DC Moshi Chang'a enzi za uhai wake
WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda ameongoza viongozi kadhaa na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam
kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo,
Bw. Moshi Chang’a ambaye alifariki dunia Aprili 20, 2014 kwenye Hospitali
ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Shughuli ya
kuuaga rasmi mwili wa marehemu Chang’a kwa wakazi wa mji wa Dar es Salaam ilifanyika
leo mchana (Jumanne, Aprili 22, 2014) nyumbani kwake Mbagala, Kibonde Maji, nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Mwili wake utasafirishwa leo jioni kwenda Kihesa,
mkoani Iringa kwa mazishi.
Akizungumza na
waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za mwisho, Waziri Mkuu Pinda alisema amemfahamu
Bw. Chang’a kwa muda mrefu kwa sababu sehemu kubwa ya utumishi wake ameifanya
akiwa Serikalini.
“Ninyi
mlimfahamu Bw. Chang’a kivingine lakini mimi nilimfahamu kwa namna ya tofauti
kutokana na jinsi alivyokuwa msaada mkubwa kwa Serikali kila tulipokuwa
tukipata shida ama migogoro ya kiuongozi.”
“Kama TAMISEMI,
tumemtumia sana kusawazisha mambo kwa sababu Mungu alimjalia kipaji cha pekee
ambacho ni ucheshi... hata jambo lingekuwa gumu vipi, huyu Bwana alijua
kufikisha ujumbe bila kumuudhi mhusika kutokana na maneno yake,” alisema Waziri
Mkuu.
Alitumia fursa
hiyo kufikisha salamu za rambirambi kwa wafiwa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete
ambaye yuko safarini kikazi.
Vilevile,
aliwataka wanafamilia ambao wamebaki bila mama wala baba, wawe na umoja na mshikamano
na kuahidi kuwa Serikali itawasaidia watoto wa marehemu wakamilishe malengo ya elimu
yao kama ambavyo baba yao alikuwa amepanga.
Marehemu Chang’a
anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumatato, Aprili 23, 2014) huko Kihesa, Manispaa ya
Iringa ambapo Serikali itawasilishwa na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa
Ghasia. Marehemu ameacha watoto watano, wa kike watatu na wa kiume wawili.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM
JUMANNE, APRILI 22, 2014
EmoticonEmoticon