COASTAL UNION YAMPAGIA SIFA CHIPO.

January 07, 2014
Na Oscar Assenga,Tanga.
UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga umemwagia sifa Kocha mkuu wa timu hiyo Yusuph Chipo kutokana na uwezo wake kiutendaji alioufanya kwa kipindi kifupi ambacho amekabidhiwa timu hiyo ambacho  kinaonyesha mafanikio makubwa kwao siku za mbeleni.
 
Akizungumza jana,Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union ya Tanga,Hemed Aurora “Mpiganaji”alisema uwezo wa mwalimu huo umeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa timu yao ya pili kuweza kuchukua ubingwa wa kombe la uhai Cup na kuweza kuipa heshima timu hiyo na mkoa wa Tanga kwa ujumla.
 
Aurora alisema kilichofanywa na kamati ya utendaji kwa kuamua kumuondoa aliyekuwa kocha wao Hemed Moroco kilikuwa ni sahihi na  cha kizalendo ambacho leo hii kimeweza kuleta mapinduzi makubwa na maendeleo ya timu yao hasa kikosi cha pili.
 
Alisema kutokana na uwezo wake wana imani kubwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara wataweza kufanya vizuri  kutokana na kocha huyo kupewa kila anachokitaka na mshikamano uliopo baina wa wapenzi viongozi na wanachama wao.
 
Mwenyekiti huyo alisema kabla ya kuanza mzunguko wa pili wa ligi kuu wanatarajiwa kuweka kambi ya wiki mbili Maskati nchini Omani ambayo itakuwa na lengo la kukipa makali kikosi chao ambacho kinakabiliwa na michezo yao ligi hiyo.
 
Alisema wakiwa nchini Omani wanatarajiwa kucheza mechi nne za kirafiki ambapo hilo linategemea na ratiba ya wanyeji wao timu ya Finya FC ya Omani ambayo inashiriki ligi kuu nchini humo.
 
Wakati huo huo,Aurora alioupongeza uongozi mpya wa shirikisho la soka nchini (TFF)chini ya Rais wake Jamali Malinzi  na Makamu wake Walece Karia kwa kuchaguliwa kuongoza shirikisho hilo na kueleza kuwa anaamini watakuwa chachu ya maendeleo ya mpira wa miguu hapa nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »