WABAKAJI WAADHIBIWA KWA KUKATA NYASI KENYA

October 11, 2013
NA MWANDISHI WETU,KENYA
Wakenya wameghadhabishwa sana na hatua ya wanaume watatu waliombaka msichana mmoja na kutupa mwili wake kwenye choo kuamrishwa na polisi kukata nyasi kama adhabu kwao.

Msichana huyo alishambuliwa na kubakwa akiwa njiani kutoka kwa mazishi ya babu yake katika kijiji kimoja Magharibi mwa nchi.

Kwa mujibu wa taarifa za gazeti la Daily Nation nchini Kenya, uti wa mgongo wa msichana huyo ulivunjika wakati wa ubakaji na sasa amelazimika kutumia kiti cha magurudumu.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu pamoja na wabunge wamelaani polisi kwa kukosa kuchunguza madai ya msichana huyo.

Msichana huyo alinukuliwa akisema kuwa anataka waliomfanyia kitendo hicho kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Idara ya polisi inawachunguza polisi waliopokea malalamishi ya msichana huyo , alisema Halima Mohammed , kamanda wa polisi katika jimbo la Busia ambako kitendo hicho kilitokea.

Hii bila shaka inaonyesha wazi ulegevu wa polisi katika kukabiliana na vitendo kama hivi na ambao wakenya wanahisi kuwa unakumba idara ya polisi , hasa baada ya mashambulizi ya kigaidi nchini humo wiki mbili zilizopita.

Msichana huyo aliwafahamu vyema waliombaka na polisi walirekodi kesi dhidi ya watatu hao.

Wanakijiji waliwapeleka watatu hao kwa polisi baada ya kusikia taarifa za kitendo hicho.

Lakini waliamrishwa kukata nyasi katika bustani la makao ya polisi na kisha baadaye kuachiliwa, alisema mamake mwathiriwa.

Masaibu ya msichana huyo yalijadiliwa na kamati ya bunge kuhusu usalama na kusema kuwa kitendo hicho ni cha kushutua sana na lazima wakifanyie uchunguzi.

Kwa mujibu wa Bi Mohammed, mama ya msichana huyo aliamrishwa kumsafisha mwanawe ili ushahidi wowote dhidi ya washukiwa uweze kupotea.

Msichana huyo sasa amelemazwa na kulazimishwa kutumia kiti cha mgurudumu.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »