Jonas Kamaleki- MAELEZO
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
kwa kushirikiana na wadau wanaohusika na uwezeshaji wa uwekezaji nchini
wamejipanga kuondoa ama kupunguza ukiritimba katika utoaji vibali kwa
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo na
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geofrey Mwambe katika mahojiano maalum na
Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam.
Mwambe amesema kuwa mashirika na
taasisi mbali zinazohusika na utoaji vibali kwa wawekezaji ikiwemo,
Idara ya Kazi, Uhamiaji, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni
(BRELA), Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na wadau
wengine wameazimia kuangalia sheria zao na kuainisha maeneo
yanayokwamisha uwekezaji na kuyafanyia kazi mara moja.
“Tutumie Sheria katika kufikia
malengo na sio kukwamisha uwekezaji, ili tuweze kufikia uchumi wa kati
unaotokana na viwanda,”alisema Mwambe.
Aidha, Mwambe amesema vibali vya uwekezaji vitolewe kwa muda mfupi ili kuvutia wawekezaji wa ndani nan je ya nchi.
Amesema hati ya umiliki wa ardhi
kwa ajili ya uwekezaji itolewe kwa wakati ili kumwondelea mwekezaji
usumbufu unaoweza kujitokeza, kwa kufanya hivyo wawekezaji wataongezeka
na hivyo kujenga viwanda vingi ambavyo vitaongeza ajira hasa kwa vijana.
Katika kuhakikisha uwekezaji nchini unarahisishwa, kimeanzishwa kituo kimoja cha kutolea huduma zinazohusu uwekezaji (One stop Centre) katika ofisi za TIC. Hii inamrahisishia mwekezaji kupata huduma zote sehemu na hivyo kumuondolea bughdha ya kupoteza muda.
Kwa mujibu wa Mwambe, TIC
inatafuta pia namna bora ya kulipia vibali mbali mbali vya uwekezaji
katika sehemu moja na malipo hayo kupelekwa katika ofisi husika kwa njia
ya kielektroniki.
Zipo hatua nyingine nyingi
zinazochukuliwa ili kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji.
Mpaka sasa TIC kwa kushirikiana na taasisi na mashirika mbali mbali ya
Serikali wameshaondoa vikwazo 53 vya uwekezaji.
Ikumbukwe kuwa Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa
akisema kuwa hataki ukiritimba na zile kauli za “njoo kesho”, “tuko
kwenye mchakato” au “tutalishughulikia”. Kwa kuzingatia hilo TIC kwa
kiwango kikubwa imeondoa na inaendelea kuondoa ukwamishaji katika eneo
la uwekezaji.
Kamati ya Taifa ya Huduma kwa
Wawekezaji inaendelea kutafuta njia ya kuhakikisha inapunguza vikwazo
ama urasimu katika uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wa ndani na
nje ya nchi ili kujenga uchumi wa viwanda.