Waziri wa Nishati na Madini,
George Simbachawene, (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari, baadhi
ya Watumishi wa Wizara na wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo
katika ngazi za Shahada za Uzamivu (Phd) na Uzamili (Masters), katika
masuala ya mafuta na gesi nchini China.
Baadhi ya wanafunzi 22 waliopata
nafasi za masomo ya shahada za Uzamili na Shahada ya Uzamivu
wakimsikiliza kwa kwa makini Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene.
Waziri akiwakabidhi nyaraka za
kusafiria na zenye maelezo baadhi ya wanafunzi waliopata ufadhili wa
masoma katika masuala ya mafuta na gesi nchini China.Katikakati ni Kaimu
Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, James Andilile.
……………………………………………………………………..
Na Clinton Ndyetabula, Dar es Salaam
Waziri wa Nishati na Madini George
Simbachawene, amewakabidhi Nyaraka za Ufadhili na kuwaaga wanafunzi 22
wa Kitanzania wanaokwenda masomoni nchini China, kusoma masuala ya
mafuta na gesi katika ngazi za Shahada za Uzamivu (Phd) na Uzamili
(Masters).
Akizungumza katika hafla ya
kukabidhi Nyaraka hizo, Makao Makuu ya Wizara, Jijini Dar es Salaam,
leo, Simbachawene amewataka wanafunzi hao kutumia fursa hiyo kusoma kwa
bidii ili hatimaye waweze kusaidia Taifa katika kuendeleza sekta ndogo
ya gesi ikiwemo kuanzisha vyanzo mbadala vya nishati ya umeme , kuongeza
usimamizi ili kuendana na kasi ya ukuaji wa sekta hiyo, na kusaidia
katika kuondoa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
“Kama mnavyoelewa Wizara yetu ni
miongoni mwa Wizara zilizo katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big
Results Now) katika sekta ya Nishati. Mpango huu unategemea kutoa
matokeo makubwa ya haraka, na hili kutekeleza ipasavyo tunahitaji
wataalamu wazalendo waliobobea katika fani za ,mafuta na gesi asilia”
alisema Simbachawene.
“Ni matumaini yangu kuwa mtatumia
vizuri fursa mliyopata, mtajifunza kwa bidii na kuiwakilisha nchi yetu
vizuri na kuleta teknolojia zitakazosaidia kupata ufumbuzi au
mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta
hii”alieleza Simbachawene
Aidha, Waziri alitumia nafasi hiyo
kuishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa kuwawezesha
Watanzania kusoma masuala ya mafuta na gesi tangu mwaka 2013 na
kuongeza kuwa , serikali hiyo imeahidi kuendelea kutoa ufadhili kwa
watanzania katika ngazi za Shahada ya Uzamivu na Uzamili hadi ifikapo
mwaka 2019.
Aidha, Simbachawene ameeleza kuwa,
Wizara ilipokea jumla ya maombi 187 na kati yao, waombaji 33 waliokidhi
vigezo walichunjwa na Serikali ya Watu wa China na kupatikana washindi
22.