FDL KUTIMUA VUMBI WIKIENDI HII

October 11, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote matatu inaendelea wikiendi hii ambapo kundi B litakuwa na mechi moja tu kati ya Lipuli na Mlale JKT itakayochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.

Transit Camp itakwaruzana na Tessema katika Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Polisi Dar itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam katika mechi za kundi A zitakazochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu).

Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kuzikutanisha Friends Rangers na Villa Squad.

Timu zote nane za kundi C zinashuka viwanjani kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kusaka pointi tatu. Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Dodoma na JKT Kanembwa ya Kigoma.

Pamba na Mwadui zitacheza katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Polisi Tabora itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati uga wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma utatumika kwa mechi kati ya Polisi Mara na Stand United ya Shinyanga.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »