kupitia unenepeshaji wa mifugo ili wananchi waweze kufuga kibiashara na kwa tija zaidi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amebainisha hayo (15.02.2023) Mkoani Tanga, wakati alipotembelea vijana waliojiunga kwenye vituo atamizi vilivyopo Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) ili kupata mafunzo ya vitendo ya ufugaji kibiashara na unenepeshaji bora wa mifugo.

Mhe. Ulega amefafanua kuwa kupitia dira na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia, serikali imeonelea kuichangamsha Sekta ya Mifugo, kupitia unenepeshaji na ufugaji wenye tija hivyo wizara kuja na programu ya Samia Ufugaji kwa Tija (SAUTI).

“Tunataka kutengeneza matokeo chanya kwa vijana katika maendeleo yao Rais Dkt. Samia anataka vijana wachakarikaji, wenye kasi ya maendeleo.” Amesema Mhe. Ulega

Nao baadhi ya vijana ambao wanapata mafunzo hayo wamemwambia Naibu Waziri Ulega kuwa wamejiwekea mikakati ya kufanya ufugaji wenye tija mara wakapomaliza mafunzo yao ambayo yanadumu kwa mwaka mmoja.

Wamebainisha kuwa ni wakati wao saa kufikiria kujiajiri na hata kutoa mafunzo kwa wafugaji wengine wa asili ili wafuge kisasa na kuingia katika biashara ya unenepeshaji wa mifugo

Programu ya SAUTI ambayo imeanzishwa kutokana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyotoa wakati wa kuhitimisha sherehe za wakulima (Nanenane) Mwaka 2022, imelenga kuwabadilisha vijana kifikra kwa kuwapatia mbinu mbalimbali za ufugaji wa kisasa na kibiashara ikiwa ni pamoja na kuwaonyesha fursa zilizopo kupitia Sekta ya Mifugo.

Mwisho.


ULEGA: MSOMERA YAZIDI KUNG’ARA MIRADI YA WAFUGAJI YAPAA

February 16, 2023


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiendesha trekta mara baada ya kufika katika moja ya mashamba darasa ya malisho ya mifugo kwenye Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, katika ziara yake ya siku moja kwenye wilaya hiyo. (16.02.2023)


Na. Edward Kondela

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo serikali inahakikisha kila sekta inafikiwa katika maendeleo wakiwemo wafugaji na wavuvi.

Naibu Waziri Ulega amebainisha hayo (16.12.2023) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali inayowahusu wafugaji, yakiwemo mabwawa ya maji, minada ya mifugo, majosho na malambo ili kusogeza huduma karibu kwa wakazi wa kijiji hicho.

Amesema mbali na wafugaji ambao serikali imekuwa ikiwafikia kwa kuwapatia huduma mbalimbali za miundombinu kwa ajili ya shughuli za mifugo, wavuvi na wafugaji wa samaki pia wanafikiwa.

“Hakuna lililosimama yote yanasonga mbele makandarasi waendelee kushirikisha vyema wenyeji ambao wanajua mazingira ya hapa na wenyeji kushirikiana na makandarasi na wenyewe kuwashirikisha viongozi kila hatua.” Amesema Mhe. Ulega

Ameongeza kuwa anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa imetenga fedha Shilingi kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwa wafugaji, ikiwemo minada takriban Shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya kujenga minada mipya na kukarabati ya zamani na Shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya kutengeneza majosho.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Albert Msando akitoa taarifa ya wilaya kwenye kikao cha Kijiji cha Msomera ambacho Naibu Waziri Ulega alikuwa mgeni rasmi, amesema hadi sasa serikali imeshajenga majosho saba kwa ajili ya kuoshea mifugo, miradi kwa ajili ya malisho ya mifugo ambapo maandalizi yamekamilika yakiwemo ya upatikanaji wa mbegu.

Mhe. Msando ameongeza kuwa idadi ya mifugo iliyopo katika kijiji hicho ni mingi kuliko idadi ya wakazi wake ambapo inafikia zaidi ya 86,234 ikiwemo ng’ombe 28,049 mbuzi 32,743 kondoo 24,795 na punda 647.

Nao baadhi ya wanakijiji cha Msomera katika kikao hicho walipata fursa ya kutoa maoni na maswali kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ambapo moja ya maoni yao ni kuwepo kwa vikundi vinavyojumuisha wanakijiji hao ili wapatiwe mashamba darasa na ng’ombe wa maziwa ili wafuge kisasa, ambapo Naibu waziri Ulega ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) kufika katika kijiji hicho na kutoa elimu juu ya mikopo kwa wafugaji hao ili waweze kufuga kwa tija na kibiashara kwa kuwa wana makazi ya kudumu.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) yuko Mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kujionea namna maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta za mifugo na uvuvi.

Mwisho.



MIRADI YA MAENDELEO INAYOTEKELEZWA KATIKA JIJI LA TANGA CHINI YA USIMAMIZI WA TANGA YETU YAMKOSHA - ULEGA

February 16, 2023

 



Na Oscar Assenga,TANGA 




Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Abdallah Ulega Leo amefanya ziara ya kukagua Miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya JijiTanga  na Kufurahishwa na Kasi ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri  Chini ya Usimamizi  wa  Tanga Yetu.



Miradi hiyo ya Maendeleo ambayo Ulega amefurahishwa nayo ni pamoja na Mradi wa Kilimo Cha Mwani na Ufugaji wa Tango Bahari ( Jongoo Bahari) ulio chini ya kikundi Cha Mchukuuni Tanga Jiji chenye Wanachama 36, Mradi wa urutubishaji Samaki aina ya kaa na Vizimba vya kufugia Samaki hao zaidi ya 600 kwa Wakati mmoja pamoja na Mradi wa Utotoreshaji wa Vifaranga 10,000  kwa Wakati mmoja  Wenye Vijana 50 .




Miradi hiyo inaratibiwa na kusimamiwa na Tanga Yetu kwa ufadhili wa  Fondation Botnar kwaajili na kuipeleka Tanga kwenye Uchumi wa Bluu kupitia mafunzo ya vitendo yanayoleta Ajira kwa Vijana na Wanawake.



Ulega aliwapongeza Wasimamizi wa Miradi hiyo kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuwatumikia Wananchi,


" Niwapongeze Sana wote mnaowatumikia Wananchi wetu kwa moyo wa kujitoa  hususani nyie Wadau Wa Maendeleo Tanga Yetu na Fondation Botnar, Niwaagize Maofisa Uvuvi na Mifugo muhakikishe Mnawatembelea Wanavikundi Hawa na kuwasaidia kero zao, Nimesikia kero ya Baadhi ya Wavuvi kuwa Wanafanya Uharibifu kwenye mashamba ya Mwani , naomba muwakamate na muwafikishe kwenye vyombo vya Sheria na mfanye Doria za Mara kwa Mara ili muwabaini Wahalifu wanaorudisha nyuma Maendeleo ya Wananchi wa Hali ya chini" Alisema Ulega



Ulega Alisema serikali imeweka Shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendeleza zao la mwani ambapo tayari Sh. Milioni 447 zimeshatolewa kwa vikundi mbalimbali  na Sh. 11.5 Bil. zimetengwa kwa ajili ya kutengeneza boti za kisasa za uvuvi na Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa vizimba vya kufugia samaki aina ya sato kwenye Ziwa Victoria.


 Ulega alisema Serikali  imejizatiti kuinua uchumi wa buluu kwa kutenga fedha nyingi huku wadau mbalimbali wa sekta hiyo wakikaribishwa kuunga mkono jitihada hizo kwaajili ya kuweka mazingira mazuri ya ukuzaji viumbe maji na kuongeza Ajira kwa katika Jamii hususani kwa Vijana.


Aidha, aliwataka wadau wa Sekta ya Uvuvi hususan vikundi vya ushirika vya wavuvi kuchangamkia fursa ambayo serikali imetoa fedha ili kuongeza mahitaji ya ukuzaji viumbe maji kutokana na masoko yaliyopo ndani na nje ya nchi.



Maagizo hayo ya kukamatwa kwa Baadhi ya Wavuvi wanaofanya uharibifu kwenye mashamba ya Mwani na maeneo ya Ufugaji wa Matango  Bahari yanafuatia Baada ya  Mwenyekiti wa  chama Cha Ushirika wa kilimo cha mwani na ufugaji Matango Bahari cha Mchukuuni  Jijini Tanga, Abdallah Mtondo Kulalamikia kitendo cha baadhi ya watu ambao siyo waaminifu kuiba matango bahari katika mashamba yao hususan nyakati ambapo maji yamefunika mashamba hayo.


Kutokana na hali hiyo wameiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria watu hao ambao wamekuwa wakiwarudisha nyuma katika shughuli za ufugaji ili kujiongezea tija jambo ambalo Naibu Waziri Ulega amelitolea kauli kali na kutaka mamlaka husika kuingilia kati jambo hilo huku akisisitiza wanunuzi wa mwani na tango bahari kununua mazao hayo kwenye vikundi vinavyotambulika na kusajiliwa.




Mwisho.