Kocha wa Simba Dylan Kerr Akimkabidhi Hamisi Kiiza Tunzo Zawadi ya Mchjezaji Bora wa Simba sport Club Mwezi September 2015
Katika
kuongeza morali na kuwazawadia wachezaji wanaofanya vizuri, Klabu ya
Simba ilianzisha Tunzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi kuanzia mwezi wa
Septemba 2015.Mshindi wa mwezi wa September, 2015 ni Hamis Kizza ambapo
amepata kura 250 kati ya kura 411 zilizopigwa na mashabiki na wapenzi wa
Simba na soka wa Tanzania kwa ujumla kupitia simu za mkononi ambao pia
wamejiunga na huduma ya Simba News.Akikabidhiwa tunzo na kocha mkuu wa
Simba Dylan Kerr, mshambuliaji wa kimataifa Hamis Kizza alisema
“namshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kufanikiwa kuwa mchezaji wa
Kwanza kabisa kuchukua tunzo ya mchezaji bora kwa mwaka 2015, napenda
kuwaahidi wapenzi na mashabiki wangu katika mchezo wa soka kuwa sasa hii
ndio itakuwa chachu yangu ya kufanya vizuri zaidi nikiwa na klabu yangu
ya Simba”.
Kocha
Kerr alipata nafasi ya kuongea na wachezaji baada ya kugawa Tunzo na
Tsh 500,000 kwa mchezaji bora ambapo alisema “Simba Nguvu Moja,
wachezaji wangu huu ni wakati wa kutoa ushindani mkubwa sana kwenye
mchezo wetu wa soka, viongozi wamekuja na wazo la kutoa mchezaji bora na
kila mtu hapa anaouwezo wa kuwa mchezaji bora ni kwa kufanya mazoezi,
nidhamu ya mchezo ukiwa uwanjani na hata nje ya uwanja na kujituma hapo
unaweza kuwa mchezaji bora wa mwezi”.Akizungumza leo jijini Dar es
salaam Rais wa Simba Evans Aveva alisema “Uongozi, wanachama na wapenzi
wa Simba wanathamini mno mchango wa wachezaji katika kuifanya timu yetu
ifanye vizuri, hivyo tumeona ni jambo la busara kuwa klabu ya kwanza
Nchini Tanzania kuwa na tunzo za mchezaji wake bora. Tunaamini kuwa
Tunzo ya Mchezaji bora wa mwezi wa Simba itaongeza ari na kujituma kwa
wachezaji wetu. Sisi tukiwa kama viongozi ni kazi yetu ya msingi
kuhakikisha kuwa wachezaji wetu hasa wale wanaojituma zaidi
wanatambuliwa na kuenziwa’’.Akizungumza jinsi tunzo ya mchezaji bora
itakavyoendeshwa, Mkurugenzi Mkuu wa EAG Group ambao ni washauri na
watekelezaji wa Masoko na Biashara wa Simba, Imani Kajula alisema
“Wanachama na wapenzi wa Simba na wapenda michezo ndio watakao kuwa
wanachagua mchezaji bora wa mwezi kwa kutuma jina la mchezaji
wanayempendekeza kwenda kwenye namba 15460, Ni wale tu ambao wamejiunga
na Simba News kupitia mtandao wa Voda na Tigo wataweza kupiga kura
kuchagua mchezaji bora wa mwezi wa Simba’’
Tukumbuke
kuwa unaweza kumchagua mchezaji bora wa mwezi ukiwa umejiunganisha na
huduma ya Simba News kwa kutuma jina la mchezaji kwenda namba 15460.
Zoezi la kumchagua mchezaji bora wa mwezi wa October, 2015 linaanza
tarehe October 10, 2015. Piga kura mara nyingi zaidi kuweza kumpata
mchezaji wako bora wa Mwezi October, 2015.
Simba
News ni huduma iliyoanzishwa na Simba ili kuwapa wapenzi wa Simba
habari mbalimbali za Simba popote pale walipo ikiwemo matokeo, majina ya
wachezaji wanaocheza mechi, usajili na habari nyingine za klabu ya
Simba. Kujiunga na Simba News tuma neno Simba kwenda namba 15460 ni
maalum kwa Tigo na Vodacom.