NA RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR
………………………………
Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi
Zanzibar (ZFDB) imeandaa miongozo ya utoaji huduma bora katika
kufanikisha Mpango wa uwiano wa Itifaki ya pamoja kwa Nchi wanachama wa
Jumuia ya Afrika Mashariki.
Mkurugenzi wa ZFDB Dkt. Burhani
Othman Simai ameeleza hayo katika Mkutano wa wadau wa Madawa Zanzibar
ulioandaliwa na Mpango wa Udhibiti wa bidhaa za Chakula na Dawa wa
Jumuia ya Afrika Mashariki katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni
nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Alisema kuanzia sasa bidhaa zote
za chakula na madawa za Zanzibar na zinazotoka nje zitasajiliwa na
Bodi yake na Viwanda vinavyotengeneza bidhaa hizo vitafanyiwa ukaguzi wa
mara kwa mara ili kuhakikisha usalama wa bidhaa hizo.
Aliongeza kuwa katika kufanikisha
mpango huo, Zanzibar inategemea kupata ithibati ya Kimataifa (ISO
Certification) mwezi Disemba na kuanzia Januari 2016 maombi na kazi zote
za udhibiti wa bidhaa za chakula na madawa zitafanywa kwa njia ya
mtandao kupitia tovuti ya ZFDB.
Dkt. Burhani aliwataka wadau wa
bidhaa za chakula na madawa kutoa ushirikiano kwa Bodi kwa kujisajili
katika Ofisi yao iliyopo Mombasa kwa Mchina na kuandaa utaratibu
mzuri wa kurahisisha ukaguzi wa bidhaa na viwanda vyao.
Alisema taratibu hizo
zinazochukuliwa na ZFDB zinalengo la kulinda afya za wananchi wa
Zanzibar na Nchi wa wananchama wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Mwakilishi kutoka Sekriteriati ya
Jumuia ya Afrika Mashariki Mjini Arusha Mwesige John Patrick aliipongeza
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa mstari wa mbele kufanikisha
Mpango wa uwiano wa Nchi wanachama wa Jumuia hiyo.
Alikumbusha kuwa Mpango huo
ulioanza mwaka 2012 kwa awamu ya kwanza ya miaka mitatu, ukizishirikisha
Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Ruwanda umeanza kuleta
mafanikio makubwa kwa nchi zote wanachama na mwaka huu umeanza awamu ya
pili ya miaka miwili.
Akifungua Mkutano huo Naibu Katibu
Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Halima Maulid ameitaka ZFDB kuendelea
kusimamia mpango wa uwiano wa Udhibiti wa Bidhaa za chakula na dawa na
kuhakikisha zinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
Mkutano huo uliokuwa na lengo la
kuwafahamisha wadau wa Zanzibar miongozo mipya iliyoandaliwa kwa pamoja
na wataalamu wa Mamlaka za udhibiti wa Chakula na Dawa wa Wanachama wa
Jumuia ya Afrika Mashariki.