Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limewapongeza
viongozi, mashabiki, wachezaji wa vilabu na timu za Taifa kwa kufanya
vizuri katika michezo mbalimbali ya kimataifa iliyochezwa mpaka sasa.
Katika kipindi cha mwezi mmoja, Tanzania imeshiriki katika michuano
mbalimbali ya kirafiki, mashindano ngazi za vilabu, timu za taifa
ikiwemo ya Wanawake (Twiga Stars), Vijana (Serengeti Boys) na Taifa
Stars.
Katika michezo kumi iliyochezwa mfululizo mpaka sasa, timu za
Tanzania hazijapoteza mchezo hata mmoja mpaka sasa, ikiwa ni kwa vilabu
pamoja na timu za taifa za Wanawake, Vijana na Taifa Stars.
Twiga Stars ilitoka sare ya bao 1- 1 dhidi ya Zimbabwe mchezo
uliochezwa Harare, Yanga ikaifunga APR mjini Kigali 2-1, kabla ya kutoka
sare ya bao 1-1 jijini Dar es salaa, wakati Azam FC ilifunga Bidvest
3-0 Johanesburg na kuendeleza tena ushindi wa 4-3 Azam Complex Chamazi.
Taifa Stars ikiwa mjini N’Djamena ilibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi
ya Chad katika mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2017, Serenegti Boys
ikiifunga The Pharaohs kutoka Misri katika michezo miwili ya kirafiki ya
kimataifa (2-1), (3-1) michezo iliyochezwa Uwanja wa Taifa na Azam
Complex Chamazi.
Mchezo wa tisa wa kimataifa, Yanga SC ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi
ya Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), huku Azam
FC ikiibuk na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Esperance ya Tunisia katika
mchezo wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC).
TFF inawaomba wachezaji, viongozi, wadau na Mashabiki kuendelea
kupigana kusaka ushindi katika michezo inayofuata na kuipeperusha vyema
bendera ya Tanzania nje ya nchi.