Tangakumekuchablog
KATIBU
Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira, Erick Shitindi, amewagiza Maofisa Kazi Wafawidhi
nchini kupiga vita utumikishaji kazi kwa watoto wadogo maeneo ya kazi ikiwa na
pamoja na kuwafikisha wahusika katika vyombo vya sheria.
Akifungua kongamano la siku tatu
lililoitishwa na Wekeza Mkoani hapa na kuwashirikisha Maofisa Kazi Wafawidhi kutoka Mikoa mbalimbali nchini jana,
Shitindi alisema tabia ya utumikishaji watoto bado ni tatizo nchini.
Alisema tabia hiyo imekuwa ikitumiwa
na matajiri na kuwalipa ujira mdogo na hivyo kuwataka kuhakikisha kila Ofisa
anasimama katika nafasi yake na kuweza kutokomeza hali hiyo ambayo inakuwa kila
kona ya nchi.
“Utumikishaji kazi watoto wadogo
kunawaathiri mambo mengi ikiwemo kuwaharibia maisha yao ya mbeleni-----elimu na
malezi wanakoseshwa na baadae kuwa watoto wa mitaani” alisema Shitindi na
kuongeza
“Unapomtumikisha kazi mtoto mdogo
utambue kuwa umemuharibia mfumo mzima wa maisha yake---na hii mara nyingi mtoto
anakuwa katika makuzi mabaya na kuweza kujitumbukiza katika vitendo vya uporaji
na ujambazi” alisema
Alisema ili kuweza kumaliza tatizo
la utumikishaji kazi kwa watoto ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha eneo lake
hakuna kero hiyo ambayo kadri ya siku linaelekea kukua kwa kasi kila Mkoa.
Akizungumza katika kongamano hilo,
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Masha Mshomba, amewataka
waajiri kuwawekea mazingira mazuri wafanyakazi wao ikiwemo ajali kazini.
Alisema waajiri wengi wamekuwa
hawawekei mazingira mazuri wafanyakazi wao hasa pale itokeapo ajali pamoja na
kifo jambo ambalo limekuwa likisababisha kesi na kupotezeana muda.
“Waajiri wengi hawana utaratibu
mzuri kwa wafanyakazi wao na kusababisha malumbano hasa wakazi wa ajali au
kifo------hili limekuwa tatizo kubwa sana kila kona” alisema Mshomba
Alisema ili kuwawezesha wafanyakazi
kufanya kazi kwa weledi ni vyema waajiri kuhakikisha wanawawekea mazingira
mazuri na salama na kuweza kutokomeza kero na usumbufu kwa mwajiri na
mwajiriwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Kazi na Ajira,
Erick Shitindi, akifungua mafunzo ya siku tatu ya Maofisa Kazi Wafawidhi kutoka
Mikoa mbalimbali nchini yaliyoandaliwa na WEKEZA ikiwa na lengo la kupunguza
kutumikishwaji kazi kwa watoto pamoja na
fidia kwa wafanyakazi, katikati ni Kamishna wa kazi Wizara ya Kazi na AJIRA
Saul Kinemela, kushoto ni Mkurugenzi
Mkuu Mradi wa Wekeza Yuonne Prempeh Furgerson .
Maofisa Wafawidhi kutoka Mikoa mbalimbali wakishiriki katika Semina ya siku tatu juu ya kupiga vita utumikishwaji kazi kwa watoto iliyoanza jana hoteli ya Tanga Beach