MELI YENYE WATALII ZAIDI YA 100 YATIA NANGA HIFADHI YA MAGOFU YA KALE KILWA KISIWANI

MELI YENYE WATALII ZAIDI YA 100 YATIA NANGA HIFADHI YA MAGOFU YA KALE KILWA KISIWANI

February 04, 2024

 



Watalii hao wakiongozwa na Kampuni ya Utalii ya Takim Holidays walipokelewa na kukaribishwa kwa ngoma za asili ya watu wa Kilwa Kisiwani iitwayo kitupolo ambayo iliwafanya waonekane wakifurahi muda wote.

Ngome ya Mreno, Msikiti mkubwa na mkongwe, Makaburi ya Malindi na Makutani Palace ni miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa na watalii hao ikiwa ni pamoja na kupata fursa ya kujifunza tamaduni za watu wa Kilwa kisiwani.

Historia na upekee wa Hifadhi hii ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara imekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka Kona mbalimbali za Dunia ambao hutembelea Hifadhi hiyo Karibu Kila Mwaka.

TAWA inatarajia kuendelea kupokea Meli nyingine zaidi katika kipindi cha Mwezi Februari na Machi, 2024, na hii yote ni kutokana na Kazi kubwa iliyofanywa na muongoza watalii “Tour Guide” namba moja Nchini Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
RPC MALLYA AWATAKA WAUMINI WA KANISA LA MORAVIANI USHIRIKA WA SONGEA KUTOKUJIINGIZA KWENYE MADENI MAKUBWA

RPC MALLYA AWATAKA WAUMINI WA KANISA LA MORAVIANI USHIRIKA WA SONGEA KUTOKUJIINGIZA KWENYE MADENI MAKUBWA

February 04, 2024





Na Issa Mwadangala

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi Theopista Mallya amewataka waumini wa Kanisa la Moraviani Ushirika wa Sogea Mjini Tunduma kutojiingiza kwenye madeni makubwa ambayo hupelekea madhara ya msongo wa mawazo baada ya kushindwa kulipa madeni hayo.

Akizungumza Februari 04, 2024 na waumini wa kanisa Moravian kwa Mchungaji Emmanuel Silungwe wakati wa ibada ya jumapili Kamanda Mallya amesema madeni makubwa ni changamoto kwani husababisha msongo wa mawazo.

“Kitendo cha baadhi ya waamini kukopa mikopo mikubwa ambayo wanashindwa kumudu malipo yake kinapelekea kuwa na msongo wa mawazo na baadhi yao kujiua” alisema Kamanda Mallya.

Aidha, Kamanda Mallya amewaomba waamini wa kanisa hilo kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto pamoja na kuacha vitendo vingine visivyompendeza Mwenyezi Mungu.

Sambamba na hayo amekemea suala la kuomba na kupokea rushwa jambo ambalo ni kosa kisheria lakini halimpendezi Mwenyezi Mungu kwani kuomba au kutoa rushwa kunapoteza haki ya mtu mwingine ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha waamini hao haki ya dhamana Kwa watuhumiwa pindi wanapolalamika kuwa mhalifu akikamatwa anaachiwa na Polisi vilevile alitoa elimu juu ya mgawanyo wa utendaji wa kazi za serikali kati ya Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama.

Kwa upande wao waamini wa Kanisa hilo wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa ushiriki wao katika ibada hiyo na kutoa elimu ambayo ni sehemu ya mafundisho mema ikiwa ni pamoja na kufanikisha zoezi la harambee la kupaua jengo la ofisi ya Kanisa hilo ambalo ujenzi wake bado unaendelea.

Utoaji huo wa elimu katika nyumba za ibada ni mkakati wa Jeshi la Polisi kuhakikisha viongozi wa dini wanakuwa sehemu ya kuukataa uhalifu nchini na kutumia nafasi zao katika mahubiri kutoa elimu na kukemea vitendo viovu katika jamii.


PINDA AKABIDHI MAGARI MAWILI YA WAGONJWA MPIMBWE

February 04, 2024

 Na Munir Shemweta, WANMM MPIMBWE


Mbunge wa Jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda amekabidhi magari mawili ya wagonjwa kwa halmashauri ya Mpimbwe iliyopo wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi ili kusaidia kusafirisha wagonjwa.

Hafla ya kukabidhi magari hayo imefanyika tarehe 3 Februari 2024 katika kituo cha Afya Isevya kilichopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele na kuhudhuriwa na viongozi wa halmashauri hiyo wakiwemo madiwani.

Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo Mhe. Pinda alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha jimbo lake katika huduma za sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.

‘’Nimshukuru Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia ujenzi wa vituo vya katika jimbo langu, kwa kweli Mhe. Rais ameifanya Mpimbwe istawi’’ alisema Mhe. Pinda.

Ameitaka halmashauri ya Mpimbwe na Kituo cha Afya cha Isevya kuhakikisha magari aliyoyakabidhi yanatunzwa vizuri sambamba na kutumika kwa yale malengo yaliyokusudiwa ya kuwahudumia wananchi wa Mpimbwe.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa jimbo la Kavuu, wakati anaingia madarakani mwaka 2020, vituo vya afya kwenye jimbo lake vilikuwa viwili na kuvitaja kuwa ni kile cha Usevya na Mamba.

Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, kwa sasa katika jimbo lake vimeanzishwa vituo vingine vitatu vya Majimoto, Kibaoni, Kasansa Pamoja na Zahanati ya Mwamapuli inayokwenda kuanza kazi.

Amesema, ataendelea na juhudi mbalimbali za kuimarisha huduma za sekta ya afya katika jimbo la Kavuu kwa kuwa afya ni muhimu huku akiwaahidi wananchi wa jimbo lake kupambana kwa hali na mali ili jimbo hilo libadilike kimaendeleo na pale atakapomaliza muda wake aache alama itakayomfanya aendelee kukumbukwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu Mwariko amesema, jukumu la halmashauri yake ni kuhakikisha magari waliyokabidhiwa yanaenda kusaidia na kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mpimbwe.

‘’Tutayalinda na kuhakikisha muda wote yanafanya kazi iliyokusudiwa ya kusaidia na kuboresha huduma kwa wananchi’’ alisema Shamimu.

‘’Nimshukuru Rais kwa kuhakikisha huduma zote za afya nchini ikiwemo Mpimbwe zinakaa vizuri na katika mwaka huu wa fedha halmashauri yetu inaenda kukamilisha vituo vyetu vya afya vitatu vya Majimoto, Kasansa na kibaoni kwa asilimia mia moja’’ Alisema.

Mhe. Pinda alikuwa jimboni kwake kwa ziara ya siku moja ambapo mbali na hafla ya kukabidhi magari ya wagonjwa aliwatembelea na kuwafariji wananchi wa jimbo lake waliopatwa na ugonjwa wa kipiundupindu katika eneo la Mwamapuli.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akikata utepe kuzindua magari mawili ya wagonjwa aliyoyakabidhi kwa halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 3 Februari 2024. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu Mwariko
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizindua magari mawili ya wagonjwa aliyoyakabidhi kwa halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 3 Februari 2024. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu Mwariko.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akiangalia moja ya gari la wagonjwa alilolikabidhi tarehe 3 Februari 2024.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akitoka katika moja ya gari la wagonjwa alilolikabidhi kwa halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 3 Februari 2024.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu Mwariko akizungumza katika hafla ya kukabidhiwa magari mawili ya wagonjwa tarehe 3 Februari 2024 mkoani Katavi.
Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza katika hafla ya kukabidhi magari mawili ya wagonjwa kwa halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 3 Februari 2024.

Magari mawili ya wagonjwa yaliyokabodhiwa kwa halmashauri ya Mpimbe na Mbunge wa Jimbo la Kavuu ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda tarehe 3 Februari 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

MKULAZI YAINGIZA FAIDA BILIONI 36 KWA SUKARI YA MAJARIBIO TU.

February 04, 2024

 Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kilichopo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro kimeanza kuingiza faida zaidi ya shilingi bilioni 36 kutokana na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali wakati uzalisha wa sukari ya majaribio yaliyofanyika mwezi Disemba 2023.


Akibainisha hayo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu Mh, Patrobas Katambi (Mb) wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mh, Fatma Toufiq ilipotembelea na kujionea maendeleo yaliyofikiwa katika kiwanda hicho.

Naibu Waziri Katambi alisema kiwanda hicho tayari kimeanza kupata faida ya shilingi bilioni 36.36 kutokana na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo molasses (Molasi) ambayo hutumika kama mbolea na mabaki ya nyuzinyuzi (Bagasse) ambayo yanatumika kwa shughuliza uzalishaji wa umeme unaotumiwa katika kiwanda hicho.

Aidha Katambi alikipongeza kiwanda hicho kwa kuendelezea kuwa bega kwa bega na Serikali kwa kuzalisha ajira ambapo mpaka sasa tayari kimeajiri vijana wa Kitanzania 2,600 huku matarajio yakiwa kutoa ajira za kudumu na zisizo za kudumu jumla ajira 11,260.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii Mh, Fatma Toufiq alisema Kiwanda hicho cha Kimkakati kitaenda kupunguza nakisi ya sukari iliyopo ya tani 250,000 kwa kuchangia asilimia 20% ambapo mkakati wa kiwanda hicho ni kuzalisha sukari tani 50,000 kwa ajili ya matumizi ya sukari za viwandani na matumizi ya majumbani.

“Huu ni mradi wa Kimkakati, na kweli ni mkakati mkubwa, kwasababu mwisho wa siku utasaidia kupunguza upungufu wa sukari hapa Nchini, Tumeona miundombinu, Tumeona sukari ambayo imeanza kuzalishwa, lakini pamoja na changamoto ya mvua za Elnino lakini tunaona kabisa kwamba huko mbele kuna mwanga kwa Watanzania” Alisema Fatma Toufiq.

Akizungumza katika ziara ya kamati hiyo, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa NSSF Masha Mshomba ambao ndio wabia wa mradi huo kwa 96% alisema NSSF imepata faraja kuona uwekezaji huo kufikia hatua ya kuanza uzalishaji, kwani lengo la mradi huo ni kuona unaanza kuleta faida ili kurudisha fedha za Wanachama wa mfuko huo.

“Niwaahidi Watanzania wote hususani wanachama wa NSSF, kwamba pesa zao zipo salama, mradi huu utalipa kwa kadiri tulivyokusudua, lakini kikubwa zaidi utasaidia kupunguza nakisi ya sukari hapa Nchini, Ndio maana tunahimizwa tujenge utaratibu wa kuwekeza katika viwanda kama hivi.” Alisema Mshomba.

Kwaupande wake Mtendaji Mkuu wa Kampuni hodhi ya Mkulazi Selestine Some alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa miongozo ya uwekezaji wa mradi huo uliogharimu shilingi bilioni 344 ambapo umeshaanza kutoa matunda kwa Watanzania.

“Mradi unafaida kubwa sana kwa jamii, mradi umejenga Zahanati inayoweza kuzihudimia jamii zinazozunguuka mradi huo, lakini pia ukipita maeneo ya Dumila utaona shughuli za kiuchumi zikiendelea na kutoa fursa za vijana kujiajiri kutokana na uwepo wa mradi huu. Alisema Some

Sambamba na uwekezaji huo wenye faida za kiuchumi kwa Watanzania, Pia Kampuni hodhi ya Mkulazi imeweza kuzingatia usalama wa Wafanyakazi wake mahala pa kazi kwa kuwapatia vifaa kinga vya kuzuia ajali (PPE)wafanyakazi wake, ambapo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mh, Patrobas Katambi alitoa cheti kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo kwa kujali usalama wa wafanyakazi mahala pa Kazi.

Meneja wa Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi Mhandisi Aron Mwaigaga akitoa maelezo ya kina juu ya hatua za uzalishaji wa Sukari kiwandani hapo kwa wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na maendeleo ya Jamii wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bi, Fatma Toufiq mapema baada ya kutembelea na kufanya ukaguzi katika Kiwanda hicho.

UTAFITI: MABAKI YA MKONGE HUZALISHA PROTINI, MBOLEA

February 04, 2024

 Imezoeleka mkonge baada ya kuchakatwa na kupatikana singa (sisal fibre) mabaki yake (sisal waste) hutupwa kama uchafu kwa kuwa hayana matumizi mengine.


Hatua hiyo ni tofauti kwa Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD), katika Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia (NM-AIST) kilichopo mkoani Arusha, Aziza Konyo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amefanya utafiti na kuzalisha nzi chuma (black soldier flies) na mbolea kwa kuongeza thamani kwa kutumia mabaki hayo ya mkonge.

Akizungumza baada ya kikao cha uwasilishaji wa ugunduzi wa utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona amesema utafiti huo ambao umesajiliwa kwa hati miliki pia umebaini licha ya kuzalisha nzi chumaa hao ambao hutumika kama protini kwenye chakula cha mifugo lakini pia mabaki ya chakula wanachokula nzi chuma hao ni mbolea nzuri inayotumika katika mazao mbalimbali.

“Bodi imepokea wasilisho la utafiti huo na imefurahi kuona kwamba zao la mkonge linazidi kupata thamani kwa sababu tumezoea baada ya kupatikana singa basi kinachobaki chote ni uchafu kinatupwa.

“TSB ina mahusiano ya muda mrefu na Chuo cha Nelson Mandela katika kufanya tafiti mbalimbali kuhusu uongezaji thamani wa zao la mkonge. Kwa hiyo Aziza chini profesa wake Anthony Mshandete na Revocatus Machunda amefanya utafiti wa kuzalisha nzi chuma (black soldier flies) kutokana na mabaki ya mkonge (sisal waste) ambayo hutumika kama protini kwenye chakula cha mifugo jamii ya ndege wanyama na binadamu,” amesema Kambona.

Utafiti huu ni wa pili kufanyika na chuo hicho ambapo utafiti wa kwanza unatekelezwa na chuo hicho kwa ushirikiano na Serikali ya Denmark kupitia Shirika lake la Maendeleo (Danida), ambapo umejikita katika maeneo matatu ambayo ni uzalishaji gesi asilia, ujenzi na kile kitakachozalishwa kutokana na gesi asilia.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Carbonovia ya nchini  Uingereza, inayohusika masuala ya biashara ya hewa ukaa (carbondioxide) Dk. Mike Mason akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona jijini Tanga alipotembelea ofisi za bodi hiyo kwa ajili ya mazungumzo ya kufanya utafiti wa kuzalisha protini kutokana na mabaki ya mkonge, wengine ni watumishi wa TSB na Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia (NM-AIST).

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Bw. Saddy Kambona akipokea nzi chuma (black soldier flies) na mbolea kutoka kwa Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD), katika Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia (NM-AIST), kilichopo mkoani Arusha, Bi. Aziza Konyo ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) aliyefanya utafiti huo kwa kuongeza thamani kwa kutumia mabaki ya Mkonge (sisal waste).

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Carbonovia ya nchini  Uingereza, inayohusika masuala ya biashara ya hewa ukaa (carbondioxide) Dk. Mike Mason akimwonyesha protini iliyozalishwa na mabaki ya mkonge (sisal waste) Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona jijini Tanga alipotembelea ofisi za bodi hiyo kwa ajili ya mazungumzo ya kufanya utafiti wa kuzalisha protini hiyo ambayo ni gharama nafuu zaidi, wengine ni watumishi wa TSB na Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia (NM-AIST).





KINANA ACHAMBUA UBORA WA SHERIA MPYA YA UCHAGUZI

February 04, 2024

 *Awashauri CHADEMA kuacha maandamano


*Asisitiza umoja, mshikamano na maridhiano


Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Makamu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhman Kinana, ameshauri vyama vya siasa vya upinzani hususan CHADEMA kuacha kufanya maandamano yasiyo na msingi badala yake wathamini nia njema aliyonayo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuleta maridhiano na kuwatumikia Watanzania.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kufafanua kwa kina ubora wa sheria ya uchaguzi ambayo imepitihswa na Bunge hivi karibuni, baada ya wadau mbalimbali nchini kutoa maoni yao ambapo amesisitiza sheria hiyo ni bora kuliko iliyopo sasa.

Kinana aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na wana CCM na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, ambapo mbali ya kutumia muda mwingi kuzungumzia, maridhiano yaliyoingiwa kati ya CCM na CHADEMA pamoja vyama vingine vya upinzani, alisema kuna mambo mengi mazuri yamefanyika.

Alisema mambo mazuzi yamefanikisha kupata mwafaka ingawa CHADEMA haitaki kueleza ukweli ikiwemo serikali kukipatia chama hicho ruzuku ya Sh.bilioni 2.7 ambayo waliikataa kwa miaka mitatu nyuma.

Akielezea kuhusu sheria mpya, Kinana alisema pamoja na uzuri wake ikiwemo kuzingatia maoni ya wadau wakiwemo CHADEMA wenyewe, lakini bado kinasema haifai.

“Nilifikiri sheria hii mpya wangesema itatufikisha mbali zaidi, lakini wao wanasema hii haifai, basi turudi kule. Sheria ya sasa ni bora kwa muundo, kwa maudhui, kwa malengo, kwa dhamira sijui mnanielewa?. Nitumie nafasi hii kuwasihi ndugu zangu wa CHADEMA waungane na Watanzania waachane na mandamano, waangalie dhamira ya Rais.

“Hivi Rais na baraza lake la mawaziri kama wasingepeleka hii sheria mpya ya uchaguzi nani angemlazimisha? Lakini Rais busara imemuongoza akasema hapana hebu twende pamoja na mimi ndio mtetezi mkubwa wa maridhiano na ustahimilivu. Hebu tupeleke sheria mpya bungeni na kila hoja aliyopelekewa, aliyoambiwa kwamba haya ndio maoni ya wadau Rais akasema sawa, nakubali.

“Sasa niwasihi ndugu zangu Watanzania, tujipange kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, tujipange kwa uchaguzi mkuu mwaka 2025. Sheria hii ni nzuri, bora kuliko sheria yoyote iliyopo katika historia ya nchi yetu, inakidhi mahitaji na matakwa ya nchi na jumuiya ya madola, inakidhi mahitaji ya nchi za Umoja wa Afrika (AU), inakidhi vile vile mahitaji ya nchi za Kusini mwa Afrika ambao na sisi ni wanachama,” alisema.

Aliongeza kwamba hakuna tume ya miujiza zaidi itakayokuwepo, huku akifafanua kila jambo ambalo litafanyika lazima litakuwa na kasoro moja au mbili, na kuhoji kwani CHADEMA wao hawana kasoro?.

“Wanazo, sasa nawaambia ninyi chama kikuu cha upinzani kuweni basi na ustahimilivu kidogo, uungwana na kusikiliza wenzenu na kuona nia njema iliyopo katika Chama Cha Mapinduzi, kwa na serikali yake,” alisema.

Akifafanua zaidi Kinana alisema kuwa kushinda uchaguzi kunatokana na sera, mipango ya uchaguzi na kusikiliza watu, kwani unaweza kuwa na tume nzuri ya uchaguzi na matokeo yakawa ni ya hovyo, usiyoyataka.

Alitoa mfano wa moja ya nchi jirani ambayo walipigania sana kuwa na tume huru kwa miaka 20, wakaipata, lakini wamegombea mara nne hawakupata.

“Hawakuingia madarakani, wale waliotengeneza hiyo tume hawakupata, sasa wanasema Katiba hii haina maana waifute, wale walioingizwa na katiba baadae nao wakashindwa wanasema katiba hii haina maana. Kwa hiyo aliyeshinda anasema Katiba haina maana na aliyeshindwa naye anasema Katiba haina maana.

“Sasa kushinda uchaguzi sio Katiba tu, Nigeria baada ya wanajeshi kutoka baradakani walitengeneza Katiba mpya mwaka 1969 na kwa sehemu kubwa walienda kuchukua Katiba ya Marekani, tume ya uchaguzi ya Rais inateuliwa na Rais kwa kushauriana na baraza la ushauri.

“Baraza la ushauri ni nani? Rais ndio Mwenyekiti, makamu mwenyekiti ni makamu wa rais, wajumbe wengine marais wastaafu, hapo vipi? Kuna mtu anatoka nje ya mfumo?

“Hao ndio wanateua, mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa tume, uchaguzi unafanyika na watu wanakubali. Hapa tunatafuta malaika wa kuja kuongoza tume, kila utakachofanya unaambiwa kinakasoro, hivi mnavyoona yote tuliyokubali wanasema hamna kitu.

“Nimesikia wanaandaa maandamano Mwanza, Mbeya na Arusha na mimi nataka niwasaidie kutangaza kama watu wengine hamjasikia. Wanakwenda kueleza haya yaliyopitishwa na CCM na Bungeni hamna kitu.

“Tume si kila kitu, Namibia kamati inatengenezwa baada ya pale anayetua Rais, kuna nchi inaitwa Mauritius na hizi nchi zote ambazo nimezitaja ni za Jumuiya ya Madola, Rais anashauriana na watu wawili tu, anashauriana na waziri mkuu na kiongozi wa upinzani bungeni hakuna mtu mwingine,” alisisitiza.

“India wana mkurugenzi na wana makamishina. Nani anateua? Waziri Mkuu na Baraza lake la Mawaziri kwisha, yaani Rais Samia akae na baraza lake la mawaziri atengeneze orodha ateue, si moto utawaka hapa? Watasema tu maigizo.

“Sasa kuna shida hapa nchini kila unalofanya halina heri ndani yake, lakini vizuri haya mambo tukayaeleza maoni mengine yakatolewa unajua siku hizi kuna watu wanapita bila kupingwa lakini ni vizuri wanaopita bila kupingwa wakapigiwa kura ya ndio au hapana Bunge likasema sawa tumekubali.

“Wanauliza kwa nini? Wanasema kuna watu wengine wanafanya ujanjaujanja wa kupita bila kupingwa, hivyo wapigiwe kura tujue kama wanakubalika Bunge limesema sawa itapigwa kura ya ndio au hapana,” alisema.


KUHUSU MARIDHIANO

Akizungumzia maridhiano ambayo yamefanyika kwa nyakati tofauti, Kinana alisema kuwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani kulikuwa na wanachama wa CHADEMA wasiopungua 400 wako mahabusu wakikabiliwa na kesi zilizotokana na sababu mbalimbali za kiuchaguzi, lakini ulitengenezwa utaratibu wa kisheria waakachiwa huru.

Kinana alisema hakuna maridhiano bila ustahimilivu, Rais alialika taasisi za kidini na kiraia ili waelewane kujiuliza nini wanahitaji kwa lengo la kuhakikisha tunakuwa na taifa liwe la watu wenye mshikamano na kupendana.

Alisema Dk. Samia aliunda tume ya kusikiliza makundi ya Watanzania kusikiliza hoja zao ikiwemo Katiba, lakini mwishowe CHADEMA waligomea kwa sababu zao.

DC BUNDA: UWEPO WA TAWA WILAYANI BUNDA UNA MANUFAA MAKUBWA KWA WANANCHI

February 04, 2024

 Na. Beatus Maganja


Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vicent Anney amesema wananchi wa wilaya yake wananufaika sana na uwepo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kutokana na ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotokana na shughuli za uwindaji wa kitalii unaofanyika katika Pori la Akiba Grumeti.

Dkt. Vicent ameyasema hayo Februari 02, 2024 wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyofadhiliwa na TAWA wilayani humo.

"Nichukue nafasi hii kuishukuru TAWA kwa uwepo wake katika wilaya ya Bunda, pia tunaishukuru Serikali kwa mipango yake kwasababu imetusaidia sisi wananchi wa Bunda kupata huduma mbalimbali za kijamii ambazo zimetokana na gawio linalotokana na shughuli za uwindaji zinazofanywa katika maeneo ya Bunda " amesema

Mkuu huyo wa wilaya amesema TAWA imefadhili miradi miwili katika Kata ya Hunyari Kijiji cha Sarakwa ambayo ni darasa moja (1) na Ofisi moja (1) ya Mwalimu Mkuu, samani za shule ambazo ni jumla ya madawati 100, vitu vya walimu 12, meza 5 za walimu na mantenki matatu yenye ujazo wa Lita 2000 kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kuhifadhi maji pamoja na nyumba mbili (2) za walimu ambazo zimesaidia kuboresha ufundishaji kwa kuwa walimu wanakuwa na utulivu wa mawazo

Wananchi wa kijiji cha Sarakwa wameishukuru Serikali na kukiri kuwa TAWA ndiyo taasisi pekee iliyojitokeza kufadhili miradi mikubwa katika Kijiji hicho tangu kuanzisha kwake, baada ya wananchi kuhangaika kwa muda mrefu kukamilisha miradi hiyo kwa nguvu zao bila mafanikio na hivyo kukibatiza Kijiji chao kwa jina la "Kijiji cha TAWA".

"Tangu kuanzishwa kwa Kijiji hiki Mwaka 2014, Kijiji hiki na shule hii (Shule ya Msingi Steven Wasira) haikuwahi kupata mradi wowote, TAWA pekee ndiyo imekuwa ya kwanza kutoa mradi mkubwa wa madawati 100, kumalizia chumba cha darasa moja (1), meza 5 na viti 12 vya walimu na ofisi 1 ya walimu kwahiyo Kijiji hiki tunakipa jina TAWA" amesema Mwenyekiti wa Kijiji Kijiji cha Sarakwa Giragu Gisunu Nyarumuga

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Steven Wasira Paulo Kisumda amesema miradi hiyo iliyofadhiliwa na TAWA katika Kijiji cha Sarakwa imesaidia kupunguza migongano kati ya wananchi na wanyamapori ambapo amekiri kuwa awali walikuwa wanawachukia Wanyamapori lakini tangu waanze kupata miradi hii wamegundua wanyamapori wana faida kubwa, na wao kama wananchi ni sehemu ya wamiliki wa rasilimali hiyo hivyo wataongeza ushirikiano katika kuwalinda na kuwahifadhi.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikifanya mambo makubwa kwa wananchi kupitia taasisi hiyo, hivyo TAWA imejidhatiti kuuhabarisha umma wa watanzania kwa kufanya ziara wilaya kwa wilaya, vijiji kwa vijiji kuhakikisha wanaelewa umuhimu na faida za shughuli za uwindaji wa kitalii Nchini.







KATIBU WA SUKI AWAONYA WANACCM WENYE KUENEZA SIASA CHAFU KWA VIONGOZI.

February 04, 2024

 NA WILLIUM PAUL, MOSHI.


WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi wameonywa kuachana na tabia ya kufanya siasa chafu ya kuwachafua viongozi waliopo madarakani na Chama kitaendelea kuwalinda viongozi hao.

Hayo yamesemwa leo na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI) na Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM, Rabia Abdallah Hamid wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro zilizofanyika kata ya Kindi wilaya ya Moshi.

Alisema kuwa, muda wa kufanya kapeni haunafika kwani Chama kinatambua kwa sasa kinawabunge na madiwani na kuwaonya wale wote wenye nia ya kugombea nafasi hizo kusubiri mpaka muda utakapofika.

"Niwaonye wanaccm kuacha tabia ya kufanya siasa chafu kwa viongozi wetu waliopo madarakani sisi tunawatambua waliopo madarakani na tutawalinda ili watimize wajibu wao na kutekeleza Ilani ya CCM" Alisema Rabia.

Na kuongeza "Wabunge na Madiwani hawana shida ila shida wanaletewa na watu wenye uchu wa madaraka ambao wamekuwa wakifanya siasa chafu za kuwachafua sasa niwaonye wanachama wenye nia hiyo kuacha".





RAIA AUSTRIA AWEKA REKODI YA KUPANDA KILIMANJARO MARA 150

February 04, 2024

 

Raia wa Austria Rudi Stangl (62) mwenye miwani (katikati) akiwa na waongoza watalii mara baada ya kufanikiwa kufika kilele cha Uhuru ,Mlima Kilimanjaro kwa mara 150 akifanya kazi ya kupandisha wageni kwa muda wa miaka 30 .
Raia wa Austria Rudi Stangl (62) akiwa njiani kuelekea kilele cha Uhuru Mlima Kilimajaro 
Mhifadhi Vitus Mgaya kutoka idara ya Utalii (KINAPA) akimpongeza na kumvisha medali Rudi Stangl mara baada ya kushuka kutoka kilele cha Uhuru alipopanda kwa mara ya 150 .

 Na Dixon Busagaga- Kilimanjaro 

RAIA wa Austria Rudi Stangl (62) amejiwekea rekodi ya kupanda na kufika kilele cha Uhuru ,Mlima Kilimanjaro mara 150 akifanya kazi ya kupandisha wageni kwa muda wa miaka 30 ,rekodi aliyoanza kuitafuta tangu mwaka 1982 .