Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhe. Mhandisi
Atashasta Nditiye (wa kwanza kushoto) akiwaeleza jambo Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard
Mayongela (kulia) na Kaimu Mkurugenzi Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka katika eneo la kuchukua
mizigo baada ya kuwasili.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyenyoosha
mkono), akimfafanulia jambo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhe. Mhandisi Atashasta
Nditiye (wa nne kulia) wakiwa kwenye eneo la abiria wanaowasili kutoka
nje ya nchi.
Bw. Kaanankira Mbise, Kaimu Mkuu
wa Kitengo cha Uhamiaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius
Nyerere (JNIA), akieleza namna abiria anavyopata huduma ya viza mbele ya
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na
Mawasiliano), Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye (kushoto), huku Kaimu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard
Mayongela (kulia) akisikiliza kwa makini.
…………………
TBIII kutumia e-visa
Na Mwandishi Wetu
JENGO la tatu la abiria la Kiwanja
cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBIII) linalotarajiwa
kukamilika Desemba 2018, litafungwa mfumo wa huduma ya viza kwa njia ya
mtandao (e-visa), ambao utarahisha na kuharakisha upatikanaji wake.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji
cha JNIA, Bw. Kaanankira Mbise amemwambia jana Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano), Mhe.
Mhandisi Atashasta Nditiye alipotembelea eneo la uombeaji viza kwa
abiria wa kimataifa wanaowasili, kuwa wanatarajia kutumia huduma hiyo
ambayo ni rahisi na haraka.
“Tayari mkakati umeanza wa
kuanzisha huduma hii ya e-visa hivyo tukifanikiwa utafungwa katika jengo
hili jipya, ambapo itasaidia kwa abiria kuipata huduma hiyo kwa haraka
kwani itatumia mtandao,” amesema Bw. Mbise.
Hata hivyo, Bw. Mbise amesema kwa
sasa wameboresha huduma hiyo kwa wasafiri wanaowasili katika jengo la
pili la abiria (JNIA-TBII) , ambapo tayari wamepatiwa mashine nne za
kisasa zinazosaidia kupunguza msongamano wa abiria wenye kuhitaji huduma
hiyo, hususan kipindi cha mchana chenye ujio wa ndege nyingi za nje ya
nchi.
“Hizi mashine zimeharakisha
upatikanaji wa huduma kwani tumeweza kuhudumia abiria wengi kwa wakati
mmoja, na msongamano umepungua kiasi tofauti na awali mashine zilikuwa
chache.” amesema Mbise.
Naye Mhe. Mhandisi Nditiye amesema
baada ya ziara yake amegundua mashine za viza ni za muda mrefu na
zinahudumia abiria mmoja kwa mrefu, na tayari ameuagiza uongozi wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuwasilisha kwa maandishi
mapendekezo yao ya namna ya kuharakisha huduma hiyo, ili serikali
iyafanyie kazi kwa kusaidia kuondoa kero hiyo.
“Nimegundua kuna baadhi ya mashine
za viza zimeongezwa lakini pia zilizopo zimechoka kwani ni za muda
mrefu na zinahudumia abiria mmoja kwa muda mrefu na hii inaharibu sifa
ya kiwanja chetu kwa wageni wanaokuja hapa nchini,” amesema Mhandisi
Nditiye.
Hata hivyo, amesema wanampango wa
kuongeza madirisha ya benki yanayolipia viza hizo ili kuharakisha huduma
hiyo, ambapo sasa ni machache kulinganisha na idadi kubwa ya abiria
wanaowasili kwa ndege kubwa. Ndege hizo ni Emirates, Etihad, Oman Air,
Qatar, South Africa Air na Ethiopia, ambazo zimekuwa zikipishana kwa
muda mfupi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TAA,
Richard Mayongela amesema tayari wanampango wa kuongeza upana wa eneo
hilo la wasafiri wanaowasili wa kimataifa, ambapo sasa kumekuwa na
msongamano kutokana na ufinyu wake.
“Hili jengo linazaidi ya miaka 30
na ukiangalia abiria waliokuwa wamekadiriwa wakati ule lilikuwa
likikidhi mahitaji, lakini sasa abiria wameongezeka na eneo limekuwa
dogo, hivyo tayari tumeanza kwa kuondoa baadhi ya ofisi ili kuongeza
upana wake, ninaimani litapunguza msongamano uliopo sasa,” amesema Bw.
Mayongela.
Lakini pia Bw. Mayongela amesema
sasa wapo katika mazungumzo na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), ili
kuangalia namna bora ya kuzipangia muda ndege zinazopishana muda mdogo
kwa wakati wa mchana ili ziachiane muda mrefu, ambapo kutasaidia
kupunguza msongamano
Awali eneo hilo linakumbwa na
changamoto kubwa ya msongamano wa abiria wanaohitaji huduma ya viza
baada ya uchache mashine zinazosimamiwa na Idara ya Uhamiaji
zilizokuwepo na kufanya abiria wanaohitaji huduma hiyo kutumia muda
mrefu kuipata.