Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu Oktoba 12,
2015 kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi hiyo jijini Dares
Salaam kuhusiana na masuala ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu na baada ya
uchaguzi huo.
Picha zote na Magreth Kinabo-Maelezo.
Msanii Mrisho Mpoto akizungumza na
waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi hiyo
jijini Dares Salaam kuhusiana na masuala ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu
na baada ya uchaguzi huo.
Mwanamziki wa nyimbo za injili
nchini, Christina Shusho akizungumza na waandishi wa habari kwenye
ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi hiyo jijini Dares Salaam
kuhusiana na masuala ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu na baada ya
uchaguzi huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
………………………………………………………………….
Na Magreth Kinabo-maelezo
Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya
Siasa imewaasa na kuwataka viongozi wote wa vyama vya siasa kutoa
kauli na maelekezo kwa wafuasi wao na wanachama wa vyama vyao
kutoshiriki katika aina yoyote ile ya uvunjifu wa amani hususan katika
kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu na baada ya uchaguzi huo.
Hayo yamesemwa leo na Msajili
wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi wakati akizungumza na waandishi
wa habari leo kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi hiyo jijini
Dares Salaam.
“Dhamana ya nchi iko mikononi
mwenu,ushawishi wenu kuhusu amani katika kipindi hiki ndio utakaoliokoa
taifa la Tanzania ama utaliingiza taifa katika vurugu na mfarakano,”
alisema Jaji Mutungi.
Jaji Mutungi alisema katika
kipindi cha kampeni kumekuwepo na viashiria vya uvunjifu wa amani
miongoni mwa jamii yakiwemo baadhi ya makundi ya wanachama, wafuasi na
mashabiki wa vyama siasa.
“Makundi hayo yanadiriki kutoa
maneno ya kejeli, matusi, kuvamia, kupigana, hata kujeruhi makundi
mengine, ambayo siyo ya upande wao. Hali iiachwe mara moja ili kuiweka
nchi yetu Tanzania katika hali ya amani na kuiepusha kuingia kwenye
vurugu, mfarakano na machafuko yasiyokuwa na ulazima.
“Dumisheni amani na kamwe
tusijiingize kwenye siasa zinazoleta mfarakano na uvunjifu wa amani,
kumbukeni kuna maisha baada ya uchaguzi na amani ya nchi yetu ni
fahari yetu sote,alisema Mutungi.
Aliongeza ni vyema Watanzania,
wakatambua kwamba utofauti wa itikadiya vyama ndio ukomavu wa demokrasia
nchini hivyo ni jambo la busara kuvumiliana na kufanya siasa za
kiustaarabu.Hivyo kutovumiliana kwa utofauti wetu wa itikadi za kisiasa
kunaweza kulata madhara makubwa kwa jamii itakatopelekea idadi kubwa ya
Watanzania kupata athari ikiwemo ulemavu, vifo, ukimbizi,njaa na
maradhi.
Aidha ofisi hiyo imetoa rai kwa
waandishi wa habari watumie kalamu zao vysema kuhubiri amani na kuepuka
kuandika habari za uchochezi, bali wawasaidie wananchi kupata taarifa
sahihi zitakazowasaidia kufanya maamuzi wakati wa kuchagua viongozi wao.
Kwa upande wao mabalozi wa
amani, ambao ni Mrisho Mpoto na Christina Shusho walisema kwa nyakati
tofauti kuwa wamejitolea kuhubiri amani kupitia fani yao ili nchi yetu
iendelee kuwa na amani.
Akizungumzia suala hilo, Mpoto
aliwapa changamoto waandishi wa habari wajiulize kuwa wana mchango
gani katika nchi yao ili kuhakikisha inakuwa na amani. Hivyo
wanapoandika habari yoyote wakumbuke kwamba kuna watoto, yatima,
walemavu na wajane, isije ikawa ni chanzo cha kuvuruga amani.
Naye Shusho alisema kwamba yeye si mfuasi wa chama chochote,bali balozi wa kuhubiri amani.
Ofisi hiyo imetoa kauli hiyo,
kwa kuwa ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha ukuaji wa demokrasia
unakuwepo kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kikatiba.