Msanii mkongwe wa muziki wa
reggae na Mkurugenzi wa Reggae Production House Innocent Nganyagwa
akiongea na wadau wa muziki huo mapema wiki hii kwenye programu maalum
ya kujadili hatma ya muziki wa reggae iliyoandaliwa na Baraza la Sanaa
la Taifa (BASATA) na kufanyika makao makuu ya Baraza hilo Ilala Sharif
Shamba jijini Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Sanaa kutoka BASATA,
Augustino Makame na Katibu wa chama cha waandishi wa Habari za Sanaa na
Utamaduni (CAJAtz) Hassan Bumbuli .
Katibu wa chama cha waandishi wa
Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz) Hassan Bumbuli akisisitiza jambo
wakati akiongea na wadau wa muziki wa reggae (hawako pichani) kwenye
programu maalum ya kujadili hatma ya muziki huo. Kushoto kwake ni Msanii
mkongwe wa Reggae Innocent Nganyagwa.
Ras Bumijah Zinyongwa ambaye pia
ni kiongozi wa Tanzania Rastafarai Movement (TARAMO) akitoa ufafanuzi wa
moja ya hoja iliyoibuka kwenye programu hiyo.
Msanii mkongwe wa muziki wa Band
John Kitime akiongea na wadau wa Sanaa (hawako pichani) kuhusu umuhimu
wa Wasanii kujiunga na Shirika la Bima la Taifa (NHIF) ili
kujihakikishia matibabu na kuepuka kuombaomba wakati wanapougua.
Msanii mkongwe wa reggae Innocent
Nganyagwa akionesha makali yake ya muziki wa Reggae wakati akitoa
burudani kwa wadau wa Sanaa waliohudhuria programu mahsusi ya kujadili
hatma ya muziki huo nchini.
Sehemu ya wadau waliohudhuria programu hiyo wakifuatilia mjadala.
……………………………………………………………………………….
Wadau wa muziki wa reggae nchini kwa kujengewa mazingira na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wameweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha wanaurudisha jukwaani muziki huo na kuainisha changamoto mbalimbali zinazoukabili. Akizungumza mapema wiki hii kwenye programu maalum iliyolenga kuujadili muziki wa reggae na kuja na mikakati ya kuurudishia hadhi iliyoandaliwa na BASATA, Msanii mkongwe wa muziki huo Innocent Nganyagwa alisema kwamba wasanii wa muziki huo kwa sasa wamejipanga kuurudisha jukwaani muziki huo kupitia kufanya maonesho maeneo mbalimbali nchini. “Tumejipanga kufanya maonesho ya muziki wa reggae katika mikoa mbalimbali nchini, tutakuwa na kundi la wasanii ambao kazi yao itakuwa kufanya maonesho ya hisani na kuurudisha jukwaani muziki huu ambao kihistoria ni muziki mama” alisema Innocent Nganyagwa. Aliitaja mikoa ambayo maonesho hayo ya reggae yatafanyika kuwa ni pamoja na Mbeya, Ruvuma, Iringa, Arusha, Mwanza, Dar es Salaam na mingine ambayo maandalizi bado yanaendelea ili kuhakikisha wanawafikia wapenzi wengi zaidi wa muziki huu ambao huko nyuma ulipata kuwa na mvuto mkubwa. Mikakati mingine iliyowekwa ukiacha kufanya maonesho mbalimbali nchini ni pamoja na wasanii wa reggae kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika kujitangaza, kuanza kuuza kazi zao kupitia mitandaoni, kubuni kazi zenye ujumbe unaoendana na soko na kuacha kuganda na falsafa ya reggae ni muziki wa ukombozi. Awali wakibainisha changamoto mbalimbali zinazoukabili muziki huo, wadau wengi walisema kwamba muziki huu unasuasua kutokana na vituo vingi vya radio kuupa kisogo, watanzania wengi kuuhusisha na imani za urasta kitu ambacho si sahihi na zaidi wadau muhimu hasa makampuni ya biashara kutoujali katika ufadhili. “Muziki huu wa reggae si wa marasta pekee, bahati mbaya watu wengi wamekuwa wakiuhusisha na imani za kirasta. Hapana. Muziki huu unafanywa na mtu yeyote na ni muziki kama ilivyo miziki mingine” alisema Ras Bumijah Zinyongwa ambaye pia ni kiongozi wa taasisi ya Tanzania Rastafarai Movement (TARAMO)
EmoticonEmoticon