Gambo Cup yaingia hatua ya pili kituo cha Mombo.

Gambo Cup yaingia hatua ya pili kituo cha Mombo.

May 14, 2013
Na Mwandishi Wetu,Korogwe.
MASHINDANO ya Vijana ya Kombe la Gambo Cup yanatarajiwa kuingia hatua ya pili katika kituo cha Tarafa ya Mombo wilayani humo ambapo timu nne zimefanikiwa kucheza hatua hiyo ambayo itachezwa kwa mtindo wa mtoano.

Mashindano hayo ambayo yalianzishwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Mrisho Gambo na kufadhiliwa na benki ya NMB yakiwa na lengo la kuinua vipaji vya wachezaji wachanga pamoja na kukuza kiwango cha soka wilayani humo.

Mratibu wa Mshindano hayo, Zaina Hassani alilimbia gazeti hili kuwa hatua hiyo katika kituo hicho inatarajiwa kuwa ni ngumu kuliko hatua iliyomalizika kutokana na ushindani uliokuwepo kwani kila timu ilitaka kuingia hatua hiyo.

Hassani ambaye pia ni katibu wa chama cha soka wilaya ya Korogwe,(KDF)alizitaja timu ambazo zilifanikiwa kucheza hatua hiyo ya mtoano katika kituo cha Mombo ni Reli Fc,Mwisho wa Shamba, Mkumbara.

Katika kituo cha Makuyuni zilizofanikiwa kuingia ni Rangers Fc,Madago Fc na Gomba huku kituo cha Mswaha kikiingiza timu mbili ambazo ni Kosovo na Mafleti.

Katibu huyo alisema timu hiyo zilifanikiwa kucheza hatua hiyo baada ya kufanya vizuri katika hatua ya makundi na kuweza kupatikana timu nane ambazo zilicheza kwa mfumo wa mtoano ili kuweza kumpata bingwa wa tarafa ya Mombo ambaye atacheza hatua ya fainali pamoja na mshindi wa pili.

Akizungumzia mashindano hayo,Mwenyekiti wa Chama cha soka wilayani humo,Peter Juma alisema yamekuwa na ushindani ikiwemo kuleta hamasa kwa wadau wa soka pamoja na kupelekea vijana kupenda michezo na kuwataka wadau wengine kuiga mfano wa mkuu huyo wa wilaya kwa kuanzisha ligi nyengine lengo likiwa ni kuinua vipaji vya soka.

        Mwisho.
Habari kutoka Shirikisho la soka hapa nchini TFF.

Habari kutoka Shirikisho la soka hapa nchini TFF.

May 14, 2013
Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam.
UFAFANUZI KUHUSU LIGI YA MABINGWA MIKOA
Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) ilianza tarehe 12 Mei 2013 ikishirikisha klabu bingwa za mikoa yote ya Tanzania Bara, isipokuwa mikoa ya Pwani na Manyara ambayo kutokana na sababu tofauti ilishindwa kuwasilisha majina ya klabu zake hadi siku ya mwisho iliyowekwa na Kamati ya Mashindano, yaani tarehe 10 Mei 2013.

Suala la kukosekana kwa wawakilishi wa mikoa hiyo miwili limezua maswali mengi kiasi kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linalazimika kutoa ufafanuzi kwa faida ya wadau wote wa mpira wa miguu.

Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, ambayo ni mpya baada ya TFF kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa mpira wa miguu, ilipangwa kuanza tarehe 5 Mei 2013, lakini hadi tarehe ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mabingwa wa mikoa, yaani tarehe 2 Mei 2013 mikoa michache ndiyo iliyokuwa imemaliza ligi zao na kupata mabingwa.

Kuchelewa huko kwa mikoa kumaliza ligi zao kuliilazimisha Kamati ya Mashindano ya TFF kuongeza muda wa mikoa kuwasilisha majina ya wawakilishi hao hadi tarehe 10 Mei 2013 na hivyo siku ya kuanza kwa Ligi kusogezwa mbele hadi tarehe 12 Mei 2013.

Hadi kufikia tarehe hiyo mpya ya mwisho ya kuwasilisha majina ya mabingwa wa mikoa, ni mikoa sita tu iliyofaidika na kuongezwa huko kwa muda na kupata wawakilishi wake. Mikoa hiyo ni Iringa, ambayo pamoja na kuongezwa kwa muda, iliandika barua ya kuihakikishia Kamati ya Mashindano kuwa itapata bingwa kabla ya kuisha kwa siku ya tarehe 10 Mei 2013.

Mikoa mingine ni Lindi, Mtwara, Geita, Tabora na Dodoma.
Mkoa wa Manyara haukuweza kumaliza ligi yake hadi mwisho wa siku ya tarehe 10 Mei 2013 na hivyo Kamati ya Mashindano iliyosubiri majina hadi saa 12:00 jioni siku hiyo kuamua kuwaondoa wawakilishi wa Manyara kwenye ratiba.

Awali, Kamati ya Mashindano iliamua kuwa ratiba ya mechi za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa ipangwe tarehe 7 Mei 2013, ikishirikisha mikoa ambayo ilishapata mabingwa wake, lakini baada ya kuona baadhi ya mikoa ilikuwa haijakamilisha ligi zake, Kamati iliamua kuwa ratiba ipangwe kwa kutumia majina ya mikoa kwa matumaini kuwa hadi kufikia tarehe 10 Mei 2013, mikoa itakuwa imeshapata wawakilishi wake na kwa kuwa ratiba inahusu mikoa jirani, ingekuwa rahisi kwa timu kusafiri kutoka kituo kimoja hadi kingine.

Lakini Mkoa wa Manyara haukuweza kufanya hivyo na Kamati kulazimika kuuondoa kwenye ratiba kutokana na kushindwa kukidhi utashi huo.
Mkoa mwingine ambao uliondolewa kwenye ratiba ni Pwani ambayo pamoja na kutuma jina la mwakilishi wake, Kamati ilipokea malalamiko kutoka klabu zilizoshiriki Ligi ya Mkoa, zikidai kuwa jina la bingwa wa Pwani lililowasilishwa TFF lilikuwa batili kwa kuwa klabu ya Kiluvia United haikustahili kushiriki Ligi ya Mkoa kutokana na ukweli kuwa haijasajiliwa mkoani Pwani na wala haikushiriki ligi ya mkoa msimu uliopita. Kamati ya Mashindano iliiondoa Pwani kwenye ratiba na kulirudisha suala hilo mkoani.

Ingawa Katibu wa Pwani alijaribu kuishawishi Sekretarieti ya TFF iliangalie suala hilo kwa undani zaidi, Sekretarieti ilimjibu kuwa lilishafanyiwa uamuzi na Kamati, hivyo uamuzi huo usingeweza kutenguliwa na kumshauri katibu huyo arejee mkoani kwake kuwasiliana na viongozi wenzake kuona ni jinsi gani mkoa unaweza kunusuru hali hiyo kwa kufanya uamuzi ambao ungeuwezesha mkoa kupata mwakilishi.

Kwa mantiki hiyo, masuala ya Manyara na Pwani yalikuwa ndani ya uongozi wa mikoa husika na si Kamati ya Mashindano ya TFF kwa kuwa Kamati ilitaka ipatiwe jina la bingwa ambaye alipatikana kwa mujibu wa mfumo mpya wa Ligi ya Mikoa.

Ligi ya Mabingwa wa Mikoa inachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na hivyo timu zilizokutana tarehe 12 Mei 2013, zitarudiana mwishoni mwa wiki hii na kupatikana timu zitakazosonga mbele kwenye raundi nyingine hadi timu tatu bora zitakazopanda daraja kwenda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zitakapopatikana.

Ligi za Mikoa, kwa mujibu wa kanuni mpya, zinatakiwa ziwe na timu kati ya 16 na 20 na zinatakiwa zicheze mechi mbili za nyumbani na ugenini, hata kama zitakuwa zinatumia uwanja mmoja.

Uamuzi wa kubadilisha mfumo huo ulifanywa ili kuhakikisha kuwa mikoa inakuwa na na mashindano kwa mwaka mzima na hivyo kuiwezesha mikoa kujikita katika kutafuta mbinu za kupata fedha na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu kwenye mikoa yao.

Uamuzi huo pia unasaidia kupunguza mtindo wa wachezaji kuzunguka klabu tofauti katika msimu mmoja kwa kuwa wanalazimika kutulia kwenye klabu moja hadi muda wa usajili unapofika.

Pamoja na wachezaji kutulia sehemu moja kwa muda mrefu, pia walimu wanapata fursa ya kujikita vizuri kwenye programu zao kwa kuwa wanakuwa na uwezo wa kufuatilia maendeleo ya wachezaji wao.
Pamoja na hayo yote, mfumo huo utasaidia kurudisha msisimko kwenye mikoa na hivyo kutoa fursa kwa vijana wengi wenye vipaji kuonekana na kuendelezwa.

TFF inatoa wito kwa viongozi wa mikoa kuanza kubuni sasa mikakati ya kuendesha ligi hizo msimu unaokuja kwa kuwa hakutakuwa na nafasi tena ya kuongeza muda kwa mikoa kuwasilisha majina ya wawakilishi wao.

         Mwisho.
 
KIINGILIO MECHI YA SIMBA, YANGA 5,000/-

Kiingilio cha chini kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Yanga itakayochezwa Jumamosi (Mei 18 mwaka huu) kitakuwa sh. 5,000. Kiingilio hicho kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648.

Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu kiingilio ni sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000, VIP C kiingilio ni sh. 15,000, VIP B itakuwa sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tu tiketi moja itapatikana kwa sh. 30,000.  

Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni.

Mwamuzi wa mechi hiyo atakuwa Martin Saanya kutoka Morogoro ambapo atasaidiwa na Samuel Mpenzu wa Arusha, na Jesse Erasmo kutoka Morogoro. Mwamuzi wa akiba ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.

Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Leslie Liunda.

                       Mwisho.

KOCHA KIM KUZUNGUMZIA MECHI YA MOROCCO

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen atakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia maandalizi ya tiketi kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco. Mkutano huo utafanyika keshokutwa (Mei 16 mwaka huu) saa 5 kamili kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Juni 8 mwaka huu kwenye jiji la Marrakech nchini Morocco. Taifa Stars ilishinda mechi yake iliyopita jijini Dar es Salaa kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Morocco.

Angetile Osiah
Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

DC Mgaza aitaka jamii kuona umuhimu wa kuhudhuria katika vituo vya Afya”

DC Mgaza aitaka jamii kuona umuhimu wa kuhudhuria katika vituo vya Afya”

May 14, 2013


Na Mwandishi Wetu,Mkinga.
MKUU wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza ameitaka jamii kuona umuhimu wa kuhudhuria katika vituo vya afya kupatiwa tiba pindi wanapokuwa wanajisikia kuwa na maradhi badala ya kwenda kupata tiba asili ambazo hazina vipimo vya kitaalamu.

Mgaza aliitoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani ambapo kimkoa yaliazimishwa katika kituo cha Afya Maramba kilichopo wilayani hapa ambapo mkuu huyo wa wilaya alitembelea kituo hicho na kugawa misaada mbalimbali kwa wagonjwa katika halfa iliyohudhuriwa na wauguzi kutoka wilaya zote mkoani hapa.

Alisema wagonjwa ambao hawatapata matibabu ya kitaalamu wapo katika uwezekano mkubwa wa kupoteza maisha kwani hawatatambulika na wala hawatajulikana kuwa wamepoteza maisha kwa magonjwa gani na pia inawezakana ugonjwa huo ukawa ni wa mlipuko ambao unaweza kusababisha hatari ya maambukizi kwa jamii inayozunguka eneo husika.

Aidha alisema kuwa ni muhimu kwa wakinamama wote wajawazito kuhudhuria klinik kupima hali zao za ujauzito na kupata ushauri wa kitaalamu juu ya afya zao na watoto wanaotarajia kuwazaa na hatimaye unapofika wakati wa kujifungua wahakikishe wanazalia hospitalini au katika vituo vya huduma za afya vyenye wataalamu ili wapate elimu ya afya na ushauri juu ya malezi ya watoto wao.

Alieleza kuwa madhumuni makubwa ya siku hiyo ni kukumbuka tarehe aliyozaliwa mwanzilishi wa uunguzi ulimwenguni Mama Florence Night Ngale ambaye alizaliwa mwaka 1820 huko Italia katika mji uitwao Florence na hatimaye wazazi wake kuamua kumwita kwa jina la mji huo.

Mkuu huyo wa wilaya alisema aliguswa sana na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema “Kuziba Mapengo kufikia malengo ya maendeleo ya Milenia”nayo ni kuhakikisha wanapunguza vifo vya watoto wachanga, kuboresha afya za mama wajawazito na kudhibiti magonjwa ya Ukimwi malaria na kifua kikuu.

Awali akisoma risali kwa mkuu huyo wa wilaya, Katibu wa Chama cha Wauguzi Mkoa wa Tanga(Tana), Hadija Mbasha alisema licha ya kuazimishwa siku hiyo lakini zipo changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili wauguzi mkoani hapa ikiwemo kukosa haki za zao za msingi kama vile malipo ya kazi saa za ziada pamoja na malipo ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi.

Mbasha alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hizo lakini pia wanaiomba jamii ya Tanzania iwatambue wauguzi kama ni watu wenye huruma, upendo na msaada ikiwemo kuchukia sifa mbaya kama jamii nyengine zilivyo kwamba sio kila muuguzi ana kauli mbaya.

Mwisho.