Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, akivizindua rasmi
vyoo vya Skuli ya Kijitoupele A, B na Sekondari pamoja na Mabomba,Tangi
la Maji vilivyojengwa na ufadhili ya Shirika la Umoja wa Mtaifa la
Kuhudumia Watoto (UNECEF).
Sehemu ya Mabomba hayo ya maji yakiwa yamezungukwa na wanafunzi
wakati wa sherehe ya kuzinduliwa rasmi ambayo imejengwa kwa ajili ya
kuhudumia wanafunzi wa Skuli ya Kijitoupele A,B na Sekondari.
Moja
kati ya madarasa ya skuli ya msingi ya Kijitoupele yanaonekana kuwa na
msongamano mkubwa wa wanafunzi wasiopunguwa idadi ya 240.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na
Mwenyekiti wa Kamati ya Skuli ya Kijitoupele Nd. Manafi Said Mwinyi mara
baada ya hafla ya kuzinduliwa kwa vyoo vya skuli hiyo.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza mwakilishi wa
UNICEF hapa Zanzibar Bibi Francesca Morandini kwa uamuzi wa shirika lake
kusaidia ufadhili wa ujenzi wa vyoo vya skuli ya Kijitoupele iliyopo
Wilaya ya Magharibi. Nyuma ya Bibi Francesca ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Nd. Abdulla Mzee Abdulla. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
*********************************************
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba misingi
ya ufundishaji wanafunzi Maskulini itaendelea kukosekana iwapo idadi
kubwa ya Wanafunzi itapindukia kiwango kilichowekwa Kitaifa au
Kimataifa.
Alisema
idadi ya kawaida ya wanafunzi ndani ya darasa moja inahitajika kuwa
watoto wasiozidi arubaini wakiwa na vikalio pamoja na vifaa vyote
wanavyohitajika kuwa navyo wanafunzi hao darasani.
Balozi
Seif alisema hayo mara baada ya kukabidhiwa na kuvizindua rasmi vyoo 18
vya Skuli za Kijitoupele za Msingi A na B pamoja na ile ya Sekondari
hafla iliyofanyika katika Skuli hiyo na kuhudhuriwa na Wanafunzi,
Walimu pamoja na Wazazi wa Wanafunzi wa Skuli hizo.
Balozi
seif alisema msongamano wa watoto wengi Darasani mbali ya kwenda
kinyume na mfumo, taratibu na maadili ya ufundishaji ndani ya darasa
lakini pia unabebesha mzigo mkubwa walimu kuweza kuhudumia wanafunzi
hao kwa wakati mmoja.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kamati
ya Skuli ya Kijitoupele kwa uamuzi wao wa kukubali Wanafunzi wao
kuhamishwa kwenda kupata taaluma skuli nyengine ili kupunguza
msongamano mkubwa wa wanafunzi ndani ya Skuli hizo.
“
Walimu wetu wamekuwa wakiendelea kupata mzigo mkubwa kuwasomesha
watoto wetu kutokana na wingi wa idadi yao darasani. Inasikitisha sana
kuona Darasa moja la Skuli hii lina wastani wa wanafunzi 240 jambo
ambalo pia ni hatari kwa afya ya wanafunzi wenyewe “. Alifafanua Balozi
Seif.
Alisema
katika kukabiliana na tatizo hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itajitahidi kuangalia maeneo mengine ya wazi ndani ya Wilaya ya
Magharibi ili kutoa fursa ya ujenzi wa Skuli nyengine Mpya
zitakazosaidia kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa maeneo hayo.
Balozi
Seif aliwasihi Wanafunzi hao kuendelea kuvitunza vyema vyoo hivyo ili
vidumu kwa muda mrefu pamoja na kuwakumbusha kupenda masomo yao kwa
lengo la kushika nafasi za Uongozi na Taaluma kwa Taifa hili hapo
baadaye.
“
Nawajibu wa kuwapongeza Walimu na Kamati ya Wazazi wa Skuli hii kwa
juhudi zao za usimamizi mzuri wa wanafunzi wao na kupelekea kutoa
wanafunzi wengi wanaofaulu vizuri kuingia katika skuli mbali mbali za
Michepuo hapa Nchini “.
Akisoma
Risala kwa niaba ya Wanafunzi, Walimu na Wazazi wa Skuli hizo Mwalimu
Hidaya Haji Mkema alilipongeza Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa
Mataifa { UNICEF } kwa msaada wa vyoo hivyo ambavyo lilikuwa na uwezo wa
kuvijenga Skuli nyengine.
Mwalimu
Hidaya alisema Skuli za Kijitoupele bado zinakabiliwa na msongamano
mkubwa wa wanafunzi changamoto ambayo iko katika hatua ya kutafutiwa
ufumbuzi wake ifikapo mwaka 2015.
Alisema
uandikishaji wa wanafunzi wapya katika skuli hizo za Kijitoupele A na B
umefikia idadi ya watoto 800 kwa mwaka kiasi ambacho ni kikubwa
kupindukia mfumo na utaratibu uliowekwa wa sera ya Elimu.
Akitoa
salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto { UNICEF }
Mwakilishi wa Shirika hilo hapa Zanzibar Bibi Francesca Morandini
alisema watoto wana haki ya msingi ya kupata elimu inayoambatana na
usafi wa mazingira.
Bibi
Francesca alisema utafiti uliofanywa miaka mitatu iliyopita na Serikali
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia
katika suala la huduma za usafi wa mazingira maskulini umethibitisha
hasara ya zaidi ya shilingi Bilioni 300 kwa mwaka.
Mwakilishi
huyo wa Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa hapa Zanzibar
alieleza kwamba Taasisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Amali Zanzibar tayari wameshatengeneza muongozo wa ujenzi
wa vyoo katika maskuli mbali mbali unguja na Pemba.
Alisema
muongozo huo una lengo la kuwajengea mazingira rafiki wanafunzi na
tayari umeshazinufaisha skuli nane za Pemba naTano kwa Unguja wakati
awamu ijayo itahusisha skuli nyengine Sita hapa Zanzibar.
Naye
kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar { WEMA } Bibi Mwanaid Saleh alisema mradi huo uliohusisha Skuli
13 Unguja na Pemba kwa ufadhili wa Unicef umegharimu Shilingi za
Kitanzania Milioni Mia Tatu na Ishirini na Tano { 325,000,000/- }.
Katibu
Mkuu Mwanaidi alizitaja Skuli zilizofaidika na mradi huo kuwa ni
pamoja na Makombeni, Vitongoji, Wingwi,Kwale,Pujini, Mabatini na Konde
kwa Pemba na Kijitoupele, Nyerere Msingi,Tunguu, Bububu na Mtopepo kwa
Unguja.
Akimkaribisha
Balozi Seif katika hafla hiyo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna alisema Madarasa 40 yanahitajika
kujengwa ndani ya Wilaya ya Magharibi ili kukidhi mahitaji yaliyopo
ndani ya Wilaya hiyo.
Waziri
Shamhuna alifafanua kwamba upo mradi maalum wa ujenzi wa Skuli kumi za
Sekondari katika Wilaya zote za Zanzibar mradi ambao utatoa upendeleo
wa kwanza kwa wilaya ya Magharibi ili kukabiliana na tatizo la
msongamano wa wanafunzi katika Skuli za Wilaya hiyo.
EmoticonEmoticon