Na Beatrice Lyimo-Maelezo Dar es Salaam.
…………………………………………………
SERIKALI imesema itaendeleza
uhusiano na ushirikiano wake na Jamhuri ya Watu wa China kwa kuimarisha
fursa mbalimbali za kijamii ikiwemo nyanja ya kiutamaduni.
Hayo yamesemwa Jumatatu (Oktoba
12, 2015) Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw.
Assah Mwambene wakati wa halfa ya uzinduzi wa chaneli mpya ya filamu ya
China –Africa Movies itakayoonyeshwa kupitia kituo cha televisheni cha
Easy Television kilichopo nchini.
Bw. Mwambene amesema kuwa uwepo
wa chaneli hiyo utasaidia wazalishaji wa Tanzania kuonekana na
kujulikana kimataifa na kuweza kujiongezea kipato na fursa kwa waandaaji
hao.
“Chaneli hii itawapa fursa kwa
pande zote mbili kwani filamu ya Tanzania itaonyeshwa china na
kutafsiriwa kwa lugha yao na kwa upande wa Tanzania filamu za china
zitaonyeshwa hapa Tanzania na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili”
Aidha Mwambene alisema Chaneli
ya China –Africa movies, licha ya kuwa daraja la kujifunza tamaduni za
kichina pia itatoa fursa kwa Watanzania kuweza kujifunza mbinu
mbalimbali za biashara na kufungua milango kwa Watanzania kufahamu hatua
mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kiutamaduni.
Mwambene ameitaka Idara ya
filamu nchini China kuitembelea Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na
Utamaduni kwani ina kitengo kinachohusika na filamu za ndani.
Kwa upande wake Waziri wa Radio,
Televisheni na usimamizi wa filamu wa Jimbo la Henan, China Bi. Song
Fengxian alisema Serikali ya China itaongeza ubunifu kwa watazamaji wa
pande zote mbili na kuwashukuru wadau wote waliosaidia kufanikisha
uzinduzi wa filamu hiyo.
Naye mwakilishi wa Kituo cha
EASY TV Bi. Sophia Selis alisema kuwa katika kuendeleza urafiki baina ya
Tanzania na China, kituo cha Easy Television imekuwa mstari wa mbele
katika kuhamasisha, kujifunza na kubadilishana utamaduni kulingana na
wakati.
“Tunarusha program zetu kwa
kutumia lugha mbalimbali ikiwemo kiingereza, kichina, kiarabu, kihindi
na Kiswahili ili kukidhi tija za watazamaji wetu wa mataifa mbalimbali
kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayotoa picha zenye ubora” alisema Bi.
Selis.
Easy television inarusha jumla
ya chaneli 33 vya televisheni ikiwemo filamu, muziki, burudani, michezo,
matukio, habari, vipindi vya watoto.