Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inakamilisha raundi ya nane kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kwa mechi tatu zitakazochezwa Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.
Simba
ina fursa ya kuendelea kukamata usukani wa ligi hiyo iwapo itaishinda
Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Tanzania Prisons inayofundishwa na
Jumanne Chale inashika nafasi ya kumi na moja katika msimamo wa ligi
hiyo.
Ili
iendelee kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo
iliyoanza Agosti 24 mwaka huu, Tanzania Prisons ambayo katika mechi yake
iliyopita ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting
inalazimika kuifunga Simba.
Licha
ya sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting,
Simba inayoongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Azam na Mbeya City
matokeo mazuri katika mchezo huo ni muhimu kwao kama ilivyo kwa
wapinzani wao Tanzania Prisons.
Viingilio
katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh.
20,000 ambapo tiketi zitauzwa uwanjani kwenye magari maalumu kuanzia saa
4 kamili asubuhi.
Mabingwa
watetezi Yanga wao watakuwa mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba
kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wanaofundishwa na Mganda Jackson Mayanja
akisaidiwa na Mrage Kabage.
Kagera
ambayo inapishana na Yanga kwa tofauti ya pointi moja ilipoteza mechi
iliyopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya kulala kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja
wa Azam Complex. Wakati Yanga ikiwa katika nafasi ya nne kwa pointi 12,
Kagera Sugar ni ya sita kwa pointi kumi na moja.
Iwapo
Kocha Ernst Brandts atawaongoza vijana wake wa Yanga kuibuka na ushindi
katika mechi hiyo na Simba kufanya vibaya kwenye mechi dhidi ya
Tanzania Prisons huenda akakamata uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha
timu 14.
Mwamuzi
Zakaria Jacob wa Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya Ashanti
United na Coastal Union itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo
Chamazi, Dar es Salaam.
Raundi
ya tisa ya ligi hiyo inaanza keshokutwa Jumapili (Oktoba 13 mwaka huu)
kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers (Mabatini, Mlandizi),
Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na JKT Ruvu (Azam
Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu,
Turiani).
Mechi
zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam TV kupitia TBC1 wikiendi
hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Jumamosi katika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu
itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.
EmoticonEmoticon