NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imewarejesha warufani wote watatu katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa
Kamati mpya ya Utendaji ya TFF utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu jijini
Dar es Salaam.
Samwel
Nyalla, Ayubu Nyaulingo na Ayoub Nyenzi walikata rufani mbele ya Kamati
hiyo inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard
Luanda kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwaondoa katika
uchaguzi huo ambapo wote wanagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji
kuwakilisha kanda mbalimbali.
Akisoma
uamuzi wao leo (Oktoba 11 mwaka huu) mbele ya Waandishi wa Habari
kwenye ofisi za TFF, Jaji Luanda amesema baada ya kusikiliza hoja za
Mrufani Nyalla walipitia Kanuni za Uchaguzi za TFF na kugundua
yafuatayo;
Ibara
ya 10(3) imeweka masharti makuu mawili ya ujazaji wa fomu za kugombea
uongozi. Fomu hiyo ni lazima iwe na saini ya mgombea na ni lazima
ithibitishwe na viongozi wa shirikisho.
Kamati
imepitia Kanuni za Uchaguzi haijaona sehemu fomu hiyo ya uongozi
imeambatanishwa ili kuifanya kuwa Kanuni ya Uchaguzi. Ni maoni ya Kamati
kuwa ni vizuri fomu za kugombea zikawa ni sehemu ya Kanuni za Uchaguzi.
Kwa
vile Kanuni za Uchaguzi za TFF za 2013 pia hazijaainisha nini adhabu
kwa mgombea aliyekosea kujaza Fomu namba 1 ya kugombea uongozi, Kamati
inaona itakuwa si haki kumnyima mgombea nafasi ya kushiriki katika
uchaguzi kwa vile tu fomu yake haijajazwa vipengele vyote.
Nyalla
aliondolewa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa maelezo
kuwa si mtu makini anayeweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu baada
ya kushindwa kujaza Fomu namba 1 kipengele cha 15 kinachohusu malengo ya
mgombea uongozi.
Kwa
upande wa Nyaulingo ambaye aliondolewa kwa kukosa uzoefu uliothibitika
kulingana na Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni
za Uchaguzi za TFF, Kamati ya Rufani imeamua ifuatavyo;
Kamati
ya Rufani ya Uchaguzi imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya
kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake
alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.
Mrufani
alifafanua historia yake katika masuala ya michezo kuanzia alipokuwa
anasema Chuo Kikuu kuanzia 2005-2009 na pia ushiriki wake kama mchezaji
wa Rukwa United iliyowahi kushiriki Ligi ya Mkoa wa Rukwa na ligi
nyingine za kitaifa.
Kwa
kusoma maana ya ‘Familia ya TFF’ iliyoko kwenye utangulizi wa Katiba ya
TFF, pamoja na Ibara ya 29(3) na 29(6) ya Katiba hiyo, Kamati
imejiridhisha kuwa Mrufani ana sifa za kugombea uongozi wa Shirikisho na
amekidhi kigezo cha sifa za ugombea.
Ameshiriki
kwenye mchezo wa mpira wa miguu kama mchezaji na mtawala, hivyo
kutimiza kigezo kilichohitajika cha ushiriki katika uongozi na utawala
wa mchezo wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
Kwa
kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya
Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani anapewa
nafasi ya kushiriki katika uchaguzi.
Kuhusu
Ayubu Nyenzi aliyeondolewa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa Ibara ya
29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF,
na pia kushindwa kuthibitisha uraia wake mbele ya Kamati ya Uchaguzi,
Kamati ya Rufani katika uamuzi wake imesema;
Imepokea
sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka
kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya
Uchaguzi.
Baada
ya uchambuzi wa kina, Kamati imeona kuwa kulingana na maelezo
yaliyotolewa na Mrufani na viambatanisho vilivyowasilishwa, Kamati haina
shaka kuhusu uraia wake. Uthibitisho wa uraia unapaswa kufanywa kwa
umakini na taasisi yenye mamlaka ya kiserikali kufanya hivyo.
Kamati
pia imejiridhisha kupitia Fomu namba 1 iliyojazwa na kusainiwa na
Mrufani kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010, Nyenzi ameshika nyadhifa za
utawala wa mpira wa miguu na hasa katika klabu ya Yanga, uzoefu
unaomfanya kuwa na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi katika TFF
kulingana na Ibara ya 29(3) ikisomwa pamoja na Ibara ya 29(6).
Kwa
kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya
Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani atashiriki
katika uchaguzi wa TFF kwa nafasi anayogombea.
Wakati huo huo,
Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF inakutana keshokutwa (Oktoba 13
mwaka huu), kufanyia mapitio (revision) ya uamuzi wa Kamati ya Maadili
kwa waombaji uongozi wanane kama ilivyoombwa na Sekretarieti ili kutoa
mwongozo wa utekelezaji wa uamuzi huo.
EmoticonEmoticon