Kikosi cha Timu ya Taifa ya
Tanzania (Taifa Stars) kimeanza mazoezi katika uwanja wa Karume
kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria kuwania kufuzu kwa Fainali za
Mataifa ya Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Wachezaji wa Taifa Stars chini ya
kocha wake mkuu Charles Mkwasa watakua wakijifua mara mbili kwa siku
asubuhi na jioni katika uwanja wa Karume katika kujiweka fit na
maandalizi ya mchezo huo.
Kufuatia baadhi ya wachezaji kuwa
na majukumu na timu zao kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Hisani
utakaochezwa Agosti 22, Mkwasa amewaongeza wachezji wengine kumi (10)
kutoka katika orodha yake ya akiba.
Lengo la kambi hii ya awali ya
siku tano, ni kocha mkuu pamoja na benchi lake la ufundi kupata nafasi
ya kuwaona wachezaji katika mazoezi hayo kabla ya safari ya kuelekea
nchini Uturuki Agosti 23 mwaka huu kwa kambi ya siku kumi.
Wachezaji walioitwa na kuanza
mazoezi leo ni Said Mohamed, Vicent Andrew (Mtibwa Sugar), Mohamed
Hussein, Ibrajim Hajibu (Simba SC), Hamis Ali, Juma Mbwana (KMKM), Tumba
Sued (Coastal Unioni), Samuel Kamuntu (JKT Ruvu), Ibrahim Hilka
(Zimamoto– Zanzibar) na Mohamed Yusuf (Prisons).
Wachezaji wengine waliopo kambini
ni Said Ndemla, Hassan Isihaka, Abdi Banda(Simba SC), Rashid Mandawa
(Mwadui FC), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Orgeness Mollel (Aspire
Academy) na Abdulhaman Mbambi (Mafunzo).
TWIGA STARS KUIVAA HARAMBEE STARLETS
Timu ya Taifa ya Tanzania ya
Wanawake (Twiga Stars) iliyopo kambini kisiwani Zanzibar, inatarajiwa
kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya Wanawake kutoka Kenya
(Harambee Starlets) Agosti 23, 2015.
Mchezo huo wa kirafiki utachezwa
katika uwanja wa Aman Kisiwani Zanzibar, ikiwa ni sehmu ya maandalizi ya
kikosi hicho kujiandaa na fainali za Michezo ya Afrika (All Africa
Games) zitakazofayika nchini Congo-Brazzavile kuanzia Septemba 4 – 19,
2015.
Twiga Stars inaendelea na mazoezi
kutwa mara mbili katika viwanja vya Aman na Fuoni chini ya kocha wake
mkuu Rogasian Kaijage kujiandaa na fainali hizo za michezo ya afrika,
wachezaji wote waliopo kambini wapo katika hali nzuri wakiendelea
kujifua na michezo ya Afrika.
USAJILI
Dirisha la usajili limeongezwa
toka tarehe 06 Agosti hadi tarehe 20 Septemba, baada ya muda huo klabu
itakayochelewesha kuleta usajili wake itatozwa kiasi cha shilingi laki
tano (Tsh 500,000) kwa kila mchezaji itakayemsajili mpaka siku ya tarehe
30 Agosti.
Mwisho wa kufanya uhamisho wa kimataifa wa wachezaji kwa njia ya mtandao TMS ni tarehe 6 Septemba.
Kikao cha kamati ya sheria
kitakaa tarehe 28 kwa ajili ya kuupitisha usajili na kitakaa tena tarehe
8/9/2015 kwa ajili ya kupitisha usajili.
Kuanzia tarehe 21 hadi 27 itakuwa
ni wiki ya pingamizi, ambapo majina yatabandikwa TFF Karume na kuwekwa
kwenye mtandao ili kuwezesha vilabu vyenye pingamizi kuwawekea wachezaji
mapingamizi.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)
inatarajiwa kuanza tarehe 12 Septemba 2015, Daraja la kwanza (FDL)
ikitarajiwa kuanza Septemba 17 na Ligi Daraja la pili inatarajiwa kuanza
Oktoba 16 mwaka huu.
MICHUANO YA COPA COCA-COLA 2015
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) bado linaendelea na mazungumzo na wadhamini wa michuano
hiyo (Coca-Cola). Kutokana na mazungumzo hayo, ratiba ya michuano hiyo
itachelewa kutoka.
Hivyo, tunawaomba kuwa na uvumilivu wakati mchakato wa mazungumzo hayo yanayokaribia ukingoni ukiendelea.
UAMUZI WA KAMATI YA RUFAA YA TFF
JUU YA RUFAA YA DR. DEVOTA JOHN MARWA,YA MAAMUZI YA KAMATI YA UCHAGUZI
WA SOKA LA WANAWAKE (TFF)
Mwomba rufani, Dr. Devota John
Marwa, (Mrufani) ni msomi mbobezi katika taaluma ya michezo, akiwa ni
mhadhiri katika kitengo kinachojihusisha na taaluma ya michezo katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akiamini kwamba anakidhi vigezo
vilivyowekwa kwa nafasi ya mgombea uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu
wa Wanawake(TWFA), alichukua fomu ya kuomba kugombea nafasi ya
Mwenyekiti wa Chama hicho.
Maombi hayo yalikumbana na
pingamizi zilizoletwa na wakereketwa wawili wa soka la Wanawake, Bi.
Chichi Mwidege na Bi. Mwajuma Noty, ambao kwa pamoja walimwekea
pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi matakwa ya kanuni za ugombea wa nafasi
ya Mwenyekiti.
Waleta mapingamizi walidai kuwa
Mrufani hakuwa na sifa zilizoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi za
T.F.F. (TFF Electoral Code) Ibara ya 9 (tisa) kipengele cha 3 (tatu),
kinachomtaka mgombea awe amejihusisha na uongozi wa mpira wa miguu kwa
muda usiopungua miaka mitano.
Aidha Ibara ya 28 (ishirini na
nane) kipengele cha 3 (tatu), kinamtaka mgombea awe amejihusisha japo
miaka 2 (miwili) katika shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Kamati ya Uchaguzi iliridhia mapingamizi hayo na kuliondoa jina la
Mrufani katika orodha ya wagombea wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti. Rufani
hii ni matokeo ya uamuzi huo wa Kamati ya Uchaguzi uliotolewa taraehe 22
Julai, 2015.
Kwa ujumla, sababu za kupinga
maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi zinaweza kuhesabiwa kuwa ni mbili. Moja ni
iliyojikita juu ya hitilafu katika kuamua kwamba Mrufani hakuwa na
uzoefu katika uongozi wa soka kwa muda ulioainishwa. Sabau nyingine ni
kwamba Kamati ya Uchaguzi illibua sababu ambayo haikuwa katika Hati ya
pingamizi iliyoletwa na Mleta pingamizi.
Wakati ambapo Mleta pingamizi
alijikita katika kipengele cha 28(3), Kamati iliibua kipengele cha
28(8), cha Katiba ya TWFA kinachomtaka mgombea awe ametimiza uzoefu wa
uongozi wa miaka mitano, ambacho hakikuwemo katika hoja za pingamizi
zilizowasilishwa na mleta pingamizi.
Katika kufikia uamuzi wake,
Kamati ya Rufani ilizipitia sababu za Mrufani kama zilivyoletwa, na
baada ya kusikiliza maelezo ya Mrufani na hoja za Mwakilishi wa TFF,
Wakili Msomi Edward Augustino, na imeamua kama ifuatavyo. Tutaanza na
hoja ya mwisho.
Je, Kamati ilikuwa sahihi kuibua
kipengele ambacho hakikuletwa katika hati ya mapingamizi? Kamati inaweza
kuibua kipengele hicho endapo kwa kufanya hivyo, itakuwa imejielekeza
katika nia njema ya maslahi ya suala linalozungumziwa.
Sharti jingine ni kwamba hoja
hiyo inyoibuliwa isiwe na athari hasi(prejudicial) kwa mhusika. Kaika
suala hili hata hivyo, hoja iliyoletwa na Mleta pingamizi, yaani hoja
chini ya kifungu cha 28 (3), imeainisha kipindi kifupi cha uzoefu
(miaka 2), na hoja iliyoibuliwa na Kamati inahitaji uzoefu wa miaka 5.
Endapo Mrufani angekuwa na uzoefu
wa miaka 3 hadi 4, bado angekwama kutokana na hoja iliyoibuliwa na
Kamati. Hii kwa vyovyote ingekuwa ni athari hasi (negative impact)
katika harakati za Mrufani. Ni vema
Kamati zinazosikiliza malalamiko
zikajikita kwenye malalamiko yaliyoletwa na wahusika wenyewe. Kama
pigamizi lingekuwa liko juu ya kipengele hicho tu, tusingesita
kukubaliana na sehemu hii ya rufani. Hata hivyo, takwa la uzoefu wa
miaka 5 limeainishwa pia katika Ibara ya 9 (3), ambayo ilikuwa ni sehemu
ya mapingamizi yaliyokuwepo kwenye hati ya mapingamizi.
Kwa sababu hiyo, Kamati ya Rufani
haioni kama hoja hiyo ina mashiko. Haitaitilia maanani. Hoja kuu ndani
ya rufaa hii ni je, Kamati ya Uchaguzi ilijielekeza vema kuhusu suala la
uzoefu wa uongozi ulioainishwa na Katiba?
Mrufani ameieleza Kamati ya
Rufani mlolongo wa shughuli ambazo amekuwa akizifanya, nyingi zikiwa
zimejikita zaidi katika taaluma. Miongoni mwa shughuli hizo ni kuandaa
Mpango Mkakati wa kuendeleza soka la wanawake. Mpango huu uliridhiwa na
kuwasilishwa Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira Duniani, yaani FIFA.
Maelezo mengine ni kushiriki
katika kuongoza timu mbali mbali kule Chuo Kikuu, zingine zikiwa za
watoto wadogo ambao baadhi ya matunda yake ni wachezaji walioibukia
kwake kama vile Simon Msuva. Alisema zaidi kuwa alishiriki kuandaa
warsha ilizoandaliwa kwa ushirikiano kati ya FIFA na TFF.
Aidha. Alisema kuwa amekuwa
kiongozi tangu akiwa bado kwenye vyuo vya ualimu, na baadaye alipohitimu
na kufanya kazi kama Mwalimu, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam aliko mpaka sasa. Akasema, hata alipokuwa Sweden kwa masomo ya
juu pia lijihusisha na programu za maendeleo ya soka la wanawake.
Wakili msomi wa TFF akijibu hoja
hizo, alikubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi kuwa Mrufani
hajaonesha popote kwamba amewahi kuongoza soka, akasema Mrufani ni
mtaalamu tu kama msomi, jambo linaloweza kufanywa na msomi yoyote.
Akamalizia kwa kuiomba Kamati ya Rufani za Uchaguzi kuitupilia mbali
rufaa ya Mrufani kwa kukosa mashiko.
Tofauti na Kamati ya Uchaguzi,
Kamati ya Rufani imeona kuwa kwa maslahi mapana ya mchezo wa soka katika
ujumla wake, ni vema kuweka tafsiri pana (wide interpretation) juu ya
sifa zinazozungumzwa, badala ya kuweka tafsiri finyu (restricted/narrow
interpretation) kama ilivyofanya Kamati ya Uchaguzi.
Baada ya kufanya hivyo, kuhusiana
na Mrufani, Kamati imeona kuwa ana sifa zinazostahili. Kupitia sababu
alizozitoa, na vielelezo vyake, Kamati ya Rufani haina wasiwasi kuwa
Mrufani ana uzoefu mbali mbali sio katika soka tu, bali pamoja na
michezo katika ujumla wake.
Tumeshuhudia katika maelezo yake
kwetu kwamba ushiriki wake katika hatua mbali mbali, japo hakuwahi
kuchaguliwa, sio ushiriki wa kitaaluma tu, kama msomi mwingine yeyote.
Ni ushiriki wenye dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko/maendeleo katika
soka la wanawake. Maelezo
yake kuwa aliaandaa programu ya
maendeleo ya soka la wanawake, hayakupingwa. Kamati ya Uchaguzi
ingeangalia namna ambavyo “visheni” iliyomo katika programu ile ambavyo
ingeweza kutekelezwa na mtu aliyeaiandaa. Kwa hiyo, katika hoja hii,
Kamati inakubaliana kuwa Mrufani
anazo sifa stahiki, na kukatwa
kwa sababu hii, Kamati ya Uchaguzi haikujielekeza vema. Kwa hiyo,
Mrufani ameshinda rufaa yake? Kamati ya Rufani inachelea kujibu swali
hili moja kwa moja. Utaratibu wa kuwasilisha rufani ulikiukwa, na hapa
ndipo rufaa hii inapokwaa kisiki. Chini ya Ibara ya 13 (1) cha Kanuni
ya
Uchaguzi (Electoral Code),
mgombea ambaye hakuridhika na maamuzi, atawasilisha rufaa yake ndani ya
siku 3 (tatu) tangu uamuzi anaoupinga ulipotolewa.
Kipengele cha 3 (tatu) cha ibara
hiyo kinasema kwamba Mrufani yoyote atakuwa na uhalali endapo rufaa yake
imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni hizo. Uamuzi unaolalamikiwa
ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu za rufaa ziliandaliwa tarehe 27
Julai na sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe 28 Julai, 2015. Ni
dhahiri kwamba rufaa ililetwa nje ya muda uliowekwa na kanuni, na kwa
hiyo inakosa uhalali kisheria na kikanuni.
Japo katika mwenedo na maamuzi
yake Kamati ya Rufani za Uchaguzi haifungwi na taratibu za kimahakama,
suala la muda wa kuwasilisha rufani sio miongoni mwa mambo ambayo Kamati
inaweza kutoyazingatia. Kwa sababu hiyo, Rufaa hii imetupwa, lakini kwa
sababu tofauti na zile za Kamati ya Uchaguzi.
Pamoja na uamuzi huu, Kamati ya
Rufani za Uchaguzi inapenda kwa namna ya kipekee kumpongeza Mrufani kwa
jitihada alizozionesha kutaka kuitumikia TWFA. Ni matumaini ya Kamati
kuwa hatokata tama, na kwamba atakuwa tayari, akitakiwa kufanya hivyo,
kupitia taalum yake, kushirikiana na wenzake katika jitihada za
kuendeleza soka la akina mama lililo na changamoto lukuki.
Imetolewa na,
JULIUS M. LUGAZIYA
Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za Uchaguzi