ASHIKILIWA NA POLISI AKIHUSISHWA NA MAUAJI

September 29, 2015
Na Mwandishi Wetu,Muheza

JESHI la Polisi mkoa wa Tanga linamshikilia mkulima mmoja na mkazi wa Kijiji cha Machemba wilayani Muheza John Dastan (30) kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Abdi Godatha (54) kwa kumpiga fimbo kichwani.

Akitoa taarifa hiyo ofisini kwake jana,Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga Zuberi Mwombeji alisema lilitokea Septemkba 28 mwaka huu majira ya saa 5.00 usiku huko kwenye kilabu cha pombe katika kijiji cha Machemba Kata ya Mkanyageni.

Kamanda Mwombeji alisema kwamba indaiwa siku ya tukio marehemu ambaye alikuwa akinywa na mtuhumiwa waliingia katika ubishani na ndipo Dastan alipochukua fimbo na kuanza kumpiga nazo maeneo ya kichwani.

“Chanzo kiuu cha mauaji hayo kwa uchunguzi wetu wa awali ni kutokana na ulevi huyu mtuhumiwa alikuwa amelewa na waliingia ubishani na marehemu na ndipo Dastan alipochukua fimbo na kumpiga nazo marehemu kichwani na kusababisha kifo chake”,alisema Mwombeji.

Hata hivyo alisema kuwa Polisi inaendelea na uchunguzi wa mauaji hayo na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Kamanda Mwombeji alitoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani kitendo cha kupigana hadharani ni makosa kwa mujibu wa sheria.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »