IBF Africa, Miss Tanzania 2012 Brigitte Alfred waandaa ngumi za kulipwa kuchangia albino

August 11, 2015

unnamed (95)
Rais wa IBF Africa, Onesmo Ngowi (wa kwanza kulia) akizungumzia mapambano ya ngumi ya kulipwa yaliyopangwa kufanyika Novemba 28 jijini kwa ajili ya kutafuta fedha za uchangia watu wenye ulemavu wa ngozi(albino), wa pili kulia ni Miss Tanzania 2012 Brigitte Alfred na wa Rais wa TPBO Limited, Yasin “Ustadh” Abdallah.
unnamed (96)
Miss Tanzania 2012, Brigitte Alfred (wa pili kushoto) akiwa na viongozi wa juu wa ngumi za kulipwa nchini, Onesmo Ngowi (Rais wa IBF Africa, wa kwanza kushoto), Emmanuel Mlundwa (rais wa PST) na Yasin Abdallah (Rais wa TPBO-Limited) mara baada ya kutangaza mapambano ya ngumi ya kulipwa yaliyopangwa kufanyika Novemba 28 jijini kwa ajili ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuchangia watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).
………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu
Shirikisho la Ngumi za kulipwa la Afrika (IBF Africa) kwa kushirikiana na Taasisi ya Miss Tanzania 2012, Brigitte Alfred Foundation (BAF) na kampuni ya Kango wameandaa mapambano ya ngumi ya kimataifa kwa kushirikisha mabondia nyota duniani.
Mapmbano hayo yamepangwa kufanyika Novemba 28 kwenye ukumbi wa Mlimani City na lengo lake kubwa ni kutafuta fedha za kusaidia watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Rais wa IBF Africa, Onesmo Ngowi alisema kuwa siku hiyo imepewa jina la  “knock out albinos killers” (piga wanaua albino) ambapo bondia kutoka Denmark, Lolenga Mock atapigana na bondia nyota wa Zambia, Chioctha Chimwemwe  katika pambano la uzito wa super middle la  IBF continental Africa super.
Pambano hilo limepangwa kuwa la raundi 12 na litafuatiwa na pambano lingine la kulipiza kisasi kati ya bondia kutoka Afrika Kusini, Phillip Ndou atakayepambana na Mtanzania, Ramadhan Shauri kuwania ubingwa wa IBF-Continental Africa welterweight  ambalo pia litakuwa la raundi 12.
Bondia nyota wa Tanzania, Cosmas Cheka naye atapanda ulingoni kupambana na Gottlieb Ndokosho wa Namibia kuwania ubingwa wa IBF continental Africa super-feather.
Mabondia wa Kenya, Geoffrey Munika na James Onyango nao wataingia ulingoni kupambana na mabondia kutoka china na Iran ambao watajulikana baadaye.
Pia kutakuwa na pambano mengine ambayo yatawakutanisha mabondia wanawake, Lulu Kayage dhidi ya bondia atakayetangazwa baadaye kuwania ubingwa wa IBF Africa flyweight.
“Lengo ni kutafuta fedha za kuchangia kununua vifaa maalum kwa albino na mpaka sasa maandalizi yanaenda vizuri, hii ni tukio kubwa sana kwa ngumi za kulipwa hapa nchini,” alisema Ngowi.
Alisema kuwa wameamua kushirikiana na Brigitte kutokana na kutambua juhudi zake za kutetea albino baada ya kuwajengea bweni eneo la Buhangija, Shinyanga na taasisi yake kwa kushirikiana na Junior Achievements (JA) wanatoa elimu ya ujasiriamali kwa jamii hiyo.
“Brigitte akiwa mwenye mashindano ya urembo ya dunia, 2012, aliweka rekodi ya kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya ‘urembo wenye malengo maalum” au Beuty with purpose”, alipeleka kazi yake ya ujenzi wa bweni la albino mkoani shinyanga, imetupa faraja sana na kuamua kumuunga mkono katika vita hiyo,” alisema.
Brigitte alishukuru kuungwa mkono na kuomba wadhamini kujitokeza kusaidia shughuli hiyo ambayo baada ya ngumi, pia kutakuwa na mbio za marathon mkoani Kilimanjaro zenye lengo hilo hilo.
“Tumeandaa mbio za Marathon mkoani Kilimanjaro wiki moja baada ya ngumi, mbali yam bio hizo, pia kutakuwa na zoezi la kupanda mlima Kilimanjaro, lengo ni kutafuta fedha na vile vile kutangaza utalii wetu, naomba makampuni yajitokeze,” alisema Brigitte.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »