MFUMUKO WA BEI WA TAIFA WAONGEZEKA

August 11, 2015

unnamed (78)

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya kuongezeka kidogo kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Mei 2015 leo jijini Dar es salaam.Mfumuko wa Bei wa  bei kwa mwezi Julai ,2015 umefikia asilimia  6.4   kutoka asilimia 6.1 iliyokuwepo Juni 2015.
……………………………………………………………
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
11/8/2015. Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai 2015 na kusema kuwa umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.4  kutoka asilimia 6.1 iliyokuwepo mwezi Juni 2015.
Hii inamaanisha kuwa  kasi ya upandaji wa bei ya  bidhaa na huduma kwa mwezi Julai 2015 imeongezeka ikilinganishwa na kasi ya upandaji bei ya bidhaa na huduma  iliyokuwepo mwezi Juni mwaka 2015.  
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam amesema kuongezeka huko kumesababishwa na kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Amezitaja bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko huo kutokana na upandaji wa bei katika masoko kwa mwezi Julai 2015 kuwa  ni mchele kwa asilimia 27.9,mahindi asilimia 2.3, unga wa muhogo asilimia 9.2, nyama asilimia 4.5, samaki 12.2, na maharage asilimia 5.9.
Kuhusu Fahirisi za Bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei ya bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya binafsi hapa Tanzania, Kwesigabo  amesema zimeongezeka hadi kufikia 158.78  kutoka 158:12 za mwezi Juni.
Amesema kuongezeka kwa fahirisi za bei kumechangiwa na ongezeko la bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo gesi ya kupikia kwa asilimia 3.7, mafuta ya dizeli 5.9, mafuta ya Petroli ailimia 4.9,  unga wa mahindi asilimia 2.5, ulezi asilimia 2.9, samaki asilimia 4.8, viazi vitamu asilimia 2.6 na ndizi za kupika asilimia 3.4.
Kwesigabo amesema uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi Julai , 2015 umefikia shilingi 62 na senti 98 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi 63 na senti 24  za mwezi Juni 2015. 
“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi Julai ,2015 na  umepungua  hii ina maana kuwa sasa mtu anahitaji kuongeza ziada ya shilingi 38 ili aweze kununua bidhaa na huduma sawa na zile alizokuwa na uwezo wa kuzinunua katika mwezi Juni”
Kwa upande wa mfumuko wa Bei kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwezi Julai, 2015 Bw.Kwesigabo amesema kuwa una mwelekeo unaofanana , Kenya umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 6.62 na kutoka 7.03 mwezi Juni 2015 huku Uganda ikiwa na mfumuko wa Bei wa  asilimia 5.4  kutoka asilimia 4.9  za mwezi Juni, 2015.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »