MWENYEKITI WA CHADEMA AONGEA NA WAANDISHI WA HABARI KUELEZEA AFYA YAKE

August 11, 2015



 
Mbowe akiongea na Waandishi wa habari leo
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mwenyekiti mwenza wa UKAWA Freeman Mbowe, ameongea na vyombo vya habari na Kuelezea maendeleo yake kiafya baada ya jana kuugua gafla na kukimbizwa Hospitali.
Freeman Mbowe ameshauriwa na madaktari apumzike baada ya jana kukimbizwa hospitali ya Taifa Muhimbili, wakati alipojisikia vibaya ghafla akiwa kwenye msafara wa kumsindikiza mgombea urais wao kuchukua fomu za kugombea urais ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).


Akiongea na waandishi wa habari juu ya afya ya Mhe. Mbowe, Daktari Bingwa Magonjwa ya Moyo, Shem Tulizo Sanga amesema Mhe. Mbowe anaonekana kuchoka sana kufuatia shughuli ambazo amekuwa akizifanya mfululizo hivyo anahitaji kupumzika ili kurejea katika hali yake ya afya ya kawaida.Freeman Mbowe jana aliugua ghafla akiwa katika maandamano ya kumsindikiza mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa baada ya kuchukua fomu za kugombea urais katika Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC)
Mbowe alishiriki katika maandamano yaliyoanzia Makao Makuu ya CUF yaliyopo Buguruni wilayani Ilala kuelekea NEC na baada ya Lowassa kuchukua fomu, mwenyekiti huyo aliendelea na msafara kwenda Kinondoni yalipo makao makuu ya Chadema.
Wakiwa njiani Mbowe na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu walikuwa wamechomoza kwenye gari wakiwapungia wananchi waliojitokeza kwenye maandamano hayo.
Hali ya Mbowe ilibadilika ghafla na aliamua kushuka juu ya gari na kukaa katika kiti, ndipo Lissu na watu waliokuwamo kwenye gari hilo wakaanza kumpatia huduma ya kwanza kwa kumfungua vifungo vya shati lake katika eneo la Kinondoni kwa Manyanya.

Wakati hali ya Mbowe ilipoanza kubadilika msafara wa Lowassa ulikuwa ukielekea katika Uwanja wa Biafra, Kinondoni na magari yalikuwa yakitembea mwendo mdogo kutokana na maelfu ya watu waliokuwa wakiandamana.


Wakati maandamano hayo yakiendelea, gari lililombeba Mbowe likiwa na walinzi wa Chadema walioning’inia milangoni, lilichomoka katika msafara huo ambao ulikuwa umeingia Barabara ya Kawawa na lilikunja kona katika barabara ya kuelekea Mahakama ya Kinondoni kwa ajili ya kumwahisha hospitali na taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa lilielekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »