CCM TANGA YAWAONYA WATENDAJI WA SERIKALI.

January 07, 2014
Na Oscar Assenga, Tanga
HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga (CCM) imekemea vikali tabia ya watendaji wa serikali wanaojifanya miungu watu na kuzitaka mamlaka husika kuhakikisha wanawachukulia hatua kali ili kukomesha vitendo vya aina hiyo.

Uamuzi huo ulifikiwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga (CCM)kilichofanyika mwishoni mwa wiki na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka wilaya mbalimbali mkoani hapa ambapo mambo mawili makubwa yaliyotawala kikao hicho ni migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na mgogoro kati ya wakulima wa chai, chama cha wakulima wa chai (Utega) pamoja na mwekazaji.



Akizungumza na waandishi wa habari jana,Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga,Gustav Mubba alisema viongozi wa serikali wanaopewa mamlaka ya kuwaongoza wananchi wanashindwa kufanya kazi zao ipasavyo na kuendekeza tabia ya kuwanyanyasa wananchi badala ya kuwaondolea kero zinazowakabili.

Mubba alisema viongozi wa ngazi za chini wameshindwa kuwajibika kwa kuwa mstari wa mbele kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi wao bali wamekuwa wakichangia kuwepo migogoro kwenye maeneo yao kutokana na kutokuzingatia namna ya utoaji wa ardhi kisheria.

Alisema kitendo hicho kimeleta manung’uniko makubwa miongoni mwa wananchi katika vijiji mbalimbali ikiwemo wilaya za kilindi, Handeni na kuwafanya wananchi kuichukia serikali yao.

Aidha katibu huyo alisema kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2014-2015 viongozi kuanzia ngazi za vijiji, madiwani na wabunge watapimwa kwa kazi walizofanya ikioenekana hawakufanya kitu chochote watashindwa kupewa ridhaa ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Akizungumzia suala la mgogoro wa wakulima wa chai na chama cha pamoja na mwekezaji,Katibu Mubba alisema halmashauri kuu ya Chama hicho imeunda kamati ya watu saba kwenda kuona  na waziri mkuu Mh.Mizengo Pinda ili kuweza kuangalia namna gani ya kuumaliza  mgogoro huo ambao ulipeleka mpaka kufungwa kwa kiwanda hicho.

Suala lengine ambalo limeonekana kuzungumzia sana lilikuwa ni maji katika wilaya za Muheza, Handeni na Kilindi ambapo kumewekwa mkakati kabambe wa kuhakikisha wanayapambia ufumbuzi ili kuweza kuwaondolea adha hiyo wananchi wa maeneo mbalimbali kwenye wilaya hizo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »