KUTOKUWA na uwakilishi wa kisheria katika mahakama za watoto
wanaokinzana na sheria, kimekuwa kikwazo kikubwa kupata haki ambayo
wanastahiki kupatiwa. Jambo hili limesababisha watoto wengi kuhukumiwa
kutumikia adhabu mbalimbali.
Hali hiyo pia imesababisha maumivu makubwa kwa jamii hasa baada ya
ndugu na jamaa zao kulazimika kuwa kizuizini kutokana na makosa
mbalimbali ambayo huenda ametenda, anatuhumiwa au amesingiziwa.
Uwepo wa changamoto hiyo kubwa kwa watoto umekipelekea Chama cha
Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) mkoani Tanga, kutoa elimu juu ya
namna ya utoaji wa msaada wa kisheria kwa watoto walio katika ukinzani
na sheria kwa wadau wake kwenye masuala ya watoto walio katika ukinzani
na sheria.
Licha ya kutoa elimu hiyo, chama hicho pia kinatoa msaada wa kisheria
kwa watoto walio katika ukinzani na sheria kwa kuwapatia wanasheria wa
kuwawakilisha mahakamani kupitia mpango wake wa Pro bono.
Kupitia mpango wake huu wa Pro bono, Tawla iliwezesha kumpatia msaada
wa kisheria mtoto, Sophia John Komba (17) ambaye alituhumiwa na kosa la
mauaji ya kondakta wa daladala inayofanya safari zake kati ya Nguvumali
na Raskazone. Mtoto Sophia aliwekwa kizuizini tangu Januari mwaka huu
katika kituo cha mahabusu ya watoto.
Binti huyo ambaye ni mtahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne,
alitakiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka huu lakini
alishindwa kwenda shule kutokana na kukabiliana kesi ambayo yeye na baba
yake mzazi zinawakabili.
Mratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake mkoani Tanga (Tawla),
Mwanasheria Latifa Mwabondo,(Pichani Juu) anasema Tawla kupitia mradi wake wa utoaji
wa msaada wa kisheria kwa watoto na wanawake waliokuwa katika ukinzani
na sheria, aliembelea mahabusu ya watoto ili kuweza kujua idadi ya
watoto walio katika ukinzani na sheria na kujua makosa yanayowakabili
ili kuwapatia msaada wa kisheria.
Anasema walipoanza kufuatilia walielezwa watoto watatu ambao walikuwa
na makosa tofauti kama mauaji, wizi wa kutumia silaha na wizi bila
kutumia nguvu ambapo watuhumiwa wamewekwa katika mahabusu ya watoto.
Baadaye walipokwenda mahabusu ili kuweza kupata maelezo ya kesi ili
kuwapatia uwakilishi, waliambiwa amebaki mtoto Sophia John ambaye
alikabiliwa na kesi ya mauaji ya kondakta wa daladala jijini Tanga.
“Kwa sababu ni mtoto na chama hicho kwa sasa kinaendesha mradi wa
uwezeshaji wa msaada wa kisheria kwa watoto na wanawake walio katika
ukinzani wa sheria, tukaona ni bora tumpatie msaada wa kisheria,”
anasema.
Anasema Tawla walifuatilia kesi na kuelezwa bado kesi ipo kwenye
hatua ya upelelezi. Na baadaye wakampatia mwanasheria ambaye atakuwa na
binti huyo ili kumhoji maswali kwa sababu habari walizozisikia ni
tofauti na zinazoelezwa.
Anaeleza kuwa siku kesi hiyo ilipotajwa walikwenda mahakamani wakawa
pande zote mbili na wanasheria kwa kuongeza kuwa wapo tayari kumtetea
binti huyo katika kesi iliyokuwa na watoto watano huku yeye akiwa
watatu.
“Tuliamua kumtetea kwa sababu yeye ni mtoto na ana haki zake za
msingi, ambapo tuliiomba mahakama ili kuharakishwa kwa upelelezi wa kesi
hiyo kwa kuwa mshtakiwa ni mwanafunzi mtahiniwa wa kidato cha nne.
Ambapo alinishauri kukutana na upande wa waendesha mashtaka na
wapelelezi ili kufanya upelelezi wao haraka baada ya kuambiwa faili lake
lipo kwa RCO,” anasema.
Anasema kesi ilipopangwa kwa mara nyingine, wao walimwakilisha
wakiongozana na wakili Tumaini Bakari ambaye ndiye atakayemwakilisha
katika kesi hiyo, ambapo katika utetezi wakili wa chama hicho waliomba
upelelezi uharakishwe.
Wakili huyo alitaka jambo hilo kufanyiwa haraka kwa kuwa mtoto huyo
ni mtahiniwa na alikuwa anatakiwa kuwepo shuleni wakati huo kwa
matayarisho ya mitihani na pili kujua hatima ya mteja wetu kama ana kesi
ya kujibu au la.
Anaeleza baada ya hilo hakimu alihimiza upande wa waendesha mashtaka
wahimize upande wa upelelezi kufanya upelelezi mapema ili kutoa nafasi
ya kusikilizwa kesi hiyo.
Latifa anasema walihimiza upande wa utetezi wamshirikishe Ofisa
Ustawi wa Jamii kufuatilia usahili wa mtuhumiwa kama umefanyika na awepo
mahakamani kwa siku ya kesi inayofuata na taarifa kamili kwa lengo la
kujua huyo mtoto amepewa namba ya kufanya mtihani.
Aliongeza kuwa walipoenda mahakamani kwa mara ya tatu mambo yakawa ni
yale yale. Ila ofisa ustawi wa jamii alitoa taarifa ya kwamba
mtuhumiwa alikuwa ametahiniwa.
Agosti 14, mwaka huu kesi ilitajwa tena ambapo mratibu huyo anasema
walipofika mahakamani, walifika mbele ya hakimu na upande wa
mwanasheria wa Serikali walisema wamepitia faili wakaona mshtakiwa
namba tatu ambaye ni mtoto Sophia John kwamba hana kesi ya kujibu.
Anaeleza upande wa waendesha mashtaka walifuta shtaka kupitia kufungu 91 (1) ya sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Anaeleza baada ya hapo wakamchukua na kumpelekea Kituo cha Polisi cha
Chumbageni ili kumtoa alama za vidole (Finger Print) na baadaye
kumpeleka kwenye mahabusu ya watoto kwa makubaliano ya wazazi na polisi.
“Kwa ajili ya usalama wa mtoto, Tawla na Ustawi wa Jamii
walikubaliana na familia ya kwamba wakati huo Sophia hawezi kwenda
kuishi na familia yake kwa sababu za kiusalama. Mpaka hapo
atakapohakikishiwa usalama wake,” anasema.
Anasema kwa sasa Sophia kulingana na mkasa alioupitia hayuko vizuri
kisaikolojia na muda wa matayarisho wa mitihani ni mdogo sana kwake.
Anasema kwa kushauriana na ustawi wa jamii, ikaonekana ni vizuri
kupitia ustawi wa jamii kuandikwe barua itakayoambatanishwa na maamuzi
ili kuliomba Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kuahirisha mitihani ili
aweze kufanya mwakani kwa sababu alikuwa kuzuizini na hakupata muda wa
kusoma.
Akizungumzia changamoto kuhusu kesi hiyo, anasema kosa ambalo
lilisababisha Sophia kufikishwa katika kituo cha mahabusu ya watoto ni
kubwa, hivyo mtoto huyo hakupata nafasi ya kuendelea kusoma wala kupata
walimu ambao wangeweza kumwendeleza kimasomo.
Aidha, Sophia anasema: “Baada ya kuachiwa huru nimekuwa nikishinda
nyumbani wakati wakiangalia sehemu salama ya kwenda kuishi kwa sababu
jamii wananiangalia kama muuaji.
“Nimekuwa nikiitwa majina mengi kama muuaji, malaya kwa sababu ya
kile kilichotokea na hali hii imekuwa ikiniumiza sana na kukosa amani.
“Katika jambo hilo nawashukuru watu wote kwa kunipa ushirikiano wao
likiwemo Jeshi la Polisi, Mahabusu ya Watoto, Ustawi, Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu-Tanga katika kuwezesha kusaidia watoto kupata
haki,” anaeleza Sophia.
Akizungumzia namna anavyojisikia baada ya Tawla kumtetea na kuwa
huru, Sophia anaanza kwa kububujikwa na machozi kwa furaha kutokana na
kutokuamini kwamba angeweza kuwa huru kutokana na namna watu walivyokuwa
wakificha ukweli wa jambo hilo.
Anasema kuwa katika tukio la kipigwa kwa kondakta huyo hadi kufikia
hatua ya kupoteza maisha, baba yake mzazi ambaye kwa sasa yupo gerezani
hakuhusika isipokuwa ni vijana waliokuwa wakiishi nao hapo kambini ndio
walishiriki katika suala la kumpiga kijana yule.
“Kiukweli nakiri kwamba baba yangu hakuhusika kwa lolote na mauaji
hayo lakini baada kutokea tukio hilo vijana wa mtaani ndio walishiriki,”
anasema.
Akizungumzia changamoto ambazo wanakutana nazo walipokuwa kizuizini,
Sophia anasema watoto wengi wanaathirika na ucheleweshwaji wa kesi na
upelelezi, jambo ambalo linasababisha kuendelea kushikiliwa huku
wakikosa haki zao za msingi ikiwemo elimu na masuala mengine muhimu.
“Lakini pia kitu kingine ambacho siwezi kukisahau ni kufungiwa
mahabusu kwa siku saba nikiwa sionani na mtu yeyote, huku niliowakuta
kuzuizini wakinidhihaki kwa kuniita muuaji, kitendo ambacho
kiliniumiza sana,” anasema.
Anaongeza kuwa suala jingine ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa
watoto wanaokuwa vizuizini ni kukosa haki ya msingi ya kupata elimu,
jambo ambalo linakwamisha ndoto zao za kupata elimu bora.
“Nawashukuru Tawla kwa kuonyesha mapenzi makubwa kwa kunitetea na hatimaye nimetoka mungu atawalipa,” anasema.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Chama hicho, Adophina Mbekenga,
anasema kesi hiyo ilikuwa maarufu, hivyo walianza kuifuatilia tangu
Machi.
Baada ya hapo waliwasiliana na Ustawi wa Jamii kuwauliza baadhi ya
maswali na kweli kama huyo mtoto yupo kwenye kituo chao na anakabiliwa
na kesi namba gani ili waweze kuona namna ya kumsaidia.
“Nilirudi ofisini kumweleza bosi wangu hali halisi na kuona kesi hiyo
ni nzuri kwao, kwani kipindi hicho walikuwa wakitekeleza mradi ambao
unajishughulisha kusaidia watoto waliopo kwenye ukinzani wa kisheria kwa
lengo ya kuangalia utekelezaji mzima wa sheria ya mtoto na mwenendo
mzima wa kesi zinazowakabili watoto,” anasema.
Anasema walikuwa wanaangalia namna gani anaweza kuepukana na adhabu
kama mtoto, kwa sababu kwa kawaida akitenda kosa bila kumfuatilia
anaweza kukosa haki zake za msingi na ndio maana wakaona namna bora ya
kuharakisha kesi hiyo kwa kuangalia sheria zinasemaje.
EmoticonEmoticon