Mkutano huu maalum umeitishwa baada ya ICC kukataa ombi la wanachama 54 wa Muungano wa Afrika kurejesha kesi za Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto nyumbani
Viongozi hao wanatarajiwa kujadili hoja ya kujiondoa kutoka kwa mahakama hiyo.
Baada ya miezi kadhaa ya kutofautiana kati ya ICC na AU, viongozi wa Afrika wanakutana katika makao makuu ya AU katika kile kinachosemekana ni kutafakari upya uhusiano wa bara hilo na mahakama ya ICC.
Kwa mujibu wa AU, mahakama hiyo ya ICC imekosa kushughulikia ombi lililowasilishwa na AU mwezi Mei kuhusu kesi za Kenya. AU inasema kuwa ICC ina njama za kibaguzi dhidi ya viongozi wa kiafrika.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wanakabiliwa na kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu katika mahakama hiyo.
Kesi yao inahusiana na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya mwaka 2007/2008 ambapo zaidi ya watu 1100 waliuawa.
Hata hivyo viongozi hao wamekanusha madai hayo.
Bunge la Kenya ambalo lina idadi kubwa ya wabunge wa mrengo wa Jubilee unaotawala nchi, tayari lieanzisha hoja ya kuondoa Kenya kutoka katika mahakama ya ICC.
Lakini serikali ya Kenya imesema haijashinikiza
nchi za Afrika kujadili hoja ya kujiondoa ICC licha ya kuungwa mkono na majirani zake kama Uganda na Rwanda.
Naibu mwenyekiti wa AU Erastus Mwencha, ameambia BBC kuwa swala hilo sasa ni zaidi ya kutaka tu kujiondoa ICC.
Wadadisi hata hivyo wanasema kuwa huenda AU isikubali kwa ujumla kujiondoa ICC. Baadhi ya nchi kama Ghana na Botswana tayari zimepinga hatua ya kujiondoa ICC.
EmoticonEmoticon