VIJANA NCHINI WATAKIWA KUJITOLEA KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

August 11, 2015

1
Mkurugenzi  wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, James Kajugusi akiongea na Vijana kutoka sehemu mbalimbali (hawapo pichani) waliohudhuria Kongamano la Vijana lililofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
2
Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizaraya Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celistine Mushy akitoa mada kwa vijana waliohudhuria Kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
3
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, James Kajugusi akisisitiza jambo kwa wanahabari mara baada ya kufungua Kongamano la Vijana lililofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo (jana).
4
Baadhi ya Vijana wakipima afya wakati wa Kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo (jana).
5
Mwakilishi Mkazi UNFPA Tanzania, Dr. Natalia Kanem akiongea na vijana waliohudhuria Kongamano la Vijana lililofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo (jana).
………………………………………………………………………….
Benjamin  Sawe  Melezo.Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa ushiriki wa Vijana katika shughuli mbalimbali bado ni mdogo kutokana na ukweli kwamba vijana wengi bado hawana utamaduni wakujitolea katika masuala ya maendeleo. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga wakati wa ufunguzi wa Siku ya Kimataifa ya Vijana Duniani iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam. Bw. Kajugusi alisema vijana wengi pia hawana elimu ya stadi za maisha, uzalendo, uraia pamoja na stadi za uongozi ikiwa ni pamoja na moyo wa kujituma na kutafuta taarifa na fursa muhimu hasa zile zinazohusu maendeleo yao. “Ni vigumu mtu kujua jambo linaloendelea mahala kama hafanyi utafiti wa kutosha juu ya mambo yanayoendelea”.AlisemaBw. Kajugusi. Amewaasa kutumia mitandao ya vijana katika ngazi za Kata na Wilaya pamoja na taasisi za kiraia ili waweze kuonekana na kupaza sauti zao. Amesema ni jukumu la Vijana kuhakikisha wanajiunga na Baraza la Vijana la Taifa ili waweze kuwa na sehemu muafaka ya kujadili mambo yanayohusu maendeleo yao ikiwa ni pamoja na kuwa na uwanja mpana wa kuishauri serikali kuhusu masuala yanayowahusu. “Hivi sasa Serikali ina shughulikia mchakato wa uundwaji wa Baraza la Vijana la Taifa ambapo tayari Mswada huo umesharidhiwa na Bunge na Mh. Rais kutia saini uundwaji wake na mara Baraza hili litakapoundwa kwa mujibu wa sheria mtakuwa na chombo madhubuti cha uwakilishi wenu katika ngazi mbalimbali za maamuzi Kitaifa na Kimataifa”.AlisemaBw. Kajugusi. Wakati huo huo Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizaraya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Celistine Mushy amewashauri vijana nchini kufanya kazi na taasisi za Umoja wa Mataifa ili kujijengea uzoefu wa kujieleza ikiwa ni pamoja na kujiamini. “Vijana wengi hamjiamini na washauri mfanye kazi na haya mashirika ya Umoja wa Mataifa, huko ndipo sehemu muhimu sana ya kujipatia uzoefu kwani mtafanya kazi na watu kutoka mataifa mbalimbali na ambao wana uzoefu wa hali ya juu”.Alisema Balozi Mushy. Siku ya Kimataifa ya Vijana ilianza tangu mwaka 1991 nchini Australia ikiwa na lengo la kuziwezesha Jumuiya za Kimataifa na Jamii kwa ujumla kupata fursa ya kusheherekea na kutambuana fasi ya vijana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi zao Maadhimisho ya Siku ya vijana hufanyika kila Agosti 12 ambapo mwaka huu kilele chake kitafanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja na kaulimbiu yake ni Ushiriki wa Vijana kwenye Maamuzi ya Maendeleo

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »